Mwl:
Furaha Amon
Utangulizi:
Watu wengi mno ndani ya
makanisa wana kiu ya kupata ujazo wa Roho Mtakatifu, lakini bado kuna tatizo
kubwa sana linalohusiana na kutomwelewa vizuri Roho Mtakatifu. Kwa kuwa kiu hii
ni kubwa, na tatizo la kutomwelewa Roho Mtakatifu ndani ya kanisa ni kubwa sana
nimeona ni vema nitumie nafasi hii kutoa mchango kidogo wa kukusaidia kuelewa
kwa kiasi habari za Roho Mtakatifu.
ROHO MTAKATIFU SIO NGUVU KAMA
YA UMEME
Watu wengine wanafikiria
kuwa Roho Mtakatifu ni nguvu kama vile
ilivyo nguvu ya umeme, mawazo hayo sio sahihi kabisa. Ni kweli kuwa mtu
anapompokea Roho Mtakatifu hufunikwa na nguvu isiyo ya kawaida. Lakini nguvu
hii sio Roho Mtakatifu. Katika kitabu cha Matendo ya mitume, Yesu aliwaambia wanafunzi
wake kuwa watapokea nguvu akiisha kuwajilia Roho Mtakatifu. Lakini ukweli ni
kwamba Roho Mtakatifu mwenyewe sio nguvu bali ni nafsi hai ya Mungu.
MAMBO YANAYODHIHIRISHA KUWA
ROHO NI NAFSI NA NI MUNGU:
ANAWEZA KUHUZUNIKA.
“Wala
msimhuzunishe Yule Roho Mtakatifu wa Mungu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa
muhuri hata siku ya ukombozi” (Efeso 4:30)
Hapa Roho Mtakatifu kama
alivyo mwanadamu, anaweza kuhuzunishwa na kuhuzunika. Ukweli ni kwamba nguvu
kama ilivyo ya umeme au nyingine iwayo yoyote ile haiwezi kuhuzunika, lakini
roho kama nafsi hai anaweza kuhuzunishwa pale watoto wa Mungu wanapoenda
kinyume na neno la Mungu.
HUTUOMBEA KWA KUUGUA
KUSIKOWEZA KUTAMKIKA:
“
kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi
ipasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa” (Rum
8:26)
Huu ni udhibitisho mwingine
unaoonyesha kuwa Roho Mtakatifu ni nafsi, huweza kutuombea kwa kuugua kusikoweza
kutamkwa. Nguvu haiwezi kumwombea mwanadamu kwa Mungu kwa kuugua, bali jambo
hili huweza kufanywa na nafsi iliyo hai pekee.
ANAWEZA KUAMBIWA UONGO.
“Petro
akasema, Anania, kwa nini shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho
Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?” (Matendo 5:3)
Hapa tunamwona Petro
akimwonya Anania kuhusiana na mali aliyoipata baada ya kuuza kiwanja chake.
Alipouza kiwanja chake hakuleta fedha yote miguuni pa mitume kama walivyokuwa
wamepatana katika kanisa! Anania alidhani kuwa kosa alilotenda
halitatambulikana, hivyo aliamua kusema uongo mbele za mtumishi wa Mungu. Petro
naye kwa njia ya ufunuo wa Roho Mtakatifu, anamwambia wazi Anania na safila
mkewe kuwa hawakumwambia uongo mwanadamu bali Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni
nafsi ndiyo maana anaweza kuambiwa uongo; nguvu haiwezi kuambiwa uongo.
ANAWEZA KUFANYIWA
KUFURU:
“Kwa sababu hii nawaambia, kila neno la kufuru
watasamehewa wanadamu, ila kumkufuru Roho Mtakatifu hawatasamehewa” (Mathayo
12:31)
Huu nao ni uthibitisho
mwingine unaoonyesha kuwa Roho Mtakatifu si nguvu bali ni nafsi iliyo hai. Kwa
kuwa ni nafsi hai anaweza kutukanwa na kunenewa maneno ya kufuru na wale
waliokwisha kupewa Nuru na kukionja kipawa cha mbinguni; wale waliofanywa
washirika na Roho huyu na kulionja neno zuri la Mungu pamoja na kuzionja nguvu
za zamani zijazo. Roho mtakatifu angelikuwa nguvu kama ilivyo nguvu ya umeme
basi asingeliweza kunenewa maneno ya kufuru maana hakuna anayeweza kuikufuru
nguvu.
ANAWEZA KUFANYIWA JEURI.
Pamoja na sababu hizi
zinazomfanya Roho Mtakatifu kuwa nafsi halisi na hai neno linatuambia kuwa Roho
Mtakatifu anaweza kufanyiwa jeuri na watoto wa Mungu. Hili hutokea pale watoto
wa Mungu wanapokataa kwa kukusudia kuitii sauti ya Roho wa Mungu ndani yao na
kuamua kuasi. Neno la Mungu katika waebrania 10:29 linatuambia kuwa;
“Kila
afanyaye dhambi kwa kukusudia baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, anamfanyia
jeuri Roho wa mema au Roho Mtakatifu”.
Kwa ujumla kuna mifano
mingi ya kimaandiko inayothibitishwa kuwa Roho Mtakatifu ni nafsi hai, ila kwa
hii michache nimeielezea ili ikusaidie kutafuta mingine inayofanana na hiyo.
MWISHO
Kwa
leo somo letu linaishia hapa, usikose kufuatilia sehemu inayofuata ya somo hili.
Kwa msaada zaidi tuwasiliane 0677 609056
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni