Kama Mungu anatamani tuwe watakatifu, mbona amewaruhusu adui hawa kuishi
miongoni mwetu? Kwani wanatimiza kusudi gani la kimungu?
Adui zetu wanaruhusiwa kukaa miongoni mwetu ili Mungu atupime, kama
alivyoruhusu mataifa maovu yabakie katika ardhi ya Israeli baada ya kufa kwa
Yoshua (ona Waamuzi 2:20 hadi 3:1). Wao wanapima upendo wetu, utii wetu –
yaani, imani yetu. Imani inaweza kupimwa wakati kunapokuwepo uwezekano wa
kutokuamini. Upendo unaweza kupimwa wakati kuna uwezekano wa chuki. Utii
unaweza kupimwa wakati kuna uwezekano wa kutokutii.
Mungu aliwaambia hivi Waisraeli wa zamani:
Kukizuka katikati yako nabii au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au
ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, ‘Na tuifuate
miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;’ wewe usiyasikilize maneno ya nabii
yule au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA Mungu wenu yuawajaribu, apate
kujua kwamba mnampenda BWANA Mungu wenu kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.
Tembeeni kwa kumfuata BWANA Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na
kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye (Kumbu. 13:1-4).
Cha ajabu ni kwamba Mungu aliwapima watu Wake kwa kutumia nabii wa uongo!
Lakini je! Hana maarifa yote pamoja na uwezo wa kujua mambo kabla? Mbona kuwe
na haja ya kupimwa tena?
Sababu ni hii: Ili Mungu ajue matokeo ya kipimo cha mtu mwenye hiari, lazima
huyo apimwe wakati fulani. Kinachoweza kujulikana kabla ni kitu kinachoweza
kujulikana wakati fulani. Basi, majaribu yetu na dhiki na vipimo, ambavyo vina
mipaka katika muda fulani, hutekeleza kusudi katika mpango wa Yule aishiye nje
ya majira na nyakati. Hutoa njia ambayo kwayo imani yetu inathibitishwa kuwa ya
kweli. Petro aliwaandikia hivi Wakristo waliokuwa wanapitia mambo magumu:
Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo ikiwa ni
lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa
kwa imani yenu ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa
hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima,
katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo … Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba
ulio kati yenu unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu
kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili
na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe. (1Petro 1:6-7; 4:12-13.
Maneno mepesi kutilia mkazo).
Hata kama hakuna sababu nyingine, tunapaswa kufurahi katika mateso kwa
sababu yanaturuhusu nafasi ya kuonyesha imani yetu thabiti. Imani yenye kuokoa
hudumu, lakini imani inaweza kuvumilia tu wakati kuna upinzani na majaribu ili
isivumilie.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni