“Lakini
yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli
yote….”Yohana 16:13
Biblia inasema mwanadamu
anatakiwa kuwa mtakatifu kama vile Mungu alivyo mtakatifu. Utakatifu ni maisha
yasiyowezekana kwa nguvu za kibinadamu, bali ni kwa msaada wa Mungu. Na
ninaposema maisha ya utakatifu, ninamaanisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia
na kuishi kwa kiasi, haki na utawa katika ulimwengu wa sasa. Tunaposoma kwenye
neno la Mungu tunaonyeshwa yale yasiyo mema kwa mtakatifu kuyafanya japo tena
si maovu yote yaliyoandikwa kwenye Biblia. Katika hili wengi wamefanya maovu
wakidai kuwa hayajakatazwa kwenye neno la Mungu.
Pamoja na udhuru huu wa
kibinadamu, hakuna mwanafunzi wa Yesu atakayepona, kwani Mungu alimtoa Roho
Mtakatifu akae ndani ya kanisa ili kuufunua ukweli wote wa Mungu katika dunia
kama tunavyosoma kwenye maandiko yaliyotangulia kwa hiyo Roho Mtakatifu
hulisaidia kanisa kuelewa zaidi mwili wa Kristo na jinsi ya kuutunza mwili wake
hasa tukifahamu kuwa Yesu Kristo ndiye kweli.
ROHO MTAKATIFU HULIPA
KANISA UJASIRI.
Hofu ni adui mkubwa mno wa
imani katika Bwana, hata Biblia inazungumzia kuwa pasipo imani haiwezekani
kabisa kumpendeza Mungu. Mwamini au kanisa linapotawaliwa na hofu haliwezi
kuishi kwa imani, hivyo basi halitampendeza Mungu daima.
Adui huyu wa imani humsonga
mno mtu kabla ya kubatizwa na Roho Mtakatifu na lazima msaada toka mbinguni
uingie ndani ya mtu na kuiondoa hofu hiyo. Tunapoyaangalia maisha ya mtume
Petro, tunaona kuwa yametawaliwa na hofu hata wakati fulani alikaribia kuzama
baharini kwa sababu ya hofu.
Hofu ya mauti ilimfanya
Petro pia amkane Bwana na mwalimu wake Yesu Kristo mara tatu, alimpenda Yesu
lakini hofu ilimsukuma kumkana Bwana Yesu. Hofu hii ilimpata kwa sababu ya kitu
fulani kilichopungua ndani yake. Lakini tunapoyaangalia maisha yake ya baada ya
kumpokea Roho Mtakatifu tunayaona kuwa yalikuwa ya tofati kabisa. Mtume Petro
hakuogopa tena kumshuhudia Yesu mbele za watu, aliweza kuutangaza umasihi na ufufuko
wake, pamoja na kupaa kwake kwa ujasiri alioupata alikuwa hata radhi kufa kwa
ajili ya injili na ndivyo livyotokea. Kuhusu ujasiri tunaoupata baada ya
kubatizwa kwa Roho Mtakatifu sio jambo la kuzusha, bali Yesu mwenyewe alitamka
hivyo kwa wale mia na ishirini wakiwemo wale thenashara katika kitabu cha
Matendo ya mitume Yesu alisema;
“Lakini
mtapokea nguvu, akiisha kuwajilieni juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa
mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika uyahudi wote na hata nje ya nchi” Matendo
ya mitume 1:8
Hapa neno shahidi lina
maana kuwa jasiri hata hatua ya mauti, haya yanawezekana tu kwa msaada wa Roho
Mtakatifu.
ROHO MTAKATIFU HUFANYA KAZI
KAMA NJIWA (HUA)
“Nuhu
akangoja siku saba tena, kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili,
njiwa akamjia jioni, na tazama alikuwa na jani bichi la mzeituni kinwani mwake
ambalo amelitunda, basi nuhu akajua ya kwamba maji yamepungua juu ya nchi” (Mwanzo
8:10-11)
Tunapoangalia ndege huyu,
tunaweza kuona kuwa ni ndege anayepatikana katika jamii zote za watu wa
ulimwengu tulionao. Katika Agano la kale ndege huyu alikuwa ni sehemu ya sadaka
iliyoweza kutolewa kwa Bwana; hata Mariamu na Yusufu waliweza kutoa njiwa
wawili kama sadaka mbele za Mungu (Luka 2:24) ni jambo la kushangaza kuona kuwa
kama vile hua (njiwa) wanavyoweza kupatikana kwa jamii zote tajiri na masikini,
vivyo hivyo Roho Mtakatifu naye anaweza kuingia mahali popote ili mradi tu awe
amefunguliwa mlango.
Njiwa (hua) ana tabia ya upole
kila wakati, tena ni ndege aliye mtulivu mnoo. Roho Mtakatifu anapoingia ndani
ya mtu humfanya mtu huyo kuwa na maisha ya utulivu na upole. Mtu aliye mkali
kwa kila hali, anapopokea zawadi hii, hali yake hubadilishwa kabisa. Badala ya
mbegu ya ukali na hasira hupandwa mbegu ya upole katika BWANA. Jambo lingine
tunapomwangalia ndege huyu, tunaona kuwa tangu zamani alitumwa kama mjumbe au
msaidizi. Nuhu alimtuma njiwa akayakague maji juu ya uso wa Nchi na kupitia kwa
njiwa, Nuhu aliweza kutambua majira ambapo maji yalipungua usoni mwa nchi. Nuhu
hakuweza kuifanya huduma hii, bali njiwa aliweza kumsaidia. Kwa hili tunaiona
kazi za Roho Mtakatifu iliyowazi, yeye ni msaidizi wa kanisa. Mwanadamu peke
yake hawezi kushinda na kumpendeza Mungu, haya huwezekana tu pale mtu
anapobatizwa kwa Roho Mtakatifu. Yeye ni msaidizi wa mambo yetu yote yaliyo ya
rohoni nay ale ya mwilini, hata Yesu mwenyewe alimwita msaidizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni