Katika kitabu cha mwanzo
sura ya 24, tunasoma juu ya watu wane maarufu katika neno la Mungu. Hapa
tunasoma habari ya mzee Ibrahim akimpatia huduma mtumishi wake ajulikanae kwa
jina la Eliazari kwenda nchi ya mbali kumtafutia mwanae isaka mwanamke
atakayeishi nae. Biblia inatuambia kuwa huyo mtumishi wa Ibrahimu hakuwa
mtumishi wa kawaida bali alikuwa ni mzee wa nyumba yake aliyetawala vitu vyake
vyote. Mtumishi alifanya kama alivyoelekezwa, akaenda nchi ya mbali na Mungu
akamtangulia hata akampata Rebeka awe mke wa Isaka mtoto pekee wa Ibrahimu.
Tunaweza kusema kuwa Ibrahimu ni mfano wa Mungu Baba, Eliazeri naye ni mfano wa
Roho Mtakatifu na Rebeka ni mfano wa kanisa na Isaka ni mfano wa Yesu Kristo
Mwana pekee wa Mungu Baba. Ni jambo linalojulikana wazi kuwa Mungu alimtuma
Roho Mtakatifu duniani ili amtayarishie Mwana bibi harusi aliye mkamilifu.
Tunapoangalia huduma na wajibu wa Eliazari kabla na baada ya kumpata Rebeka,
tunaiona picha halisi ya huduma ya Roho Mtakatifu katika kanisa la Mungu. Baada
ya Eliazari kumpata Rebeka iliwalazimu kuanza safari ndefu jangwani kuyaendea
makao ya Isaka. Katika jangwa lile Rebeka hakupungukiwa na kitu maana Eliazari
alifanya yafuatayo kwa ajili yake;-
ALIMUELEZA YOTE
YANAYOMUHUSU ISAKA
Rebeka hakuwa amewahi
kumwona Isaka mume wake lakini Eliazari alimweleza Rebeka vile ambavyo Isaka
anafanana. Alimweleza yale anayoyapenda na yale asiyoyapenda au ambayo yako
kinyume naye. Kwa ujumla alimweleza tabia yote ya Isaka.
Hivyo japokuwa walikuwa
hawajaonana, lakini Rebeka tayari alishafahamu yote yamhusuyo bwana wake. Hivi
ndivyo ilivyo kwa kanisa, kanisa linaitwa bibi harusi wa Mwana pekee wa Mungu
Yesu Kristo. Kanisa halijawahi kuonana na Bwana wake uso kwa uso, hata hivyo
linamfahamu mno, maana kama Eliazari alivyomweleza Rebeka yote yamhusuyo Isaka,
vivyo hivyo na Roho Mtakatifu wa Mungu ana huduma ya kulielezea kanisa mambo
yote yamhusuyo Mwanakondoo Yesu Kristo.
ELIAZARI ALIMPATIA REBEKA
MAHITAJI YOTE NJIANI
Safari ya kupitia jangwani
ina mahitaji mengi sana, kwa wingi wa mahitaji wengi huanza safari wasiweze
kuimaliza. Katika jangwa Rebeka angeona kiu na njaa au pengine angeliona shida
fulani, haya yote yalipotokea Eliazari alimpa kila alichohitaji. Roho Mtakatifu
naye hulipa kanisa yale yote linalohitaji ili kulipatia kanisa au Bibi harusi
wa Mwanakondoo furaha idumuyo.
ELIAZARI ALIMPATIA REBEKA
ULINZI.
Katika jangwa kuna hatari
nyingi mno, zikiwemo hatari za wanyama wakali. Hatari za majambazi na hatari za
magonjwa. Kwa hatari hizi haingekuwa rahisi kwa mwanamke kusafiri peke yake
katika jangwa. Hatari hizi hazikumletea Rebeka hofu yoyote ile kwani alikuwa
mikononi mwa Eliazari aliyempatia uponyaji na ulinzi aliouhitaji. Kanisa nalo
linapita katika magumu mengi katika safari ya kwenda mbinguni, katika mazito
haya, Roho Mtakatifu ndiye anayelilinda na kulipigania kanisa katika mambo
yote.
ELIAZARI ALIMWONYESHA
REBEKA NJIA
Kwa ujumla safari ndani ya
jangwa inahitaji uangalifu wa hali ya juu mno. Nasema hivi kwani sehemu nyingi
za jangwa zimefanana hivyo ni rahisi sana mtu kupotea katika jangwa, Eliazari
aliifahamu mno njia itakayowafikisha kwa Isaka hivyo alimuongoza Rebeka
jangwani hadi pale walipokutana na Isaka. Kanisa nalo haliijui njia ya
kuwafikisha kwa Mungu, linahitaji kushikwa mkono na kuongozwa.
Roho Mtakatifu ndiye aliye
na wajibu huu mkubwa wa kuliongoza kanisa hadi pale litakapokuwa limekutana na
Bwana wake Yesu Kristo. Kwa ujumla Eliazari alifanya mambo mengi mno kwa ajili
ya Rebeka, tunaweza hata kukesha kuchambua na kuelezea yale yaliyotendwa na
Eliazari kwa Rebeka. Tuseme tu kuwa mtumishi huyu alikuwa ni yote kwa Rebeka
kazi ya Roho Mtakatifu kwa kanisa nazo ni nyingi mno. Yeye ni Mungu, hivyo
tunaweza kumaliza kalamu zote duniani na kalatasi zote bila kumaliza masimulizi
ya kazi zake hizo tulizozitaja katika sura hii ni msingi tu wa kazi zake na
matendo yake makuu na nimeziandika ili ujue kuwa Roho Mtakatifu ni Nafsi hai
nan i Mungu kweli.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni