Ubatizo wa Roho Mtakatifu
ni muujiza wa ajabu mno unapotokea kwa mtu. Muhusika huelewa fika kuwa amepokea
kitu ambacho sio cha kawaida. Wengi wanaodai kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu wakati bado
hujipoteza kwa hiari yao wenyewe, na kama yanenavyo maandiko kwamba huangamizwa
kwa kukosa maarifa. Ninasema hivi kwa sababu Mungu ametoa ishara za wazi mno
hata kwa wale walio nje kuthibitisha kuwa mtu huyu amepokea ubatizo wa Roho
Mtakatifu.
Kwa ujumla ziko ishara
nyingi zinazothibitisha tendo hili, ishara nyingi zinatokea ndani ya mtu
mwenyewe, lakini zipo zingine zinazotokea nje ya mtu na kuwa ushuhuda hata kwa
watu wengine. Tunapoziangalia zile zitokeazo nje tunaweza kuona kuwa iko ishara
moja inayotokea mar azote kwa kila mwamini anayepokea ubatizo huu; ishara hii
ni ile ya mwamini kunena kwa lugha nyngine kama vile Roho anavyomjalia kutamka.
Katika hili, mtu yoyote
asije akadanganywa na shetani kwamba mtu anaweza kubatizwa kwa Roho Mtakatifu
bila ishara hii kutimia au kuonekana kwa kulielewa jambo hili vizuri zaidi hebu
tuangalie jinsi wale waliotutangulia walivyopokea ahadi hii.
WALE 120 WAKIWEMO MITUME
WALINENA KWA LUGHA MPYA
“Hata
ilipotimia siku ya pentekoste walikuwa wote mahali pamoja, kukaja ghafla toka
mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote
waliyokuwa wameketi. Kukatokea ndimi zilizogawanyika kama ndimi za moto
uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa
lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka” (Matendo 2:1-4)
Biblia inasema wazi kuwa
kanisa limejengwa katika msingi wa Mitume na manabii, Yesu mwenyewe akiwa jiwe
kuu la pembeni, kwa usemi huu ni vema kuangalia jinsi mitume walivyopokea Nafsi
hii ya Mungu. Nasema hivi kwani mitume ndio wa kwanza katika Agano la kale na
jipya kumpokea Roho Mtakatifu ikiambatana na ishara ya kusema kwa lugha
nyingine na wale waliowazunguka walishuhudia tendo hilo, hata wakadhihaki
wakisema kuwa wamelewa kwa mvinyo mpya.
MTUME PAULO ALISEMA KWA
LUGHA NYINGINE.
“Namshukuru
Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote” 1Wakorinto 14:18
Paulo alipookoka, Mungu
alimtumia Anania ili amwekee mikono Paulo apate kuona tena kiroho na kimwili.
Biblia inasema kuwa Anania alifanya hivyo pale Dameski Paulo alijazwa Roho
Mtakatifu maana ndilo lilikuwa kusudi la kutumwa kwake.
Tunaposoma ushuhuda wa
Paulo katika mistari iliyotangulia, Paulo anatuambia kuwa yeye ananena kwa
lugha; kwa hiyo ni wazi kuwa siku ile alipoombewa na Anania alipokea Roho
Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya.
KORNELIO NA WALIOKUWA
PAMOJA NAYE WALINENA KWA LUGHA NYINGINE.
Kornelio alikuwa mtu
aliyekuwa na kiu ya kuurithi uzima wa milele, hata hivyo kiu yake haikumzalia
matunda aliyoyatazamia kwa kutoielewa njia ya wokovu kwa usahihi. Mungu alipoiona
kiu na njaa yake hii ya muda mrefu, alimtuma mtume Petro ilia pate kumwelezea
njia ya Bwana kwa usahihi.
Katika mji huu wa Kaisaria
Mtume Petro alipata nafasi ya kuongea mambo mengi yahusuyo usahihi wa njia ya
Bwana na wale walioyasikia waliyaamini kuwa ni maneno yatokayo kwa Mungu aliye
hai. Kwa kule kuamini kwao, maandiko yanasema kuwa;-
“Roho
Mtakatifu akawashukia wote waliosikia lile neno, na wasiotahiriwa walioamini
wakashangaa watu wote waliokuja na Petro, kwa sababu mataifa mataifa nao
wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha
na kumwadhimisha Mungu” Matendo 10: 44-46
Maandiko haya
yanatuthibitishia kuwa kanisa la Kaisaria lilipokea ubatizo wa Roho Mtakatifu,
kila mmojawapo alinena kwa lugha mpya; nasema hivi kwani maandiko yanasema kuwa
wale waliokuja na Petro walishangaa? Kwa sababu mataifa nao wamemwagiwa kipawa
cha Roho Mtakatifu kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha na kumwadhimisha
Mungu.
WANAFUNZI KULE EFESO
WALISEMA KWA LUGHA
“Basi,
enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la Baba na
Mwana na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha yote niliyowaamuru ninyi, na tazama
mimi nipo pamoja nanyi hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28: 19-20)
Maandiko haya yanaonyesha
kazi kubwa iliyoachwa mabegani mwa mitume na kanisa kwa ujumla, wakati Yesu
alipokuwa tayari kupaa kuelekea mbinguni wengi walioachiwa huduma hii hapo
mwanzo ukiondoa mitume, hawakuwa na ufahamu mkubwa jinsi wawezavyo kuifanya
huduma hii kubwa, hawakuwa pia na zana za kazi kama hizi tulizonazo sasa,
pamoja na upungufu huu, walikuwa waaminifu kukifanyia kazi kile kidogo
walichonacho ili kuonyesha utii wao mbele za Mungu kwa ufahamu huu mdogo huduma
nyingi ziliweza kufanywa nusunusu bila ya kukamilika.
Katika mji wa Efeso mtume
Paulo alikutana na waamini ambao licha ya kuokoka bado walibakiza mambo fulani
fulani waliyotakiwa kufundishwa. Maandiko yanasema kuwa
“Ikawa
Apolo alipokuwa Korinto, na wanafunzi kadhaa wa kadhaa huko; akawauliza, je
mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, la hata kusikia kwamba kuna Roho
Mtakatifu hatukusikia (Matendo 19:1-2)
Paulo alihojiana na
wanafunzi hawa aligundua kuwa walihitaji kuelezwa na kufundishwa mambo fulani
fulani waliyopungukiwa ndani yao, likiwemo hili la ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Baada ya kuwafundisha
maandiko yanasema kuwa;-
“Paulo
akaweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa
lugha na kutabiri”(Matendo 19:6)
Wanafunzi hawa hawakuwa
wachache, neno linasema walikuwa kumi na wawili, wanaume tu, bila kutaja
wanawake, na hawa wote walijazwa Roho Mtakatifu na kusema kwa lugha nyingine.
WAAMINI WA SAMARIA WALISEMA
KWA LUGHA.
Wakati wa mateso ya mwanzo
kwa kanisa, wandugu walitawanyika huko na huko wakihubiri neno. Mtu mmoja
aliyeitwa Filipo alipata nafasi ya kuhubiri katika Samaria, lakini kwa sababu
ambazo hazikutajwa; mtumishi huyo hakuwafanyia huduma ya ubatizo wa Roho
Mtakatifu. Maandiko yananena kuwa, mitume waliposikia wakamwendea na kuwaombea
ili wapokee ahadi hii. Kwa kweli hatuoni mahali palipotamkwa wazi kuwa walinena
kwa lugha nyingine, ila hapa kuna maneno yanayonifanya namini kuwa ishara hii
ilitokea.
Biblia inatuambia;-
“Hata
Simoni alipoona ya kuwa wanapokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mkono ya Mitume,
akataka kuwapa fedha akisema nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu
nitakayemuwekea mikono yangu apokee Roho Mtakatifu. (Matendo 8:18-19)
Hapa kuna swali la
kujiuliza, Je! Simoni alijuaje kuwa watu wale wamepokea Roho Mtakatifu? Ni
dhahiri kuwa hawakuwa kimya; asingelielewa kuwa wamepokea Roho Mtakatifu. Ni
lazima kuwa kuna ishara ya wazi iliwatokea watu wale na kwa Simoni mwenyewe.
Ninaamini kuwa hata hawa walinena kwa lugha nyingine kama ilivyokuwa kwa
wengine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni