Mwl:
Furaha Amon
Utangulizi:
Mwishoni mwa mwaka 1999 nilipata
nafasi ya kwenda kuhubiri katika kanisa moja la Assemblies of God.
Ni umbali wa kama kilometa 78 kutoka katika mji
ambao nilikuwa naishi kwa wakati huo. Kanisa hili lilikuwa na mtumishi Mchungaji
ambaye tulikuwa tunafanya kazi wote serikalini lakini yeye baadae neema
ilimzidi akaamua kuacha kazi na kuingia shambani kwa Bwana.
Mtumishi huyu
alikuwa ni kama baba yangu wa kiroho, kwa sababu ndiye niliokokea mikoni mwake
na kiukweli ndiye aliyenilea kwa uangalizi wa karibu sana, tangu siku ile nilipokata
shauri na kuamua kumfuata Bwana Yesu. Wakati huu Napata nafasi ya kwenda
kuhubiri nilikuwa nakaribia miaka kumi kwenye maisha ya wokovu. Kwa kuwa
ilikuwa ndio nasimama kwa mara kwanza kufanya huduma hiyo katika kanisa lake,
ilibidi Mchungaji anitambulishe kwa washirika wake wapatao kama mia nne hivi
kwa ibada ile ya asubuhi.
Mchungaji aliwaeleza washirika wake jinsi alivyokutana
na mimi na mwonekano wangu, aliwaambia kwamba mimi nilipohamishiwa kikazi
sehemu aliyokuwepo tulikuja vijana kama sita, kati yetu mimi ndio nilikuwa
naonekana mtata zaidi. Na kwa hiyo hawakuwa na mpango kabisa wa kunipa habari
njema za wokovu. Na kwa kweli nakumbuka nilikuwa jeuri sana, na wasingeweza
kunikabili wakati huo bila kukorofishana, na ilikuwa hatari sana kukorofishana
na mimi wakati huo kwa sababu naweza kukuvizia na kukujeruhi japo kisirisiri. Na
hii hali hata baada ya kuokoka ilikuwa bado ipoipo kidogo. Ilikuja kwisha baada
ya kuoa, na kwa sababu mke wangu ni mtu mwenye huzuni nyingi sana, hapendi
kabisa nifanye ukorofi wa aina yeyote ile, hivyo kila ninapotaka kufanya
maamuzi fulani sijiangalii mwenyewe binafsi kama ilivyokuwa zamani, pamoja na
kumuangalia Mungu lakini huwa namfikiria sana mke wangu asije akahuzunika. Lakini
pamoja na familia yangu kwa ujumla.
Mchungaji mwenyeji wangu
aliwaambia washirika wake kwamba, katika kundi letu walimlenga kijana mmoja wa
kichaga ambaye alikuwa anaonekana anamwelekeo wa kuokoka mapema ingawa hakuweza
kusimama katika wokovu baadae alianguka kiroho, na mwisho alifariki dunia bila
kupata neema ya wokovu.
Kwa sababu tulikuwa tunakaa chumba kimoja na huyo
ndugu, nilikuwa naona juhudi zao za kumfuatilia mara kwa mara. Na mimi
nakumbuka siku moja nilitafakari sana kuhusu uwepo wa Mungu. Nikajisemea moyoni
kwamba, ngoja nifanye utafiti kujua kama kweli Mungu yupo au hayupo, ingawa
nimelelewa katika familia ya kikristo lakini mwenyewe binafsi nilikuwa sina
uhakika kama kweli Mungu yupo. Niliamini zaidi katika sayansi kwamba uhai
ulijitokeza wenyewe kwa njia ya mageuzi.
Katika utafiti wangu nikijua kwamba Mungu hayuko, nitachagua maisha
ya kuishi kwa bahati nikakuta yupo. Kwa hiyo nikaona utafiti huu niufanye kwa
makanisa yenye msimamo wa imani kali, na walokole wa kipentekoste nikaona ndio
watakaonifaa. Kwa hiyo bila kuhubiriwa na mtu yeyote, nilimfuata huyo Mchungaji,
na kumwambia mimi nataka kuokoka!. Mchungaji anawaambia washirika wake kwamba wao
walishangaa na pia hawakuamini, wakajua shetani anataka kunitumia kuvuruga mpango
wao kumpata mtu waliyemlenga. Kwa hiyo wakakubaliana kwamba nikikubali
kuongozwa sala ya toba tu wataunganisha na ubatizo wa Roho Mtakatifu, bila hata
kubatizwa kwa maji mengi, hata kama sijui habari za Roho Mtakatifu, mwenyewe
anasema walitaka Roho Mtakatifu mwenyewe anibane kisawasawa. Na kweli siku
iliyofuata walinipeleka katika kakanisa fulani kadogo kana washirika kama
ishirini hivi. Wanaendesha ibada zao
katika shule moja ya msingi karibu ya sehemu yetu ya kazi. Na kweli baada ya
kuongozwa sala ya toba alinipeleka sehemu moja yenye majengo ya ghorofa ambayo hajaisha
ujenzi wake yametelekezwa bila kukamilika. Akanipandisha kwenye ghorofa ya
pili, tukiwa watu wawili tu. Akaniambia piga magoti, akanielekeza maneno ya
kusema, harafu akawa ananilazimisha niyaseme maneno hayo kwa kasi sana ya
kujichanganya na nilipokuwa nikikosea ndio akawa ananiambia hiyo ndio lugha anayoitaka.
Na kunihimiza endelea hivyohivyo kuongea vitu visivyoeleweka. Kwa kweli sababu
nilikuwa katika utafiti sikufungua moyo wangu kabisa. Tulikaa eneo hilo la
upweke karibu masaa matatu. Huku yeye anaendelea na maombi huku akinisikilizia
mimi, nikiongea lugha ambavyo akili yangu haina matunda kabisa ni kama
najifanyisha fanyisha tu. Kwa kweli maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga.
Ilibidi
tu nifanye kujisemeshasemesha maneno yale huku magoti yakiniuma kama mtu
aliyepewa adhabu ya kijeshi ya kutembelea magoti. Baadae aliniambia tayari
nimepokea ujazo wa Roho Mtakatifu. Kwa kweli mpaka wakati huo mimi sikuwa
nimeona badiliko lolote zaidi ya kujihisi kama mtahiniwa aliyefanya mtihani ambao
hajafundishwa na hana uhakika wa majibu yake, nilikaa nikisubiri majibu ambayo
sina uhakika nayo. Kila siku namshukuru sana Mungu kwa ajili ya ndugu zangu
hawa. Japo wao walikuwa na vyeo vikubwa kazini, lakini walishuka chini na
kunitumikia, kuhakikisha kwamba ninasimama. Nakumbuka ni kama walikuwa
wanafanya zamu. Kuhakikisha sipati nafasi ya kushirikiana na marafiki zangu wa
zamani. Kwa hiyo walihakikisha ninafuatana nao kwa kubadilisha kwenda kwenye
huduma mbalimbali walikokuwa wanaitwa kuhudumu. Kwa kweli walikuwa na uwezo na
nguvu kubwa sana kiroho, kiasi kwamba waliweza kuamuru mvua isimame ili wafanye
kitu fulani na mvua ilitii. Hayo mambo yalikuwa yakifanyika mbele ya macho
yangu. Wakikwambia nenda nyumbani kuna hiki na kile, ukienda unakuta kama vile
walivyokwambia. Kwa ujumla hawa marafiki zangu walinifaa sana. Sasa pamoja na
kunihakikishia kuwa nimepokea ujazo wa Roho Mtakatifu, ilichukua siku kama tatu
hivi, nikiwa kwenye maombi yangu ya kubangaiza ghafla nikaona ulimi umekuwa
mwepesi ninaongea lugha ambayo siielewi na nimeingiwa na hali fulani ya furaha
na amani na kutamani kuendelea kuomba. Ndio nikaanza kujua kwamba huyo ndio
Roho Mtakatifu ambaye Mungu alituahidi kwamba tutampokea. Kama ilivyokuwa
kwangu mimi ndivyo ilivyo hata sasa. Watu wengi mno ndani ya makanisa wana kiu
ya kupata ujazo wa Roho Mtakatifu, lakini bado kuna tatizo kubwa sana
linalohusiana na kutomwelewa vizuri Roho Mtakatifu. Kwa kuwa kiu hii ni kubwa
na tatizo la kutomwelewa Roho Mtakatifu ndani ya kanisa ni kubwa sana nimeona
ni vema nitumie nafasi hii kutoa mchango kidogo wa kukusaidia kuelewa kwa kiasi
habari za Roho Mtakatifu.
Kwa kupitia mafundisho
haya, wale wenye kiu ya kumpokea Roho Mtakatifu na nguvu zake wataweza kupokea;
na kwa wale wasio na kiu ya kupokea, kutokana na kutomwelewa Roho Mtakatifu na
faida zake wataweza kuumbiwa kiu na
hatimaye kupokea. Ni matumaini yangu kuwa mafundisho haya, yatayaondoa kwa
kiasi kikubwa matatizo yaliyopo ndani ya kanisa yanayohusiana na huduma hii ya
Roho Mtakatifu.
Kwa
leo naishia hapa, usikose kufuatilia somo hili katika sehemu inayofuata. Mungu
akubariki sana, kwa maoni na ushauri tuwasiliane kwa namba 0677 609056
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni