MWL: Furaha Amon
Utangulizi;
Wakati nilipokuwa nikifiria
kuandika hili somo, nilikuwa namkumbuka mchungaji wangu mmoja ambaye alikuwa ni
mchungaji msaidizi katika kanisa nililokuwa mshirika. Huyu mchungaji ni kama
alikuwa hana swali jingine, kila tukikutana ananisomea mstari huu wa Biblia
“Bali
utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa”. (Mathayo
6:33)
Halafu ananiuliza nijibu
ufalme ni nini na haki yake ni nini? Kila jibu nililompa alikuwa haridhiki,
halafu yeye mwenyewe hatoi jibu. Na kila jibu ninalompa analikataa, hatimaye
nikaamua kuwa jeuri na mimi nikawa namjibu kwamba sijui nay eye mpaka wakati
naandika somo hili hajawahi kunipa jibu na tumepoteana kwa karibu miaka saba
sasa. Lakini hii haikunifanya niache kufikiria kutafuta jibu sahihi ya swali
hili, kwa sababu natambua kwamba Biblia haijawahi kuweka maandiko hewa, kwa
sababu kila andiko lenye pumzi ya Mungu liko hai. Kwa hiyo ni muhimu
tukashirikiana pamoja katika kujifunza na kutafakari kwa mapana kuhusu ufalme
wa Mungu na haki yake. Biblia inasema;-
Torati
na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa
Mungu hutangazwa na kila mtu hujiingiza kwa nguvu. (Luka 16:16)
UFALME NI NINI?
Ufalme ni mamlaka, ni
utawala wenye uwezo wa juu wa kufanya maamuzi katika maeneo yanayomilikiwa na
ufalme huo. Tofauti na utawala mwingine wa kidemokrasia ambao unatafsiriwa kama
utawala wa watu uliowekwa na watu kwa ajili ya kuwatala watu. Ambao ki- msingi
hauna nguvu na unaweza kuondolewa tu maandamano ya watu waliokuweka, na kila
uamuzi unaofanya unaweza kuhojiwa na taasisi mbalimbali zikiwemo za utawala
bora na haki za binadamu. Ufalme ni tofauti kabisa na tawala za kidemokrasia,
katika ufalme watu na vitu vyote ambavyo viko katika miliki ya mfalme ni mali
yake. Na anaweza akaamua vyovyote anavyotaka bila kuhojiwa na mamlaka yeyote,
kwa sababu vitu vyote ni mali yake, ikiwa ni pamoja na watu walioko katika
himaya yake.
HAKI NI NINI?
Haki ni hukumu inayotolewa
bila ya kuwa na chembe chembe za upendeleo wa aina yeyote kulingana na sheria zinazohusika
kutoa haki katika utawala fulani ama wa nchi husika au katika miliki yeyote
ambayo watu wanaishi kulingana na sheria zinazowaongoza kama ilivyo kwamba kuna
utawala wa Mungu na pia kuna utawala wa shetani.
Mtu mmoja ambaye Biblia
inasema ndio mtu mkuu zaidi kati ya watu waliozaliwa na mwanamke Yohana
Mbatizaji wakati anawaandaa wayahudi kuhusu ujio wa Yesu, alikuwa na kauli mbiu moja kubwa ambayo Yohana
aliwaambia wayahudi.
“Tubuni;
kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia. Mathayo : 3:2
Kwa maana hiyo Yesu alikuja
duniani pamoja na kuleta wokovu kwa wanadamu lakini pia alikuja kuleta ufalme
wake. Ufalme wa Mungu, ambao ni tofauti
na ufalme wa dunia hii au ufalme wa shetani.
Kwa kawaida kila utawala unakuwa
na sheria zake ambazo zinaweza kuwa za kikatiba kwa maana ya kuandikwa, au
kutokuandikwa yaani kwa kutumia amri, lakini Yesu alikuja kuleta ufalme na haki
yake na ili uweze kuingia na kuishi katika ufalme huu unahitaji zaidi kujua
maana ya haki yake. Tafsiri nyepesi ya ufalme ni kama udikteta sababu
unalimbikiza nguvu na madaraka kwa mtu mmoja ambaye ndie mfalme.
Kwa hiyo ili uweze kuwa
mfalme mzuri inatakiwa uwe mtu ambaye unazingatia haki katika kutoa maamuzi
yako kwa sababu ya nguvu kubwa na mamlaka uliyonayo. Usipotenda haki ni hatari
sana kwa watu na vitu unavyomiliki. Kwa maana hiyo Yesu alipokuja kuuleta
ufalme wake ni muhimu kujua kwamba ili uishi katika ufalme huo ni muhimu kujua
haki yake, kwa maana hiyo haki ndio sheria yenyewe itakayokuwezesha kuishi
katika ufalme wa Mungu.
SIO LAZIMA HAKI NA SHERIA
ZIFANANE KATIKA NCHI
Inawezekana sheria za nchi
moja zikawa tofauti kabisa na sheria za nchi nyingine, kwa mfano hapa kwetu
Tanzania kutumia mirungi ni kosa, sawa na kutumia madawa ya kulevya mengine
kama bangi na heroin. Lakini kwa sheria ya nchi kama ya Kenya, kukutwa na Mirungi
sio kosa, huko ni zao la biashara. Na inaruhusiwa kutumiwa na kuuzwa popote.
Kwa hiyo raia wa Kenya akija Tanzania analazimika kuacha kutumia mirungi
vinginevyo akikamatwa na mirungi akiwa katika ardhi ya Tanzania anakuwa na kosa,
hata kama kwao anaruhusiwa, lakini sheria za ufalme wa Tanzania hiyo kitu ni
marufuku, hapa lazima apate haki yake ambayo ni kifungo.
kama leo utaenda katika
nchi zilizotawaliwa na mfaransa, mfano nchi jirani kama Rwanda na Burundi, wao
sheria yao ya barabarani inaruhusu magari yanapotembea barabarani kutumia
upande wa kulia wa barabara, kinyume na utawala wa nchi ambazo zimetawaliwa na
Mwingereza kama nchi za Tanzania, Uganda na Kenya ambazo magari yanatumia
upande wa kushoto wa barabara.
Sasa wewe unapoendesha gari
kutoka kwenye utawala wa Tanzania ukaingia Rwanda ni lazima ubadilishe upande
wa barabara na kama utaendelea kutumia sheria za barabara za Tanzania katika
nchi ya Rwanda basi uwe na uhakika kwamba hutafika mbali kabla ya kugongwa au
kukamatwa na watunza sheria wa nchi husika.
Sasa Bwana Yesu alikuja
kuleta ufalme wake na haki yake,ufalme aliouleta Bwana Yesu una sheria zake za
namna ya kuishi, kwa mfano wewe umetoka kuishi kwenye ufalme wa giza, utapata
shida sana kuishi kwenye ufalme wa nuru. Kwa tafsiri nyingine ni kwamba,
kinachokuwezesha kuishi katika ufalme wa Mungu ni kwa kufuata sheria ambazo
ziko katika ufalme wa Mungu. Na moja kati ya kazi za mfalme ni kutoa hukumu au
kufanya maamuzi ya haki, Biblia inasema;-
Tazama,
Mfalme atamiliki kwa haki. Na wakuu watatawala kwa hukumu (Isaya 32:1)
Kwa maana hiyo Yesu anapoongelea
haki kama kitu muhimu katika kuupata ufalme wake. Maana yake ni lazima wakati
wote tusimame katika kweli na haki ndipo ambapo tutakuwa tunaishi katika ufalme
wa Mungu. Na hii inamhusu mtu binafsi
jinsi anavyoyatawala mazingira yake, familia yake, jamii yake, mji na Taifa kwa
ujumla. Kitu cha kwanza ambacho kinaashiria kwamba ufalme wa Mungu uko ndani
yako, ni jinsi ambavyo wewe unaamua mambo mbalimbali katika familia yako, kwa
ndugu, jamaa, marafiki na majirani zako, sehemu yako ya kazi, kwa watu walio
juu yako na kwa watu walio chini yako.
Ni namna gani unavyoamua
mambo yao. Je unaamua kwa haki au kwa woga na upendeleo? Je wewe mwenyewe
unapokosea upo tayari kukiri kosa lako? Kama unaamua kwa haki, na unatimiza
mambo yote, basi uko ndani ya ufalme wa Mungu na utakuwa na nguvu katika kutawala
mahali popote utakapokuwa katika ulimwengu wa roho na mwili.
“Na
alipouzwa na mafarisayo, ufalme wa Mungu utakuja lini? aliwajibu akawaambia
ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza;. Wala hawatasema tazama, upo huku, au,
kule, kwa maana, tazama ufalme wa Mungu umo ndani yenu” (Luka 17:20-21)
Ufalme wa Yesu hautaonekana
kwa kila mtu. Yesu alikuja na kuleta
ufalme wake na akasema ufalme wa Mungu upo hata sasa ila ni siri kuujua na
ukiugundua utaishi maisha ya kifalme bila kujali mazingira utakayopitia.
Mambo yanayohusu ufalme wa
Mungu ni mambo ya siri. Na ni muhimu kujifunza masomo kama haya ili uweze
kupata ufunuo wa siri ambazo ziko kwenye maandiko. Ndio maana Yesu anawaambia
wasifikiri ufalme wa Mungu utaonekana waziwazi au tutautazama toka mbali.
Wakati ninatafakari mambo
haya nikaona nitafute mtu mmoja ambaye alipitia maisha magumu lakini bado alijitahidi
kuhakikisha anaishi akiwa ndani ya ufalme wa Mungu.
Hebu tuangalie kidogo maisha
ya Yusufu mtoto wa Yakobo. Huyu alipata bahati ya kupendwa na baba yake kama
ambavyo Biblia inasema;-
“Basi
Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake
akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko
ndugu zake wote, wakamchukia wala hawakuweza kusema naye kwa amani”. (Mwanzo
37:3-4)
Ukifuatilia kwa makini kisa
hiki cha kusisimua unaweza kujifunza mambo mengi sana aliyopitia Yusufu ambayo
yanasikitisha na kuumiza sana nafsi hata ya msomaji, wengi tunajua kuwa
kulikuwa kuna tabia ya upendeleo katika taifa na tunajua kwamba hata isaka
alimpenda sana mwanae wa kwanza Esau na Rebeka akampenda zaidi Yakobo, inawezekana
kwa sababu ya tabia zao, maana Esau alikuwa mwindaji aliyeleta nyama nyumbani
na Yakobo yeye alikuwa kama mtoto wa mama akishinda nyumbani kumsaidia mama
kazi. Tunajua uadui ambao ulitokea kwa Esau na Yakobo ambapo ilibidi Yakobo
akimbie maana ndugu yake aliapa kumuua. Lakini cha kushangaza Yakobo naye
anafanya kosa kama hilo la baba yake la kuonyesha kumpenda Yusufu kuliko watoto
wake na hivyo kusababisha chuki kwa ndugu zake ambao yeye aliwapenda na
kujisikia yupo salama akiwa karibu nao, lakini matokeo yake walitaka kumuua na
hatimaye kuishia kumuuza kwa potifa akida wa jeshi la farao. Biblia inasema;-
“Basi
Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa Farao mkuu wa askari, mtu wa
Misri, akamnunua mkononi mwa hao waishmaeli waliomleta huko. Bwana akawa pamoja
na Yusufu naye akasitawi naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, Yule Mmisri.
Bwana wake akaona ya kwamba Bwana yu pamoja naye, na ya kuwa Bwana anafanikisha
mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye
akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake. Na yote yaliyomo akayaweka mkononi
mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote
vilivyomo. Bwana akabariki nyumba ya Yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka
wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.
Akayaacha yote aliyokuwa nayo mikononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu
chochote chake, ila hicho chakula alichokula tu.” (Mwanzo 39:1-6)
Katika maandiko haya
tunaona kwamba pamoja na ugumu wa mazingira ya maisha ya Yusufu, kutoka kwa
baba yake mzazi aliyempenda na kumshonea
kanzu ndefu na kuwa mtumwa wa mkuu wa majeshi katika nchi ya kigeni, hapo
inahitaji uwe na moyo safi usio wa kawaida ili uweze kumuona Mungu na kuuvuta
ufalme wake. Lakini tunaona Yusufu aliweza kutulia na kutawala katika nyumba
hiyo ya potifa, alikabidhiwa kila kitu kasoro mke wa Potifa na chakula cha
potifa, hapo kwenye chakula nafikiri ni kwa sababu ya usalama kwa sababu huyu
Potifa ni mkuu wa majeshi na huyu kijana ni raia wa kigeni kwa hiyo kiusalama
hawezi kumwandalia chakula. Lakini mambo mengine yote alikuwa anaamua yeye,
akiamua kuchinja ng’ombe, kuku, bata n.k.
Lakini baadae linatokea
tena balaa lingine mke wa bosi wake anaanza kumtamani azini naye, sharia hiyo ni
kinyume na sharia za ufalme wa Mungu, huyu mama alikuwa anataka kuizima nuru ya
ufalme wa Mungu na haki yake Yusufu akaona sio sawa akaamua kukimbia.
Tunafundishwa katika hili kwamba dhambi ya zinaa inakimbiwa usijadiliane nayo.
Baada ya kitendo hicho hatimaye Yusufu anajikuta yupo jela, mazingira
yamebadilika tena kutoka mtumwa aliyekabidhiwa kila kitu na kuwa mfungwa jeuri
asiye na adabu anashitakiwa kwa kosa la kutaka kumbaka mke wa bosi wake, Biblia
inasema;-
“Ikawa
baada ya mambo hayo mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia lala nami.
Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama bwana wangu hajui kitu
kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu.
Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu chochote ila
wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu? (Mwanzo
39: 7-9)
Kwa hiyo Yusufu akajikuta
matatani tena lakini bado pamoja na kuwa jela akajikuta ameupeleka tena ufalme wa
Mungu kiasi kwamba biblia inasema;-
“Lakini
Bwana akawa pamoja na Yusufu akamhifadhi. Akampa kibali machoni pa mkuu wa
gereza. Mkuu wa gereza akawatia mikononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa,
waliomo gerezani na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya. Wala mkuu wa
gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu kwa kuwa Bwana alikuwa
pamoja naye. Bwana akayafanikisha yote aliyoyafanya”. (Mwanzo 39:21-23)
Hapa tunaona Yusufu
anajikuta anaishi tena kama mfalme ndani ya gereza! watu wote wamewekwa chini
yake, kwa hiyo na mipango yote ya kazi juu kazi gani zifanyike na nani azifanye
alikuwa anapanga yeye. Mtu mwingine anaweza akafikiria kwamba ilikuwa kazi
rahisi sana, lakini matukio yote mawili yaliyompata yalikuwa yanaiharibu kabisa
nafsi yake, kumbuka waliotaka kumuua ni kaka zake ambao kwa kawaida walipaswa
kuwa walinzi wake yaani kujihisi kuwa salama ukiwa nao, na hakuwa na kosa kwa
sababu sio yeye aliyemwambia baba yake mzazi ampendelee, mbele za Mungu alikuwa
na haki. Fikiria inavyouma kutenganishwa na baba yako ambaye unajua kwamba yeye
ni kipenzi chako, wakati mwingine unaweza usijifikirie wewe zaidi bali
ukafikiria ugumu wa zile taarifa atakazopatiwa kuhusu wewe na uchungu
atakaokuwa nao akikaa huku anaamini kwamba umekufa. Biblia inatuambia mzee
Yakobo aliomboleza kwa siku nyingi sana na akajiapiza kwamba mpaka siku anakufa
atakuwa anahuzunika kwa ajili ya mtoto wake aliyempenda sana. Halafu anafika
ugenini mambo yameanza kukaa sawa halafu linkuja balaa ambalo unazushiwa jambo
na mtu ambaye ndio kama mama mlezi wake, harafu anakuwa huwezi kujitetea, kisha
anatupwa kwenye gereza ambalo sio la kawaida tunaambiwa ni gereza wanalofungwa
wafanyakazi wa mfalme na viongozi wengine wakuu, magereza ya namna hii ni
magereza wanayofungwa wahaini. Maana kuwakosea viongozi ni sawa na kuasi, haya
matukio mawili pekee yalitosha kabisa kumkatisha tamaa, na pengine ingemfanya
atumie muda mrefu sana kutuliza maumivu na majeraha aliyoyapata kutokana na
majanga aliyopata. Lakini yeye alikubaliana na mazingira yote aliyopitia na
kuhakikisha anautafuta ufalme wa Mungu na haki yake. Ambayo hatimaye alijikuta
Mungu amemuinua kutoka gerezani hadi kuwa waziri mkuu. Hii ni habari ya ajabu
sana. Yusufu anakuja kuivusha dunia katika kipindi kigumu cha miaka saba ya
njaa. Na tunaona jinsi anavyoungana na ndugu zake katika namna ambayo
inasisimua sana. Kiasi ambacho unaona kabisa anavyowapenda kiasi cha kutoka
machozi. Kuna wakati fulani Mungu anatulazmisha kukaa kimya hata tunapozuliwa
mambo magumu sana. Shetani yuko kila mahali na kwa viwango tofauti. Shetani
anayeishi kanisani anakiwango kikubwa kuliko shetani anayeishi vilabuni na
kwenye madangulo. Wakati mwingine uongo unaotengenezwa ndani ya makanisa
unakuwa ni mbaya zaidi kuliko unaotengenezwa vilabuni na kwenye madangulo.
Mtumishi mmoja rafiki yangu alikuwa na neema kubwa sana kanisani kwake, kiasi
kwamba washirika wengi walikuwa wanakwenda kwake kuombewa na kufanyiwa huduma
zingine za kiroho, na wengine walimwalika maeneo mengine mbalimbali majumbani
kwao, hali hii haikumfurahisha shetani na wajumbe wake wakasema yeye ni nani
anataka kujifanya zaidi ya mchungaji, wakaamua kutengeneza fitina wakajipanga
vizuri na kuweka ushahidi wa uongo kwamba huko anakokwenda kufanya huduma anazini
na wakaweka watu kiasi cha kwamba neno hilo lilipofika kwa mchungaji mchungaji
akaamua kuitisha kikao cha wazee na kusikiliza ushahidi ule wa kupangwa na
wakaamua kufanya maamuzi ya kumfukuza Yule mtumishi kanisani kumtangaza katika
makanisa yote katika jji lile ili asipokelewe na kumtumikia Mungu kwa namna
Yeyote. Waswahili wanasema watu watakunyima chakula lakini hawakunyimi neno.
Habari zikamfikia Yule mtumishi juu ya kila kilichoongelewa na uamuzi ambao
umechukuliwa dhidi yake, alikasirika na kukata tamaa kabisa akapania kwamba wakimwita
kwenye hicho kikao, ndio watajua kwamba kukaa kwake kimya sio kwamba hajui
kusema. Kwa hiyo alipania kwenda kupambana nao kwa akili zake yaani kuwapa
vidonge vyao. Siku iliyofuata wakati huo hakuna simu alitumwa mjumbe kuja
kumwita aende kanisani kukutana na mchungaji, anasema wakati analetewa huo
ujumbe alikuwa yupo kitandani lakini hana usingizi bali anapangilia maneno
magumu atakayokwenda kuwapaka wabaya wake mbele ya wakuu wake wa dini. Kwa hiyo
baada ya kupata huo ujumbe huku akiwa na hasira kiasi kwamba hata wakati anavaa
nguo alikuwa anatetemeka kwa hasira. Wakati anatoka chumbani kwake kwenda
sebuleni ilia toke kwenda nje ndipo akaona kitndo ambacho sio cha kawaida. Vile
anafungua tu mlango anakutana na mtoto wake ambaye alikuwa ni mdogo sana hajui
hata kuongea, anakaribia miaka mitatu hivi akasimama halafu akamwambia kwa
sauti ya ukali, huku amemnyooshea kidole “wewe nakwambia usiende kuja juu
kanisani, umesikia, nasema usiende kuja juu kanisani” huyu mtumishi akashituka
inakuwaje mtoto ambaye hajui hata kusema aongee kwa ukali namna hii! Akamwita kwa
jina lake akamuuliza kwa upole unasemaje mwanangu, akaona yuko kimya wala
haelewi hata anachoulizwa. Ndipo akajua kuwa hiyo ni sauti ya Mungu na ikabidi
kutii huku machozi yanamtoka.
Alipofika kwenye kikao
alionekana mtulivu sana maana maneno yaliyokuwa akiambiwa alikuwa anayajibu kwa
utlivu na hekima ya hali ya juu. Mwisho Askofu wake anamwambia kwa kweli
tulikuwa tumepanga kukufukuza na kutwanya barua nchi nzima ili usipokelewe,
lakini kwa jinsi ulivyoongea kwa ushirikiano hatuoni kosa lako, lakini pamoja
na hayo mimi nakuruhusu uende kesho uniletee jina la kanisa lingine unalotaka
kwenda, maana hapa umeshachafuka sana. Akwajibu basi sawa. Sasa kivumbi
kikatokea wakati wanasema tuombe kwa ajili ya kufunga kikao, anasema ilishuka
nguvu kubwa na kila mtu alianguka chini na kunena kwa lugha kama watu
wanaoomboleza na hawakuacha mpaka mama mmoja alipopata ufunuo na kuwaambia
jamani hili jambo liishe na huyu mtumishi asiondolewe hapa kanisani, ndio
wakapata nguvu na kutawanyika. Na baada ya siku si nyingi wale watu waliopanga
uovu huo wakaeleza ukweli kwamba walipanga maneno.
Mwisho napenda kukushauri
ndugu yangu utafute kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote
utazidishiwa.
MUNGU AKUBARIKI. Tunaweza
kuwasiliana na mimi kwa namba ya simu 0677 609056