Jumamosi, 22 Aprili 2017

MAISHA BAADA YA KUBATIZWA NA ROHO MTAKATIFU.


Mtu anapozaliwa mara ya pili kwa kumkaribisha Bwana Yesu ndani ya maisha yake, huingia katika maisha mapya na kutembea katika uongozi wa Mungu aliye hai. Mtu huyu aliyezaliwa mara ya pili anapofikia mahali pa kukutana na Nafsi ya tatu ya Mungu (Roho Mtakatifu) ana kwa ana katika kipimo cha kufurika (tele), huingia katika ufunuo mpya na maisha mapya ya kushuhudia uthihirisho wa nguvu za Mungu katika maisha yake. Katika maisha haya ya kutembea na Roho Mtakatifu, ni vema kila mwamini apate mafundisho yaliyo sahihi jinsi ya kutembea na Roho Mtakatifu huyu wa Mungu ili kwa kufanya hivi “moto uendelee kuwaka ndani yake daima pasipo kuzimika”(Law 6:12) hebu sasa tuendelee kuwa katika Roho ili tujifunze yale yatupasayo kufanya baada ya kupokea ubatizo huu wa Roho Mtakatifu udhihirishwao na ishara ya lugha mpya.
JENGA TABIA YA KUMWOMBA MUNGU.
Akawaambia mfano ya kwamba imepasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa (Luka 18:1). Ni vyema ufahamu kuwa maombi ni mkono uwezao kuyaleta mapenzi ya Mungu duniani, na kila adumuye katika kuomba hudumu katika ushirika (Fellowship) na Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Katika maombi tunavuta hazina ya Mungu iliyofichika kutoka katika ulimwengu wa Kiroho kuja katika ulimwengu unaoonekana. Maombi n kusema na Mungu Baba kama vile baba wa dunia anavyoweza kusema na watoto wake awapendao. Sehemu nyingine Yesu alipokuwa anaongea na wanafunzi wake aliwakazania kuwa inawapasa kuomba ili wasije kuingia majaribuni. Maombi yanamfanya mtu ayaone majaribu hata kabla hayajatokea, badala ya kushitukizwa na majaribu hayo. Yesu alipokuwa anasema ombeni ili msije mkaingia majaribuni, hakuwa na maana iliyo nyepesi bali alikuwa anawatahadhalisha kuwa waangalie wasije wakaingia majaribuni na kushindwa. Nasema hivi kwani kuingia majaribuni  hilo si jambo lililo geni katika kanisa na hata tunasoma kuwa; “Ni Furaha tupu mtu anapoangukia katika majaribu mbalimbali” (Yak 1:2) kwa hiyo maombi ni silaha zinazomwezesha mwamini kutoka akiwa mshindi, baada ya kuingia au kuangukia katika majaribu. Mtu anapoingia majaribuni na akishindwa kuendelea na hali ya kiroho aliyokuwa nayo, basi husababisha ubaridi mkubwa ndani ya roho ya mtu, na kwa ubaridi huo Roho yule aliyempokea huzimika ndani yake. Roho anapozimika ndani si rahisi tena kulisikia bubujiko la uzima ndani ya mtu na hapo huyapoteza maisha ya ushindi yaletwayo na Roho Mtakatifu. Kwa maneno haya nataka kusema kuwa mara tu baada ya kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu anza kujenga tabia ya kuomba. Hii ni hatua muhimu sana katika maisha haya mapya ya kutembea na Roho wa Mungu. Maombi hayatakiwi kuwa mzigo, yaani kitu cha kujilazimisha badala yake lazima iwe tabia ya mwanafunzi. Ninaposema tabia ninapenda kuyafananisha na kuvuta hewa ya oxygen. Mtu havuti hewa kwa kujilazimisha bali hufanya hivyo kwa sababu ni raha tena ni afya tunapofanya hivyo. Tunapojenga tabia hii ya kuomba ni lazima tuombe kwa ufahamu pia tuombe kwa kunena kwa lugha mpya. Maana tukinena kwa lugha tunakuwa tunajijenga kama tulivyotangulia kusema katika sura zilizopita. Kumbuka kuwa hujapokea Roho Mtakatifu ili tu unene kwa lugha, bali umepokea Roho Mtakatifu ili uwe na manufaa katika kuujenga ufalme wa Mungu.
DAMU KATIKA USHIRIKA WA ROHO NA WATU WA MUNGU.
“Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na Roho mmoja na wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu chochote alichonacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika” (Matendo 4:32)
Katika maisha haya mapya uliyonayo, unahitajika kujengwa na kujifunza zaidi mafundisho haya na kuimarika, vitu hivi vinaweza kupatikana  pale watu wa Mungu wanamtafuta Mungu katika Roho na kweli, maana ndivyo yesu alivyomwambia yule mama Msamaria. Alimwambia wakati unakuja ambao wamwabuduo Mungu halisi watamwabudu Baba katika Roho na kweli (Yohana 4:23). Wewe sasa ni kondoo mchanga mwenye moto wa kuijua kweli ya Mungu, basi tafuta malisho (chakula cha kiroho) toka kwa mchungaji wa kweli, maana huyo ana uchungu na maisha yako ya kiroho. Nasema hivyo kwani ni vema ujitambue kuwa u msafiri wa kwenda mbinguni na kwa sababu hiyo lazima utafute gari litakalokupeleka mbinguni. Mchungaji ni sawa na gari la kuwapeleka watu mbinguni, tatizo linalotokea ni kuwa yako magari (wachungaji) ambayo yameegeshwa mahali na hayatembei, ni jambo la kuchekesha kuwaona wakristo wengine wakiingia mle ndani na huku wanategemea kusafiri! Kama kweli u msafiri wa mbinguni tafuta gari (mchungaji) linalotembea.
Kwa maneno haya nataka kukutafutia malisho zaidi au mahali utakaponeemeka kiroho na mafundisho yaliyo hai. Katika ushirika huu, ni vema usifungwe na madhehebu, bali uwe tayari kukumbatiana na mwamini yeyote wa dhehebu lolote, maana hao ndio ndugu zako wa kweli. Pia ukumbuke kupima yale uliyoyasikia kama yanaendana na neno la Mungu, ni vema uwe karibu na yule aliyekabidhiwa kwako kama baba yako wa kiroho.
VIPINGE NA KUVISHINDA VIKWAZO VYOTE ATAKAVYOKULETEA SHETANI.
“Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yeyote kwa jina hili, wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. Petro na Yohana wakawajibu wakamwambia, kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe. Maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia” Matendo 4:17-20
Mtu anapompokea YESU kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake, husababisha chuki na hasira kubwa kutoka kwa shetani dhidi yake. Tendo la mtu kuamua kutoka kwenye ufalme wa giza na kuingia kwenye UFALME WA MUNGU, humsisimua shetani mnoo hata kumfanya aende vitani dhidi ya mwamini huyu mpya. Ili katika vita hiyo aweze kumrejesha tena mikononi mwake.
Katika vita hii ya shetani dhidi ya mwamini, ibilisi hutuma mishale ya kila namna ili kumwangusha mtu, na hachoki katika mapambano hayo, ila siku kwa siku huzidisha makali ya mapigo yake kwa mwamini. Kwa kusema hivi nina maana kuwa kila mwamini anapopiga hatua moja mbele kiroho, shetani naye huongeza mapigo yake ili ikibidi kumteketeza mtu wa Mungu. Mwamini anapobatizwa kwa Roho Mtakatifu huwa amepiga hatua kubwa mno kiroho, hatua ambayo huutetemesha sana ufalme na mamlaka ya shetani.
Kwa sababu hii, mtu anapojazwa Roho Mtakatifu kwa kipimo cha tele, atakumbana na matatizo ambayo hayakuwepo kabla ya kuingia katika hatua ya kuzaliwa upya. Majaribu yatakuwa yamezidishwa ukali wake kama alivyofanya mfalme Nebukadneza kwa kina Shadraka , Meshaki na Abednego. Biblia inatuambia kwamba Nebkadneza alizidisha moto wa tanuru mara saba kuliko ulivyokuwa kawaida yake, ili uwateketeze watu wa Mungu (Danieli 3:19) kwa vijana hawa watatu wa kiebrania, shetani aliwatumia watu mbalimbali hata wafalme ili kushusha imani yao. Hata kwako wewe pia anaweza kutumia vitu kama hivyo, au ndugu zako, marafiki na hata viongozi wa dhehebu lako ili kumpinga Roho Mtakatifu uliyempokea, basi kwa vyovyote vile itakavyokuwa lazima uyashinde majaribu na vishawishi vyote vile vya yule mwovu. Kumbuka kuwa hata mitume walipita katika majaribu makali mno mara tu baada ya kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, wengine walipigwa kwa mawe, au kukatwa shingo kwa msumeno, au kuwekwa ndani ya mafuta yaliyochemka hadi kufa. Ni jambo la Baraka na la kutia moyo kuona kuwa katika mambo yote hayo waliyofanyiwa na shetani, wao walikaza uso wao kama gumegume na kuchagua hata kufa kwa ajili ya imani waliyopokea, kuliko kuishi wakiwa wameasi imani waliyopokea kwa njia ya mauti ya mwana pekee wa Mungu pale msalabani.
Niseme tena kuwa sasa kwa kuwa umejazwa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya, endelea kuvipiga vita vile vyema vya imani maana katika kila gumu litakalokupata, hutakuwa peke yako; bali yule aliyeanza kazi njema ndani yako ndiye atakayekushindia. Kumbuka kuwa kila utakapompinga shetani atakimbia, na kwa kufanya hivyo utaendelea kumpendeza Mungu aliyekununua.
ILI UIMARIKE ANZA KUTOA USHUHUDA WA KUFUFUKA KWA BWANA YESU.
Dunia leo ina watu zaidi ya bilioni moja wanaojiita wafuasi wa Kristo. Watu hawa wanadai kuwa ni mashahidi wa Bwana wetu Yesu Kristo na ya kwamba wanao ushuhuda wa Yesu kwa dunia nzima. Ukichukua maana halisi ya ushahidi kwa kuzingatia lugha kongwe kwa mfano kiyunani, utaona kuwa watu hawa si mashahidi.
Katika kiyunani neno shahidi linaitwa Martyria yaani kufa au kuuawa kwa ajili ya kitu fulani kwa hiyo shahidi wa Yesu ni yule anayeusimamia ushuhuda wake pasipo kuyumbishwa hata kama ikibidi auawe kwa sababu ya ushuhuda huo. Shahidi na yule anayesimamiwa kwa ushahidi huo ni kitu kimoja, hawatenganishwi kwa namna iwayo yeyote ile. Kwa kuwa wakristo wanatakiwa kuwa mashahidi wa Yesu, ni lazima watene na kuishi kama Yesu anavyotaka na kuyashikilia maungamo yao hata mauti.
Tunapowaangalia wakristo wa leo, utaona kuwa hawafai kuitwa mashahidi, maana yale Kristo anayoyakataa ndiyo wanayoyafanya. Dhambi imeharibu ushahidi wao kwa ukweli huu, unaweza kuona kuwa wakristo hawa hawatoi ushuhuda wa kufufuka kwa Yesu, bali hutoa ushuhuda wa kufa kwa Yes utu. Na mtu anayetoa ushuhuda wa Yesu na kuishia hapohapo tu asiendelee mbele, huyo ni shahidi wa uongo. Kwa maneno haya tunaweza kusema kuwa kuna mashahidi wa uongo wa Yesu zaidi ya bilioni moja duniani, ukiwaondoa wale wanaomwabudu Yesu Kristo kwa roho na kweli.
Mtu anaposhuhudia juu ya mauti ya Bwana pamoja na kufufuka kwake, huyo anaudhihirishia ulimwengu kuwa yeye anamwabudu yesu aliye hai anaweza kufanya mambo yafuatayo;-
-         Yesu aliye hai analeta ondoleo la dhambi. Tayari nimekwambia kuwa kuna zaidi ya wakristo wa uongo 1,000,000,000 duniani. Watu hawa humwabudu Yesu aliyekufa, maana ni yesu aliyekufa tu ndiye anayeweza kuabudiwa na majambazi, waasherati, wazinzi, walevi, waongo,wavutaji wa unga, wezi na watu watendao mambo ya jinsi hiyo. Hata hivyo katika dunia hii, wapo wanao mwabudu Yesu kwa roho na kweli, watu hawa hawakwenda na Yesu hadi kaburini tu, bali walifufuka pamoja naye! Kufa na kufufuka pamoja na Bwana ni kupokea ondoleo la dhambi na kuzaliwa mara ya pili kwa kupokea asili mpya kutoka kwa Mungu aliye hai. Yeye alipokea ondoleo la dhambi hawi tena mtumwa wa mwili na tamaa za kidunia, bali hupokea asili mpya ya kiMungu na kwa msaada wa Roho wa Mungu huishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi.
-         Yesu aliye hai hutenda miujiza, ishara na maajabu “Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo” (Marko 16:20) ni vema tufahamu kwamba kuna imani na dini nyingi mno duniani, katika imani au dini hizo zimesimamia kati ya imani hizo ni hii ya ukristo, chini ya kinara au nguzo yake iitwayo YESU KRISTO. Imani hii imekuwa ya pekee mno ukilinganisha na zile zingine zilizopo, naweza kusema kuwa ni imani iliyo hai. Maana kila inapokigusa kitu kilichokuwa katika hali ya kufa kiroho au kimwili, uhai mpya uliweza kuonekana ndani ya kitu kile. Mtu aliyepoteza uhai wake kiroho na kupotea katika dhambi, anapoamini na kujiunga na imani hii; roho yake hufufuliwa na kuwa hai tena, na kwa mgonjwa aliyekata tamaa ya kuishi hurejeshewa afya yake kwa kumwamini Yesu huyu aliye hai. Miujiza na ishara zinazotokea katika imani hii ya ukristo na maajabu mengine mengi huifanya imani hii ya ukristo kuwa ya pekee kuliko imani nyingine zote duniani. Mhubiri mmoja alisema kuwa ukristo pasipo miujiza ni sawa na imani nyingine zilizokufa na hii ni kweli kabisa. Na hapa uelewe kuwa miujiza tunayoizungumzia ni pamoja na ule wa mtu kuzaliwa mara ya pili na kuachana na dhambi. Kwa kumalizia hebu tuseme kuwa ni vema uanze sasa kutoa ushuhuda kwa watu wengine, ukiwaeleza kule Yesu alikokutoa , na pale alipokuweka sasa, pale atakapokuweka baada ya maisha haya na jinsi anavyokupa ushindi siku hadi siku
-         Toa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana “Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao” (Matendo 4:32) baada ya kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, ile chemchem inayojaa hata kufurika, hatua au jambo jingine hutokea kutoka katika chemchem hiyo. Kwa maneno mengine ni kuwa ndani yako sasa kuna mito ya Roho Mtakatifu iliyojaa uzima kwa ukweli huu ni lazima ufahamu kuwa mito sio kwa ajili ya mtu mmoja peke yake, bali mito ni lazima ilete maendeleo na mabadiliko kwa wale wote watakaofikiwa na mto huo. Mtu anapoamua kufunga chanzo au pale mto unapoanzia, huyo ni muuaji; maana atasababisha hasara kubwa ikiwa ni pamoja na mauti kwa wote waliokuwa wakiutegemea mto huo. Mto ni lazima uachwe utiririke wakati wote pasipo kufungwa.
-         Kutoa ushuhuda ni sawa na kuuacha mto ububujike daima neno hili kushuhudia linatokana na neno ushuhuda, shuhuda na shahidi ni maneno ambayo unapoyachambua hatima yake unapata kitenzi hiki, kushuhudia , shahidi ni mtu aliyekuwepo jambo lilipokuwa linatokea, ni mtu anayelifahamu jambo kwa usahihi na kwa mapana marefu yake. Kwa hiyo yale shahidi atakayo yasema kuhusiana na jambo fulani alilolishuhudia, ndiyo tunayaita ushuhuda, yaani maelezo yaliyo sahihi na hai yaliyotolewa na yule aliyekuwapo wakati wa kutukia jambo hilo. Ninaposema maelezo yaliyo hai, hapa nina maana kuwa ushuhuda kamwe si hadithi za uongo, au habari za kutungwa, bali ni maelezo ya kweli yanayothibitishwa na nafsi ya mtu, roho yake na mwili wake pia.
-         Tumia mamlaka uliyonayo kwa jina la Yesu. “Lakini Petro akasema, mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilichonacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende” (Matendo 3:6) kwa miaka mitatu, wanafunzi wa Yesu walikuwa wameshuhudia matendo makuu ya Mungu yaliyotendwa kwa mkono wa Bwana wao na mwokozi wa ulimwengu Yesu Kristo. Biblia inatuambia kuwa, kwa mamlaka Yesu aliamuru pepo wabaya nao wakamtii, vilema, viziwi, bubu, na wenye maradhi mengi waliponywa pale Yesu alipoamuru ifanyike hivyo kwa mamlaka aliyokuwa nayo. Kwa mamlaka aliweza hata kuamuru upepo na dhoruba vitulie navyo vikatulia. Wanafunzi walipoona haya yakitendeka walishangaa mno, huku wakitamani mamlaka ile iliyotenda kazi ndani ya Bwana wao hata wakafikia hatua ya kumwambia Yesu kuwa awaongezee imani! Yesu alipopaa aliwaacha wanafunzi wake katika huzuni nzito huku wakiwa wamevunjika moyo, haya yalitokea kwani waliamini kuwa kwa kuondoka kwa Bwana wao basi na ile mamlaka nayo inmeondoka pamoja naye. Kujihisi kupungukiwa huku kuliendelea sana hadi pale hadi pale walipobatizwa Roho Mtakatifu mara tu baada ya kumpokea Roho Mtakatifu kwa kipimo cha tele. Moto ulilipuka tena ndani yao na wakapata ufunuo mpya wa kuitumia mamlaka iliyokuwa ndani yao, angalia hapa; KWA MUDA MREFU Petro na Yohana walikuwa wanampita huyu kiwete akiwa katika mlango wa hekalu pasipo kumsaidia. Lakini baada ya ubatizo wa Roho Mtakatifu uliotokea katika sura ya pili ya kitabu cha matendo ya mitume, sasa Petro anajitambua kuwa yeye ni nani katika mitume, tena anatambua kuwa mamlaka ileile iliyotenda kazi ndani ya Yesu ipo ndani yao. Nasema hivyo kwani Yesu aliwaambia katika Luka 10:19 kuwa “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka, nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru “Kwa ufunuo huo mpya Petro aliweza kumwendea yule kiwete na kumwamuru atembee katika jina la YESU na ikatendeka hivyo. Ni vema ufahamu kuwa sasa umefanya safari ya kuendea mti wa uzima na ile mana iliyofichwa, katika safari hii mambo hayatakwenda kama unavyotaka, bali daima shetani atataka mambo yaendekama atakavyo yeye, basi kama utakunja mikono na kujihisi mnyonge na duni, utashindwa kuishi maisha ya ushindi, kumbuka kuwa yeye ashindaye ndiye atakayepewa kula matunda ya mti wa uzima ulio katika bustani ya Mungu (Ufunuo 2:7b). ili upate ushindi ni lazima ujifahamu kuwa wewe ni mtoto wa Mungu na mrithi pamoja na Yesu Kristo nay a kuwa una haki ya kisheria ya kutumia mamlaka iliyo katika jina la Yesu Kristo. Kwa hiyo unapoona hali isiyobariki inajitokeza katika safari yako, iamuru kuwa ihame katika jina la Yesu na kwa kutumia jina hilo, fungulia ile hali unayotaka iwepo. Kwa maneno haya napenda ufahamu kuwa mambo hayatakuwa marahisi kila wakati maishani mwako; hivyo pale yanapokwenda visivyo, tumia mamlaka kukemea na kuharibu kila kilicho kiovu, na itatendeka kama ulivyoamuru. Wakati wa kufanya hayo usijisikie upweke na duni, ujue kuwa uko pamoja na Yesu na kwa jina lake kila goti litapigwa na kila ulimi utakiri kuwa YESU NI BWANA. Baada ya kubatizwa na Roho Mtakatifu ishi maisha matakatifu. “hata masaa matatu baadae mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea, Petro akamjibu, niambie mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema ndiyo, kwa thamani hiyo, Petro akamwambia, imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Anagalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. Mara akaanguka miguuni pake akafa” (Matendo 5: 7-10) tunasoma kuwa Mungu hapo zamani katika Agano la kale aliishi katika hema la ushuhuda au katika hekalu. Katika Agano jipya, Mungu anaendelea kuishi katika hema au katika hekalu, ila safari hii si katika hema iliyojengwa kwa mikono ya wanadamu, bali hema lile alilolijenga yeye mwenyewe yaani mwili wa Kristo. Na Yesu alipopaa mbinguni alimwomba Mungu baba ili Roho Mtakatifu aje duniani na kuchukua nafasi aliyoiacha, naye akashuka siku ya hamsini baada ya kufufuka kwake. Katika sura katika sura ya mwanzo ya kitabu hiki tumejifunza juu ya kusudi la kuja kwake, basi alikuja ili kuyakamilisha makusudi haya, na alifanya au anafanya hivyo pale anapopata maskani hiyo si kwenye majumba yam awe  na mbao bali ni kanisa lake, yaani wale waliozaliwa mara ya pili kwa kutakaswa kwa damu ya thamani ya mwana pekee wa Mungu YESU KRISTO.

-         Kwa kuwa wewe mwenyewe umeshuhudia  kuja kwake Mungu Roho Mtakatifu na kufanya makao ndani yako; ni vema ufahamu kuwa Roho Mtakatifu ni mtakatifu kweli. Yeye huichukia sana dhambi ikiwa katika umbo lolote lile, nan i rahisi kumkasirisha na kumhuzunisha pale utakaporuhusu dhambi maishani mwako. Katika maandiko yaliyotangulia tunawaona watu hawa waliokuwa wamezaliwa mara ya pili na kupokea uwezo wa Roho Mtakatifu lakini wakashindwa kuishi maisha ya utakatifu. Kwa maisha yao ya dhambi waliweza kupokea tunda la mauti, sawasawa na maandiko yasemavyo kuwa mshahara wa dhambi ni mauti. Kwa hiyo pale unaposhindwa kuishi maisha ya utakatifu baada ya kumpokea Roho huyu wa BWANA. Matokeo yake ni kumzimisha Roho Mtakatifu uliyempokea awe msaidizi wako katika mambo ya kiroho. Roho akishazimika na ule moto wa wokovu nao huzimika, hatimaye mtu hupatwa na mauti ya kiroho. Basi muda wako uliobakia sasa ishi kwa kumpendeza Mungu. Daima msalaba ukiwa mbele na dunia nyuma; kwa kufanya hivi utazaa matunda mema na watu watakuja kutoka kila kona kuonja matunda hayo. Na ufahamu kuwa kila atakayeonja matunda yatokanayo na maisha yako ya ujazo katika Roho Mtakatifu, atafanyika sadaka katika ufalme wa Mungu, na kama yanenavyo maandiko pale roho yako ilipo ndipo na sadaka yako itakapokuwepo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni