LUGHA
Lugha ni kitu ambacho kinaweza kuwatambulisha watu
na aina ya watu kulingana na kundi wanaloliwakilisha. Kwa maana hiyo unaweza
kumtambua mtu na kundi lake kutokana na lugha anayoitumia.
Kuna lugha wanayoitumia watu wa dunia ambayo
inawafanya wafanikiwe katika mambo ya dunia. Hali kadhalika tukiokoka tunapata
lugha nyingine yaani ipo lugha ambayo ni tofauti na ya dunia ambayo inatufanya
tufanikiwe katika mambo ya kiroho.
Ukiingia na lugha za dunia ndani ya wokovu huwezi
kupata mpenyo katika mambo ya kiroho. Hii ni kwa sababu ndiyo inatambulisha
watu na mfumo wao wa maisha.
Lugha inakuwezesha kutambua aina ya mtu unayeongea
naye, lugha au maneno ya mtu hutengeneza taswira fulani ya maisha ambayo
huumbika na hatimaye huja kutokea kweli.
Watu wengi hapa duniani wanaishi maisha ambayo
waliyafikiria na kuyasema kabla hayajakuwa dhahiri. Unaposema sana juu ya jambo
fulani, hatimaye jambo hilo huumbika na hatimaye hutokea hata kama hukulitaka.
Nguvu ya roho mtakatifu na roho chafu hutegemea
sana mambo matatu ambayo ni;-
1. Neno
2. Imani
3. Ukiri
Tukianza na neno, tunajifunza kwamba neno ni kama
mwongozo wa jambo au ni kama katiba, ambayo ndani yake kuna maelekezo ya haki
yako na wajibu wako kwa unayehusiana naye.
Kama vile ambavyo Mungu hutumia kitabu chake Biblia
lakini pia hata shetani ana vitabu vyake anavyotumia ingawa pia shetani anaijua
vizuri sana Biblia na haki za mtu aliyeokoka.
Katika matendo 19:18 – 20 tunaona habari kwamba
kuna watu waliokuwa wanatumia vitabu kwa uganga wakavikusanya na kuvichoma.
IMANI.
Imani ni kuwa na uhakika wa jambo unalolitarajia,
na katika mambo ya kiroho imani ni kitu cha lazima sana, hata wachawi hutumia
imani ya kiwango cha juu sana katika kufanya kazi zao za kichawi. Hebu fikiria
mwenyewe mtu anakaa kwenye ungo na anafanya mambo yake na hatimaye ungo unapaa
na kuelekea anakotaka, jambo hili huwezi kulifanya kama una imani ya
kubahatisha.
UKIRI.
Ukiri au usemi ni wa lazima sana katika mambo ya
kiroho, unaweza kuwa una neno, na pia una imani ya kutosha, lakini bila kusema
hakuna kinachoweza kufanyika. Maneno tunayokiri yana nguvu kubwa sana na
ukiitumia vizuri ni lazima ushinde.
Wakati mfalme Daudi
anapambana na Goliathi, pamoja na Goliati kumuona Daudi kuwa ni kijana
mdogo mwenye uso mzuri, lakini Goliati kuna maneno ambayo alimsemea kwamba
angemuua na kuwapa ndege nyama yake.
Daudi naye wakati anamwendea Goliati naye alisema maneno
ambayo yalikuwa mengi kuliko aliyoyasema Goliati, na aliahidi kukata kichwa
chake na kwa upanga ijapokuwa hakuwa na upanga bali alikuwa na kombeo tu,
lakini maneno yake yalitimia na akamkata kichwa Goliati kwa upanga wake
mwenyewe.
Kila mara kabla ya ugomvi kutokea mara nyingi
huanza na maneno, na mwenye maneno mengi mara nyingi hushinda , angalia hata
kwa mabondia au wanamieleka.
Wakati wa vita vya kagera pia kulikuwa na maneno
kabla ya vita kuanza. Idi Amin dada wa Rais wa Uganda wakati ule alisema
atahakikisha chai anakunywa Mwanza, chakula cha mchana Dodoma na chakula cha
usiku Dar es salaam. Amin hakufafanua atawezaje kufanya mambo hayo bila kutueleza
ana uwezo kiasi gani.
Lakini kwa upande wa Tanzania Rais wa wakati huo
mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiongea na wazee wa Dar es salaam katika
ukumbi wa Karimjee alisema maneno machache kwamba sasa tunampiga Amin, uwezo wa
kumpiga tunao, nia ya kumpiga tunayo, na sababu za kumpiga tunazo. Tunataka dunia ituelewe hivyo.
Na matokeo yake idi amini alipigwa na utawala wake
kuangushwa.
Kwa sababu hiyo lugha zetu na za watu wa dunia ni
lazima zitofautiane ili tuweze kufanikiwa katika mambo ya Mungu.
Ni lazima tujitofautishe na watu wa dunia
wanavyokiri kuhusu uchumi, maisha, biashara, nk.
Hii ni kwa sababu lugha ndiyo inayotumika kusukuma
nguvu ya Mungu, ni lazima tujue Biblia inatagiza kufanya nini kwa mfano
tunapokuwa katika hali ya hasira, tukiwa na majirani, kazini, nyumbani kwenye
familia n.k.
Biblia natuambia katika kitabu cha Mwanzo 11: 1 – 9
kwamba nchi yote ilikuwa na lugha moja na watu hawakutaka kutawanyika.
Waliamua kujenga mnara mrefu ufike mbinguni ili
wasitawanyike. Walijenga mnara huu kwa kutumia lami na matofali, na Mungu
alijua kwamba watafanikiwa kwa sababu ya hamasa waliyokuwa nayo. Kwa kawaida
tulitegemea kwamba Mungu angewanyanganya lami na matofali, lakini hapana Mungu
aliamua kuchukua lugha yao nah ii iliwafanya wasambaratike.
Nguvu ya watu hao haikuwa katika katika lami na
matofali bali ilikuwa katika lugha na katika usemi, na Mungu alijua hakika
kwamba wangefanikiwa. Kwa sababu ukiri wao ulikuwa katika usemi.
Angewanyanganya lami na matofali wangeweza
kushauliana cha kufanya ili ujenzi wa mnara uendelee.
Lugha ndiyo inaymtambulisha mtu ni nani na ni wa
kundi gani, kwa kutumia lugha unaweza kumjua kahaba, msomi, ameokoka n.k. kwa
sababu lugha ndiyo inayomtambulisha mtu na kundi lake, lugha ndiyo
inayomtambulisha mtu
kama ni wa kufa au ni wa kuishi.
Katika kitabu cha Waamuzi 12: 5 – 6 kuna habari ya
vita kati ya Wagileadi na Waefraimu na kuna askari aliyejichanganya na
walimgundua kutokana na usemi, alishindwa kutamka neno shibolethi akasema
siboleth.
Wakati wa matatizo ya Ayubu katika kitabu cha
(Ayubu 2:9-10) Ayubu alimwambia mke wake ameongea kama wanawake wapumbavu, kumbe wanawake wapumbavu
nao wana lugha zao.
Katika injili ya Mathayo 26 tunasoma habari za
Petro kwamba lugha yake ilimtambulisha kwamba yuko na Yesu.
Ukitaka kumshinda shetani ni lazima kwanza
ubadilishe lugha unayotumia wakati unapoongea naye, huwezi kumshinda shetani
kwa kutumia lugha yake.
Mithali 6: unakamatwa na maneno yako mwenyewe,
katika kitabu cha Waamuzi 15:7 Samsoni alijiapiza kwa sauti kwamba atawapiga
Wafilisti halafu atakoma.
Ni vizuri kwa waliookoka wakajifunza kwamba
wasikubali kuwaacha watu wanawaongelesha mambo ya ajabu na wakakaa kimya
Mzee anapomwambia mtoto mchumba anamfunika katika
ulimwengu wa roho .
MUNGU AKUBARIKI KWA KUFUATILIA SOMO HILI.
Furaha Amon
- Tanga Mob: 0713 461593