Jumatatu, 17 Februari 2014

USHUHUDA MKUBWA WA KHOSROW



Alipokuwa mtoto mdogo Khosrow alijiuliza “maana ya maisha”. Vitu vyote vilivyokuwa vikimzingira vilizua maswali mengi. Kwa nini maua yana rangi? Kuna nini kwa juu ya nyota? Tunaenda wapi tukisha kufa? Ni akina nani wale “watu waliomo” ndani ya TV? Je wanaenda wapi baada ya kuzimwa kwa TV? Alipokosekana mtu wa kumpa majibu ya kumridhisha kwa maswali yake mengi, alisikitika sana na kubaki na mawazo mazito.
Siku moja kijana huyu alipita karibu na kanisa la Wakristo wa Kiashuru na akaamua aingie ndani, akifikiri kuwa ataweza kupata majibu kwa baadhi ya “maswali” yake. Kumbe kulikuwepo wanawake wachache tu na mchungaji kiongozi ambaye alimpatia box la vitabu aende nalo. Vitabu vyote vilikuwa katika lugha ya kifarsi na pia kulikuwa na nakala ya Agano Jipya, ambayo Khosrow aliisoma kuanzia jalada hadi jalada. Lakini hali ya kusoma peke yake haikuweza kumsaidia kugundua majibu ya maswali yake. Alipohangaika akakitupa kitabu kile chumbani mwake. Ndipo umbo la mtu alifika kwake katika maono. Mtu huyu alimnyoshea mikono yake na kumwambia: “Shika mikono yangu na kila kitu kitabadilika kwako hata milele.” Khosrow alichukua mikono ya mtu yule na aliona hali ambayo aliielezea kama “Umeme ” ilipita mwilini mwake. Alipiga magoti, akaanza kulia. Kwa kupiga kelele kitu ambacho kiliwafanya wazazi wake kumkimbilia chumbani kwake. Walishikwa na butwaa walipomwona kijana wao akilia, jambo ambalo walikuwa hawajaliona kwake kwa miaka mingi sasa.
Maono ya Khosrow hayakuwa mambo ya kubuniwa kichwani mwake! Alirudi tena kwa mchungaji yule aliyekuwa amempatia vitabu na akamwelezea yaliyomtokea. Ndani ya miaka iliyofuata Khosrow alikua kiimani akiwa mwanafunzi wa Bwana Yesu. Kisha hata yeye mwenyewe amekuwa Mchungaji!
Lakini mateso kwa Wakristo huko Iran yalimsababisha akimbilie Uturuki pamoja na mkewe na watoto wao wawili. Hata huko Uturuki kulikuwa na mateso na magumu pia, lakini Khosrow na familia yake waliwafika watu kwa uvumilivu na upendo. Khosrow alianzisha makanisa mengi huko, kabla yeye na familia yake walipolazimika kukimbia tena. Wakati huu walitafuta usalama kwenye makambi ya wakimbizi huko Austria. Walipanda ndege kutoka Uturuki hadi Bosnia na kisha kutoka pale walitembea kwa miguu kupitia milima mikali yenye hatari wakiipita usiku. Walipokuwa wakivuka mto, kijana wao aitwae Yusufu, alikosea na kutokukanyaga vizuri kwenye daraja lisolokuwa imara na hivyo kuangukia kwenye maji ya baridi sana, akimvuta baba yake pia mtoni. Mto ulikuwa umejaa maji mengi na kina kikawa kirefu, na Khosrow alihangaika gizani kwenye maji, alimtafuta bila kumpata kijana wake. Punde si punde, mkewe pia alirukia mtoni ili kuweza kusaidia, lakini alikuwa katika hatari ya kuzama majini. Ghafla Khosrow alihisi kama mtu fulani akimweka Yusufu katika mikono yake. Pia alihisi kama mtu fulani - asiyeonekana machoni pake - alikuwa akimsaidia kumbeba Yusufu kando ya mto. Wote kwa jumla kama familia walikuwa salama, waliendelea kuvumilia majaribu mengi zaidi, hatimaye waliweza kufika Austria kwa usalama.
Khosrow anailinganisha mikono isiyoonekana iliyomwokoa yeye na familia yake usiku ule na mikono ile jinsi alivyohisi siku ile alipomwona Yesu kwenye maono. Aliposimulia habari yake mtu alimdadisi na kumwuliza ikiwa maono yale aliyoyaona yamebuniwa tu kichwani mwake! Ndipo Khosrow alimwuliza mtu huyo ikiwa alikuwa amevaa nguo. Mtu yule alishtuka sana na kushangaa swali, lakini mambo yalieleweka. Maono ya Khosrow yalikuwa ya kweli.

USHUHUDA MKUBWA WA MOHAMED




Mohamedi wa kabila la Fulani alianza kufuga mifugo alipokuwa na umri wa miaka sita. Alifanya hivyo kwa miaka kumi hivi mpaka alipoenda kwenye shule ya kiarabu kujifunza zaidi Kurani. Kabla ya hapo, Mohamedi alikuwa amejifunza juu ya Uislamu kutoka kwa baba yake.
Baada ya miaka kadhaa ya kjifunza hapo shuleni, alirudi nyumbani. Usiku mmoja aliota ndoto ya kuogofya sana. Aliona watu kandokando ya barabara waliokuwa wakipata shida. Aliingia ndani ya geti moja na watu walimchukua na kuanza kumpiga. Kisha akafungiwa kwenye chumba kilichokuwa na joto kali. Ilikuwa ni joto kali kiasi kwamba mwili wake ulianza kuchunika kama vile kujivua magamba. Na alipoanza kupiga kelele na kuupiga mlango teke ili uweze kufunguka, mara akaamuka toka usingizini. Hakuweza kulala tena usiku ule. Usiku uliofuata alipata ndoto nyingine. Safari hii alikuwa kwenye barabara nyingine na aliona miili iliyooza. Alienda kwenye geti lile lile, alipigwa na kuchukuliwa kwenye chumba kile kile. Ngozi yake iliyeyuka mwilini wakati mtu mmoja aliyekuwa amevaa nguo nyeupe alipomtokea. Ghafla chumba kikawa na ubaridi mzuri na wale watu waliokuwa wakimpiga wakatoweka. Mtu yule alinyosha mkono wake na kuishika mikono ya Mohamedi na kusema: “Mwanangu, unafanya nini hapa? Je, unapenda nikupeleke nyumbani?” Mohamedi akasema: “Ndani ya sekunde moja nilikuwa nimesharudi nyumbani na aliniambia, ’Ninakupenda mwanangu.’”
Wiki mbili baadaye Mohamedi alipata ndoto ya tatu. Alikuwa porini na hapo palikuwa na shimo refu mbele yake na hakujua jinsi ya kulivuka. Alipoangalia ndini yake aliogopa zaidi na akafikiri kuwa pengine angetumbukia ndani yake na kufia humo. Akamwona mtu amevaa nguo nyeusi akitembea haraka. Mtu huyu alimwambia kuwa simba alikuwa akija nyuma yake Mohamedi na kwamba ili kujiokoa alitakiwa aliruke shimo lile kabla ya simba kumfikia. Mohamedi akamsikia simba akinguruma. Mara tu alipotaka kuliruka shimo lile, mtu mwingine aliyekuwa amevaa nguo nyeupe alitokea mbele yake. Mtu huyu ni yule yule aliyemwona kwenye ile ndoto iliyokuwa imetangulia, akamwuliza hivi: “Mwanangu unaenda wapi?” Mtu yule mwenye vazi jeusi akawa ametoweka na ngurumo ya simba ikakoma. Mohamedi akamwambia mtu yule mwenye vazi jeupe kuwa alikuwa akienda nyumbani. Akamwuliza Mohamedi kama anahitaji msaada. Mtu yule mwenye vazi jeupe alinyosha mguu wake juu ya shimo lote. Alipofanya vile, shimo lile likafukiwa kabisa. Kisha akamwambia Mohamedi apite juu yake na aende nyumbani. Walipokuwa karibu na nyumbani kwake Mohamedi mtu yule alisema: “Ninakupenda mwanangu.”
Kwa siku sita mfululizo kila usiku, alipata ndoto zilizofanana. Kila wakati alijiona yuko katika sehemu tofauti tofauti, bila kujali mahali alipokuwa, mtu yule yule aliyekuwa amevaa nguo nyeupe alikuwa akija na kumsaidia. Katika ndoto ya mwisho ya tisa, alijiona amekaa chini ya mti akisoma vitabu ambavyo hakuweza kuvielewa. Mtu yule mwenye nguo nyeupe, yaani YESU alikuwa amekaa pembeni mwake. Alimwuliza: “Je unasoma juu ya nini?” Naye akamjibu kuwa alijaribu kuongeza ujuzi. Yesu akamwuliza Mohamedi kama alitaka msaada na kwamba angeweza kumwonesha mambo maalumu ya kusoma. Yesu alichukua kitabu kile na kusema: “Kitabu kinatoka kwa Bwana na kina ujumbe wa Mungu ndani yake. Katika kitabu hiki nitakuonesha mistari itakayokusaidia wewe.” Yesu alimsomea maandiko Mohamedi, pamoja na Yohana 14:6, kinachosema hivi: “Mimi ndimi njia, na kweli na uzima. Mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi.” Alimfafanulia na kumwambia kwamba Yeye Ndiye njia, na Mwokozi wa Ulimwengu. Pia Bwana Yesu alimwambia kuwa atapitia majaribu na mateso mengi baada ya kuwa Mkristo. Akamwambia kuwa alitaka awe Mwokozi wake na kumwelezea kwamba yeye ndiye aliyekuwa mtu yule katika ndoto zake, mtu aliyemkomboa au kumsaidia. Bwana Yesu alipomwambia kwamba alitaka ampe wokovu, na kumwuliza: ”Je unaupokea?” Mohamedi akasema “Ndiyo” na Yesu akatoweka.
Siku iliyofuata Mohamedi alimwendea Mkristo mmoja aliyefahamiana naye akamwambia juu ya ndoto hii. Huyu rafiki alimtambulisha kwa vijana wengine kutoka katika kanisa lingine na wakamwongoza Mohamedi kumpokea Yesu. Aliwaambia wazazi wake kuwa sasa yeye amekuwa Mkristo. Baada ya miezi kadhaa, Baba yake Mohamedi alimlazimisha kunywa sumu. Aliwaagiza watu wengine kutoka pale kijijini kumzunguka Mohamedi ili asiweze kukwepa ama kukimbia. Cha ajabu ni kwamba siku mbili kabla ya siku ile Yesu alikuwa amemtokea Mohamedi na kumwambia kuwa japokuwa atapitia magumu atakayokutana nayo, Yesu mwenyewe atamfanyia njia ili aweze kutoka. Hivyo Mohamedi alimwomba baba yake kama anaweza kuomba kwanza kabla ya kuinywa ile sumu. Aliomba kisha akainywa ile sumu, na akaenda kulala. Asubuhi iliyofuata, baba yake alishangaa sana alipomwona Mohamedi alikuwa hai! Hata hivyo baadaye watu wa familia yake walijaribu kumwua kwa kumlenga na mshale wenye sumu! Alilazwa wiki moja hospitalini, hata hivyo alipona vizuri!
Baada ya majaribio hayo ya kumaliza uhai wake, familia yake walipanga mikakati mingine kwa kumshawishi aache Ukristo. Baba yake alimpa ng’ombe mia moja na akamwambia kuwa angeweza kumwoza wanawake watatu kama angeachana na imani ya Kikristo! Hatimaye, Mohamedi alifanya uamuzi – lakini ilikuwa ni kuiacha familia yake hapo nyumbani. Alimshukuru baba yake kwa kundi kubwa hilo la ng’ombe, na nafasi ya wanawake hao watatu. Kisha akamwambia baba: “Bado hujafikia kile kiwango ambacho Bwana Yesu aliniahidi mimi kupata, ikiwa utaniahidi na kunipatia ahadi hizo itakuwa sawa kwangu. Je una uwezo wa kunipatia mimi uzima wa milele?” Baba yake akasema: “Hapana.” Kwa vile hataweza kumpatia uzima wa milele, hivyo kwa vyo vyote vile asingeweza kumwacha Yesu Kristo!
Miaka michache baadaye, Baba yake Mohamedi alipolala taabani karibu na kufa alimwomba msamaha Mohamedi na akasema kuwa, na yeye sasa alikuwa tayari kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wake. Mohamedi alimwongoza baba yake sala ya toba na baada ya masaa matatu alikufa. Kwa upande mwingine kifo cha baba wa Mohamedi lilikuwa ni tukio la huzuni, lakini bado katika upande mwingine, ilikuwa ni sababu ya furaha. Siyo tu kwa vile baba na mwanawe wamepatana kabla ya baba mtu kuiaga dunia, ila aliiaga dunia kwa amani, akijua kuwa katika ulimwengu ujao, atakuwa pamoja na Yesu milele yote, na – baadaye kwa siku za usoni - atakuwa na mwanawe tena mbinguni.

USHUHUDA MKUBWA WA KHALIL




Khalil alianza kuikariri Kurani Tukufu alipokuwa bado mdogo sana na akaendelea na hali hiyo aliyoiita kuwa ni upendo kwenye neno la Mungu. Kwa kadri alivyoendelea kukua, akaanza kusoma vitabu vya kiislamu hasa vile vilivyofafanua Kurani. Alipoendelea kuisoma Kurani na alichanganua walio Waislamu kufuatana na mafundisho hayo kutoka kwa wale wasio Waislamu. Hatimaye aliafiki hata wazazi wake kuwa makafiri. Vitu vidogo vidogo kama vile mwanamke kutokuvaa hijabu kungemfanya mtu kutokuwa Mwislamu wa kweli kulingana na vile alivyoelewa Kurani. Kama mwanaume asingezifuga ndevu zake hata zikakua angeeleweka kuwa yeye pia si Mwislamu. Alizingatia kuwa Wakristo ni maadui zake wakubwa, na hivyo akaanza kujihusisha na mashambulizi dhidi ya Wakristo na kanisa kwa jumla. Kikundi hicho kilijitoa kuipindua serikali ya Misri na kuunda serikali ya kiislamu yenye msimamo mkali. Walimwandikisha kuwa mpiganavita hata kumpandisha cheo na kumchagua kuwa kiongozi wa mahali pale. Kikundi chake kilijihusisha na utekaji nyara kwa mwandishi mashuhuri wa kiislamu asiye na msimamo mkali aliyethubutu kuukosoa kikundi cha Uislamu.
Hatimaye mamlaka ilimtia mbaroni Khalil na wenzake wengi wa kikundi chake. Huko gerezani alikaa miaka miwili, alipata mateso yenye maumivu makali, na mara alipoachiwa huru, alienda Yemen pamoja na wenzake washika dini sana. Kutoka kwenye kituo hiki waliendelea na mipango yao ya kupindua serikali ya Misri kwa silaha.
Hata hivyo mipango yao iligundulika na mamlaka ya eneo lile. Wengi wao walikamatwa tena. Hata hivyo njia ya mapinduzi ya jeshi haijaachwa kamwe. Waliporudi tena Misri walihitaji kukanusha shughuli zao za awali. Siku moja wakiwa Kairo walisoma makala gazetini juu ya kukamatwa kwa Wakristo! Khalil na kikundi chake waliamua kwamba sasa “imepitwa na wakati” kufanya kazi kutetea Uislamu. Hata hivyo katika uchache wao, waliamua kuwa, mapambano yao sasa yangechukua sura mpya kwa kutumia akili. Utafiti ufanywe wa kuandika kitabu kwa kuthibitisha kuwa Mohammad ndiye nabii wa kweli wa Mungu, na kwamba Biblia ya Wakristo na ya Wayahudi ni maandiko yaliyobatilishwa! Khalil alichaguliwa na shehe wake aliyekuwa Kiongozi wa kikundi chake cha kiislamu, ili kufanya utafiti na baada ya hapo aandike kitabu. Kwanza alikataa katakata, kisha aliazimu kuifanya hii kazi, ambayo baadaye aliielezea kuwa katika kazi zote alizowahi kuzifanya maishani mwake kazi hii ilikuwa ni “kazi iliyojaa maudhi!”
Khalil alipomaliza kusoma Biblia, na kulinganisha bayana maneno aliyosoma katika vitabu mbalimbali vya kiislamu, alishangaa sana alipogundua Biblia ilikuwa haina makosa na haijabatilishwa. Badala yake alishangaa juu ya mafundisho ya Biblia yaliyohusu msamaha na upendo usio na kosa, ulioonekana katika maisha na maneno ya Yesu. Alishangazwa hasa aliposoma kuwa Yesu mwenyewe aliwaonya wafuasi wake juu ya mateso na jinsi ilivyotokea miaka elfu mbili baadaye, vilevile ambavyo Yesu mwenyewe alikuwa amesema ingelitokea. Kusoma kwake kulimsaidia kuelewa kwa nini Wakristo wa Misri hawakuwa wakilipiza kisasi kabisa dhidi ya Waislamu na kwa nini kusamehe na kusahau kwao ilikuwa rahisi. Jinsi ambavyo alichukia kuisoma Biblia, ndivyo alivyojisikia kuupenda ujumbe na mafundisho yake.
Hata hivyo alikuwa na kazi ya kufanya, na aliendelea na uamuzi wa kutoka ndani kuthibitisha kuwa Yesu si Mungu, na hakuwahi kusulibiwa. Aliposoma Kurani kwa nia au lengo lake hili, alikusanya sifa na majina ya Mungu jinsi zilivyotajwa katika Kurani. Kisha akatafiti zaidi juu ya sifa za Yesu katika Kurani. Kulingana na Kurani, Mungu ndiye mwumbaji, mponyaji, mfadhili, mmoja pekee anayeweza kufufa wafu, mmoja pekee anayetenda miujiza, mmoja pekee atoaye hukumu ya haki na mambo kama hayo. Kwa mshangao Khalil aligundua kwamba huu ni mtazamo ule ule ambao Kurani inamtaja Yesu (Isa) ikimthibitishia kwamba, Yesu na Mungu ndiye ni yuleyule mmoja.
Khalil alipatwa na mashaka maishani mwake kiasi kwamba aliweza kujisikia mnyonge sana. Aliupenda sana Uislamu na kuamini kuwa njia pekee ya kumfikia Mungu ilikuwa ni kupitia Mohammad. Lakini ikiwa Yesu na Mungu ni yuleyule mmoja, sasa Mohammad ndiyo yupi na ni njia ipi ya kwendea mbinguni? Siku moja shehe wake bila ya kumtaarifu ujio wake aliamua kumtembelea nyumbani kwake, na hapo ndipo alipogundua kuwa utafito wote ambao Khalil alikuwa ameufanya ni kuhusu Uungu wa Yesu! Yaani kuwa Kurani si neno la Mungu n.k. Kwa kifupi ni kwamba hakukiamini kile alichokisoma kwa Khalil. Akamtahadharisha Khalil kuwa angeliweza kumwua endapo angemwambia Mwislamu yeyote kile alichokiandika. Pia akasema kuwa kuanzia pale alianza kumhesabu kuwa ni kafiri!
Hata hivyo, Khalil, hakuweza kuacha msimamo kwamba Ukristo ulikuwa ndiyo njia sahihi. Ili ajifunze zaidi aliamua kujiunga na kanisa. Na kwa vile alivyojulikana kuwa ni mtu mwenye tabia mbaya, mwenye msimamo mkali wa kiislamu, hakuna hata mmoja aliyemwamini. Kila mtu alikataa kukutana naye, hata na wachungaji! Jambo hilo lilimsikitisha sana, na hata akafikiri kwamba pengine aliamua kimakosa, pengine imani ya kikristo haikuwa ndiyo njia pekee ya kufika mbinguni. Hata hivyo sauti ndani yake ilimwambia kwamba asiwaangalie watu.
Siku moja alipokuwa akijaribu kupiga simu kwenye mgahawa, vitu vyake alivyokuwa navyo pale viliibiwa. Begi lake lililokuwa limebeba karatasi zake zote alizokuwa amefanya utafiti, Biblia yake na kitambulisho chake. Alishikwa na hofu kwa sababu mambo yote aliyokuwa ameyaandika yangeonekana ni maeneo ya kumkufuru Mungu. Alikimbilia nyumbani, akiwa amejaa mahangaiko na hofu. Aliporudi chumbani mwake, alianza kutubu kwa yale yote aliyokwisha kuyafanya na hata alifikiri kuwa Mungu alikuwa akimwadhibu kwa kuthubutu kufikiri kwamba Mohammad hakuwa ametumwa na Mungu na kwamba hata Kurani yenyewe haikuwa neno la Mungu. Alitubu, akatawadha au kunawa kulingana na sheria za kiislamu, kisha akachukua zulia lake ili aombe, lakini hata hakuweza kupiga magoti yake, wala hata kufungua mdomo wake kusema japo neno moja toka kwenye Kurani. Alikaa chini na kusema: “Mungu unajua kabisa kwamba ninakupenda, na ninajua kabisa kwamba unanitaka mimi nipite katika njia iliyo sahihi. Mungu nashindwa kuendelea kukupinga. Yale yote niliyoyafanya nilikuwa ninajaribu kukupendeza wewe. Tafadhali sana ninaomba unitoe nje ya giza hili nilimo.” Usiku ule Khalil alilala usingizi mnono ambao kwa miaka mingi hakuwa amelala hivyo. Katika ndoto alimwona mtu aliyemjia na kumwambia kwamba ni yeye ambaye Khalil amekuwa akimtafuta. Hata hivyo Khalil hakujua mtu huyo alikuwa ni nani. Mtu yule alimwambia kuwa, aangalie kwenye kitabu, yaani Biblia. Khalil alisema kuwa Biblia na karatasi zote zimepotea, ndipo mtu yule alimjibu na kumwambia: “Kitabu hakiwezi kupotea kamwe. Amka na ufungue kabati na utaiona, na zile karatasi zako zingine zitarudishwa kwako mwishoni mwa wiki.”
Khalil aliamka toka usingizini akafungua kabati yake. Biblia yake ileile ilionekana ndani ya kabati kwenye shelfu. Kwa kujua kuwa amemwona Yesu aliharakisha na kwenda chumbani kwa mama yake, akamwamsha, kisha akamwomba msamaha, kwa jinsi alivyokuwa mkali na alivyozoea kuitendea familia kwa miaka yote iliyopita. Kutafuta suluhu hakuishia hapa kwa familia yake tu, bali mara kulipopambazuka siku ileile tu asubuhi, Khalil alienda mitaani akiwasalimu marafiki na watu wengine. Hata aliweza kuwatafuta wafanyabiashara Wakristo wale ambao aliwahi kuwaibia, au hata kuwatendea vibaya, hao wote aliwaomba msamaha pia.
Miezi iliyofuata Khalil aliendelea kuimarika katika imani yake mpya. Polepole alianza kupata mazoea na matumaini na Wakristo waliokaa pale. Na alianza kushirikiana kanisani. Alibatizwa na akaendelea kusimama imara aliposhambuliwa kimwili na kutishiwa maisha yake. Maana alijisikia kana kwamba hakukuwa na bei yoyote kubwa ambayo ingeliweza kulipa kwa Yeye Yule aliyetoa kila kitu kwa ajili yake.