Mtu anapozaliwa mara ya
pili kwa kumkaribisha Bwana Yesu ndani ya maisha yake, huingia katika maisha
mapya na kutembea katika uongozi wa Mungu aliye hai. Mtu huyu aliyezaliwa mara
ya pili anapofikia mahali pa kukutana na Nafsi ya tatu ya Mungu (Roho
Mtakatifu) ana kwa ana katika kipimo cha kufurika (tele), huingia katika ufunuo
mpya na maisha mapya ya kushuhudia uthihirisho wa nguvu za Mungu katika maisha
yake. Katika maisha haya ya kutembea na Roho Mtakatifu, ni vema kila mwamini
apate mafundisho yaliyo sahihi jinsi ya kutembea na Roho Mtakatifu huyu wa
Mungu ili kwa kufanya hivi “moto
uendelee kuwaka ndani yake daima pasipo kuzimika”(Law 6:12) hebu sasa
tuendelee kuwa katika Roho ili tujifunze yale yatupasayo kufanya baada ya
kupokea ubatizo huu wa Roho Mtakatifu udhihirishwao na ishara ya lugha mpya.
JENGA TABIA YA KUMWOMBA
MUNGU.
Akawaambia mfano ya kwamba
imepasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa (Luka 18:1). Ni vyema
ufahamu kuwa maombi ni mkono uwezao kuyaleta mapenzi ya Mungu duniani, na kila
adumuye katika kuomba hudumu katika ushirika (Fellowship) na Mungu Baba, Mwana
na Roho Mtakatifu. Katika maombi tunavuta hazina ya Mungu iliyofichika kutoka
katika ulimwengu wa Kiroho kuja katika ulimwengu unaoonekana. Maombi n kusema
na Mungu Baba kama vile baba wa dunia anavyoweza kusema na watoto wake
awapendao. Sehemu nyingine Yesu alipokuwa anaongea na wanafunzi wake
aliwakazania kuwa inawapasa kuomba ili wasije kuingia majaribuni. Maombi
yanamfanya mtu ayaone majaribu hata kabla hayajatokea, badala ya kushitukizwa
na majaribu hayo. Yesu alipokuwa anasema ombeni ili msije mkaingia majaribuni,
hakuwa na maana iliyo nyepesi bali alikuwa anawatahadhalisha kuwa waangalie
wasije wakaingia majaribuni na kushindwa. Nasema hivi kwani kuingia majaribuni hilo si jambo lililo geni katika kanisa na
hata tunasoma kuwa; “Ni Furaha tupu mtu
anapoangukia katika majaribu mbalimbali” (Yak 1:2) kwa hiyo maombi ni
silaha zinazomwezesha mwamini kutoka akiwa mshindi, baada ya kuingia au
kuangukia katika majaribu. Mtu anapoingia majaribuni na akishindwa kuendelea na
hali ya kiroho aliyokuwa nayo, basi husababisha ubaridi mkubwa ndani ya roho ya
mtu, na kwa ubaridi huo Roho yule aliyempokea huzimika ndani yake. Roho
anapozimika ndani si rahisi tena kulisikia bubujiko la uzima ndani ya mtu na
hapo huyapoteza maisha ya ushindi yaletwayo na Roho Mtakatifu. Kwa maneno haya
nataka kusema kuwa mara tu baada ya kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu anza
kujenga tabia ya kuomba. Hii ni hatua muhimu sana katika maisha haya mapya ya
kutembea na Roho wa Mungu. Maombi hayatakiwi kuwa mzigo, yaani kitu cha
kujilazimisha badala yake lazima iwe tabia ya mwanafunzi. Ninaposema tabia
ninapenda kuyafananisha na kuvuta hewa ya oxygen. Mtu havuti hewa kwa
kujilazimisha bali hufanya hivyo kwa sababu ni raha tena ni afya tunapofanya
hivyo. Tunapojenga tabia hii ya kuomba ni lazima tuombe kwa ufahamu pia tuombe
kwa kunena kwa lugha mpya. Maana tukinena kwa lugha tunakuwa tunajijenga kama
tulivyotangulia kusema katika sura zilizopita. Kumbuka kuwa hujapokea Roho
Mtakatifu ili tu unene kwa lugha, bali umepokea Roho Mtakatifu ili uwe na
manufaa katika kuujenga ufalme wa Mungu.
DAMU KATIKA USHIRIKA WA
ROHO NA WATU WA MUNGU.
“Na jamii ya watu
walioamini walikuwa na moyo mmoja na Roho mmoja na wala hapana mmoja aliyesema
ya kuwa kitu chochote alichonacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu
vyote shirika” (Matendo 4:32)
Katika maisha haya mapya
uliyonayo, unahitajika kujengwa na kujifunza zaidi mafundisho haya na
kuimarika, vitu hivi vinaweza kupatikana
pale watu wa Mungu wanamtafuta Mungu katika Roho na kweli, maana ndivyo
yesu alivyomwambia yule mama Msamaria. Alimwambia wakati unakuja ambao
wamwabuduo Mungu halisi watamwabudu Baba katika Roho na kweli (Yohana 4:23).
Wewe sasa ni kondoo mchanga mwenye moto wa kuijua kweli ya Mungu, basi tafuta
malisho (chakula cha kiroho) toka kwa mchungaji wa kweli, maana huyo ana
uchungu na maisha yako ya kiroho. Nasema hivyo kwani ni vema ujitambue kuwa u
msafiri wa kwenda mbinguni na kwa sababu hiyo lazima utafute gari
litakalokupeleka mbinguni. Mchungaji ni sawa na gari la kuwapeleka watu
mbinguni, tatizo linalotokea ni kuwa yako magari (wachungaji) ambayo
yameegeshwa mahali na hayatembei, ni jambo la kuchekesha kuwaona wakristo
wengine wakiingia mle ndani na huku wanategemea kusafiri! Kama kweli u msafiri
wa mbinguni tafuta gari (mchungaji) linalotembea.
Kwa maneno haya nataka
kukutafutia malisho zaidi au mahali utakaponeemeka kiroho na mafundisho yaliyo
hai. Katika ushirika huu, ni vema usifungwe na madhehebu, bali uwe tayari
kukumbatiana na mwamini yeyote wa dhehebu lolote, maana hao ndio ndugu zako wa
kweli. Pia ukumbuke kupima yale uliyoyasikia kama yanaendana na neno la Mungu,
ni vema uwe karibu na yule aliyekabidhiwa kwako kama baba yako wa kiroho.
VIPINGE NA KUVISHINDA
VIKWAZO VYOTE ATAKAVYOKULETEA SHETANI.
“Lakini
neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye
yeyote kwa jina hili, wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha
kwa jina la Yesu. Petro na Yohana wakawajibu wakamwambia, kwamba ni haki mbele
za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe. Maana sisi
hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia”
Matendo 4:17-20
Mtu anapompokea YESU kuwa
Bwana na Mwokozi wa maisha yake, husababisha chuki na hasira kubwa kutoka kwa
shetani dhidi yake. Tendo la mtu kuamua kutoka kwenye ufalme wa giza na kuingia
kwenye UFALME WA MUNGU, humsisimua shetani mnoo hata kumfanya aende vitani
dhidi ya mwamini huyu mpya. Ili katika vita hiyo aweze kumrejesha tena mikononi
mwake.
Katika vita hii ya shetani
dhidi ya mwamini, ibilisi hutuma mishale ya kila namna ili kumwangusha mtu, na
hachoki katika mapambano hayo, ila siku kwa siku huzidisha makali ya mapigo
yake kwa mwamini. Kwa kusema hivi nina maana kuwa kila mwamini anapopiga hatua
moja mbele kiroho, shetani naye huongeza mapigo yake ili ikibidi kumteketeza
mtu wa Mungu. Mwamini anapobatizwa kwa Roho Mtakatifu huwa amepiga hatua kubwa
mno kiroho, hatua ambayo huutetemesha sana ufalme na mamlaka ya shetani.
Kwa sababu hii, mtu
anapojazwa Roho Mtakatifu kwa kipimo cha tele, atakumbana na matatizo ambayo
hayakuwepo kabla ya kuingia katika hatua ya kuzaliwa upya. Majaribu yatakuwa
yamezidishwa ukali wake kama alivyofanya mfalme Nebukadneza kwa kina Shadraka ,
Meshaki na Abednego. Biblia inatuambia kwamba Nebkadneza alizidisha moto wa
tanuru mara saba kuliko ulivyokuwa kawaida yake, ili uwateketeze watu wa Mungu
(Danieli 3:19) kwa vijana hawa watatu wa kiebrania, shetani aliwatumia watu
mbalimbali hata wafalme ili kushusha imani yao. Hata kwako wewe pia anaweza
kutumia vitu kama hivyo, au ndugu zako, marafiki na hata viongozi wa dhehebu
lako ili kumpinga Roho Mtakatifu uliyempokea, basi kwa vyovyote vile
itakavyokuwa lazima uyashinde majaribu na vishawishi vyote vile vya yule mwovu.
Kumbuka kuwa hata mitume walipita katika majaribu makali mno mara tu baada ya
kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, wengine walipigwa kwa mawe, au kukatwa shingo kwa
msumeno, au kuwekwa ndani ya mafuta yaliyochemka hadi kufa. Ni jambo la Baraka
na la kutia moyo kuona kuwa katika mambo yote hayo waliyofanyiwa na shetani,
wao walikaza uso wao kama gumegume na kuchagua hata kufa kwa ajili ya imani
waliyopokea, kuliko kuishi wakiwa wameasi imani waliyopokea kwa njia ya mauti
ya mwana pekee wa Mungu pale msalabani.
Niseme tena kuwa sasa kwa
kuwa umejazwa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya, endelea kuvipiga vita
vile vyema vya imani maana katika kila gumu litakalokupata, hutakuwa peke yako;
bali yule aliyeanza kazi njema ndani yako ndiye atakayekushindia. Kumbuka kuwa
kila utakapompinga shetani atakimbia, na kwa kufanya hivyo utaendelea
kumpendeza Mungu aliyekununua.
ILI UIMARIKE ANZA KUTOA
USHUHUDA WA KUFUFUKA KWA BWANA YESU.
Dunia leo ina watu zaidi ya
bilioni moja wanaojiita wafuasi wa Kristo. Watu hawa wanadai kuwa ni mashahidi
wa Bwana wetu Yesu Kristo na ya kwamba wanao ushuhuda wa Yesu kwa dunia nzima.
Ukichukua maana halisi ya ushahidi kwa kuzingatia lugha kongwe kwa mfano
kiyunani, utaona kuwa watu hawa si mashahidi.
Katika kiyunani neno
shahidi linaitwa Martyria yaani kufa au kuuawa kwa ajili ya kitu fulani kwa
hiyo shahidi wa Yesu ni yule anayeusimamia ushuhuda wake pasipo kuyumbishwa
hata kama ikibidi auawe kwa sababu ya ushuhuda huo. Shahidi na yule anayesimamiwa
kwa ushahidi huo ni kitu kimoja, hawatenganishwi kwa namna iwayo yeyote ile.
Kwa kuwa wakristo wanatakiwa kuwa mashahidi wa Yesu, ni lazima watene na kuishi
kama Yesu anavyotaka na kuyashikilia maungamo yao hata mauti.
Tunapowaangalia wakristo wa
leo, utaona kuwa hawafai kuitwa mashahidi, maana yale Kristo anayoyakataa ndiyo
wanayoyafanya. Dhambi imeharibu ushahidi wao kwa ukweli huu, unaweza kuona kuwa
wakristo hawa hawatoi ushuhuda wa kufufuka kwa Yesu, bali hutoa ushuhuda wa
kufa kwa Yes utu. Na mtu anayetoa ushuhuda wa Yesu na kuishia hapohapo tu
asiendelee mbele, huyo ni shahidi wa uongo. Kwa maneno haya tunaweza kusema
kuwa kuna mashahidi wa uongo wa Yesu zaidi ya bilioni moja duniani, ukiwaondoa
wale wanaomwabudu Yesu Kristo kwa roho na kweli.
Mtu anaposhuhudia juu ya
mauti ya Bwana pamoja na kufufuka kwake, huyo anaudhihirishia ulimwengu kuwa
yeye anamwabudu yesu aliye hai anaweza kufanya mambo yafuatayo;-
-
Yesu aliye hai analeta ondoleo la dhambi.
Tayari nimekwambia kuwa kuna zaidi ya wakristo wa uongo 1,000,000,000 duniani.
Watu hawa humwabudu Yesu aliyekufa, maana ni yesu aliyekufa tu ndiye anayeweza
kuabudiwa na majambazi, waasherati, wazinzi, walevi, waongo,wavutaji wa unga,
wezi na watu watendao mambo ya jinsi hiyo. Hata hivyo katika dunia hii, wapo
wanao mwabudu Yesu kwa roho na kweli, watu hawa hawakwenda na Yesu hadi
kaburini tu, bali walifufuka pamoja naye! Kufa na kufufuka pamoja na Bwana ni
kupokea ondoleo la dhambi na kuzaliwa mara ya pili kwa kupokea asili mpya
kutoka kwa Mungu aliye hai. Yeye alipokea ondoleo la dhambi hawi tena mtumwa wa
mwili na tamaa za kidunia, bali hupokea asili mpya ya kiMungu na kwa msaada wa
Roho wa Mungu huishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi.
-
Yesu aliye hai hutenda miujiza, ishara na
maajabu “Nao wale wakatoka, wakahubiri
kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibisha lile neno kwa ishara
zilizofuatana nalo” (Marko 16:20) ni vema tufahamu kwamba kuna imani na
dini nyingi mno duniani, katika imani au dini hizo zimesimamia kati ya imani
hizo ni hii ya ukristo, chini ya kinara au nguzo yake iitwayo YESU KRISTO.
Imani hii imekuwa ya pekee mno ukilinganisha na zile zingine zilizopo, naweza
kusema kuwa ni imani iliyo hai. Maana kila inapokigusa kitu kilichokuwa katika
hali ya kufa kiroho au kimwili, uhai mpya uliweza kuonekana ndani ya kitu kile.
Mtu aliyepoteza uhai wake kiroho na kupotea katika dhambi, anapoamini na
kujiunga na imani hii; roho yake hufufuliwa na kuwa hai tena, na kwa mgonjwa
aliyekata tamaa ya kuishi hurejeshewa afya yake kwa kumwamini Yesu huyu aliye
hai. Miujiza na ishara zinazotokea katika imani hii ya ukristo na maajabu
mengine mengi huifanya imani hii ya ukristo kuwa ya pekee kuliko imani nyingine
zote duniani. Mhubiri mmoja alisema kuwa ukristo pasipo miujiza ni sawa na
imani nyingine zilizokufa na hii ni kweli kabisa. Na hapa uelewe kuwa miujiza
tunayoizungumzia ni pamoja na ule wa mtu kuzaliwa mara ya pili na kuachana na
dhambi. Kwa kumalizia hebu tuseme kuwa ni vema uanze sasa kutoa ushuhuda kwa
watu wengine, ukiwaeleza kule Yesu alikokutoa , na pale alipokuweka sasa, pale
atakapokuweka baada ya maisha haya na jinsi anavyokupa ushindi siku hadi siku
-
Toa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana “Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa
Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao” (Matendo 4:32) baada
ya kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, ile chemchem inayojaa hata kufurika, hatua au
jambo jingine hutokea kutoka katika chemchem hiyo. Kwa maneno mengine ni kuwa
ndani yako sasa kuna mito ya Roho Mtakatifu iliyojaa uzima kwa ukweli huu ni
lazima ufahamu kuwa mito sio kwa ajili ya mtu mmoja peke yake, bali mito ni
lazima ilete maendeleo na mabadiliko kwa wale wote watakaofikiwa na mto huo.
Mtu anapoamua kufunga chanzo au pale mto unapoanzia, huyo ni muuaji; maana
atasababisha hasara kubwa ikiwa ni pamoja na mauti kwa wote waliokuwa
wakiutegemea mto huo. Mto ni lazima uachwe utiririke wakati wote pasipo
kufungwa.
-
Kutoa ushuhuda ni sawa na kuuacha mto
ububujike daima neno hili kushuhudia linatokana na neno ushuhuda, shuhuda na
shahidi ni maneno ambayo unapoyachambua hatima yake unapata kitenzi hiki,
kushuhudia , shahidi ni mtu aliyekuwepo jambo lilipokuwa linatokea, ni mtu
anayelifahamu jambo kwa usahihi na kwa mapana marefu yake. Kwa hiyo yale
shahidi atakayo yasema kuhusiana na jambo fulani alilolishuhudia, ndiyo
tunayaita ushuhuda, yaani maelezo yaliyo sahihi na hai yaliyotolewa na yule
aliyekuwapo wakati wa kutukia jambo hilo. Ninaposema maelezo yaliyo hai, hapa
nina maana kuwa ushuhuda kamwe si hadithi za uongo, au habari za kutungwa, bali
ni maelezo ya kweli yanayothibitishwa na nafsi ya mtu, roho yake na mwili wake
pia.
-
Tumia mamlaka uliyonayo kwa jina la Yesu. “Lakini Petro akasema, mimi sina fedha,
wala dhahabu, lakini nilichonacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa
Nazareti, simama uende” (Matendo 3:6) kwa miaka mitatu, wanafunzi wa Yesu
walikuwa wameshuhudia matendo makuu ya Mungu yaliyotendwa kwa mkono wa Bwana
wao na mwokozi wa ulimwengu Yesu Kristo. Biblia inatuambia kuwa, kwa mamlaka
Yesu aliamuru pepo wabaya nao wakamtii, vilema, viziwi, bubu, na wenye maradhi
mengi waliponywa pale Yesu alipoamuru ifanyike hivyo kwa mamlaka aliyokuwa
nayo. Kwa mamlaka aliweza hata kuamuru upepo na dhoruba vitulie navyo vikatulia.
Wanafunzi walipoona haya yakitendeka walishangaa mno, huku wakitamani mamlaka
ile iliyotenda kazi ndani ya Bwana wao hata wakafikia hatua ya kumwambia Yesu
kuwa awaongezee imani! Yesu alipopaa aliwaacha wanafunzi wake katika huzuni
nzito huku wakiwa wamevunjika moyo, haya yalitokea kwani waliamini kuwa kwa
kuondoka kwa Bwana wao basi na ile mamlaka nayo inmeondoka pamoja naye.
Kujihisi kupungukiwa huku kuliendelea sana hadi pale hadi pale walipobatizwa
Roho Mtakatifu mara tu baada ya kumpokea Roho Mtakatifu kwa kipimo cha tele.
Moto ulilipuka tena ndani yao na wakapata ufunuo mpya wa kuitumia mamlaka
iliyokuwa ndani yao, angalia hapa; KWA MUDA MREFU Petro na Yohana walikuwa
wanampita huyu kiwete akiwa katika mlango wa hekalu pasipo kumsaidia. Lakini
baada ya ubatizo wa Roho Mtakatifu uliotokea katika sura ya pili ya kitabu cha
matendo ya mitume, sasa Petro anajitambua kuwa yeye ni nani katika mitume, tena
anatambua kuwa mamlaka ileile iliyotenda kazi ndani ya Yesu ipo ndani yao.
Nasema hivyo kwani Yesu aliwaambia katika Luka 10:19 kuwa “Tazama, nimewapa
amri ya kukanyaga nyoka, nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu
kitakachowadhuru “Kwa ufunuo huo mpya Petro aliweza kumwendea yule kiwete na
kumwamuru atembee katika jina la YESU na ikatendeka hivyo. Ni vema ufahamu kuwa
sasa umefanya safari ya kuendea mti wa uzima na ile mana iliyofichwa, katika
safari hii mambo hayatakwenda kama unavyotaka, bali daima shetani atataka mambo
yaendekama atakavyo yeye, basi kama utakunja mikono na kujihisi mnyonge na
duni, utashindwa kuishi maisha ya ushindi, kumbuka kuwa yeye ashindaye ndiye
atakayepewa kula matunda ya mti wa uzima ulio katika bustani ya Mungu (Ufunuo
2:7b). ili upate ushindi ni lazima ujifahamu kuwa wewe ni mtoto wa Mungu na
mrithi pamoja na Yesu Kristo nay a kuwa una haki ya kisheria ya kutumia mamlaka
iliyo katika jina la Yesu Kristo. Kwa hiyo unapoona hali isiyobariki
inajitokeza katika safari yako, iamuru kuwa ihame katika jina la Yesu na kwa
kutumia jina hilo, fungulia ile hali unayotaka iwepo. Kwa maneno haya napenda
ufahamu kuwa mambo hayatakuwa marahisi kila wakati maishani mwako; hivyo pale
yanapokwenda visivyo, tumia mamlaka kukemea na kuharibu kila kilicho kiovu, na
itatendeka kama ulivyoamuru. Wakati wa kufanya hayo usijisikie upweke na duni,
ujue kuwa uko pamoja na Yesu na kwa jina lake kila goti litapigwa na kila ulimi
utakiri kuwa YESU NI BWANA. Baada ya kubatizwa na Roho Mtakatifu ishi maisha
matakatifu. “hata masaa matatu baadae
mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea, Petro akamjibu, niambie
mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema ndiyo, kwa thamani hiyo, Petro
akamwambia, imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Anagalia, miguu
yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. Mara akaanguka
miguuni pake akafa” (Matendo 5: 7-10) tunasoma kuwa Mungu hapo zamani
katika Agano la kale aliishi katika hema la ushuhuda au katika hekalu. Katika
Agano jipya, Mungu anaendelea kuishi katika hema au katika hekalu, ila safari
hii si katika hema iliyojengwa kwa mikono ya wanadamu, bali hema lile
alilolijenga yeye mwenyewe yaani mwili wa Kristo. Na Yesu alipopaa mbinguni
alimwomba Mungu baba ili Roho Mtakatifu aje duniani na kuchukua nafasi
aliyoiacha, naye akashuka siku ya hamsini baada ya kufufuka kwake. Katika sura katika
sura ya mwanzo ya kitabu hiki tumejifunza juu ya kusudi la kuja kwake, basi
alikuja ili kuyakamilisha makusudi haya, na alifanya au anafanya hivyo pale
anapopata maskani hiyo si kwenye majumba yam awe na mbao bali ni kanisa lake, yaani wale
waliozaliwa mara ya pili kwa kutakaswa kwa damu ya thamani ya mwana pekee wa
Mungu YESU KRISTO.
-
Kwa kuwa wewe mwenyewe umeshuhudia kuja kwake Mungu Roho Mtakatifu na kufanya
makao ndani yako; ni vema ufahamu kuwa Roho Mtakatifu ni mtakatifu kweli. Yeye
huichukia sana dhambi ikiwa katika umbo lolote lile, nan i rahisi kumkasirisha
na kumhuzunisha pale utakaporuhusu dhambi maishani mwako. Katika maandiko
yaliyotangulia tunawaona watu hawa waliokuwa wamezaliwa mara ya pili na kupokea
uwezo wa Roho Mtakatifu lakini wakashindwa kuishi maisha ya utakatifu. Kwa
maisha yao ya dhambi waliweza kupokea tunda la mauti, sawasawa na maandiko
yasemavyo kuwa mshahara wa dhambi ni mauti. Kwa hiyo pale unaposhindwa kuishi
maisha ya utakatifu baada ya kumpokea Roho huyu wa BWANA. Matokeo yake ni
kumzimisha Roho Mtakatifu uliyempokea awe msaidizi wako katika mambo ya kiroho.
Roho akishazimika na ule moto wa wokovu nao huzimika, hatimaye mtu hupatwa na
mauti ya kiroho. Basi muda wako uliobakia sasa ishi kwa kumpendeza Mungu. Daima
msalaba ukiwa mbele na dunia nyuma; kwa kufanya hivi utazaa matunda mema na
watu watakuja kutoka kila kona kuonja matunda hayo. Na ufahamu kuwa kila
atakayeonja matunda yatokanayo na maisha yako ya ujazo katika Roho Mtakatifu,
atafanyika sadaka katika ufalme wa Mungu, na kama yanenavyo maandiko pale roho
yako ilipo ndipo na sadaka yako itakapokuwepo.