Jumamosi, 26 Aprili 2014

KUSHINDANA NA DHAMBI






“Dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde” (Mwanzo 4:7).

KAMA tulivyoona katika sura iliyopita, utakaso wetu ni juhudi za pamoja kati ya Mungu na sisi wenyewe. Tunaendelea kuwa kama Yesu zaidi tunapozidisha ushirikiano na Baba. Yeye anatupa uwezo na hamasa ya kuwa watakatifu. “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa” (2Petro 1:3 – Maneno mepesi kutilia mkazo). Yeye hutupa sisi asili mpya na kutuongoza kwa Roho Wake anayekaa ndani yetu. Lakini, anatuachia na sisi kitu cha kufanya. Bado tuna hiari yetu. 

Ni lazima tumfuate Roho anayekaa ndani yetu, na hili linafanywa na kila Mkristo wa kweli kwa kiwango fulani. Vinginevyo anajionyesha kuwa ni mwamini bandia (ona Warumi 8:5-14).

Vile vile ni wajibu wetu kufanya upya nia zetu kwa Neno la Mungu, maana lazima tujue mapenzi Yake kabla ya kuyatenda. Hata katika hilo pia Mungu hutusaidia kwa njia ya huduma ya kufundisha ya Roho Mtakatifu na kwa kupitia wanadamu waliotiwa mafuta kuwa waalimu. 

Nia zetu zinapofanywa upya na kweli Yake, tunabadilishwa (ona Yohana 8:31-36; Warumi 12:2). Kisha, tuna wajibu wa kutokuwa wasikilizaji tu wa neno bali watendaji pia (Yakobo 1:22).

Lazima mlingano huo utunzwe. Japo Maandiko yanafundisha juu ya wajibu wa Mungu na wa binadamu, watu wengi hukazia kimoja na kuacha kingine.  Yamekuwepo makundi mawili kihistoria – wanaojaribu kuwa watakatifu kwa nguvu zao wenyewe, na wanaopinga juhudi zozote za kibinadamu kwa habari ya utakatifu, wakimwachia Mungu kila kitu. 

Pande zote mbili zina orodha ndefu ya maandiko, na kama wangetazama orodha zao wote wangetambua kwamba wote wako sawa na wote wamekosea. Ukweli uko katikati, mahali ambapo orodha zote mbili zinaheshimiwa. Hakuna mstari mmoja unaoeleza vizuri mlingano huo kuliko Wafilipi 2:12 na 13. Unasema hivi:
Basi wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema (Maneno mepesi kutilia mkazo).
Tunda ambalo Roho huzaa ndani yetu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi, lakini, matunda hayo yataonekana maishani mwetu kwa ushirikiano wetu tu. Ni lazima tufanye kitu fulani kwa sababu, kulingana na Maandiko, zipo nguvu kama tatu hivi zinazopinga matunda hayo.
(1) Mungu ameturuhusu sisi kubakia “duniani”, dunia ambayo inatujaribu tusiwe na upendo au kupendeka, tuwe na huzuni, tuwe na wasiwasi, tusivumilie, tusiwe wema, tuwe waovu, tusiwe waaminifu, tuwe wakali na wenye kujitosheleza.

(2) Ingawa Mungu ametujaza kwa Roho Wake, na kutupa asili mpya na kuvunja nguvu za dhambi juu yetu, Yeye pia ameruhusu mabaki ya asili yetu ya kale ya dhambi kubakia ndani yetu. Kitu hicho Paulo anakiita “mwili”.

(3) Ingawa tumekombolewa kutoka ufalme wa Shetani na sisi si watoto wake tena kiroho, tunajikuta kama wale Wakristo wa zamani tukiwa katika uwanja mkubwa uliojaa simba wanaounguruma, wenye lengo la kutumeza (ona 1Petro 5:8). Shetani na mapepo yake hutusumbua na kutunyanyasa na kutujaribu ili tufanye yale ambayo Mungu amekataza.
Hao watatu ndiyo adui zetu: dunia, mwili na shetani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni