Ijumaa, 10 Februari 2017

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU (9)



Usisahau Kwamba Yesu Alikuwa Anazungumza Na Mafarisayo. Baada ya kujua hayo, tutaelewa vizuri zaidi kilichokuwa kinamkabili Yesu. Mbele yake walisimama kundi la waalimu wa dini wanafiki, wengi ambao – kama si wote basi – walikuwa na talaka moja au zaidi, na pengine ni kwa sababu walikuwa wamepata wanawake warembo zaidi. (Si bahati kwamba maneno ya Yesu kuhusu talaka katika Mahubiri ya Mlimani yanafuata maonyo Yake makali sana kuhusu tamaa, na kusema ni aina ya uzinzi.) Na bado walikuwa wanajihesabia haki, wakidai kwamba wameishika Torati ya Musa.
Swali lao tu linadhihirisha jinsi walivyoegemea upande mmoja. Waliamini kabisa kwamba mtu angeweza kumwacha mke wake kwa sababu yoyote. Yesu akadhihirisha ufahamu wao mbovu wa kusudi la Mungu kuhusu ndoa kwa kurejea maneno ya Musa juu ya ndoa katika Mwanzo sura ya 2. Mungu hakukusudia kuwepo na talaka zozote, achilia mbali talaka “kwa sababu yoyote,” lakini viongozi wa Israeli walikuwa wanawaacha wake zao kiholela tu!
Inaonekana Mafarisayo walijua tayari msimamo wa Yesu kuhusu talaka, maana alikwisha kuutamka hadharani. Basi wakawa na pingamizi tayari:
“Mbona basi Musa aliagiza apewe hati ya talaka na kumwacha?” (Mathayo 19:7).
Hapo tena swali lao linaonyesha jinsi walivyogemea upande mmoja. Limeulizwa kana kwamba Musa alikuwa anawaagiza wanaume wawaache wake zao baada ya kugundua “neno ovu,” mradi tu watoe hati ya talaka. Lakini, kama tujuavyo kutokana na Kumbukumbu 24:1-4, Musa hakusema hivyo hata kidogo. Yeye alikuwa anaweka sawa ndoa ya tatu ya mwanamke – akimzuia asiolewe tena na mume wake wa kwanza.

Kwa vile Musa alitaja talaka, bila shaka talaka ilikuwa inaruhusiwa kwa sababu fulani. Lakini ona kwamba neno alilotumia Yesu katika jibu lake – aliruhusu – ni tofauti na chaguo la Mafarisayo – aliamuru. Musa aliruhusu talaka, hakuamuru. Na sababu ya Musa kuruhusu talaka ni ugumu wa mioyo ya Waisraeli. Yaani – Mungu aliruhusu talaka kama tendo la huruma tu kwa hali ya dhambi ya watu. Alijua watu wasingekuwa waaminifu kwa wana ndoa wenzao. Alijua uchafu ungekuwepo. Alijua mioyo ya watu ingevunjika. Basi, akatoa ruhusa kwa talaka. Hakuwa amekusudia hivyo tangu mwanzo, lakini dhambi ililazimisha hivyo.
Kisha Yesu akaweka sheria ya Mungu wazi kwa Mafarisayo, akifafanua kile ambacho Musa anakiita “neno ovu”.
“Yeyote amwachaye mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, akamwoa mwanamke mwingine, azini” (Mathayo 19:9).
Machoni pa Mungu, uzinzi ndiyo sababu halali pekee kwa mwanamume kumwacha mke wake. Na ni rahisi kueleweka. Ni kitu gani kingine ambacho mwanamume au mwanamke anaweza kufanya, kikawa kibaya kwa mwenzake kuliko hicho? Mtu anapozini, anatuma ujumbe mchungu sana. Kwa hakika Yesu hakuwa anazungumzia uzinzi tu aliposema hayo. Bila shaka hata kumbusu mwenzi wa mwingine na kumshika-shika ni kitu kibaya sana, kama ilivyo tabia ya kuangalia picha mbaya za ngono, au matendo mengine yasiyofaa ya mahusiano kimwili. Kumbuka kwamba Yesu alifananisha tamaa na uzinzi katika Mahubiri Yake ya Mlimani.
Tusije kusahau Yesu alikuwa anasema na nani – ni Mafarisayo waliokuwa wanaachana na wake zao kwa sababu yoyote na kuoa haraka haraka, lakini hao hao wasingezini kamwe ili wasivunje amri ya saba. Yesu aliwaambia wanajidanganya wenyewe. Walichokuwa wanafanya hakikuwa tofauti na uzinzi. Ndiyo ukweli huo. Yeyote aliye mkweli anaweza kuona kwamba mwanamume anayemwacha mkewe ili amwoe mwanamke mwingine anafanya kitu ambacho mzinzi hufanya. Tofauti ni kwamba, huyu mwingine anahalalisha uzinzi wake.

MWISHO WA SEHEMU HII YA SOMO

Tutakutana katika inayofuata ya somo hili Mungu akuinue kwa kufuatilia somo hili.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni