Jumapili, 5 Februari 2017

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU (6)


Mwl Furaha Amon



Katazo La Pili Lililo Dhahiri Kinyume Cha Kuoa Tena
Je, Mungu alitoa “nafasi nyingine” ngapi kwa wanawake walioachika? Je, tuamue kwamba Mungu aliwapa wanawake walioachika nafasi moja zaidi katika Torati ya Musa, akiwaruhusu kuolewa tena mara moja tu? Huo ni uamuzi usio sahihi. Tunasoma hivi baadaye katika Torati ya Musa,
Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake na kumtoa katika nyumba yake. Naye akiisha kuondoka katika nyumba yake, ana ruhusa kwenda akawa mke wa mtu mwingine. Na huyo mumewe wa sasa akimchukia, na kumwandikia hati ya kumwacha na kumpa mkononi mwake na kumtoa katika nyumba yake; au akifa yeye mumewe wa sasa aliyemtwaa kuwa mkewe; yule wa kwanza aliyemwacha asimtwae kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa unajisi; kwa kuwa haya ni machukizo mbele za BWANA; kwa hiyo usiitie dhambini nchi, akupayo BWANA Mungu wako, iwe urithi (Kumbu. 24:1-4).
Ona kwamba katika mistari hii, kitu kinachokatazwa peke yake ni yule mwanamke aliyeachika mara mbili (au aliyeachika mara moja na kuwa mjane mara moja) kuolewa tena na mumewe wa kwanza.
Hakuna kinachosemwa kwamba ana hatia kwa sababu ameolewa mara ya pili. Na baada ya kuachika mara ya pili (au kuwa mjane kwa mume wake wa pili), alichokatazwa tu ni kumrudia mumewe wa kwanza. Ni kwamba, angekuwa huru kuolewa na mwanamume mwingine yeyote (ambaye yuko tayari kujaribu bahati yake!). Ingekuwa ni dhambi kwake kuolewa na mtu mwingine yeyote, kusingekuwepo haja kwa Mungu kutoa maagizo hayo ambayo ni wazi kabisa. Kitu cha pekee ambacho Mungu angesema ni hiki: “Watu walioachika hawaruhusiwi kuoa au kuolewa tena.”

Tena – Kama Mungu alimruhusu mwanamke aina hii kuolewa mara ya pili, basi yule mwanamume aliyemwoa baada ya kuachika mara ya kwanza asingekuwa na hatia yoyote. Na kama aliruhusiwa kuolewa mara ya tatu, basi mwanamume yeyote ambaye angemwoa baada ya kuachika mara mbili asingekuwa na dhambi (isipokuwa kama alikuwa ndiye mumewe wa kwanza). Basi – Mungu anayechukia talaka anawapenda watu walioachika, na kwa rehema aliwapa nafasi nyingine.
                
                       MWISHO WA SEHEMU YA TANO


Endelea kufuatilia somo hili katika sehemu ya sita, na kama una maswali au unahitaji msaada zaidi tunaweza kuwasiliana kwa simu namba 0677 609056

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni