Alhamisi, 27 Aprili 2017

UTAWALA WA KANISA (9)

Utawala Kanisani
Pia ni dhahiri kabia kutokana na maandiko yaliyotajwa hapo nyuma kwamba, wazee/wachungaji/waangalizi hawajapewa usimamizi wa kiroho tu kwa kanisa, bali pia wamepwa mamlaka ya kutawala. Yaani, wazee/wachungaji/waangalizi ndiyo wasimamizi na wenye mamlaka, na washirika wanapaswa kuwatii.
Watiini wenye kuwaongoza na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu (Waebrania 13:17).
Lakini, hakuna Mkristo anayetakiwa kumtii na kumnyenyekea mchungaji ambaye si mtii wala mnyenyekevu kwa Mungu, bali anapaswa kutambua kwamba hakuna mchungaji aliye mkamilifu.
Wachungaji/wazee/waangalizi wana mamlaka juu ya makanisa yao, sawa na jinsi ambavyo baba ana mamlaka juu ya familia yake.
Basi imempasa askofu [mchungaji/mzee] awe mtu asiyelaumika. … Mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) (1Timo. 3:2-5).

Paulo akaendelea kusema hivi:
Wazee [wachungaji/waangalizi] watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha (1Timo. 5:17).
Ni dhahiri kwamba wazee wanapaswa kutawala au kusimamia kanisa.
Wazee Kinyume Na Maandiko
Makanisa mengi yanaamini mpango wao wa utawala ni wa KiBiblia kwa sababu wana kundi la wazee wanaosimamia, lakini, tatizo ni kwamba wazo lao la wazee si sahihi. Wazee wao huchaguliwa kila mara na hubadilishana nafasi kutoka katika kusanyiko. Mara nyingi wanaitwa “Baraza la Wazee.” Lakini watu hao si wazee kulingana na tafsiri ya Biblia. Tukitazama sifa ambazo Paulo anataja kwa ajili ya mtu kuwa mzee, hilo linaonekana wazi kabisa. Paulo aliandika kwamba mzee hushikilia nafasi ya kudumu ya kufundisha na kuhubiri na kusimamia katika kanisa, na kwa maana hiyo analipwa (ona 1Timo. 3:4-5; 5:17-18; Tito 1:9). Katika watu wanaosemekana ni “Baraza la Wazee” kwenye makanisa mengi, ni wachache sana – kama wapo basi – ambao wanatimiza sifa hizo. Hawalipwi; hawahubiri wala kufundisha; si wafanya kazi wa kanisa; na wala hawajui jinsi ya kusimamia au kutawala kanisa.
Utawala wa kanisa ambao si wa kiMaandiko ndiyo sababu ya matatizo mengi sana kanisani kuliko kitu kingine chochote. Wakati watu wasiostahili wanaposimamia kanisa, shida ziko njiani. Mlango hufunguka kwa ajili ya vurugu, faraka na hata kuangamia kabisa kwa kanisa. Mpango wa utawala wa kanisa ambao si kulingana na Maandiko ni kama mkeka wa ukaribisho kwa Shetani.
Natambua kwamba nawaandikia wachungaji wa makanisa jengo na wa makanisa yanayokutanikia nyumbani. Baadhi ya wachungaji wa makanisa jengo wanaweza kuwa wanaongoza makanisa ambayo mfumo wa uongozi si wa kiMaandiko, ambapo wazee huchaguliwa kutoka katika kusanyiko. Mifumo hiyo haiwezi kubadilishwa bila ya kuleta vurugu.
Ushauri wangu kwa wachungaji kama hao ni huu: Fanya vizuri uwezavyo kwa msaada wa Mungu kubadilisha mfumo wa utawala wa kanisa, na uvumilie vurugu za muda zitakazotokea, maana vurugu za kudumu zinazokuja baadaye hazitaweza kuepukika kama hutafanya chochote sasa. Ukifanikiwa kuvumilia vurugu za muda, utajikuta umeepukana na vurugu zote za baadaye. Ukishindwa, anzisha kanisa jipya mahali na kufuata mpango wa Biblia.
Japo hilo linaumiza, mwisho wa siku utazaa matunda mengi zaidi kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Kama wale wanaotawala kanisa lako kwa sasa ni wafuasi wa kweli wa Kristo, unayo nafasi nzuri tu ya kufanikiwa kuwashawishi kubadilisha mfumo, kama utaweza kuwaonyesha kutoka Maandiko kinachopaswa, na jinsi ya kufanya hayo mabadiliko yanayohitajika sana.
Wazee Wengi Je?
Kuna wenye kuonyesha kwamba katika Maandiko wazee hutajwa katika wingi. Hoja hapo ni kwamba kuwa na mzee/mchungaji/mwangalizi mmoja anayesimamia kundi si kimaandiko. Huo si ushahidi wa kutosha kuamua kitu hicho. Kweli Biblia inataja kwamba, katika miji fulani fulani, waliokuwa wanasimamia kanisa walikuwa zaidi ya mzee mmoja, lakini haisemi kwamba hao wazee walikuwa wote wanalingana kimadaraka katika kusanyiko hilo. Kwa mfano: Wakati Paulo alipokusanya wazee kutoka Efeso (Matendo 20:17), ni dhahiri kwamba hao wazee walitoka kwenye mji ambao pengine kanisa lilikuwa na washirika maelfu kwa makumi elfu (ona Matendo 19:19). Basi, yawezekana kulikuwa na makundi mengi katika Efeso, na inawezekana kila mzee mmoja alisimamia kanisa moja.
Katika Maandiko, hakuna mahali popote ambapo Mungu aliita kamati ifanye kazi yoyote. Wakati alipotaka kutoa Waisraeli Misri, alimwita Musa – mtu mmoja – awe kiongozi. Wengine waliitwa kumsaidia Musa, lakini wote walikuwa chini yake kimadaraka, nao kama yeye walikuwa na majukumu binafsi juu ya kundi fulani la watu. Mtindo huo unapatikana katika Maandiko mara kwa mara. Wakati Mungu anapokuwa na kazi, anamwita mtu mmoja kuwajibika, kisha anamwita mwingine kumsaidia huyo.
Basi, haiwezekani kwamba Mungu anaweza kuita kamati ya wazee wenye mamlaka sawa ili kusimamia kila kanisa dogo linalokutania nyumbani, la watu ishirini. Hapo ni kama mwaliko kwa watu kuvurugana!
Lakini – hiyo haimaanishi kwamba kila kanisa la nyumbani lisimamiwe na mtu mmoja tu – mzee mmoja. Ila, maana yake ni kwamba, kama kuna mzee zaidi ya mmoja katika kanisa, yule ambaye ni kijana na asiyekomaa kiroho awe tayari kunyenyekea chini ya yule aliye mkubwa na aliyekomaa kiroho. Kulingana na Maandiko, makanisa ndiyo yanatakiwa kuwa maeneo ya kufundishia wachungaji vijana/wazee/waangalizi – si Shule za Biblia. Basi, inawezekana kabisa na inatakiwa kwamba wawepo wazee/wachungaji/waangalizi kadhaa katika kanisa la mahali, na wale ambao ni wadogo kiroho wafundishwe na wale ambao ni wakubwa kiroho.
Mambo hayo utayaona hata katika makanisa yanayodaiwa kusimamiwa na wazee “wanaolingana”. Yupo mmoja ambaye kila mara anapewa nafasi kubwa na wale wenzake. Au utakuta kuna mmoja ambaye ni kama mkuu, huku wengine wakiwa watazamaji tu. Vinginevyo kutakuwa na vurugu tu. Ni ukweli pia kwamba hata kamati huchagua mtu mmoja kuwa mwenyeketi. Wakati kundi la watu wanaolingana wanapochukua hatua ya kufanya kitu, wanatambua kwamba lazima kuwe na kiongozi mmoja. Ndivyo ilivyo pia kanisani.
Tena, Paulo analinganisha majukumu ya wazee na majukumu ya baba katika 1Timotheo 3:4, 5. Wazee lazima wasimamia nyumba zao, la sivyo hawafai kusimamia kanisa. Lakini tujiulize: Nyumba yenye baba wawili wenye mamlaka sawa itasimamiwaje? Bila shaka kutakuwa na matatizo.

Wazee/wachungaji/waangalizi wanapaswa kuunganika katika kusanyiko la mahali ili kuwe na uwajibikaji mmoja kwa mwingine miongoni mwao, ili kama kuna tatizo, waweze kusaidiana. Paulo aliandika kuhusu “wazee” (ktk 1Timo. 4:14). Pengine maana yake ni mkutano au mkusanyiko wa presbuteros (wazee) pamoja na watu wengine wenye karama za huduma. Kama kuna mtume mwanzilishi, yeye pia anaweza kutoa msaada ikiwa kuna matatizo katika kusanyiko, yanayotokana na mzee aliyekosea. Wachungaji wenye makanisa jengo wanapopotoka, matokeo yake huwa ni matatizo makubwa kwa sababu ya mfumo wa kanisa. Kuna jengo na taratibu za kufuata. Lakini, makanisa yanayokutanika nyumbani yanaweza kuvunjwa mara moja wakati mchungaji anayehusika anapopotoka. Washirika watajiunga na kundi lingine. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni