Jumamosi, 26 Aprili 2014

WAJIBU WETU KWA MUNGU NI NINI?




Siku hizi wengi wanaojiita Wakristo wanamwachia Mungu wajibu wao ambao wamepewa na Biblia. Hii ni kwa sababu mafundisho ya kisasa ya kiinjili yamechafuliwa sana na mawazo ya kupinga kushika sheria, yenye kupotosha neema ya Mungu na kubatilisha wajibu wa mwanadamu. 

Kwa sababu wamedanganyika na mafundisho ya uongo kuhusu neema, ukiwatajia tu juhudi za kibinadamu unaonekana umekufuru, na huku wakidai kwamba wanatetea utukufu wa Mungu, wanasema fundisho lolote kuhusu utakatifu ni kuwafanya watu waishi kwa kufuata sheria.  
Matendo ni neno chafu ambalo halifai katika msamiati wa Kikristo. Hakika hatutaki liwepo wazo lolote kwamba sisi inatupasa kutenda chochote sasa kwa kuwa kazi ya Kristo imemalizika. Hiyo ni sawa na kuongezea matendo kwenye wokovu wetu (na Mungu apishe mbali!).

Kwa matazamio ya kujaribu kutibu shida hiyo ambayo haitokani na Maandiko, nimeorodhesha mambo ambayo sehemu kubwa ya Agano Jipya inasema tunapaswa kufanya. Sehemu muhimu ya wajibu wa mwanadamu katika mpango wa utakaso inaeleweka kirahisi kutokana na mistari mingi yenye maagizo na mashauri. Tunapoisoma, hatuwezi kuwa na mashaka tena kwamba Wakristo ni watu wenye hiari wanaoweza kuamua kuwa watakatifu. Pia, ule udanganyifu kwamba Mungu anaibiwa utukufu wakati tunapoongeza juudi zetu kwa habari ya utakaso unadhihirishwa wazi. Ni hivi: Mungu anawatazamia wale walio na Roho Wake Mtakatifu kufanya mambo fulani kwa nguvu za Roho. Kwa kifupi ni kwamba, sisi tunapaswa kushindana na dhambi katika hali zake zote. Sisi  lazima tutafute utakatifu, ambao “hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao” (Webrania 12:14).
Orodha ifuatayo inafunua matazamio ya Mungu juu ya tabia yetu. Orodha imetolewa katika Injili zote nne na kitabu cha Warumi. Kama Agano Jipya linasema tabia fulani ni mbaya au ni kosa au ni dhambi, basi Mungu bila shaka anawawajibisha watu kwa tabia hiyo, kuonyesha kwamba wajibu wa mwanadamu ni kitu kinachohusika katika tabia hiyo mbaya.
Japo unaweza kujaribiwa kuiruka orodha hii ifuatayo, ningekushauri uisome pole pole kwa manufaa yako mwenyewe. Inaweza kukugusa kwa njia itakayobadili maisha yako.

Je, Mungu anatutazamia tufanye nini? Ifuatayo ni orodha. Ni dhahiri kwamba hakuna chochote katika haya yafuatayo kitakachotokea maishani mwetu bila sisi kufanya Mungu anavyosema.
Mungu anatutazamia:
Tusimjaribu (Mathayo 4:7).
Tumwabudu Bwana Mungu wetu na kumtumikia Yeye tu (Mathayo 4:10).
Tutubu ili tuokolewe (Mathayo 4:17).
Tufurahi na kushangilia wakati tunapoteswa (Mathayo 5:12).
Tuache nuru yetu iangaze mbele za watu ili wayaone matendo yetu mema (Mathayo 5:16).
Tushike amri za Mungu na kuzifundisha, hata zile zilizo ndogo kabisa (Mathayo 5:19).
Tusiue, kumchukia wala kumdhuru mtu yeyote kwa njia yoyote ile (Mathayo 5:21-22).
Tujishughulishe kupatana na wale ambao tumewakosea (Mathayo 5:24-25).
Tusizini wala kuwa na tamaa mbaya (Mathayo 5:27-28).
Tuondoe chochote kinachotufanya tuangukie dhambini (Mathayo 5:29-30).
Tusivunje ndoa isipokuwa kwa uasherati (Mathayo 5:32).
Tusiape na tusidanganye. Kila mara tutimize maneno yetu (Mathayo 5:33-37).
Tusijilipize kisasi bali tuwavumilie sana wengine, hata kuwatendea mema wanaotutendea mabaya (Mathayo 5:38-42).
Tuwapende adui zetu na kuwaombea wanaotutesa (Mathayo 5:44-47).
Tujaribu kuwa wakamilifu (Mathayo 5:48).
Tusifanye mema ili tupokee sifa za watu (Mathayo 6:1).
Tutoe sadaka (Mathayo 6:2-4).
Tuombe (Mathayo 6:5-6).
Tusirudie-rudie maneno yasiyo na maana tunapoomba (Mathayo 6:7).
Tuombe kwa kufuata mfano wa “Sala ya Bwana” (Mathayo 6:9-13).
Tuwasamehe wengine (Mathayo 6:14).
Tufunge, yaani tusile chakula (Mathayo 6:16).
Tusijiwekee hazina duniani, bali mbinguni (Mathayo 6:19-21).
Tumtumikie Mungu, siyo fedha (Mathayo 6:24).
Tusiwe na wasiwasi kuhusu mahitaji yetu (Mathayo 6:25-32).
Tutafute kwanza ufalme wa Mungu na haki Yake (Mathayo 6:33).
Tusiwahukumu wengine (Mathayo 7:1-5).
Tusiwape mbwa kilicho kitakatifu (7:6).
Tuombe, tutafute, tubishe (Mathayo 7:7-11).
Tuwatendee wengine tunavyotaka kutendewa (Mathayo 7:12).
Tuingie kwa kupitia mlango mwembamba (Mathayo 7:13).
Tujihadhari na manabii wa uongo (Mathayo 7:15-20).
Tufanye aliyosema Yesu au tuangamie (Mathayo 7:24-27).
Tumwombe Bwana awatume watenda kazi katika shamba Lake (Mathayo 9:38).
Tumkiri Yesu mbele ya wengine. Tusimkane (Mathayo 10:32-33).
Tumpende Yesu kuliko watu walio karibu nasi (Mathayo 10:37).
Tujitwike msalaba na kumfuata Yesu (Mathayo 10:38).
Tupoteze maisha yetu kwa ajili ya Yesu (Mathayo 10:39).
Tujitie nira ya Yesu (Mathayo 11:28-30).
Tuwe “pamoja” na Yesu kukusanya (Mathayo 12:30).
Tusimkufuru Roho Mtakatifu (Mathayo 12:31).
Tufanye mapenzi ya Baba (Mathayo 12:50).
Tuwaheshimu wazazi wetu (Mathayo 15:4-6).
Tusinajisike kwa mawazo machafu, mauaji, uasherati, uzinzi, wizi, udanganyifu na hila (Mathayo 15:19-20).
Tujikane (Mathayo 16:24).
Tuongoke na kuwa kama watoto. Tujinyenyekeze (Mathayo 18:3-4).
Tusimfanye mtoto yeyote anayemwamini Yesu ajikwae (Mathayo 18:6).
Tusimfanye yoyote ajikwae (Mathayo 18:7).
Tusiwadharau watoto (Mathayo 18:10).
Tumkemee kibinafsi ndugu yeyote anayetukosea (Mathayo 18:15).
Tutii agizo la Yesu kuhusu adhabu kikanisa (Mathayo 18:16-17).
Tuwasamehe ndugu zetu kutoka moyoni (Mathayo 18:35).
Tumpende jirani yetu kama tunavyojipenda wenyewe (Mathayo 19:19).
Tuwe watumishi wa wengine (Mathayo 20:26-28).
Tulipe kodi halali kwa serikali na kumpa Mungu sehemu Yake (Mathayo 22:21).
Tumpende Bwana Mungu kwa moyo wote, roho yote na akili (Mathayo 22:37).
Tusikubali yeyote kutuita ‘mwalimu’ au ‘bwana’ na tusimwite yeyote baba isipokuwa Baba yetu wa mbinguni (Mathayo 23:8-10).
Tusijiinue bali tujishushe (Mathayo 23:12).
Tusimzuie yeyote kuingia katika ufalme wa Mungu (Mathayo 23:13).
Tusiwaonee wajane (Mathayo 23:14).
Tusiwashawishi wengine kuwa wanafiki (Mathayo 23:15).
Tusipuuzie mambo makuu katika Torati kama vile haki, rehema na uaminifu (Mathayo 23:23).
Tusiwe wanafiki kwa njia yoyote ile (Mathayo 23:25-28).
Tusiogope kuhusu vita au matetesi ya vita kabla ya kurudi kwa Yesu (Mathayo 24:6).
Tusianguke, au kusaliti au kumchukia ndugu (Mathayo 24:10).
Tusikubali kupotoshwa na manabii wa uongo (Mathayo 24:11).
Tusiruhusu pendo letu kupoa kwa sababu maasi yameongezeka (Mathayo 24:12).
Tuvumilie mpaka mwisho (Mathayo 24:13).
Tusiamini taarifa za uongo kuhusu kurudi kwa Kristo (Mathayo 24:23-26).
Tutambue ishara za kurudi kwake Kristo (Mathayo 24:32-33).
Tuwe macho kwa ajili ya kurudi kwa Kristo (Mathayo 24:42).
Kila mara tuwe watumwa waaminifu, tukitazamia kurudi kwa Bwana wetu upesi. Tusirudi nyuma bali kila wakati tumtii (Mathayo 24:45-51).
Tutumie muda, vipawa na hazina ambavyo Mungu ametupa kwa ajili ya utumishi Wake (Mathayo 25:14-30).
Tuwape Wakristo maskini chakula, cha kunywa na mavazi. Tuwatembelee Wakristo waliofungwa na walio wagonjwa (Mathayo 25:34-40). Tushiriki Meza ya Bwana (Mathayo 26:26-27).
Tufanye wanafunzi katika mataifa yote, tukiwabatiza katika jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu na kuwafundisha kuyashika yote aliyoamuru Yesu (Mathayo 28:19-20).
Tujihadhari tunasikia nini (Marko 4:24).
Tusipuuze amri za Mungu kwa ajili ya kushika mapokeo (Marko 7:9).
Tusimwonee Yesu aibu, wala maneno Yake (Marko 8:38).
Tuwe na amani sisi kwa sisi (Marko 9:50).
Tusiwazuie watoto kwenda kwa Yesu (Marko 10:14).
Tuwe na imani kwa Mungu (Marko 11:22).
Tuamini kwamba tumepokea yote tuyaombayo (Marko 11:24).
Tujihadhari na waalimu wa uongo waliovaa mavazi yanayowafanya waonekane, wanaopenda kusalimiwa kwa heshima, viti vya mbele na mahali pa heshima, wanaowaonea wajane na kuomba sala ndefu ili waonekane tu (Marko 12:38-40).
Tusiogope tutasema nini tukifikishwa mahakamani kwa ajili ya imani yetu bali tuseme kile ambacho Roho Mtakatifu atatwambia wakati huo (Marko 13:11).
Tubatizwe (Marko 16:16).
Tuwabariki wanaotulaani (Luka 6:28).
Tumpe  kila atuombaye, wala tusidai vitu tulivyonyang’anywa (Luka 6:30).
Tuwakopeshe wengine, wala tusitazamie kulipwa (Luka 6:35).
Tuwe wenye rehema (Luka 6:36).
Tusiwahukumu wengine (Luka 6:37).
Tutoe (Luka 6:38).
Tusinyoshe kidole kuhusu kibanzi katika jicho la ndugu wakati sisi tuna boriti katika jicho letu (Luka 6:41-42).
Tusimwite “Bwana” kama hatufanyi asemayo (Luka 6:46-49).
Tulipokee Neno la Mungu mioyoni mwetu na kulishika ili tuzae matunda kwa saburi (Luka 8:12-15).
Tulisikie Neno la Mungu na kulitenda (Luka 8:21).
Tuwapokee watoto katika jina la Kristo (Luka 9:48).
Tusiangalie nyuma baada ya kutia mkono kwenye jembe (Luka 9:62).
Tuombe kupewa Roho Mtakatifu (Luka 11:13).
Tujihadhari nuru ndani yetu isiwe giza (Luka 11:35).
Tusipende viti vya heshima na salaamu (Luka 11:43).
Tusiwalemee watu wengine kwa mizigo mizito ambayo sisi hatuko tayari kuibeba (Luka 11:46).
Tusiwatese manabii Wake (Luka 11:49).
Tusiondoe ufunguo wa maarifa wala kuwazuia watu wasiingie katika maarifa ya kweli ya Mungu (Luka 11:52).
Tujihadhari na viongozi wa dini walio wanafiki (Luka 12:1).
Tusiogope wale wanaoweza kutuua kimwili tu (Luka 12:4).
Tumwogope yeye ambaye, baada ya kuua ana mamlaka ya kutupa kuzimuni (Luka 12:5).
Tusinene mabaya wala kumkufuru Yesu au Roho Mtakatifu (Luka 12:10).
Tujihadhari na kujilinda na choyo (Luka 12:15).
Tusijiwekee hazina bali tuwe matajiri kwa Mungu (Luka 12:21).
Tuuze mali zetu na kuwapa maskini (Luka 12:33).
Tuzae matunda (Luka 13:6-9).
Tujitahidi kuingia kwa kupitia mlango mwembamba (Luka 13:24).
Tusichukue mahali pa heshima, tukijitukuza wenyewe. Bali tujinyenyekeze, tukikaa kiti cha nyuma (Luka 14:8-10).
Tumpende Yeye kuliko wapendwa wetu (Luka 14:26).
Kwanza tuhesabu gharama ya kuwa wanafunzi Wake (Luka 14:28-32).
Tuweke mali yetu yote chini ya mamlaka Yake (Luka 14:33).
Tufurahi wakati Mungu anapowahurumia wenye dhambi kwa kuwaokoa (Luka 15:1-32).
Tuwe waaminifu katika mambo madogo, na fedha (Luka 16:9-11).
Tuwahurumie maskini (Luka 16:19-31).
Tumkemee ndugu akikosa, na kumsamehe akitubu (Luka 17:3-4).
Tujihesabu kuwa watumwa wasiofaa hata baada ya kufanya yote tuliyoagizwa kufanya (Luka 17:7-10).
Tuombe wakati wote wala tusikate tamaa (Luka 18:1).
Tusijione kwamba ni wenye haki, wala tusiwadharau wengine (Luka 18:9).
Tuupokee ufalme kama mtoto (Luka 18:17).
Tuwe macho wakati wote na kuomba ili tuweze kuepukana na majaribu yatakayokuwepo kabla ya kurudi kwa Kristo, na tuweze kusimama mbele zake (Luka 21:36).
Tutangaze toba na msamaha wa dhambi katika Jina la Yesu kwa mataifa yote (Luka 24:47).
Tuzaliwe mara ya pili (Yohana 3:3).
Tumwamini Yesu (Yohana 3:16).
Tumwabudu katika roho na kweli (Yohana 4:23-24).
Tumheshimu Yesu (Yohana 5:23).
Tutafute utukufu kutoka kwa Mungu (Yohana 5:44).
Tuamini aliyoandika Musa (Yohana 5:46-47).
Tusikitendee kazi chakula kiharibikacho, bali kidumucho mpaka uzima wa milele kinachotolewa na Yesu (Yohana 6:53-54).
Tusihukumu kwa jinsi mtu anavyo-onekana, bali kwa haki (Yohana 7:24).
Tukae katika neno la Yesu (Yohana 8:31).
Tulishike neno la Yesu (Yohana 8:51).
Tumtumikie (na kumfuata) Yesu (Yohana 12:26).
Tupendane, kama Yesu anavyotupenda (Yohana 13:34).
Tuamini kwamba Yeye ni ndani ya Baba, na Baba ndani Yake (Yohana 14:11).
Tufanye matendo ya Yesu, na hata makubwa zaidi (Yohana 14:12).
Tumpende Yesu na kuzishika amri Zake (Yohana 14:15).
Tukae katika pendo la Yesu (Yohana 15:9).
Tuombe lolote katika Jina la Yesu (Yohana 16:24).
Tuwe na ujasiri katika dhiki (Yohana 16:33).
Huo ndiyo mwisho wa amri za Yesu zipatikanazo katika Injili. Hayo ndiyo mambo ambayo tunapaswa kuwa tunawafundisha wanafunzi wa Kristo kwamba wayatii  (ona Mathayo 28:20).
Amri na maagizo kwa ajili ya waamini katika nyaraka si tofauti sana na Injili. Sasa hebu tutazame wajibu wa mwanadamu kutoka kitabu cha Warumi tu.
Mungu anatazamia tufanye haya yafuatayo:
Tusifiche au kugandamiza ukweli (Warumi 1:18).
Tusiwe na hatia ya kuabudu sanamu (Warumi 1:23).
Tusibadili kweli ya Mungu kwa uongo (Warumi 1:25).
Tusihusike katika ulawiti (Warumi 1:26, 27).
Tusiwe wachoyo, wenye wivu, wadanganyifu, wabaya, wenye dharau, wakorofi, wenye kiburi, wasiotii wazazi, wasioaminika, wasiopenda na wasio na rehema (Warumi 1:29-31).
Tusiwasengenye watu wala kuwasingizia uongo (Warumi 1:29-30).
Tusiwaunge mkono watendao dhambi (Warumi 1:32).
Tusipuuzie utajiri wa wema Wake, ustahimilivu na uvumilivu (Warumi 2:4).
Tudumu katika kutenda mema (Warumi 2:7).
Tutafute utukufu, heshima na kutokuharibika (Warumi 2:7).
Tusiwe na tamaa ya ubinafsi (Warumi 2:8).
Tusilaani au kusema maneno yenye uchungu (Warumi 3:14).
Tujihesabu wafu kwa dhambi bali hai kwa Mungu katika Kristo (Warumi 6:11).
Tusiruhusu dhambi itawale miili yetu. Tusitii tamaa yake (Warumi 6:13).
Tujitoe kwa Mungu kama walio hai kutoka kwa wafu, na viungo vyetu kama vyombo kwa ajili ya haki kwa Mungu (Warumi 6:13).
Tusitamani (Warumi 7:7).
Tusiishi kulingana na mwili, bali tuyafishe matendo ya mwili kwa njia ya Roho (Warumi 8:12-13).
Tuitoe miili yetu kama dhabihu iliyo hai na takatifu (Warumi 12:1).
Tusifananishwe na dunia hii, bali tufanywe upya kwa kugeuzwa nia zetu (Warumi 12:2).
Tusinie makuu kuliko inavyopasa (Warumi 12:3).
Tutumie vipawa vyetu kulingana na neema tuliyopewa (Warumi 12:6).
Tuwapende wengine bila unafiki (Warumi 12:9).
Tukatae lililo ovu na kushika lililo jema (Warumi 12:9).
Tupendane kindugu na kupeana heshima (Warumi 12:10).
Tusilegee (Warumi 12:11).
Tuwe na juhudi tunapomtumikia Bwana (Warumi 12:11).
Tufurahi katika tumaini (Warumi 12:12).
Tuvumilie katika dhiki (Warumi 12:12).
Tudumu katika maombi (Warumi 12:12).
Tusaidie mahitaji ya watakatifu (Warumi 12:13).
Tuwe wakarimu (Warumi 12:13).
Tuwabariki wanaotulaani, tusiwalaani sisi (Warumi 12:14).
Tufurahi na wanaofurahi, tulie na wanaolia (Warumi 12:15).
Tusiwe wenye majivuno bali tushirikiane na wa hali ya chini (Warumi 12:16).
Tusiwe wenye hekima machoni petu wenyewe (Warumi 12:16).
Kamwe tusilipe ovu kwa ovu (Warumi 12:17).
Tujali lililo jema machoni pa watu wote (Warumi 12:17).
Kadiri iwezekanavyo, tukae kwa amani na watu wote (Warumi 12:18).
Tusijilipizie kisasi (Warumi 12:19).
Adui yetu akiwa na njaa tumlishe, akiwa na kiu tumnyweshe (Warumi 12:20).
Tusishindwe na ubaya, bali tuushinde kwa wema (Warumi 12:21).
Tukubali mamlaka ya wakuu wa serikali (Warumi 13:1).
Tusidaiwe chochote na mtu isipokuwa kupendana (Warumi 13:8).
Tuweke kando matendo yote ya giza na kuvaa silaha za nuru (Warumi 13:12).
Tuenende ipasavyo mchana, sio katika vurugu na ulevi, uasherati na tamaa mbaya, wivu au fujo. Tumvae Kristo na tusitoe nafasi kwa mwili na tamaa zake mbaya (Warumi 13:13-14).
Tuwapokee walio dhaifu katika imani (Warumi 14:1).
Tusimhukumu ndugu wala kumdharau (Warumi 14:10).
Tusiweke vikwazo mbele ya ndugu (Warumi 14:13).
Tufuate mambo yaletayo amani na kujengana (Warumi 14:19).
Tuichukue mizigo ya walio dhaifu kama sisi tuna nguvu. Tusijipendeze wenyewe (Warumi 15:1).
Tupokeane na kukubaliana, kama Kristo alivyofanya kwetu (Warumi 15:7).
Tuwatazame wenye kuleta matengano na vipingamizi kinyume cha kweli za Biblia na kuachana nao (Warumi 16:17).
Sasa niulize hivi: Je, Wakristo wanawajibika kama wanadamu? Tuseme nini juu ya mtu yule anayesema kwamba yeye ameliacha jambo la utakaso wake mikononi mwa Mungu, asije akamwibia Mungu utukufu wake na kuwa na hatia ya kuongezea matendo yake kwenye wokovu?

KWA NINI MUNGU AMETUACHA KWENYE ENEO LA ADUI?



Kama Mungu anatamani tuwe watakatifu, mbona amewaruhusu adui hawa kuishi miongoni mwetu? Kwani wanatimiza kusudi gani la kimungu?
Adui zetu wanaruhusiwa kukaa miongoni mwetu ili Mungu atupime, kama alivyoruhusu mataifa maovu yabakie katika ardhi ya Israeli baada ya kufa kwa Yoshua (ona Waamuzi 2:20 hadi 3:1).  Wao wanapima upendo wetu, utii wetu – yaani, imani yetu. Imani inaweza kupimwa wakati kunapokuwepo uwezekano wa kutokuamini. Upendo unaweza kupimwa wakati kuna uwezekano wa chuki. Utii unaweza kupimwa wakati kuna uwezekano wa kutokutii.
Mungu aliwaambia hivi Waisraeli wa zamani:
Kukizuka katikati yako nabii au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, ‘Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;’ wewe usiyasikilize maneno ya nabii yule au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA Mungu wenu yuawajaribu, apate kujua kwamba mnampenda BWANA Mungu wenu kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote. Tembeeni kwa kumfuata BWANA Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye (Kumbu. 13:1-4).
Cha ajabu ni kwamba Mungu aliwapima watu Wake kwa kutumia nabii wa uongo! Lakini je! Hana maarifa yote pamoja na uwezo wa kujua mambo kabla? Mbona kuwe na haja ya kupimwa tena?
Sababu ni hii: Ili Mungu ajue matokeo ya kipimo cha mtu mwenye hiari, lazima huyo apimwe wakati fulani. Kinachoweza kujulikana kabla ni kitu kinachoweza kujulikana wakati fulani. Basi, majaribu yetu na dhiki na vipimo, ambavyo vina mipaka katika muda fulani, hutekeleza kusudi katika mpango wa Yule aishiye nje ya majira na nyakati. Hutoa njia ambayo kwayo imani yetu inathibitishwa kuwa ya kweli. Petro aliwaandikia hivi Wakristo waliokuwa wanapitia mambo magumu:
Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo … Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe. (1Petro 1:6-7; 4:12-13. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Hata kama hakuna sababu nyingine, tunapaswa kufurahi katika mateso kwa sababu yanaturuhusu nafasi ya kuonyesha imani yetu thabiti. Imani yenye kuokoa hudumu, lakini imani inaweza kuvumilia tu wakati kuna upinzani na majaribu ili isivumilie.

KUSHINDANA NA DHAMBI






“Dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde” (Mwanzo 4:7).

KAMA tulivyoona katika sura iliyopita, utakaso wetu ni juhudi za pamoja kati ya Mungu na sisi wenyewe. Tunaendelea kuwa kama Yesu zaidi tunapozidisha ushirikiano na Baba. Yeye anatupa uwezo na hamasa ya kuwa watakatifu. “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa” (2Petro 1:3 – Maneno mepesi kutilia mkazo). Yeye hutupa sisi asili mpya na kutuongoza kwa Roho Wake anayekaa ndani yetu. Lakini, anatuachia na sisi kitu cha kufanya. Bado tuna hiari yetu. 

Ni lazima tumfuate Roho anayekaa ndani yetu, na hili linafanywa na kila Mkristo wa kweli kwa kiwango fulani. Vinginevyo anajionyesha kuwa ni mwamini bandia (ona Warumi 8:5-14).

Vile vile ni wajibu wetu kufanya upya nia zetu kwa Neno la Mungu, maana lazima tujue mapenzi Yake kabla ya kuyatenda. Hata katika hilo pia Mungu hutusaidia kwa njia ya huduma ya kufundisha ya Roho Mtakatifu na kwa kupitia wanadamu waliotiwa mafuta kuwa waalimu. 

Nia zetu zinapofanywa upya na kweli Yake, tunabadilishwa (ona Yohana 8:31-36; Warumi 12:2). Kisha, tuna wajibu wa kutokuwa wasikilizaji tu wa neno bali watendaji pia (Yakobo 1:22).

Lazima mlingano huo utunzwe. Japo Maandiko yanafundisha juu ya wajibu wa Mungu na wa binadamu, watu wengi hukazia kimoja na kuacha kingine.  Yamekuwepo makundi mawili kihistoria – wanaojaribu kuwa watakatifu kwa nguvu zao wenyewe, na wanaopinga juhudi zozote za kibinadamu kwa habari ya utakatifu, wakimwachia Mungu kila kitu. 

Pande zote mbili zina orodha ndefu ya maandiko, na kama wangetazama orodha zao wote wangetambua kwamba wote wako sawa na wote wamekosea. Ukweli uko katikati, mahali ambapo orodha zote mbili zinaheshimiwa. Hakuna mstari mmoja unaoeleza vizuri mlingano huo kuliko Wafilipi 2:12 na 13. Unasema hivi:
Basi wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema (Maneno mepesi kutilia mkazo).
Tunda ambalo Roho huzaa ndani yetu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi, lakini, matunda hayo yataonekana maishani mwetu kwa ushirikiano wetu tu. Ni lazima tufanye kitu fulani kwa sababu, kulingana na Maandiko, zipo nguvu kama tatu hivi zinazopinga matunda hayo.
(1) Mungu ameturuhusu sisi kubakia “duniani”, dunia ambayo inatujaribu tusiwe na upendo au kupendeka, tuwe na huzuni, tuwe na wasiwasi, tusivumilie, tusiwe wema, tuwe waovu, tusiwe waaminifu, tuwe wakali na wenye kujitosheleza.

(2) Ingawa Mungu ametujaza kwa Roho Wake, na kutupa asili mpya na kuvunja nguvu za dhambi juu yetu, Yeye pia ameruhusu mabaki ya asili yetu ya kale ya dhambi kubakia ndani yetu. Kitu hicho Paulo anakiita “mwili”.

(3) Ingawa tumekombolewa kutoka ufalme wa Shetani na sisi si watoto wake tena kiroho, tunajikuta kama wale Wakristo wa zamani tukiwa katika uwanja mkubwa uliojaa simba wanaounguruma, wenye lengo la kutumeza (ona 1Petro 5:8). Shetani na mapepo yake hutusumbua na kutunyanyasa na kutujaribu ili tufanye yale ambayo Mungu amekataza.
Hao watatu ndiyo adui zetu: dunia, mwili na shetani.