Mwanamume Anamfanyaje Mkewe Azini?
Ona maneno ya Yesu, kwamba,
“Yeyote
amwachaye mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi.”
Hili tena linatufanya tuamini kwamba hakuwa anaweka sheria
mpya ya kuoana tena, bali alikuwa anadhihirisha tu ukweli kuhusu dhambi ya mtu
anayemwacha mkewe bila sababu nzuri. “Amfanya kuwa mzinzi.” Kuna wanaosema kwamba Yesu
alikuwa anamzuia huyo mwanamke kuolewa tena, kwa sababu anasema huo ni uzinzi.
Lakini si hivyo.
Mkazo uko kwenye dhambi ya mwanamume anayemwacha mkewe,
kwamba, kwa sababu ya kile anachokitenda, mke wake atakuwa hana lingine
la kufanya isipokuwa kuolewa tena, ambayo si dhambi kwa upande wake maana yeye
ameathirika kutokana na ubinafsi wa mumewe.
Machoni pa Mungu ni kwamba, kwa kuwa mwanamume alimwacha
mkewe na kumwingiza kwenye kuolewa tena, ni kama amemlazimisha aingie kitandani
na mwanamume mwingine.
Basi, yule anayedhani hajatenda uzinzi anakuwa na
hatia kwa uzinzi mara mbili – wa kwake na wa mkewe.
Yesu hakusema kwamba Mungu anamhesabu mke aliyeathiriwa na
talaka kwamba ana hatia ya uzinzi, maana hiyo isingekuwa halali, tena ingekuwa haina
maana kabisa kama huyo mke aliyeathiriwa asingeolewa.
Mungu angewezaje kusema kwamba ni mzinzi kama asingeolewa?
Isingekuwa na maana kabisa. Basi, ni dhahiri kwamba Mungu anamhesabu huyo
mwanamume kuwa na hatia kwa uzinzi wake mwenyewe na “uzinzi” wa mkewe, ambao
kweli si uzinzi kwake maana ni ndoa ya pili ambayo ni halali kabisa.
Sasa – vipi kuhusu maneno ya Yesu yafuatayo kwamba, “na mtu akimwoa mwanamke aliyeachwa
anazini”? Ni mawili tu yanayoweza kueleweka. Aidha Yesu alikuwa anaongeza
hatia ya uzinzi wa tatu dhidi ya mtu anayedhani kwamba hajawahi kuzini (kwa
sababu ile ile kama aliyotumia kuongeza hatia ya pili), au Yesu alikuwa anasema
kuhusu huyo mwanamume anayemtia moyo mwanamke aachane na mumewe ili waoane,
“asizini”. Kama Yesu alikuwa anasema kwamba mwanamume yeyote duniani anayemwoa
mwanamke aliyeachwa anazini, basi kila mwanamume wa Israeli alizini katika
kipindi cha miaka mia nyingi ambaye, katika kutimiza Torati ya Musa, alimwoa
mwanamke aliyeachika. Ukweli ni kwamba kila mwanamume siku hiyo aliyekuwa
anamsikiliza Yesu, aliyekuwa amemwoa mwanamke aliyeachika kwa kufuatana na
Torati ya Musa, alikuwa na hatia ya kosa ambalo hakuwa na hatia yake muda mfupi
kabla ya hapo, na Yesu akawa amebadilisha sheria ya Mungu hapo hapo. Tena, kila
mtu katika wakati ujao ambaye alimwoa mtu aliyeachwa, kwa kuamini neno la Paulo
katika barua yake kwa Wakorintho kwamba hilo si dhambi, alikuwa ametenda dhambi
– ni mzinzi.
Jinsi Biblia ilivyo inapelekea mtu kumstahi sana mwanamume
aliyeoa mwanamke aliyeachwa. Kama yeye ni mwathirika wa ubinafsi wa mume wake
wa kwanza, asiye na hatia, ningemstahi sana mwanamume huyo, kama ambavyo
ningemstahi sana mwanamume anayeoa mjane na kumtunza. Kama huyo mwanamke
alikuwa na sababu ya kulaumiwa kwa talaka yake, bado ningemstahi sana kwa kuwa
na moyo wa Kristo kwa kuamini kwamba kuna kilicho bora kwake, na kwa neema yake
ya kukubali kusahau yaliyopita na kujaribu. Kwa nini mtu yeyote aliyesoma
Biblia, mwenye Roho Mtakatifu ndani yake aamue kwamba Yesu alikuwa anamkataza
kila mtu asioe au kuolewa na yeyote aliyeachika? Hilo linaingiaje kwenye ukweli
kwamba Mungu ni mwenye haki – haki ambayo haimwadhibu yeyote kwa kuwa
mwathirika – kama mwanamke ambaye anaachwa pasipo kuwa na kosa? Hoja kama hiyo
inaingiaje kwenye ujumbe wa Injili, wenye kutoa msamaha na nafasi nyingine kwa
wenye dhambi wanaotubu?
Biblia inasema tena na tena kwamba talaka inahusisha dhambi
kwa mmoja au kwa wenzi wote wawili. Mungu hakukusudia mtu yeyote aachane na
mwenzake katika ndoa, lakini kwa rehema Zake alitoa mwanya wa talaka kama
uasherati ukitokea. Kwa rehema pia aliweka mpango kwa watu walioachika kuoa na
kuolewa tena.
Kama si kwa sababu ya maneno ya Yesu kuhusu kuoa na kuolewa
tena, hakuna msomaji yeyote wa Biblia ambaye angedhani kwamba kuoa na kuolewa
tena ni dhambi (isipokuwa kwa habari za matukio mawili nadra sana katika agano
la kale, na moja la nadra sana katika agano jipya, yaani, kuoa na kuolewa tena
baada ya mtu kuachana na mwingine aliyeokoka). Ila, tumepata njia inayokubalika
ya kulinganisha kile alichosema Yesu kuhusu kuoa na kuolewa tena, na sheria
kali zaidi yenye kukataza kuoa au kuolewa tena kwa kila hali. Hii sheria
haifanyi kazi kwa wale ambao wamekwisha achana na kuingia katika ndoa zingine
(maana ni sawa na kurudisha mayai yaliyopikwa yawe mabichi), na ni moja ambaye
ingesababisha mkanganyiko wa hali ya juu na kuwapelekea watu kuvunja sheria
zingine za Mungu. Badal ayake, tumeona kwamba Yesu alikuwa anawasaidia watu
kutambua unafiki wao. ALikuwa anawasaidia wale walioamini kwamba hawatazini
kamwe waone kwamba walikuwa wanazini kwa njia zingine, kwa tamaa zao na kwa
mtazamo wao mwepesi kuhusu sababu za kuachana.
Kama Biblia nzima inavyofundisha, msamaha hutolewa kwa wenye
dhambi wanaotubu, bila ya kujali dhambi yao, na nafasi ya pili na ya tatu
hutolewa kwa wenye dhambi – pamoja na walioachika. Hakuna dhambi katika kuoa na
kuolewa tena kwa aina yoyote katika agano jipya, isipokuwa kwa mwamini
aliyeachana na mwamini mwenzake. Na hilo halipaswi kutokea kwa sababu waamini
wa kweli hawafanyi mambo ya uchafu, na kwa sababu hiyo hakuna sababu halali ya
kuachana. Ikitokea kwa nadra, wote wawili wabaki kama walivyo au wapatane.
MWISHO
WA SOMO LOTE
Mungu akuinue kwa kufuatilia somo hili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni