Jumatatu, 30 Januari 2017

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU (4)


Mwl Furaha Amon

Utangulizi;
Katika sehemu ya tatu tumeangalia kwa uchache kuhusu msingi wa ndoa, na maelekezo aliyoyatoa Mungu kupitia kwa mtumishi wake Musa, lakini pia maagizo ya Yesu kuhusu ndoa, sasa tuendelee na sehemu hii ambayo zaidi itahusu sheria za Mungu kuandikwa moyoni.
Sheria Za Mungu Kuandikwa Mioyoni
Hapa ni lazima niseme kwamba hata wale ambao hawajawahi kusoma sura ya pili ya kitabu cha Mwanzo kinachozungumzia kuhusu uumbaji wa Mungu, wanajua wazi ndani yao kwamba kuachana na kupeana talaka ni kosa, kwa sababu agano la maisha ya ndoa ni kawaida katika tamaduni nyingi tu za kipagani, ambapo hakuna maarifa yoyote ya Biblia. Kama alivyoandika Paulo katika barua yake kwa Warumi:
Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao wakionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao yenyewe kwa yenyewe, yakiwashtaki au kuwatetea (Warumi 2:14-15).
Ukweli ni kwamba, hata kama tutakuwa na mafundisho mazuri kiasi gani kuhusu uimara wa ndoa, bado tunahitaji taratibu za Mungu na maadili yenye hofu ya Mungu yawe yameandikwa katika moyo wa kila mwanandoa. Kanuni  hiyo ya maadili na hofu ya Mungu inayozungumza kupitia katika dhamiri zetu ndiyo njia pekee ambayo Mungu ametoa kwa yeyote, tangu Adamu mpaka wakati wa Yesu.
Yeyote anayefikiri kutoa talaka atagundua kwamba kuna dhamiri ya kushughulika nayo. Na njia ya pekee ya kuishinda dhamiri yake ni kutafuta haki nzuri kwa ajili ya talaka. Akiendelea na talaka bila ya haki nzuri, dhamiri yake itamshtaki, hata kama atajaribu kuigandamiza.
Kwa kadiri tunavyofahamu, tangu Adamu mpaka wakati wa kutolewa Torati ya Musa kwa Waisraeli mwaka wa 1440 KK, sheria ya dhamiri ndiyo ufunuo pekee ambao Mungu alitoa kwa yeyote kwa vizazi 27 hivi – hata kwa Waisraeli – kuhusiana na talaka na kuoa tena. Na Mungu alihesabu kwamba hiyo inatosha. (Kumbuka tu kwamba Musa hakuandika habari za uumbaji katika Mwanzo 2 mpaka wakati wa Kutoka Misri.) Basi, ni halali kabisa kufikiri kwamba katika kipindi cha vizazi hivyo 27 kabla ya Torati ya Musa – ambapo ni pamoja na kipindi cha gharika ya Nuhu – kiasi fulani cha ndoa katika zile milioni nyingi za miaka mia nyingi zilimalizika kwa kuachana.
Pia inaonekana ni sawa kusema kwamba, Mungu asiyebadilika, alikuwa tayari kuwasamehe wale waliopatikana na hatia ya talaka kama walitubu na kuacha dhambi yao. Tuna hakika kwamba watu walikuwa wanaokoka au kutangazwa kuwa wenye haki na Mungu kabla ya Torati ya Musa kutolewa, kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu kwa imani yake (ona Warumi 4:1-12). Kama watu waliweza kutangazwa kuwa wenye haki kwa njia ya imani yao – tokea Adamu hadi kwa Musa – maana yake ni kwamba wangeweza kusamehewa chochote, pamoja na dhambi ya talaka. Basi, tunapoanza kuchunguza swala la talaka na kuoa tena baada ya talaka, kuna swali hapa: Je, watu waliopatikana na dhambi katika talaka zao kabla ya Torati ya Musa, waliosamehewa na Mungu, waliweza kuhukumiwa na dhamiri zao na kupata hatia kama wangeoa tena? (Maana haikuwepo sheria iliyoandikwa.) Ni swali la kufikiri.
Vipi kuhusu waathirika wa talaka ambao hawakuwa na dhambi – yaani, walioachwa kwa kosa lisilokuwa lao, bali kwa sababu ya wenzi wao wenye ubinafsi? Je, dhamiri zao zingewazuia kuoa tena? Nadhani si hivyo. Kama mwanamume alimwacha mke wake kwa sababu ya mwanamke mwingine, nini kingemwongoza huyo mwanamke aliyeachwa kufikia uamuzi kwamba hana haki ya kuolewa tena? Maana, aliachwa, lakini si kosa lake.

       
       MWISHO WA SEHEMU YA NNE

Mungu akubariki sana kwa kufuatilia sehemu ya nne ya somo hili. Mungu akupe neema tena tukutane katika sehemu ya tano.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni