Tusisahau kwamba wale watu Yesu aliosema nao wakati akihubiri Mlimani pia walikuwa wameishi maisha yao chini ya ushawishi wa Mafarisayo wanafiki, waliokuwa viongozi na waalimu wa Israeli. Kama tulivyokwisha jifunza hapo mapema tulipotazama Mahubiri ya Mlimani, ni dhahiri kwamba sehemu kubwa ya yale ambayo Yesu alisema yalikuwa kama masahihisho tu ya mafundisho ya uongo ya Mafarisayo. Yesu hata aliwaambia watu kwamba hawataingia mbinguni ikiwa haki yao haitazidi ile ya waandishi na Mafarisayo (Mathayo 5:20), ambayo ilikuwa njia nyingine ya kusema kwamba waandishi na Mafarisayo walikuwa njiani kwenda jehanamu. Mwisho wa mahubiri yake, watu walishangazwa kwa sehemu kwa sababu Yesu alikuwa anafundisha kitofauti, “si kama waandishi wao” (Mathayo 7:29).
Mapema katika mahubiri Yake, Yesu aliweka wazi unafiki wa wale waliodai kwamba hawajawahi kuzini, ila wanatamani na kuachana na wenzi wao na kuoa tena. Akapanua maana ya uzinzi kwamba ni zaidi ya tendo la kimwili la dhambi baina ya watu wawili walio na ndoa. Na aliyosema yalikuwa wazi kabisa kwa yeyote mwenye akili nzuri na mkweli,
ambaye angefikiri kidogo tu. Lakini kumbuka kwamba, mpaka wakati wa mahubiri ya Yesu, wengi wa watu katika lile kundi wangekuwa na mawazo kwamba ilikuwa halali kwao kuachana “kwa sababu yoyote” ile. Yesu alitaka wafuasi Wake pamoja na wengine wote wajue kwamba kusudi la Mungu tangu mwanzo lilikuwa kiwango cha juu zaidi.
Mmesikia kwamba imenenwa, ‘Usizini’. Lakini mimi nawaambia, Kila mtu amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe. Kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanamu. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe. Kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanmum. Imenenwa pia, ‘Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka.’ Lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya usherati, amfanya kuwa mzinzi, na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini (Mathayo 5:27-32).
Kama tulivyokwisha ona mapema, ona kwamba maneno ya Yesu kuhusu talaka na kuoa tena yanafuata moja kwa moja maagizo aliyotoa kuhusu tamaa, hivyo kuyaunganisha pamoja. Tena, Yesu anasema vyote viwili ni uzinzi, na kuviunganisha zaidi. Basi tunaona kwamba kuna muunganiko wa kitu kinachofanana katika maelezo hayo ya fungu hili lote la Maandiko. Yesu alikuwa anawasaidia wafuasi Wake kuelewa maana ya kutii amri ya saba.
Maana yake ni kutotamani, na kutoachana na kuoana tena.
Kila mtu katika wasikilizaji Wake wa Kiyahudi alikuwa amesikia amri ya saba ikisomwa katika sinagogi (maana hawakuwa na Biblia binafsi siku zile), pamoja na mafafanuzi yaliyotolewa, na kuona jinsi waalimu wao – waandishi na Mafarisayo – walivyoyafanyia kazi maishani mwao. Ndipo Yesu akasema, “lakini mimi nawaambia”, ila hakuwa anataka kuongeza sheria zingine mpya. Yeye alitaka kudhihirisha tu mpango wa Mungu tokea mwanzo.
Kwanza – tamaa ilikuwa inakatazwa kabisa na amri ya kumi, na hata bila amri ya kumi, yeyote aliyefikiri vizuri angetambua kwamba ilikuwa ni kosa kutamani kufanya kitu ambacho Mungu amekataza.
Pili – tangu mwanzoni kabisa mwa kitabu cha Mwanzo, Mungu aliweka wazi kwamba ndoa ilitakiwa kuwa makubaliano ya maisha yote. Tena, yeyote aliyefikiri vizuri juu ya hilo angetambua kwamba kuachana na kuoana tena ni sawa tu na uzinzi, hasa kama mmoja atapanga kumwacha menzake kwa kusudi la kuoa tena.
Lakini tena katika mahubiri haya, ni wazi kwamba Yesu alikuwa anawasaidia tu watu waone ukweli kuhusu tamaa na ukweli kuhusu kuachana kwa sababu yoyote, na kuoana tena. Yeye hakuwa anaweka sheria mpya ya kuoana tena ambayo haikuwa “vitabuni” hadi wakati huo.
Inashangaza kwamba ni watu wachache sana kanisani ambao wamewahi kutimiza maneno ya Yesu ya kung’oa jicho au kukata mikono, maana mawazo hayo yanapingana sana na Maandiko mengine, na ni dhahiri kwamba kazi yake ni kutia nguvu hoja kuhusu kuepukana na kujaribiwa kuwa na mahusiano kimwili yasiyofaa. Lakini wengi sana kanisani wanajaribu kutafsiri moja kwa moja maneno ya Yesu juu ya yule mwenye kuoa au kuolewa tena kufanya uzinzi, hata ingawa tafsiri hizo zinapingana moja kwa moja na Maandiko mengine.
Lengo la yesu lilikuwa kuwafanya wasikilizaji Wake wakabiliane na ukweli, kwa tumaini kwamba talaka zingepungua baada ya hapo. Kama wafuasi Wake wangepokea moyoni yale aliyosema kuhusu tamaa, kusingekuwepo na uasherati au uchafu miongoni mwao. Kama usingekuwepo, kusingekuwepo na sababu halali za talaka. Basi, talaka isingekuwepo, kama Mungu alivyokusudia tangu mwanzo.
MWISHO WA SEHEMU HII
Tutakutana katika sehemu inayofuata ya somo hili Mungu akuinue kwa kufuatilia somo hili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni