Jumatatu, 26 Novemba 2012

USHUHUDA MKUBWA WA ALI



Ali
Ali ni mkubwa kati ya watoto tisa lakini hana kumbukumbu yoyote nzuri ya kuwa miongoni mwa familia kubwa hivyo. Walikuwa wakimtania na kumwambia kuwa alikuwa hafanani na mtu yeyote katika familia yake. Mama yake alisema kuwa alikuwa akimchukia na kwamba alikuwa ni mtoto ambaye amefanana naye kidogo sana. Kila siku Ali alijihisi kukataliwa na familia yake na hivyo alipokuwa mtoto alilia sana.
Kwa muda wa miezi minne kila mwaka, Ali alifanya kazi ya kuchunga kondoo. Alianza kazi hiyo alipokuwa na umri wa miaka nane na kuendelea na kazi hiyo hadi alipofikia umri wa miaka kumi na nane. Aliwapeleka kondoo milimani na kwa vile alitumia muda mwingi peke yake alihitaji mtu mwingine wa kuongea naye “alijitengenezea mungu“ moyoni mwake. Mungu huyu alikuwa kama rafiki yake. Angeweza kuongea naye kwa mazungumzo marefu kama vile:“ni vizuri kama nini viumbe vyako ulivyoviumba,“ alipoyaangalia maua, jua, miamba na nyasi. Pengine angeweza kumwuliza huyo mungu swali hili: „Je, utamu wa tunda la apple unatokana na nini?“ Maana aliamini kuwa kulikuwa na Mungu aliyetengeneza au kuviumba vitu vyote vizuri.
Alipokuwa na umri wa miaka ishirini, alianza kunywa pombe sana. Na alipofikia miaka ishirini na mitano alikuwa mlevi wa kupindukia. Wakati mwingine alianza kunywa kabla hata ya saa tatu asubuhi! Aliporudi nyumbani mkewe mara nyingi alikuwa akimwuliza endapo ametoka kunywa pombe. Jambo hili lilimkasirisha mno na kwa hiyo akaanza kumpiga kila siku. Watoto wake walishuhudia manyanyaso hayo na walikuwa na hofu kurudi nyumbani baada ya kutoka shule, kwa hiyo walienda kwenye nyumba za marafiki zao mpaka walipojua kuwa baba yao ameshalala. Ali alitaka sana kuacha kunywa pombe na alichukia sana kwa jinsi alivyokuwa akimnyanyasa mkewe. Hivyo aliamua kuhamia Saudi Arabia ili kufanya kazi kama mkandarasi (fundi mwashi) kwa sababu alikuwa amesikia kuwa ulevi ni kitu kilichokuwa kimekatazwa kisheria. Hata hivyo usiku wa kwanza alipokuwa Saudi Arabia aliona kilevi na akanywa.
Pamoja na kwamba Ali hakuwa ni mtu wa dini, familia yake walisema kuwa ni waislamu lakini hawakujua zaidi kuhusu dini yao. Ali aliamua kwenda Mekka, akitumaini kuwa kwa kutembelea kule kungeweza kumfanya huru kutokana na shida yake ya ulevi. Alisema: „Nilifanya maamuzi moyoni mwangu. Ninaenda kufanya hija ya kweli. Nitakuwa mwislamu halisi na nitaacha kabisa kunywa pombe.“ Usiku ule ule wa kwanza alipokuwa Mekka, Ali aliota ndoto. Katika ndoto ile, alimwona Yesu akishika mkono wake na kumwambia: „Wewe ni wangu.“ Pia aliweka kidole chake kwenye paji la uso la Ali na kusema: “Unahitaji kutoka mahali hapa na kuondoka sasa.” Ali alipoamka alihisi kama alikuwa akielea hivyo akaligusa zulia lake kuhakikisha kuwa alikuwa kwenye nchi kavu. Aliendelea kuisikia sauti ya Yesu ikisema: „Unahitaji kufuatana nami, wewe ni wangu.“ Marafiki zake Ali waliona alama iliyokuwa iking’aa katika paji lake la uso mahali pale ambapo Yesu mwenyewe alikuwa amemgusa, lakini yeye mwenyewe Ali alipojitazama kwenye kioo hakuona chochote. (Alama hii kwenye paji lake ilionekana kama vile „sim,“ aina ya mng’ao ambao hutumika kwa kuwapamba mabibiarusi wa kituruki.)
Ali aliendelea na hija yake. Hata hivyo gari lake alilokuwa nalo kwa mwezi mmoja hivi, liligoma kuwaka ili lianze kutembea. Aliendelea kuisikia sauti ya Yesu: „Unahitaji kuondoka hapa.“ Mara tu alipobadilisha mawazo yake na kuondoka pale Mekka, gari lake liliwaka na kuanza kutembea! Alienda nyumbani kwenye chumba chake alichokuwa amepanga na akasikia sauti ile ile tena. Hapa Bwana Yesu alimwambia kuwa anatakiwa aende Uturuki. Baada ya siku tatu alikuwa Uturuki kwenye sherehe ya „kumkaribisha nyumbani“. Hapo tena akasikia sauti. Wakati huu Yesu alimwambia kuwa awaambie watu wote waliokuwepo pale kuwa, yeye amekuwa Mkristo sasa. Alifanya hivyo, lakini watu hawakutilia maanani juu ya jambo lile la kuokoka.
Hakujua hilo mpaka baada ya miaka michache baada ya ile ndoto ndipo Ali alipoanza kufahamu ina maana gani kuwa Mkristo aliyeokoka. Alikuwa akisikiliza redio aliposikia sauti ikisema: „Yesu alikufa, akafufuka kutoka kwa wafu baada ya siku tatu na sasa anakaa mkono wa kuume wa baba.“ Alimwita mkewe na kumwambia kwamba ameshaipata sauti ya Yesu – ndani ya redio. Kupitia kipindi hicho katika redio, alipokea masomo ya Biblia na pia alipokea Agano Jipya mpya! Alikuwa na umri wa miaka 38 wakati ule na alisema kuwa siku aliyopokea Agano Jipya lile kwa njia ya posta “pengine ilikuwa ni siku ya furaha kubwa maishani mwake kuliko siku yoyote.” Baada ya kumaliza baadhi ya masomo kwa njia ya posta, Ali pamoja na familia yake walihamia Istanbul ili kuweza kusoma shule ya Biblia.
Mpaka leo anaendelea kushuhudia imani yake ya kikristo kwa uwazi na hata bila ya aibu. Ulevi haukuendelea tena kumtawala, na akawa akimtunza na kumpenda mkewe ambaye hapo kwanza alikuwa akimtenda vibaya. Kweli, sasa amekuwa ‚kiumbe kipya ndani ya Kristo.‘


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni