Utangulizi;-
Somo langu leo linaanza
kama swali, lakini nafikiri nitalimalizia kama ushauri usio na masharti ya kukulazimisha
ukubali ushauri wangu. Siku moja nimekwenda mahali fulani kwenye kanisa fulani,
nikakuta mtumishi mmoja yuko na mtu ambaye amepagawa na pepo wachafu. Lakini kilichoniogopesha ni vile kuona yule mtumishi
ameshika daftari na kalamu! Halafu anamuuliza yule pepo ambaye amempagaa yule
mtu! wewe ni nani? Pepo anajibu mimi maimuna! Umetumwa na nani? Nimetumwa na
mama yake mdogo. Mko wangapi? n.k. baada ya majibizano hayo na yule mgonjwa
kurudi kwenye fahamu zake anaanza kumsomea yale majibizano, kama alivyoelekezwa
na pepo, kwamba katumwa na nani na wako wangapi n.k. Sasa mambo kama haya mimi
nikiita ni ya kipumbavu na yanafanywa na mawakala wa shetani ndani ya kanisa,
watu wengine wanasema nakosea. Maana mimi sioni tofauti kati ya mpiga ramli na
hawa watu. Kwa nini nione haya kumfananisha mtumishi wa aina hii na mganga wa
kienyeji. Na hali ndio kwa sasa imeshamiri katika makanisa ambayo tunayaita ya
kiroho, kwa kweli ni janga kwa kanisa
UMUHIMU WA KUFUATA USHAURI WA MUNGU.
Mara nyingi ninapopata
nafasi maalumu ya kuhubiri au kufundisha masomo ya Biblia au semina. Huwa namuomba Mungu kwa unyenyekevu mkubwa sana juu
ya hitaji la wale watu ambao ninakwenda kuwahudumia, katika ufahamu wangu
ninakuwa na maelfu ya masomo ambayo ninatamani kuyafundisha. Lakini mara nyingi
huwa ninamuomba Mungu anisaidie kunipa kile anachotaka yeye watu wajifunze.
Ninakumbuka siku moja nilikuwa nnaongea na rafiki yangu mmoja ambaye ni Askofu
kuhusu umuhimu wa tabia hii, akaniunga mkono na akanishuhudia yeye mwenyewe
jinsi Mungu alivyomuepusha na mtego mbaya sana ambao shetani alikuwa ameutega
katika huduma yake.
Anasema Mungu alimwelekeza kwenye semina fulani kwamba siku
ya kwanza akipanda madhabahuni asifundishe kitu chochote bali aongoze maombi
tu. Alijaribu kushindana na maelekezo hayo lakini hatimaye aliamua kutii sauti
ya Mungu, na ndivyo alivyofanya.
Na baadae mwisho wa hiyo semina ndio akagundua
ni kwa nini Mungu alimshauri afanye hivyo. Anasema hilo kanisa wakati huo
alikuwa ameitwa kwa mara ya pili, kwa sababu alipokwenda kwa mara ya kwanza
alifanya semina ambayo ilifanikiwa sana. Mungu alifanya mambo makubwa sana. Karibu
wiki yote ile makanisa mengine ilibidi yafungwe kwa muda kwa sababu washirika
wao walikimbilia kwenda kupata huduma katika semina hiyo ambayo Mungu alishuka
kwa nguvu sana. Mpaka semina hiyo inaisha watu walitamani siku zigande, Kwa
hiyo Mchungaji wa kanisa hilo akawa amejipanga kwa ajili ya semina nyingine
ambayo alitaka iwe kubwa zaidi kuliko ile iliyopita. Kwa hiyo maandalizi
yakafanyika na hatimaye tarehe ikapangwa na mhubiri akataarifiwa. Siku chache baada ya matangazo ya semina na mialiko
kuanza kusambazwa kikatokea kituko!, Mwanakwaya mmoja wakiwa katika mazoezi ya
kujiandaa na semina akaangushwa na mapepo! Na wale wenye ujuzi wa kukemea na
kuuliza maswali wakaanza kazi. Lile pepo likajibu kwamba mimi niliwekwa humu na
huyo mtumishi anayekuja kufundisha!.
Aliniweka alipokuja kufundisha kwa mara ya
kwanza. Habari ile ikachukuliwa kama ilivyo na viongozi wa kwaya huku ikiwa
imevuviwa na roho ya pepo, ikapelekwa kwa viongozi wengine wa kanisa, na
hatimaye ikafika kwa Mchungaji kiongozi ikiwa na maelekezo ya kipepo na
kupelekwa kama ombi la kufuta hiyo semina. Wakataka huyo askofu kabla hajafika atumiwe
ujumbe haraka sana kwamba semina imeahirishwa. Mchungaji wao alikuwa vizuri
zaidi kiroho, na mtu mwenye msimamo, akasema kama mtu angetoa unabii kupitia
Roho Mtakatifu, bado Biblia inaturuhusu kuupima huo unabii. Akaona haiwezekani
mapepo kumuelekeza jinsi ya kufanya kazi
ya Mungu.
Pamoja na msukumo mkubwa uliokuwepo kutoka kwa wazee na viongozi
wengine wa kanisa lile, Mchungaji yule akakataa kabisa kubadilisha kitu
chochote akawaambia mimi pia nina Roho Mtakatifu, sio lazima shetani anielekeze.
Wakati ulipofika yule Askofu akaja. Lakini akiwa katika maombi Mungu akamwambia
siku ya kwanza usifundishe kitu chochote. Tumia kipindi kizima kufanya maombi.
Yeye hakuelewa kitu chochote kinachoendelea mahali pale ila alikuwa mtii kwa
Mungu wake. Baada ya kuimba nyimbo za kusifu na kuabudu, ndipo Mchungaji mwenyeji
akapanda na hatimaye alimkaribisha Askofu kwa ajili ya kufundisha semina.
Akaniambia alipopanda akaanzisha kawimbo ka kuabudu na kisha kuanza kunena kwa
lugha, nguvu ya Mungu inashuka na kanisa zima linanena kwa lugha muda mrefu,
akiona nguvu ya Mungu inapungua anaendeleza kale kawimbo kake nguvu ya Mungu
inashuka tena kwa kasi kubwa, watu wananena kwa lugha mpaka wanaanguka wenye
mapepo yanawatoka na wengine wanapokea uponyaji mubashara.
Mpaka muda wake
ulipoisha hakuna mtu aliyeweza kutoka nje. Kila mtu aliyefika siku ile akaamini
kwamba yule aliyetenda yale ni Mungu. Siku iliyofuata ndio akaanza kufundisha masomo
aliyopanga, watu walifunguliwa na kila mtu akaamini kwamba yule mwanakwaya,
pengine bila kujua au kwa sababu ya kutokukaa vizuri na Mungu, alitumiwa na
shetani kutaka kukwepa kipigo anachokipata. Mwisho wa semina ndio yule Mchungaji
mwenyeji akamweleza kilichotokea. Na ndipo yeye akajua kwamba Mungu aliamua
asifundishe ili alainishe kwanza mioyo ambayo ilitiwa sumu na shetani kupitia
kwa yule mdada wa kwaya. Akaniambia angelazimisha kufundisha pengine watu
wasingepokea kitu, kwa sababu walikuwa tayari wameshafunga mioyo yao, au
shetani angeendelea kuwapa tafsiri tofauti ya fundisho lake, ili kuthibitisha
maneno ya uwongo wa pepo wake.
Elizabet Yohana na Rejoice George |
Rev Martin Pyuza |
nabii mmoja Afrika kusini akiwa katika maombezi |
nabii mwingine akimlisha mtu nyoka kwenye maombi |
KUNA WATUMISHI ITABIDI WAJE
KANISANI NA TUNGULI
Iwapo kweli wewe mtumishi
umeamua kukubali kutumia mapepo kwa ajili ya kuwatafutia watu wako uvumbuzi wa
matatizo yao, huna tofauti na watu wanaoulizia mambo mbalimbali kutokana na
mizimu.
tuko katika nyakati za hatari |
Ukweli ni kwamba sasa hivi
kanisa limeingiliwa sana na watu kama hao, na kwa sababu Yesu alisema kwamba
tuyaache magugu yakue pamoja na ngano. Lakini si vibaya watu wa Mungu wakajua
kabisa kwamba, pamoja na kwamba tumeambiwa tusiyang’oe kwa kila dalili hili ni
gugu tujaribu kuliepuka. Nimeona mtu mmoja anajiita nabii. Mtu akifika kwake
anaanza kumtabilia kama mganga wa kienyeji, Eti! Unakumbuka juzi ulikwenda kwa
shangazi yako. Alikupa maji kwenye kikombe cha bati, uliporudi nyumbani
ukasikia maumivu ya tumbo! Sasa Roho Mtakatifu huwa hafanyi vitu vya kipumbavu
na kichonganishi kama hivyo.
Yeye ni Roho wa amani tena hfanyi hivyo kama hujatoa pesa anayokutajia bila kupungua. Sasa hiyo kama sio kuingiza biashara za mizimu kanisani ni nini?
Inawezekana tukawa hatuna
maarifa sana ya kiroho, lakini mambo mengine hata akili ya kawaida inakataa
kabisa kuamini kama ndipo kanisa lilipofikia. Siku moja mwanangu alitaka sana
niongozane naye kwenda kwa nabii fulani maana amemweleza mambo mengi sana
kuhusu mimi. Nilijaribu sana kumkwepa lakini siku moja nikaona busara ni kwenda
naye ili nisimkatishe tamaa. Mimi najua hakika mafundisho yake hayawezi
kunidhuru. Maana Biblia imenihakikishia kwamba nitakula kitu cha kufisha na
hakitanidhuru. Kwa hiyo niliamua kwenda kujifunza maana huwa siamini hata kama
mtu atauchambua ukoo wangu wote. Nilipofika nilianza kuona mambo ndivyo sivyo,
kwanza mwanangu akaniambia kama una pesa kubwa tafuta chenji maana kila maombi
yana sadaka. Na kweli ni kama wamejipanga kuhakikisha kwamba hakuna fedha inayobaki
mfukoni kwa watu waliokuja. Pia nikaona kipande cha kitambaa cheupe, wenyewe
wanasema kina upako wa mtumishi kwa hiyo ukikinunua unaweza kukitumia kwenye
maombi mbalimbali. Mara kuna mafuta ya upako n.k.
Mambo haya ukiyaangalia kwa
ujumla wake, unaona kabisa kwamba hawa jamaa wameshindwa kuwavalisha watu
hirizi tu. Lakini mambo mengi ni kama waganga wa kienyeji tu. Mpaka hapo
nafikiri ni juu yako wewe kuamua kama unaona busara kuwasikiliza mapepo wakisema eti wametumwa na muhubiri
fulani, halafu na wewe ukiamini ujue kwamba shetani anakuona kuwa wewe ni
dhaifu sana. Shetani ni baba wa uongo, halafu wewe unategemea kuupata ukweli
kutoka kwa shetani. Kama na wewe unafanya hivyo ujue hakika kuwa unamtumikia
shetani, kanisa halijaanza leo kushambuliwa na watu wa aina hii. Kipindi fulani
kuna kundi kubwa la vijana waliokuwa wanajifanya wametoka kuzimu au kwamba
walikuwa wachawi wa kiwango cha juu, kwa hiyo wameokoka na sasa wanamtumikia
Mungu. Katika kundi lile sikumbuki kama kuna aliyebaki kwenye wokovu mpaka leo!
Lakini tuliwapokea na haraka sana tukawaamini tukawapa mpaka madhabahu
watufundishe mambo yao ya kishirikina waliyokuwa wanayafanya kabla ya kuokoka
na wengine mpaka wakaoa kanisani. Unakuta mtu anakwambia wakati mimi sijaokoka
niliwahi kufanya hivi na vile. Au nilifanya mkataba huu na ule unamuuliza sasa
baada ya hapo ulifanya nini ili kufuta ile mikataba uliyoichukua kuzimu.
Utakuta hana jibu anabaki kujiumauma tu. Na hao ndio wapo makanisani leo
wanajifanya kutabiri na kulielekeza kanisa la Mungu. Ukweli ni kwamba kanisa
lipo kwenye giza nene ni lazima watu fulani wapaze sauti na kusema wazi kwamba
hawa sio watumishi wa Mungu aliye hai
SOMO HILI LITAENDELEA