Jumatatu, 17 Februari 2014

USHUHUDA MKUBWA WA KHALIL




Khalil alianza kuikariri Kurani Tukufu alipokuwa bado mdogo sana na akaendelea na hali hiyo aliyoiita kuwa ni upendo kwenye neno la Mungu. Kwa kadri alivyoendelea kukua, akaanza kusoma vitabu vya kiislamu hasa vile vilivyofafanua Kurani. Alipoendelea kuisoma Kurani na alichanganua walio Waislamu kufuatana na mafundisho hayo kutoka kwa wale wasio Waislamu. Hatimaye aliafiki hata wazazi wake kuwa makafiri. Vitu vidogo vidogo kama vile mwanamke kutokuvaa hijabu kungemfanya mtu kutokuwa Mwislamu wa kweli kulingana na vile alivyoelewa Kurani. Kama mwanaume asingezifuga ndevu zake hata zikakua angeeleweka kuwa yeye pia si Mwislamu. Alizingatia kuwa Wakristo ni maadui zake wakubwa, na hivyo akaanza kujihusisha na mashambulizi dhidi ya Wakristo na kanisa kwa jumla. Kikundi hicho kilijitoa kuipindua serikali ya Misri na kuunda serikali ya kiislamu yenye msimamo mkali. Walimwandikisha kuwa mpiganavita hata kumpandisha cheo na kumchagua kuwa kiongozi wa mahali pale. Kikundi chake kilijihusisha na utekaji nyara kwa mwandishi mashuhuri wa kiislamu asiye na msimamo mkali aliyethubutu kuukosoa kikundi cha Uislamu.
Hatimaye mamlaka ilimtia mbaroni Khalil na wenzake wengi wa kikundi chake. Huko gerezani alikaa miaka miwili, alipata mateso yenye maumivu makali, na mara alipoachiwa huru, alienda Yemen pamoja na wenzake washika dini sana. Kutoka kwenye kituo hiki waliendelea na mipango yao ya kupindua serikali ya Misri kwa silaha.
Hata hivyo mipango yao iligundulika na mamlaka ya eneo lile. Wengi wao walikamatwa tena. Hata hivyo njia ya mapinduzi ya jeshi haijaachwa kamwe. Waliporudi tena Misri walihitaji kukanusha shughuli zao za awali. Siku moja wakiwa Kairo walisoma makala gazetini juu ya kukamatwa kwa Wakristo! Khalil na kikundi chake waliamua kwamba sasa “imepitwa na wakati” kufanya kazi kutetea Uislamu. Hata hivyo katika uchache wao, waliamua kuwa, mapambano yao sasa yangechukua sura mpya kwa kutumia akili. Utafiti ufanywe wa kuandika kitabu kwa kuthibitisha kuwa Mohammad ndiye nabii wa kweli wa Mungu, na kwamba Biblia ya Wakristo na ya Wayahudi ni maandiko yaliyobatilishwa! Khalil alichaguliwa na shehe wake aliyekuwa Kiongozi wa kikundi chake cha kiislamu, ili kufanya utafiti na baada ya hapo aandike kitabu. Kwanza alikataa katakata, kisha aliazimu kuifanya hii kazi, ambayo baadaye aliielezea kuwa katika kazi zote alizowahi kuzifanya maishani mwake kazi hii ilikuwa ni “kazi iliyojaa maudhi!”
Khalil alipomaliza kusoma Biblia, na kulinganisha bayana maneno aliyosoma katika vitabu mbalimbali vya kiislamu, alishangaa sana alipogundua Biblia ilikuwa haina makosa na haijabatilishwa. Badala yake alishangaa juu ya mafundisho ya Biblia yaliyohusu msamaha na upendo usio na kosa, ulioonekana katika maisha na maneno ya Yesu. Alishangazwa hasa aliposoma kuwa Yesu mwenyewe aliwaonya wafuasi wake juu ya mateso na jinsi ilivyotokea miaka elfu mbili baadaye, vilevile ambavyo Yesu mwenyewe alikuwa amesema ingelitokea. Kusoma kwake kulimsaidia kuelewa kwa nini Wakristo wa Misri hawakuwa wakilipiza kisasi kabisa dhidi ya Waislamu na kwa nini kusamehe na kusahau kwao ilikuwa rahisi. Jinsi ambavyo alichukia kuisoma Biblia, ndivyo alivyojisikia kuupenda ujumbe na mafundisho yake.
Hata hivyo alikuwa na kazi ya kufanya, na aliendelea na uamuzi wa kutoka ndani kuthibitisha kuwa Yesu si Mungu, na hakuwahi kusulibiwa. Aliposoma Kurani kwa nia au lengo lake hili, alikusanya sifa na majina ya Mungu jinsi zilivyotajwa katika Kurani. Kisha akatafiti zaidi juu ya sifa za Yesu katika Kurani. Kulingana na Kurani, Mungu ndiye mwumbaji, mponyaji, mfadhili, mmoja pekee anayeweza kufufa wafu, mmoja pekee anayetenda miujiza, mmoja pekee atoaye hukumu ya haki na mambo kama hayo. Kwa mshangao Khalil aligundua kwamba huu ni mtazamo ule ule ambao Kurani inamtaja Yesu (Isa) ikimthibitishia kwamba, Yesu na Mungu ndiye ni yuleyule mmoja.
Khalil alipatwa na mashaka maishani mwake kiasi kwamba aliweza kujisikia mnyonge sana. Aliupenda sana Uislamu na kuamini kuwa njia pekee ya kumfikia Mungu ilikuwa ni kupitia Mohammad. Lakini ikiwa Yesu na Mungu ni yuleyule mmoja, sasa Mohammad ndiyo yupi na ni njia ipi ya kwendea mbinguni? Siku moja shehe wake bila ya kumtaarifu ujio wake aliamua kumtembelea nyumbani kwake, na hapo ndipo alipogundua kuwa utafito wote ambao Khalil alikuwa ameufanya ni kuhusu Uungu wa Yesu! Yaani kuwa Kurani si neno la Mungu n.k. Kwa kifupi ni kwamba hakukiamini kile alichokisoma kwa Khalil. Akamtahadharisha Khalil kuwa angeliweza kumwua endapo angemwambia Mwislamu yeyote kile alichokiandika. Pia akasema kuwa kuanzia pale alianza kumhesabu kuwa ni kafiri!
Hata hivyo, Khalil, hakuweza kuacha msimamo kwamba Ukristo ulikuwa ndiyo njia sahihi. Ili ajifunze zaidi aliamua kujiunga na kanisa. Na kwa vile alivyojulikana kuwa ni mtu mwenye tabia mbaya, mwenye msimamo mkali wa kiislamu, hakuna hata mmoja aliyemwamini. Kila mtu alikataa kukutana naye, hata na wachungaji! Jambo hilo lilimsikitisha sana, na hata akafikiri kwamba pengine aliamua kimakosa, pengine imani ya kikristo haikuwa ndiyo njia pekee ya kufika mbinguni. Hata hivyo sauti ndani yake ilimwambia kwamba asiwaangalie watu.
Siku moja alipokuwa akijaribu kupiga simu kwenye mgahawa, vitu vyake alivyokuwa navyo pale viliibiwa. Begi lake lililokuwa limebeba karatasi zake zote alizokuwa amefanya utafiti, Biblia yake na kitambulisho chake. Alishikwa na hofu kwa sababu mambo yote aliyokuwa ameyaandika yangeonekana ni maeneo ya kumkufuru Mungu. Alikimbilia nyumbani, akiwa amejaa mahangaiko na hofu. Aliporudi chumbani mwake, alianza kutubu kwa yale yote aliyokwisha kuyafanya na hata alifikiri kuwa Mungu alikuwa akimwadhibu kwa kuthubutu kufikiri kwamba Mohammad hakuwa ametumwa na Mungu na kwamba hata Kurani yenyewe haikuwa neno la Mungu. Alitubu, akatawadha au kunawa kulingana na sheria za kiislamu, kisha akachukua zulia lake ili aombe, lakini hata hakuweza kupiga magoti yake, wala hata kufungua mdomo wake kusema japo neno moja toka kwenye Kurani. Alikaa chini na kusema: “Mungu unajua kabisa kwamba ninakupenda, na ninajua kabisa kwamba unanitaka mimi nipite katika njia iliyo sahihi. Mungu nashindwa kuendelea kukupinga. Yale yote niliyoyafanya nilikuwa ninajaribu kukupendeza wewe. Tafadhali sana ninaomba unitoe nje ya giza hili nilimo.” Usiku ule Khalil alilala usingizi mnono ambao kwa miaka mingi hakuwa amelala hivyo. Katika ndoto alimwona mtu aliyemjia na kumwambia kwamba ni yeye ambaye Khalil amekuwa akimtafuta. Hata hivyo Khalil hakujua mtu huyo alikuwa ni nani. Mtu yule alimwambia kuwa, aangalie kwenye kitabu, yaani Biblia. Khalil alisema kuwa Biblia na karatasi zote zimepotea, ndipo mtu yule alimjibu na kumwambia: “Kitabu hakiwezi kupotea kamwe. Amka na ufungue kabati na utaiona, na zile karatasi zako zingine zitarudishwa kwako mwishoni mwa wiki.”
Khalil aliamka toka usingizini akafungua kabati yake. Biblia yake ileile ilionekana ndani ya kabati kwenye shelfu. Kwa kujua kuwa amemwona Yesu aliharakisha na kwenda chumbani kwa mama yake, akamwamsha, kisha akamwomba msamaha, kwa jinsi alivyokuwa mkali na alivyozoea kuitendea familia kwa miaka yote iliyopita. Kutafuta suluhu hakuishia hapa kwa familia yake tu, bali mara kulipopambazuka siku ileile tu asubuhi, Khalil alienda mitaani akiwasalimu marafiki na watu wengine. Hata aliweza kuwatafuta wafanyabiashara Wakristo wale ambao aliwahi kuwaibia, au hata kuwatendea vibaya, hao wote aliwaomba msamaha pia.
Miezi iliyofuata Khalil aliendelea kuimarika katika imani yake mpya. Polepole alianza kupata mazoea na matumaini na Wakristo waliokaa pale. Na alianza kushirikiana kanisani. Alibatizwa na akaendelea kusimama imara aliposhambuliwa kimwili na kutishiwa maisha yake. Maana alijisikia kana kwamba hakukuwa na bei yoyote kubwa ambayo ingeliweza kulipa kwa Yeye Yule aliyetoa kila kitu kwa ajili yake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni