Alhamisi, 27 Aprili 2017

NAFASI YA MCHUNGAJI KATIKA KANISA (8)

Nafasi Ya Mchungaji
Tumeona katika sura mbili zilizopita mlinganisho kati ya nafasi ya mchungaji KiBiblia na jinsi ilivyo kwa kawaida. Ila, kuna mengine tena ya kusema juu ya huduma ya mchungaji.
Ili kuelewa vizuri kile ambacho Biblia inafundisha kuhusu nafasi ya mchungaji, tunahitaji kuelewa maneno matatu muhimu sana ya Kiyunani. Hayo ni (1) poimen, (2) presbuteros na (3) episkopos. Yanatafsiriwa hivi: (1) mchungaji wa mifugo au mchungaji wa watu, (2) mzee, na (3) mwangalizi au askofu.
Neno poimen linapatikana mara kumi na nane katika Agano Jipya, nalo linatafsiriwa mchungaji wa mifugo mara kumi na saba, na mchungaji wa watu mara moja. Neno lenyewe kama kitendo – poimaino – linapatikana mara kumi na moja, na mara nyingi linatafsiriwa mchungaji wa mifugo.
Neno presbuteros linapatikana mara sitini na sita katika Agano Jipya. Mara sitini limetafsiriwa mzee au wazee.
Neno episkopos linapatikana mara tano katika Agano Jipya, na linatafsiriwa mwangalizi mara nne. Biblia yetu ya Kiswahili inatumia neno askofu.
Hayo maneno yote matatu yanataja nafasi moja katika kanisa, nayo yanatumika kwa kubadilishana. Popote ambapo mtume Paulo alianzisha makanisa, aliweka wazee (presbuteros) ambao waliwaacha kushughulika na makanisa yamahali (ona Matendo 14:23; Tito 1:5). Majukumu yao yalikuwa kusimamia (episkopos) na kuchunga (poimaino) makundi yao. Angalia mfano katika Matendo 20:17, kama ifuatavyo:
Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee [presbuteros] wa kanisa.
Je, aliwaambia nini hao wazee wa kanisa?
Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi [episkopos] ndani yake, mpate kulilisha [poimaino] kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe (Matendo 20:28.
Ona jinsi hayo maneno matatu yanavyotumika kwa kubadilishana. Si nafasi tatu tofauti. Paulo aliwaambia wazee kwamba wao ni wasimamizi au waangalizi ambao walipaswa kufanya huduma yao kama wachungaji.
Petro naye aliandika hivi katika waraka wake wa kwanza:
Nawasihi wazee [presbuteros] walio kwenu, mimi niliye mzee mwenzi wao na shahidi wa mateso ya Kristo na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni [poimaino] kundi la Mungu lililo kwenu na kulisimamia, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka (1Petro 5:1-4.
Petro aliwaambia wazee wawe wachungaji kwa makundi yao. Kitendo hapa kinachotafsiriwa mchungaji kinatumiwa kama jina katika Waefeso 4:11.
Naye [Yesu] alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu.
Hilo linatufanya tuamini kwamba wazee na wachungaji ni kitu kimoja.
Pia, Paulo alitumia neno mzee (presbuteros) na mwangalizi au askofu (episkopos) kwa kubadilishana, katika Tito 1:5-7.
Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru. … Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshtakiwa neno.

Hivyo, si rahisi kujenga hoja kwamba nafasi ya mchungaji, mzee na mwangalizi ni tatu tofauti. Basi, chochote kilichoandikwa kuhusu wasimamizi na wazee katika nyaraka za Agano Jipya kinawahusu na wachungaji pia.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni