Jumatano, 15 Februari 2017

MAISHA NI KAMA VILE NDOTO


Unaweza ukalala wakati wowote hasa usiku, ukajiona uko na ndugu wengi mmeizunguka meza, mnakula na kufurahiana sana. Wakati mwingine mnabishana, mnafokeana na kukasirikiana na kuchongeana kwa wazazi au wakubwa wenu wa familia. Wakati mwingine unaota uko na mafanikio makubwa katika viwango vyetu kama watanzania, ambao mafanikio tunahesabu ni kuwa na kipato cha kukuwezesha kuishi kila siku na kuweka akiba kidogo. Nyumba nzuri, shamba na usafiri wako binafsi.
Lakini unaamka asubuhi unajikuta kumbe huna kitu! Ilikuwa ni ndoto tu. Bilionea mmoja Billy Gates aliwaeleza waandishi wa habari kwamba akifa mali zake zote zitumike katika kufanya utafiti wa magonjwa yaliyoshindikana ukiwapo ukimwi, aliwaeleza waandishi kwamba maisha ni kama mchezo ambao kila mtu anatakiwa aucheze kwa kadri anavyoweza. Alisema kwa utajiri alionao watoto wake na vizazi vyao wanaweza kula bila kufanya kazi kwa miaka mingi sana, kwa hiyo hawataweza kufaidi mchezo wa maisha ambao wakati mwingine ni kama kuchanga karata au kutupa kete.
Kuna wakati katika maisha ya kawaida unapita kwenye kipindi chenye uchungu sana kiasi unajisemea moyoni kwamba unaweza kujuta kuzaliwa. Lakini kwa neema ya Mungu unapita na kusahau inabaki kuwa kama historia tu.

Na hasa kwa kufikiria kwamba jambo likishatokea haliwezi kurudi, inabidi ufute machozi na kuangalia nini kinachoendelea mbele. Wakati napoteza mama yangu mzazi nilikuwa bado mdogo sana nina umri wa miaka kama mitano hivi. Katika umri huu mtoto ndio anakuwa anamuona mama yake ndio kila kitu katika dunia hii. Na chochote anachotaka mama atampatia tu. Kuanzia ulinzi kutoka kwa ndugu wakubwa wanaomchokoza au watoto wa majirani n.k.
Ilikuwa ni kawaida ukichelewa kurudi nyumbani ni lazima utafutwe na ukipatikana ni lazima uchapwe. Lakini ikatokea ghafla hakuna mtu wa namna hiyo unaporudi nyumbani umechelewa moyo unadunda kwa hofu ya kuadhibiwa. Unakwenda jikoni kuchungulia kwa tahadhari labda utamuona mama lakini hukuti mtu, unajaribu kuingia sebuleni kwa kunyatia pia huoni mtu. Harafu unakumbuka siku ile walipokuwa wanaufukia mwili wake kwenye shimo. Unajisikia kwenye moyo ni kama kuna mtu anauchanja moyo wako na kiwembe.
Unakaa chini kwa muda, ukiangalia ulivyochafuka kwa vumbi la mpira uliokuwa unacheza limekujaa mwilini. Na baridi la kwetu mwezi wa sita na wa saba ni kali balaa! bila kuoga maji ya moto ni adhabu kubwa sana. Lakini sasa hakuna jinsi, mtu aliyekuwa anakujali kwa kukuchemshia maji ya kuoga hayupo tena duniani. Una namna mbili ya kufanya kuamua ama ulale bila kuoga au uoge maji baridi, na baridi yake ni kama barafu iliyoyeyuka. Wakati unatafakari haya ukiwa pembeni ya jiko la mkaa ili upate joto. Ndio mtu mwingine hasa dada anakumbusha umuhimu wa usafi wa mwili kwa afya.
Unajaribu kumwangalia kwa jicho la hasira, lakini haisaidii. Unalazimishwa kwenda kuoga maji ya baridi bila huruma. Mtetezi wako ambaye angalau ulikuwa ukilia anaumia moyo sasa hayupo tena. Hayo ndio yanakuwa ndio maisha yako ya kila siku kujipigania mwenyewe. Hata kama baba yupo lakini huwezi kujieleza vizuri mbele yake. Na yeye hana ujuzi wa kujua sana tabia za watoto, kwa hiyo wanachosema kaka na dada zako ndicho anachoamini.
Hapo inabidi mwenyewe ujiongeze na kukubaliana na hali ili mradi maisha yaendelee. Wakati mwingine unajikuta wakubwa wako wametawanyika hawapo nyumbani wamekwenda sehemu mbalimbali za nchi kutafuta maisha. Na wewe ndio unajikuta umekuwa mkubwa hapo. Baba yuko mbali mnaonana mara moja kwa juma. Hapo inabidi wewe ndio uwe baba na mama kwa kuwalea wadogo na wajomba zako. Unachojua  kupika ni chai tu, labda na kuchemsha maharage ambayo umekatia nyanya na kitunguu na kumiminia mafuta juu kwa juu bila kukaanga. Lakini muda umefika wadogo na wajomba zako wanatakiwa kula. Unajaribu kupika ugali lakini kabla maji hayachemka unatia unga, matokeo yake ugali unatota haujaiva haufai kuliwa! Unachungulia nje kuona kama kuna mtu anakuangalia kisha unachimba shimo na kubeba sufuria ya ugali na kuumwaga.

Kisha unaanza kupika tena mwingine kwa sababu hakuna mtu wa kukufundisha unakuwa unatumia zaidi makosa kwa kujifunza. Hapo hakuna jinsi, wadogo zako wanatakiwa wale, hatimaye unajitahidi ugali unaiva lakini una maruturutu ya unga kibao! lakini kwa sababu wote mna njaa mnabaki kula huku mkiusifia kwamba hakuna ugali mtamu kama huu! Na kwa sababu kati yetu wote ni wavulana kazi zote tunapangiana wenyewe na nyingine zinaamuliwa kwa kupigana ngumi,
na watu wakianza kupigana mnawatengenezea uwanja, hakuna kuamulia anayepigwa ndio anayekwenda kufanya hiyo kazi. Ukifanya kosa lolote ni push up au kichurachura na adhabu zingine za kujenga mwili. Baada ya muda hakuna mtu mnyonge pale nyumbani! watu wote ni wababe ukianzisha ugomvi unaweza usiishe na kila silaha inatumika kuanzia mawe, meno n.k. Na ile sheria ya asiyefanya kazi asile kwetu ilikuwa inatekelezwa sawasawa. Unaweza kupewa ugali lakini mboga ukatafute mwenyewe kama utakula na chumvi au limao ni wewe tu. Wakati mwingine ninapokutana na marafiki zangu wa zamani. Tukikumbushana hayo huwa tunacheka mpaka machozi yanatoka. Lakini namshukuru sana Mungu kwa kunipa maisha ambayo yamenifanya kuwa jasiri na kuwaheshimu watu. Wakati naanza kujitegemea ili niweze kutoa mchango katika familia nilikuwa katikati ya ndugu wengi.
Kiasi cha kwamba nilijiona sina majukumu makubwa katika familia. Lakini baadae akaanza kupotea mmoja baada ya mwingine mpaka unahisi au niko ndotoni? Mpaka unaogopa lakini ninajipa moyo kwa kuwa nimeokoka na kwa kweli siogopi kifo kwa sababu najua maisha ni kama zawadi tu kutoka kwa Mungu na ni lazima niishi katika kusudi lake. Mungu wetu ni mwaminifu sana na anazijua sana huzuni zetu. Lakini pia anajua namna ya kutufariji.

Maneno haya yawe faraja kwa wote waliopoteza wapenzi wao kwa nyakati mbalimbali.