Alhamisi, 2 Februari 2017

KUSIKIA SAUTI YA MUNGU KUPITIA PICHA, MAONO NA NDOTO (1)




NDOTO NI NINI?
Ndoto ni picha au matukio mbalimbali ambayo mtu anaweza kuyaona wakati akiwa macho au akiwa kwenye usingizi.
Ndoto ni njia mojawapo ya mawasiliano ya mtu na ulimwengu wa roho, Mungu anaweza kuzungumza na wewe kupitia ndoto, lakini pia hivyo hivyo na shetani naye anaweza kuzungumza na wewe kupitia ndoto.
Lakini pia hata wewe mwenyewe unaweza kuota ndoto kutokana na uchovu au kuwa na mawazo mengi, na kwa sababu hiyo upo umuhimu wa kugusia jambo hili la ndoto katika somo letu.
Kuna ndoto zingine ukiota zinajieleza waziwazi wala hazihitaji tafsiri kwa maana ya kwamba ndoto inavyosema ndivyo itakavyomaanisha, lakini pia kuna ndoto zingine zinakuja kimafumbo hizi zinahitaji tafsiri.

MAONO NI NINI?
Maono ni uwezo wa kuona mambo kwa macho ya kiroho kama vile Mungu ayaonavyo, mtu anaweza kuwa na fahamu kamili na macho yaliyo wazi na akaona mambo kama vile tunavyotazama luninga.
Lakini vilevile mtu anaweza kuondolewa ufahamu kama vile amelala usingizi na akaona vitu waziwazi na kusikia sauti ikisema anagalia (Matendo 10:9 - 20)
Petro alikuwa amezimia, lakini macho yake ya kiroho yaliweza kuona maono ya kifurushi cha wanyama mbalimbali. Akiwa katika hali hiyo aliweza kuongea na kuisikia sauti ya Mungu.

Tukilala usingizi ni mwili unaolala kwa maana roho zetu zinakuwa macho. na kama kuna nguvu za giza roho yako huwa inaziona na inapambana nazo katika harakati za kuurudisha mwili katika ufahamu wa kawaida, na hapo ishara kwako itakuwa ni kuota ndoto za kupigana na kuweweseka.
Vivyo hivyo hata kifo kinapotokea ni mwili huharibika lakini roho huwa hai.
UJUMBE WA MUNGU KATIKA NDOTO
Je, unaamini ya kuwa Mungu anaweza kusema na wanadamu kwa njia ya ndoto? Najua na inawezekana ikawa ni lahisi kuamini kuwa Mungu alisema na watu wa zamani kwa njia ya ndoto kama tunavyosoma katika Biblia;
lakini  je! Unaamini ya kuwa Mungu anasema na watu kwa njia ya ndoto siku hizi?
AINA TATU ZA NDOTO
Kwa mujibu wa Biblia kuna ndoto za aina tatu (3)
1. Ndoto kutoka kwa Mungu.                     Sikilizeni basi maneno yangu! Akiwapo nabii kati yenu, mimi Bwana nitajifunua kwake katika maono, nitasema naye katika ndoto.” (Hesabu 12:6)                                                       



Biblia inasema tena;- “Hata itakuwa baada ya hayo. Ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili ; na wana wenu waume kwa wake, watatabiri wazee wenu wataota ndoto na vijana watapata maono”   (Yoeli 2: 28)

2. Ndoto za uchovu                                      ndoto hizi zinazokuja kwa sababu ya shughuli nyingi Biblia inasema “kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi” (Mhubiri 5:3)


3. Ndoto za uongo
                                   ndoto hizi ni zile zinazotoka kwa shetani baba wa uongo Tazama,mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema Bwana, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao na kwa majivuno yao ya upuuzi;lakini mimi sikuwatuma, wala kuwapa amri; wala hawatafaidia watu hawa hata kidogo asema Bwana. (Yeremia 23: 32)                                                 Ninyi ni wa baba yenu ibilisi, na tama za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa sababu yeye ni mwongo. Na baba wa huo (Yohana 8:44)
Tukutane tena katika sehemu ya pili, ambayo tutaangalia mambo ya msingi kuhusu kutafsiri ndoto.
Furaha Amon Mob: 0713 461593 - Tanga

Jumatano, 1 Februari 2017

SOMO: ROHO MTAKATIFU NA MAMBO YAKE (4)


Mwl: Furaha Amon

Utangulizi:
Watu wengi mno ndani ya makanisa wana kiu ya kupata ujazo wa Roho Mtakatifu, lakini bado kuna tatizo kubwa sana linalohusiana na kutomwelewa vizuri Roho Mtakatifu. Kwa kuwa kiu hii ni kubwa, na tatizo la kutomwelewa Roho Mtakatifu ndani ya kanisa ni kubwa sana nimeona ni vema nitumie nafasi hii kutoa mchango kidogo wa kukusaidia kuelewa kwa kiasi habari za Roho Mtakatifu.

TOFAUTI YA HUDUMA YA ROHO MTAKATIFU KATIKA AGANO LA KALE NA KATIKA  AGANO JIPYA
Roho Mtakatifu hakuanzia wakati wa Agano Jipya, yeye kama nafsi ya tatu ya Mungu, hivyo hana mwanzo wala mwisho. Kwa maneno haya, napenda utambue kuwa Roho Mtakatifu alikuwa akihudumu kwa namna fulani hata wakati wa Agano la kale. Ijapokuwa ilikuwa tofauti sana ilivyo sasa katika Agano jipya. Zipo tofauti nyingi za huduma ya Roho Mtakatifu wakati wa maagano haya mawili; zifuatazo ni baadhi ya tofauti hizo.
Wakati wa agano la kale makao makuu ya Roho Mtakatifu yalikuwa mbinguni. Tunapoyaangalia maisha ya mashahidi wa kazi ya Mungu katika Agano la kale, na wale wanaojulikana kama mashujaa wa imani, tunaweza kuona kwa dhahiri jinsi huduma ya Roho Mtakatifu livyozifaikisha njia zao.
n Roho Mtakatifu aliwasaidia kuwaonya watu na kuwakemea
n Kwa Roho mtakatifu mashujaa hawa waliua samba na dubu
n Mashujaa hawa walitenda mambo mengi makuu yasiyoelezeka kwa akili za kibinadamu.
Wakati wakutenda huduma zote hizi. Roho Mtakatifu alikuwa na makao yake ya kudumu mbinguni pamoja na Mungu Baba na Mwana.

KATIKA AGANO JIPYA, TUNAONA UHAMISHO WA MAKAO YA ROHO MTAKATIFU HUYU WA MUNGU; BADALA YA KUKAA MBINGUNI ALIHAMIA NA KUKAA NDANI YA KANISA, KAMA YANENAVYO MAANDIKO.
Yesu alipokuja kukaa duniani; mbinguni aliwaacha wawili, ambao ni Mungu Baba na Mungu Roho Mtakatifu. Alipomaliza  huduma yake duniani alisema maneno haya kabla ya kwenda kwa Baba yake; Alisema,
“Nami nitamwomba Baba, naye atawapa msaidizi mwingine, ili akae nanyi milele”. (Yohana 14:16.)
Kwa hiyo baada ya Yesu kupaa mbinguni, walikuwepo tena watatu mbinguni kwa muda wa siku kumi. Watatu hawa ni Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, baada ya siku hizo kumi baada ya kupaa kwa Bwana, Roho alikuja duniani kuchukua nafasi ya Yesu; na kuanzia wakati huo hadi wakati huu, wako wawili mbinguni, Baba na Mwana na duniani yuko mmoja naye ni Roho Mtakatifu.

KATIKA AGANO LA KALE ROHO MTAKATIFU ALIKUWA KWA WATU WACHACHE TU;
Udhihirisho wa huduma ya Roho Mtakatifu katika Agano la kale ulikuwa tofauti sana na ilivyo sasa. Katika agano la kale Roho Mtakatifu alikuwa anafanya huduma na kudhihirisha nguvu zake kwa watu wachache waliokuwa na huduma maalumu mbele za Mungu au kwa taifa teule la Bwana, ili tupate picha iliyo kamili hebu tuangalie baahi ya watu walioshuhudia huduma na udhibitisho wa nguvu za Roho Mtakatifu vikitenda kazi ndani yao wakati wa Agano la kale.
KWA WAAMUZI NA WAFALME WA TAIFA LA ISRAELI
Waamuzi na wafalme katika taifa la Israel walikuwa ni muhimu mno katika taifa hilo. Makundi haya mawili ndiyo yaliyotunza nuru ya Mungu wakati taifa lao lilipokuwa linaingia katika giza nene. Kwa umuhimu huo waliokuwa nao. Mungu Roho Mtakatifu alifanya kazi katika maisha yao yote, ila walipomwacha Mungu Roho wa Mungu naye aliweza kuwaacha kwa huduma hii ya Roho Mtakatifu, waamuzi na wafalme, waliweza kuzima nguvu za majeshi yenye nguvu, walirarua simba na muda wote walipopigana au kuongoza chin ya uongozi wa Roho Mtakatifu, waliweza kushinda na zaidi ya kushinda.
MANABII NA MAKUHANI
Manabii na makuhaniwalihusika sana kuongoza taifa la Israeli kiroho; wao walikuwa ni mkono na sauti ya Mungu katika taifa la Israel kiroho; nasema hivi kwani kupitia kwao, Mungu aliyaweka maneno yake aliyotaka kunena na watu wake, kupitia kwao Mungu pia aliweza kupokea toba ya watu wake na dhabihu zao.
MWISHO WA SOMO LA NNE

Kwa leo somo letu linaishia hapa, usikose kufuatilia sehemu inayofuata ya somo hili. Kwa msaada zaidi tuwasiliane 0677 609056

SOMO: ROHO MTAKATIFU NA MAMBO YAKE (3)


Mwl: Furaha Amon

Utangulizi:
Watu wengi mno ndani ya makanisa wana kiu ya kupata ujazo wa Roho Mtakatifu, lakini bado kuna tatizo kubwa sana linalohusiana na kutomwelewa vizuri Roho Mtakatifu. Kwa kuwa kiu hii ni kubwa, na tatizo la kutomwelewa Roho Mtakatifu ndani ya kanisa ni kubwa sana nimeona ni vema nitumie nafasi hii kutoa mchango kidogo wa kukusaidia kuelewa kwa kiasi habari za Roho Mtakatifu.
ROHO MTAKATIFU SIO NGUVU KAMA YA UMEME
Watu wengine wanafikiria kuwa  Roho Mtakatifu ni nguvu kama vile ilivyo nguvu ya umeme, mawazo hayo sio sahihi kabisa. Ni kweli kuwa mtu anapompokea Roho Mtakatifu hufunikwa na nguvu isiyo ya kawaida. Lakini nguvu hii sio Roho Mtakatifu. Katika kitabu cha Matendo ya mitume, Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa watapokea nguvu akiisha kuwajilia Roho Mtakatifu. Lakini ukweli ni kwamba Roho Mtakatifu mwenyewe sio nguvu bali ni nafsi hai ya Mungu.

MAMBO YANAYODHIHIRISHA KUWA ROHO NI NAFSI NA NI MUNGU:
ANAWEZA KUHUZUNIKA.
“Wala msimhuzunishe Yule Roho Mtakatifu wa Mungu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi” (Efeso 4:30)
Hapa Roho Mtakatifu kama alivyo mwanadamu, anaweza kuhuzunishwa na kuhuzunika. Ukweli ni kwamba nguvu kama ilivyo ya umeme au nyingine iwayo yoyote ile haiwezi kuhuzunika, lakini roho kama nafsi hai anaweza kuhuzunishwa pale watoto wa Mungu wanapoenda kinyume na neno la Mungu.

HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKIKA:
“ kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi ipasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa” (Rum 8:26)
Huu ni udhibitisho mwingine unaoonyesha kuwa Roho Mtakatifu ni nafsi, huweza kutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Nguvu haiwezi kumwombea mwanadamu kwa Mungu kwa kuugua, bali jambo hili huweza kufanywa na nafsi iliyo hai pekee.

ANAWEZA KUAMBIWA UONGO.
“Petro akasema, Anania, kwa nini shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?” (Matendo 5:3)
Hapa tunamwona Petro akimwonya Anania kuhusiana na mali aliyoipata baada ya kuuza kiwanja chake. Alipouza kiwanja chake hakuleta fedha yote miguuni pa mitume kama walivyokuwa wamepatana katika kanisa! Anania alidhani kuwa kosa alilotenda halitatambulikana, hivyo aliamua kusema uongo mbele za mtumishi wa Mungu. Petro naye kwa njia ya ufunuo wa Roho Mtakatifu, anamwambia wazi Anania na safila mkewe kuwa hawakumwambia uongo mwanadamu bali Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni nafsi ndiyo maana anaweza kuambiwa uongo; nguvu haiwezi kuambiwa uongo.

ANAWEZA KUFANYIWA KUFURU:
“Kwa sababu hii nawaambia, kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kumkufuru Roho Mtakatifu hawatasamehewa” (Mathayo 12:31)
Huu nao ni uthibitisho mwingine unaoonyesha kuwa Roho Mtakatifu si nguvu bali ni nafsi iliyo hai. Kwa kuwa ni nafsi hai anaweza kutukanwa na kunenewa maneno ya kufuru na wale waliokwisha kupewa Nuru na kukionja kipawa cha mbinguni; wale waliofanywa washirika na Roho huyu na kulionja neno zuri la Mungu pamoja na kuzionja nguvu za zamani zijazo. Roho mtakatifu angelikuwa nguvu kama ilivyo nguvu ya umeme basi asingeliweza kunenewa maneno ya kufuru maana hakuna anayeweza kuikufuru nguvu.

ANAWEZA KUFANYIWA JEURI.
Pamoja na sababu hizi zinazomfanya Roho Mtakatifu kuwa nafsi halisi na hai neno linatuambia kuwa Roho Mtakatifu anaweza kufanyiwa jeuri na watoto wa Mungu. Hili hutokea pale watoto wa Mungu wanapokataa kwa kukusudia kuitii sauti ya Roho wa Mungu ndani yao na kuamua kuasi. Neno la Mungu katika waebrania 10:29 linatuambia kuwa;
“Kila afanyaye dhambi kwa kukusudia baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, anamfanyia jeuri Roho wa mema au Roho Mtakatifu”.

Kwa ujumla kuna mifano mingi ya kimaandiko inayothibitishwa kuwa Roho Mtakatifu ni nafsi hai, ila kwa hii michache nimeielezea ili ikusaidie kutafuta mingine inayofanana na hiyo.
MWISHO
Kwa leo somo letu linaishia hapa, usikose kufuatilia sehemu inayofuata ya somo hili. Kwa msaada zaidi tuwasiliane 0677 609056

SOMO: ROHO MTAKATIFU NA MAMBO YAKE (2)


Mwl: Furaha Amon

Utangulizi:
Watu wengi mno ndani ya makanisa wana kiu ya kupata ujazo wa Roho Mtakatifu, lakini bado kuna tatizo kubwa sana linalohusiana na kutomwelewa vizuri Roho Mtakatifu. Kwa kuwa kiu hii ni kubwa na tatizo la kutomwelewa Roho Mtakatifu ndani ya kanisa ni kubwa sana nimeona ni vema nitumie nafasi hii kutoa mchango kidogo wa kukusaidia kuelewa kwa kiasi habari za Roho Mtakatifu.
ROHO MTAKATIFU NI NANI?                                       
“Upepo huvuma uendako, na sauti yake wasikika, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho” (Yohana 3:8)
Tunapoangalia kwa lugha ya Kiyunani, tunaweza kuona kuwa kitu ambacho ni roho hufananishwa au huelezewa kwa mfano huu uliotangulia. Hapa tunajifunza kuwa, hakuna mtu anayeweza kuukamata au kuuona upepo kwa macho ya kibinadamu, bali anachoweza kuona ni kazi au matunda yaletwayo na upepo. Hali kadhalika hatuwezi kumwona Roho Mtakatifu kwa macho ya kibinadamu wala kumkamata, bali aliyempokea anaziona kazi zake waziwazi kabisa

ROHO MTAKATIFU HAKUUMBWA.
Roho Mtakatifu hakuumbwa, bali ni mojawapo katika Nafsi takatifu za Mungu. Kwa hiyo ni sahihi kusema kwamba Roho Mtakatifu pia ni Mungu. Kumbuka kuwa tunaposema Nafsi tatu za Mungu hatumaanishi kuwa kuna Miungu watatu, bali ni Mungu mmoja katika nafsi tatu, yaani Baba Mwana na Roho Mtakatifu.
Ni vema pia tufahamu kuwa ufalme wa Mungu ni ufalme wa siri, kwa hiyo hata kumfahamu Mungu kwa ufasaha na utatu wake ni kitu kisichowezekana kwa akili za kibinadamu zilizoghoshiwa na dhambi, ni lazima tukubali kwamba ni kwa neema ya Mungu tu. Kwa kawaida ufahamu huu unapatikana kwa Yule tu aliyeokoka kwa kuzaliwa mara ya pili, na kumpokea Roho Mtakatifu aliye mwalimu wa kweli. Neno la Mungu linasema;-
“Hakuna ajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake na vivyo hivyo mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu” 1 Wakorinto 2:11
Kuna sehemu nyingi sana kwenye Biblia zinazoelezea nafsi hizi za Mungu na mfano mzuri tunaupata katika injili ya Luka wakati wa kubatizwa kwa Yesu Kristo;-
“Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye Kristo amebatizwa , naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, wewe ndiwe mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe” (Luka 3: 21-22)
Kwa maelezo ya mistari hii, tunaziona nafsi zote tatu za Mungu zikijidhihirisha waziwazi kwa wakati mmoja yaani;-
1.  MWANA alikuwa majini akibatizwa
2.  ROHO MTAKATIFU akamshukia kwa mfano wa hua.
3. BABA akatoa sauti kutoka mbinguni. “Wewe ndiwe mwanangu, mpendwa; nimependezwa nawe”
Kwa kuwa Roho Mtakatifu ni nafsi hai ya Mungu, hapana shaka kwamba naye pia ni Mungu na ana sifa ya kuwa Alfa na Omega kwa maana ya kwamba hana mwanzo wala mwisho na ni makosa kuamini kwamba Roho Mtakatifu ameumbwa na Mungu.

Kwa leo somo letu linaishia hapa, usikose kufuatilia sehemu inayofuata ya somo hili. Kwa msaada zaidi tuwasiliane 0677 609056

SOMO: ROHO MTAKATIFU NA MAMBO YAKE (1)


Mwl: Furaha Amon

Utangulizi:
Mwishoni mwa mwaka 1999 nilipata nafasi ya kwenda kuhubiri katika kanisa moja la Assemblies of God. 

Ni  umbali wa kama kilometa 78 kutoka katika mji ambao nilikuwa naishi kwa wakati huo. Kanisa hili lilikuwa na mtumishi Mchungaji ambaye tulikuwa tunafanya kazi wote serikalini lakini yeye baadae neema ilimzidi akaamua kuacha kazi na kuingia shambani kwa Bwana. 

Mtumishi huyu alikuwa ni kama baba yangu wa kiroho, kwa sababu ndiye niliokokea mikoni mwake na kiukweli ndiye aliyenilea kwa uangalizi wa karibu sana, tangu siku ile nilipokata shauri na kuamua kumfuata Bwana Yesu. Wakati huu Napata nafasi ya kwenda kuhubiri nilikuwa nakaribia miaka kumi kwenye maisha ya wokovu. Kwa kuwa ilikuwa ndio nasimama kwa mara kwanza kufanya huduma hiyo katika kanisa lake, ilibidi Mchungaji anitambulishe kwa washirika wake wapatao kama mia nne hivi kwa ibada ile ya asubuhi. 

Mchungaji aliwaeleza washirika wake jinsi alivyokutana na mimi na mwonekano wangu, aliwaambia kwamba mimi nilipohamishiwa kikazi sehemu aliyokuwepo tulikuja vijana kama sita, kati yetu mimi ndio nilikuwa naonekana mtata zaidi. Na kwa hiyo hawakuwa na mpango kabisa wa kunipa habari njema za wokovu. Na kwa kweli nakumbuka nilikuwa jeuri sana, na wasingeweza kunikabili wakati huo bila kukorofishana, na ilikuwa hatari sana kukorofishana na mimi wakati huo kwa sababu naweza kukuvizia na kukujeruhi japo kisirisiri. Na hii hali hata baada ya kuokoka ilikuwa bado ipoipo kidogo. Ilikuja kwisha baada ya kuoa, na kwa sababu mke wangu ni mtu mwenye huzuni nyingi sana, hapendi kabisa nifanye ukorofi wa aina yeyote ile, hivyo kila ninapotaka kufanya maamuzi fulani sijiangalii mwenyewe binafsi kama ilivyokuwa zamani, pamoja na kumuangalia Mungu lakini huwa namfikiria sana mke wangu asije akahuzunika. Lakini pamoja na familia yangu kwa ujumla.
Mchungaji mwenyeji wangu aliwaambia washirika wake kwamba, katika kundi letu walimlenga kijana mmoja wa kichaga ambaye alikuwa anaonekana anamwelekeo wa kuokoka mapema ingawa hakuweza kusimama katika wokovu baadae alianguka kiroho, na mwisho alifariki dunia bila kupata neema ya wokovu. 

Kwa sababu tulikuwa tunakaa chumba kimoja na huyo ndugu, nilikuwa naona juhudi zao za kumfuatilia mara kwa mara. Na mimi nakumbuka siku moja nilitafakari sana kuhusu uwepo wa Mungu. Nikajisemea moyoni kwamba, ngoja nifanye utafiti kujua kama kweli Mungu yupo au hayupo, ingawa nimelelewa katika familia ya kikristo lakini mwenyewe binafsi nilikuwa sina uhakika kama kweli Mungu yupo. Niliamini zaidi katika sayansi kwamba uhai ulijitokeza wenyewe kwa njia ya mageuzi.
 



Katika utafiti wangu  nikijua kwamba Mungu hayuko, nitachagua maisha ya kuishi kwa bahati nikakuta yupo. Kwa hiyo nikaona utafiti huu niufanye kwa makanisa yenye msimamo wa imani kali, na walokole wa kipentekoste nikaona ndio watakaonifaa. Kwa hiyo bila kuhubiriwa na mtu yeyote, nilimfuata huyo Mchungaji, na kumwambia mimi nataka kuokoka!. Mchungaji anawaambia washirika wake kwamba wao walishangaa na pia hawakuamini, wakajua shetani anataka kunitumia kuvuruga mpango wao kumpata mtu waliyemlenga. Kwa hiyo wakakubaliana kwamba nikikubali kuongozwa sala ya toba tu wataunganisha na ubatizo wa Roho Mtakatifu, bila hata kubatizwa kwa maji mengi, hata kama sijui habari za Roho Mtakatifu, mwenyewe anasema walitaka Roho Mtakatifu mwenyewe anibane kisawasawa. Na kweli siku iliyofuata walinipeleka katika kakanisa fulani kadogo kana washirika kama ishirini hivi. Wanaendesha  ibada zao katika shule moja ya msingi karibu ya sehemu yetu ya kazi. Na kweli baada ya kuongozwa sala ya toba alinipeleka sehemu moja yenye majengo ya ghorofa ambayo hajaisha ujenzi wake yametelekezwa bila kukamilika. Akanipandisha kwenye ghorofa ya pili, tukiwa watu wawili tu. Akaniambia piga magoti, akanielekeza maneno ya kusema, harafu akawa ananilazimisha niyaseme maneno hayo kwa kasi sana ya kujichanganya na nilipokuwa nikikosea ndio akawa ananiambia hiyo ndio lugha anayoitaka. Na kunihimiza endelea hivyohivyo kuongea vitu visivyoeleweka. Kwa kweli sababu nilikuwa katika utafiti sikufungua moyo wangu kabisa. Tulikaa eneo hilo la upweke karibu masaa matatu. Huku yeye anaendelea na maombi huku akinisikilizia mimi, nikiongea lugha ambavyo akili yangu haina matunda kabisa ni kama najifanyisha fanyisha tu. Kwa kweli maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga. 

Ilibidi tu nifanye kujisemeshasemesha maneno yale huku magoti yakiniuma kama mtu aliyepewa adhabu ya kijeshi ya kutembelea magoti. Baadae aliniambia tayari nimepokea ujazo wa Roho Mtakatifu. Kwa kweli mpaka wakati huo mimi sikuwa nimeona badiliko lolote zaidi ya kujihisi kama mtahiniwa aliyefanya mtihani ambao hajafundishwa na hana uhakika wa majibu yake, nilikaa nikisubiri majibu ambayo sina uhakika nayo. Kila siku namshukuru sana Mungu kwa ajili ya ndugu zangu hawa. Japo wao walikuwa na vyeo vikubwa kazini, lakini walishuka chini na kunitumikia, kuhakikisha kwamba ninasimama. Nakumbuka ni kama walikuwa wanafanya zamu. Kuhakikisha sipati nafasi ya kushirikiana na marafiki zangu wa zamani. Kwa hiyo walihakikisha ninafuatana nao kwa kubadilisha kwenda kwenye huduma mbalimbali walikokuwa wanaitwa kuhudumu. Kwa kweli walikuwa na uwezo na nguvu kubwa sana kiroho, kiasi kwamba waliweza kuamuru mvua isimame ili wafanye kitu fulani na mvua ilitii. Hayo mambo yalikuwa yakifanyika mbele ya macho yangu. Wakikwambia nenda nyumbani kuna hiki na kile, ukienda unakuta kama vile walivyokwambia. Kwa ujumla hawa marafiki zangu walinifaa sana. Sasa pamoja na kunihakikishia kuwa nimepokea ujazo wa Roho Mtakatifu, ilichukua siku kama tatu hivi, nikiwa kwenye maombi yangu ya kubangaiza ghafla nikaona ulimi umekuwa mwepesi ninaongea lugha ambayo siielewi na nimeingiwa na hali fulani ya furaha na amani na kutamani kuendelea kuomba. Ndio nikaanza kujua kwamba huyo ndio Roho Mtakatifu ambaye Mungu alituahidi kwamba tutampokea. Kama ilivyokuwa kwangu mimi ndivyo ilivyo hata sasa. Watu wengi mno ndani ya makanisa wana kiu ya kupata ujazo wa Roho Mtakatifu, lakini bado kuna tatizo kubwa sana linalohusiana na kutomwelewa vizuri Roho Mtakatifu. Kwa kuwa kiu hii ni kubwa na tatizo la kutomwelewa Roho Mtakatifu ndani ya kanisa ni kubwa sana nimeona ni vema nitumie nafasi hii kutoa mchango kidogo wa kukusaidia kuelewa kwa kiasi habari za Roho Mtakatifu.
Kwa kupitia mafundisho haya, wale wenye kiu ya kumpokea Roho Mtakatifu na nguvu zake wataweza kupokea; na kwa wale wasio na kiu ya kupokea, kutokana na kutomwelewa Roho Mtakatifu na faida zake  wataweza kuumbiwa kiu na hatimaye kupokea. Ni matumaini yangu kuwa mafundisho haya, yatayaondoa kwa kiasi kikubwa matatizo yaliyopo ndani ya kanisa yanayohusiana na huduma hii ya Roho Mtakatifu.



Kwa leo naishia hapa, usikose kufuatilia somo hili katika sehemu inayofuata. Mungu akubariki sana, kwa maoni na ushauri tuwasiliane kwa namba 0677 609056





Jumatatu, 30 Januari 2017

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU (4)


Mwl Furaha Amon

Utangulizi;
Katika sehemu ya tatu tumeangalia kwa uchache kuhusu msingi wa ndoa, na maelekezo aliyoyatoa Mungu kupitia kwa mtumishi wake Musa, lakini pia maagizo ya Yesu kuhusu ndoa, sasa tuendelee na sehemu hii ambayo zaidi itahusu sheria za Mungu kuandikwa moyoni.
Sheria Za Mungu Kuandikwa Mioyoni
Hapa ni lazima niseme kwamba hata wale ambao hawajawahi kusoma sura ya pili ya kitabu cha Mwanzo kinachozungumzia kuhusu uumbaji wa Mungu, wanajua wazi ndani yao kwamba kuachana na kupeana talaka ni kosa, kwa sababu agano la maisha ya ndoa ni kawaida katika tamaduni nyingi tu za kipagani, ambapo hakuna maarifa yoyote ya Biblia. Kama alivyoandika Paulo katika barua yake kwa Warumi:
Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao wakionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao yenyewe kwa yenyewe, yakiwashtaki au kuwatetea (Warumi 2:14-15).
Ukweli ni kwamba, hata kama tutakuwa na mafundisho mazuri kiasi gani kuhusu uimara wa ndoa, bado tunahitaji taratibu za Mungu na maadili yenye hofu ya Mungu yawe yameandikwa katika moyo wa kila mwanandoa. Kanuni  hiyo ya maadili na hofu ya Mungu inayozungumza kupitia katika dhamiri zetu ndiyo njia pekee ambayo Mungu ametoa kwa yeyote, tangu Adamu mpaka wakati wa Yesu.
Yeyote anayefikiri kutoa talaka atagundua kwamba kuna dhamiri ya kushughulika nayo. Na njia ya pekee ya kuishinda dhamiri yake ni kutafuta haki nzuri kwa ajili ya talaka. Akiendelea na talaka bila ya haki nzuri, dhamiri yake itamshtaki, hata kama atajaribu kuigandamiza.
Kwa kadiri tunavyofahamu, tangu Adamu mpaka wakati wa kutolewa Torati ya Musa kwa Waisraeli mwaka wa 1440 KK, sheria ya dhamiri ndiyo ufunuo pekee ambao Mungu alitoa kwa yeyote kwa vizazi 27 hivi – hata kwa Waisraeli – kuhusiana na talaka na kuoa tena. Na Mungu alihesabu kwamba hiyo inatosha. (Kumbuka tu kwamba Musa hakuandika habari za uumbaji katika Mwanzo 2 mpaka wakati wa Kutoka Misri.) Basi, ni halali kabisa kufikiri kwamba katika kipindi cha vizazi hivyo 27 kabla ya Torati ya Musa – ambapo ni pamoja na kipindi cha gharika ya Nuhu – kiasi fulani cha ndoa katika zile milioni nyingi za miaka mia nyingi zilimalizika kwa kuachana.
Pia inaonekana ni sawa kusema kwamba, Mungu asiyebadilika, alikuwa tayari kuwasamehe wale waliopatikana na hatia ya talaka kama walitubu na kuacha dhambi yao. Tuna hakika kwamba watu walikuwa wanaokoka au kutangazwa kuwa wenye haki na Mungu kabla ya Torati ya Musa kutolewa, kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu kwa imani yake (ona Warumi 4:1-12). Kama watu waliweza kutangazwa kuwa wenye haki kwa njia ya imani yao – tokea Adamu hadi kwa Musa – maana yake ni kwamba wangeweza kusamehewa chochote, pamoja na dhambi ya talaka. Basi, tunapoanza kuchunguza swala la talaka na kuoa tena baada ya talaka, kuna swali hapa: Je, watu waliopatikana na dhambi katika talaka zao kabla ya Torati ya Musa, waliosamehewa na Mungu, waliweza kuhukumiwa na dhamiri zao na kupata hatia kama wangeoa tena? (Maana haikuwepo sheria iliyoandikwa.) Ni swali la kufikiri.
Vipi kuhusu waathirika wa talaka ambao hawakuwa na dhambi – yaani, walioachwa kwa kosa lisilokuwa lao, bali kwa sababu ya wenzi wao wenye ubinafsi? Je, dhamiri zao zingewazuia kuoa tena? Nadhani si hivyo. Kama mwanamume alimwacha mke wake kwa sababu ya mwanamke mwingine, nini kingemwongoza huyo mwanamke aliyeachwa kufikia uamuzi kwamba hana haki ya kuolewa tena? Maana, aliachwa, lakini si kosa lake.

       
       MWISHO WA SEHEMU YA NNE

Mungu akubariki sana kwa kufuatilia sehemu ya nne ya somo hili. Mungu akupe neema tena tukutane katika sehemu ya tano.

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU (3)


Mwl Furaha Amon


Baada ya kuweka msingi katika sehemu ya kwanza na ya pili ya somo hili, nafikiri sasa tunaweza sasa kuendelea kuangalia zaidi mambo ambayo Mungu amesema kuhusu watu kuachana kwa talaka na kuoa tena. Kwa kuwa maneno mengi yenye kuleta ukakasi kuhusu kupeana talaka, na kuoa tena ni yale ambayo Yesu aliwaambia Waisraeli, itatusiadia kwanza kuona Mungu alichosema miaka mia nyingi kabla, juu ya jambo hilo hilo kwa Waisraeli wa zamani. Tukikuta kwamba alichosema Mungu kwa njia ya Musa na alichosema Mungu kwa njia ya Yesu vinapingana, basi tutajua ya kwamba sheria ya Mungu ilibadilika au kwamba sisi ndio tumetafsiri vibaya tofauti kitu fulani kilichosemwa na Musa au na Yesu.
Basi, tuanze kwa kutazama yale ambayo Mungu alifunua hapo mwanzo kuhusu talaka na kuoa tena baada ya talaka.
Tayari nimekwisha taja Maandiko ya Mwanzo 2 ambayo kulingana na mafundisho ya Yesu, yana umuhimu kwa somo letu hili linalohusu mambo ya talaka. Hebu sasa tuyaone moja kwa moja kutoka Mwanzo kwenyewe.
Na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, ‘Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja (mwanzo 2:22-24).
Basi huo ndiyo mwanzo wa ndoa. Mungu alimfanya mwanamke wa kwanza kutoka kwa mwanamume wa kwanza, na kwa ajili ya mwanamume wa kwanza, kisha Yeye Mwenyewe binafsi akamleta kwa Adamu.

Yesu anaeleza hilo hivi, “Mungu … aliwaunganisha [pamoja]” (Mathayo 19:6,). Hii ndoa ya kwanza iliyopangwa na Mungu inatoa mfano kwa ajili ya ndoa zingine zote zilizofuata. Katika maeneo yote ya maisha ya mwanadamu, Mungu yuko makini sana Mungu huumba wanawake wa kutosha wanaume, Naye huwaumba ili kila mmoja avutiwe na mwenzake. Ndio maana tunasisitiza sana kwamba kunahitajika maombi na utulivu sana katika kuchagua mwenza wa kuishi naye. Tunaweza kusema kwamba Mungu bado anapanga ndoa za watu kwa hali ya juu sana (japo siku hizi watu wanaangalia zaidi mambo ya mwili, pamoja na mali.) lakini pia kuna wanaoanza mambo ya mapenzi kabla ya kuona na hivyo kuzuwia kabisa kupata msaada wa Mungu kama wameingia mahali sahihi au wameingilia ubavu wa mtu mwingine.

Kwa hiyo mtu anapokuwa kwenye ndoa nab ado anachepuka kwa kuwa wapenzi wengi zaidi, kuliko ilivyokuwa kwa Adamu na Hawa). Basi, kama Yesu alivyosema, mwanadamu yeyote asitenganishe wale ambao Mungu amewaunganisha. Halikuwa kusudi la Mungu kwamba wale wana ndoa wa kwanza waishi maisha binafsi kila mmoja, bali kwamba wapate baraka katika kuishi pamoja kwa hali ya kutegemeana. Kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu katika eneo hili ni dhambi. Basi, kutoka katika sura ya pili ya Biblia, ukweli ni kwamba talaka haikuwa kusudi la Mungu kwa ndoa yoyote ile. Nakumbuka wakati fulani mchungaji wangu alimualika muhubiri mmoja kutoka Malawi ambaye walikutana naye ufaransa. Muhubiri huyu alitoa ushuhuda ambao unaweza kusaidia katika somo letu. Alisema kwamba yeye alikuwa anafanya kazi benki na akatokea kumpenda msichana mmoja ambaye alikuwa ameokoka, kwa sheria ambazo sio rasmi, vijana waliookoka huwa hawaoani na watu wasiookoka (watu wa mataifa) kwa sababu hiyo huyu mtumishi ilibidi ajivalishe ngozi ya kondoo na kuingia kanisani na kujifanya ameokoka. Na kwa sababu ya nafasi yake katika jamii, hata kanisani alianza kupewa nafasi za uongozi na baada ya muda akamtokea yule binti na kumtamkia kwamba anataka kumuoa. Binti bila hata ya kuomba akakubali. Nafikiri aliangalia zaidi hali ya kimwili na sio kiroho. Baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria, hatimaye walifunga harusi kubwa sana. 
Yule muhubiri anasema zilichukua wiki mbili tu kuanza kuonyesha hali yake halisi, anasema kwanza alianza kurudi nyumbani akiwa amelewa. Na kuanza kumfanyia fujo mke wake na kumfukuza, baadae akaanza kuleta makreti ya bia, anakuja na marafiki zake halafu anamlazimisha mke wake ndio awe anawafungulia hizo bia kama madada wauza bar. Yule mwanamke akikataa, anakula kichapo cha haja. 
Akijaribu kukimbilia kwa wazazi wake wanamrudisha, akienda kanisani anaona kila mtu kamchoka maana kila siku kesi haziishi. Akaishi maisha ya shida sana kila siku anapigwa na kutukanwa, kisha analala nje ya nyumba yao kwenye jengo ambalo halijamalizwa kujengwa. Lakini sifa kubwa ya huyu mwanamke alikuwa anamwamini sana Mungu, na kuendelea kuomba kwa ajili ya mume wake. Yule mtumishi anasema siku moja akiwa na pikipiki kubwa. Wakati anarudi nyumbani akiwa ameonja kidogo pombe, alipata ajali mbaya ya pikipiki. Alitunyesha kichwa chake kilikuwa kama kimesukwa. Anasema kichwa kilichanikachanika, na alipoteza fahamu kwa zaidi ya mwezi. Anasema wakati hana fahamu Mungu alikuwa anamuonyesha mambo yote mabaya aliyokuwa akimfanyia mke wake. Anasema siku anapata fahamu anamuona mke wake ameinamia miguu yake akiendelea kumuombea kwa machozi, baadae akagundua kuwa pamoja na ubaya wote ule lakini mke wake alionyesha upendo wa hali ya juu sana. Na baada ya kupona aliacha na kazi, akaamua kumtumikia Mungu kwa ujumla. Kwa huyu msichana imekuwa ni bahati kwamba Mungu mwenyewe aliamua kumsaidia kutokana na uvumilivu wake.

               MWISHO WA SOMO LA TATU


Tutaendelea na sehemu ya nne ya somo hili. Kwa maoni na msaada zaidi wasiliana nami kwa mobile namba 0677 609056