Umaskini ndani ya
kundi la wasomi unazidi kuingia kwa kasi ya ajabu kadili siku zinavyozidi
kwenda. Kundi la watu ambao wako kwenye hatari kubwa zaidi ni hasa wale walioko
kwenye “ajira”. Ukweli ni kwamba watu wengi walioko kwenye ajira, kitu pekee
wanachouza ili kupata kipato ni “nguvukazi” tena ambayo bado ni “ghafi”.
Uzoefu unaotokana na
tafiti zilizofanywa, unathibitisha kuwa zipo sababu nyingi zinazosababisha
waajiriwa na hasa wasomi wengi kuwa maskini. Lakini kubwa zaidi ni utamaduni wa
wasomi kuendelea kuuza nguvukazi ikiwa bado ni “ghafi” (nguvukazi ambayo
haijachakatwa).
Katika ulimwengu wa
“uwekezaji” nguvu kazi ghafi ni mtaji muhimu sana, ambao ukichanganywa na
mitaji mingine kama vile mashine, una uwezo wa kuzalisha bidhaa na huduma zenye
thamani kubwa kwa watu wengine.
Ukiuza nguvukazi
ghafi unakuwa umeuza “mtaji” wako: Waajiriwa wengi wanaendelea kukumbwa na adha
kubwa ya umasikini kutokana na kushindwa kutambua ukweli kwamba mara nyingi
kwenye maisha ya ajira wamekuwa wakifanya zaidi biashara ya kuuza mtaji
walionao (nguvukazi) kwa matajiri wenye hitaji la mitaji.
Ikumbukwe kuwa, ili
uweze kuzalisha bidhaa na huduma unahitaji mitaji ya aina mbalimbali ikiwemo
nguvu kazi ghafi. Ndiyo maana matajiri wengi wanapendelea zaidi kununua mitaji
kwa ajili ya kuzalisha bidhaa na huduma, ambazo huwapatia faida kubwa
sana.
Katika biashara
yoyote duniani, kuuza mtaji ni kufirisika jumla. Kwahiyo, umasikini tulionao
umetokana na kuuza mtaji wetu kila siku tunapotumikia ajira zetu. Kwa maana
nyingine waajiriwa wengi wanafirisika kila siku ya pale wanapokwenda kazini.
Watu wanaouza zaidi
nguvu kazi ghafi wanabaki kuwa maskini kutokana na ukweli kwamba thamani ya
nguvu kazi ghafi huwa ni ndogo sana, kwasababu inapatikana kwa wingi na haina
usumbufu kuipata.
Kwa mfano:
ukijifanya kutoza bei kubwa nguvu kazi yako; waajiri wengi watakukimbia na
chapuchapu watapata watu wengine wenye kuuza nguvu kazi ile ile kwa bei nafuu
sana.
Hivi ndivyo
unavyouza nguvu kazi ghafi: Unauza nguvu kazi ghafi pale unapotumia nguvu yako
kufanyakazi ya kuzalisha bidhaa na huduma ambazo siyo mali yako bali ni mali ya
mtu aliyekuajiri (mwajiri).
Unahitaji kufahamu
kuwa, mwajiri amekuajiri ili umpatie (umuuzie) nguvu kazi ambayo ni mtaji wa
kuzalisha bidhaa na huduma ambazo ni mali yake binafsi.
Kwakuwa bidhaa
zinazozalishwa ni za thamani kwa watu wengine, basi ni wazi kwamba watu hao
watampatia pesa mwajiri wako ili kupata bidhaa; LAKINI hawatakupatia pesa wewe,
kwa sababu wewe unayo nguvu kazi peke yake, ambayo siyo hitaji muhimu kwa wateja
wenye pesa zao.
Ukiuza nguvukazi
ghafi unauza “muda” wako: Kwakuwa umeajiriwa kwa madhumuni ya kutoa nguvu kazi
kwa mwajiri wako, basi thamani yako inapimwa kwa kuangalia muda unaoutumia
kufanya kazi.
Ili uweze kulipwa ni
lazima kila siku ufike kazini na kusajiri muda wako. Usipoonekana kazini hakuna
malipo yoyote, kwasababu muda wako utakuwa hujauwekeza kwa mwajiri.
Kwahiyo, unapouza
nguvu kazi ghafi basi ujue umeuza “muda” na binadamu wa kawaida hawezi kufanya
kazi zaidi ya masaa nane kwa siku. Masaa yote haya unafanya kazi bila kupumzika
na kuzalisha vitu vyenye thamani kubwa kuliko mshahara unaolipwa na mwajiri
wako.
Haijalishi, thamani
ya vitu vilivyozalishwa ni kubwa kiasi gani, mshahara wako unaolipwa unaendelea
kubaki pale pale kila mwezi. Hali hii ndiyo inakufanya wewe mwajiriwa kukosa muda
wa kufanya vitu vyenye kukuletea faida kubwa na mafanikio maishani, na hivyo
kuzidi kuwa maskini kadiri umri wako unavyoongezeka.
Ukiuza nguvukazi
ghafi huna cha kurithisha familia yako: Kama unauza nguvukazi ghafi siyo rahisi
kuirithisha kwa watu wako wa karibu, kwasababu nguvukazi kama ilivyo
haihamishiki kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Kama kitu hakihamishiki
ni vigumu pia kukibadilisha kwa urahisi kuwa pesa.
Hali hii inazidi
kutukumba wasomi na waajiriwa waliowengi kutokana na ukweli kwamba unakuta
umeajiriwa kwenye kampuni kubwa na una cheo kikubwa lakini ukifukuzwa au
kufariki, haitokei mke au mtoto wako akapewa nafasi kama uliyokuwa nayo na wala
familia haiwezi kutumia vyeti vyako vya elimu kuomba kazi.
Lakini kama ungekuwa
kwa mfano umeandika vitabu, hata ukifa hakimiliki ya kuendelea kuvichapisha na
kuviuza inahamishiwa kwa warithi wako na wanaendelea kufaidi sawa na wewe
ulivyokuwa ukifaidi.
Ukiuza nguvukazi
ghafi unapata hasara: Hasara kubwa unayoipata kutokana na kuuza nguvu kazi ni
pale unapoishia kuuza kitu kimoja tu! Nacho ni nguvu kazi.
Hali hii inakubana
kiasi kwamba unajikuta unalazimika kumtegemea mteja mmoja ambaye ni “mwajiri”
na inakuwa siyo rahisi kubadilisha mteja kadiri unavyotaka.
Endapo ukiamua
kuchakata nguvukazi yako na hatimaye kuzalisha bidhaa na huduma za thamani ni
rahisi kupata wateja wengi, ambao ndio huleta mapato makubwa.
Hasara nyingine
unayopata pindi unapouza nguvu kazi ghafi ni kuendelea kubaki kwenye kundi la
watu maskini ambao wanapata kipato hai (active income), yaani unapata pesa
unapofanya kazi tu, ukiacha pesa hakuna. Endapo, ikitokea unaumwa au umesafiri
basi ujue hakuna pesa itakayoingia.
Ndiyo maana unakuta
mtu ni tajiri leo kwasababu anafanya kazi ya kibarua, lakini baada ya muda
mfupi unakuta ni maskini na kwa waajiriwa ni hivyo hivyo wanakuwa na pesa
wakiwa bado kazini LAKINI wanapostaafu ajira wanarudia kwenye hali ya umaskini
jambo ambalo huwafanya watu wengi kufa miaka michache baada ya kustaafu.
Washindi dhidi ya
umaskini ni wale walioamua kuchakata nguvu kazi yao: Ukweli ni kwamba kila
mchakato wowote lazima utoe matokeo. Matokeo ya kuchakata nguvu kazi ghafi ni
“bidhaa au huduma” zenye thamani kubwa kwa watu wengine.
Kitendo cha
kuchakata nguvu kazi kinatokana na matumizi ya nguvu ya akiri pamoja na nguvu
ya mwili kwenye rasilimali kama ardhi, maliasili, ujuzi, pesa n.k, kwa lengo la
kupata mali au bidhaa kwaajili ya watu wengine.
Ukishapata bidhaa
zenye thamani (manufaa) kwa watu wengine, basi mara moja watakuletea pesa ili
kujipatia bidhaa na huduma muhimu kutoka kwako. Kadiri utakavyotengeneza bidhaa
nyingi na zenye thamani kubwa ndivyo utakavyopata pesa nyingi ambayo haina
kikomo.
Ni wakati sasa
tuamke na tujibidishe sana kwa kuandaa mazingira yatakayotuwezesha hasa sisi
wataka mafanikio kuuza “matokeo” ya nguvu kazi badala ya utamaduni wa sasa wa
kuuza nguvu kazi ghafi.
Ukweli ni kwamba,
unapokuwa mtu wa kuuza matokeo ya nguvu kazi ambayo ni bidhaa na huduma
mbalimbali, tayari unakuwa umemaliza kazi, kinachofuatia ni kuendelea kuuza
bidhaa hizo na wakati huo huo unakwenda kuwekeza muda wako huo kwenye kuzalisha
vitu vingine, huku akiendelea kufaidi matunda ya kazi aliyoifanya mwanzo.
Kwa watu wote na
hasa waajiriwa tunaotaka mafanikio makubwa, ni lazima kila mmoja wetu ajiwekee
tarehe ya mwisho ya kuacha kuuza nguvu kazi ghafi.
Kila mmoja akifikia
tarehe yake ya mwisho kuuza nguvu kazi ghafi, mara moja aanze kujikita katika
kubadili nguvu ya akiri na hisia kuwa bidhaa na huduma zenye kuwa suruhisho la
kudumu kwa matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wengine.
Kwakuwa utazalisha
bidhaa na huduma zenye kuwa na manufaa makubwa kwa watu wengine, basi na wao
watakupatia zawadi ambayo ni pesa, ili kujipatia kila kilicho bora kutoka
kwako. Tukiweza kufanikisha azima hii, basi tutatajirika kutokana na ukweli
kwamba watu wengi kwasasa wanataka bidhaa na huduma ambazo ni suruhisho ya
changamoto zao.
Wateja ni wengi
ambao wako tayari kununua kila kitu kitakachozalishwa ilimradi kina thamani
kwao, kwa hiyo soko ni kubwa. Nchi yetu inapokaribia kuingia uchumi wa kati,
mahitaji ya bidhaa na huduma zitokanazo na nguvu ya akiri/fikra zitazidi
kuongezeka.
Bidhaa zenyewe ni
kama vile muziki, sanaa, vitabu, program za mafunzo ya
ujasiriamali/biashara/afya/kilimo/majengo pamoja na machapisho juu miongozo
mbalimbali ya uwekezaji katika mambo ya utalii, uwindaji, gasi, mafuta, madini,
kilimo n.k.
Uchumi wa watanzania
ukizidi kuongezeka na idadi ya wasomi ambao ndio wahitaji wakubwa itazidi
kuongezeka huko tuendako ~ Kwa hiyo ewe mtanzania mwenzangu, anza kuchukua
hatua leo, wakati ni sasa.