Jumatano, 17 Oktoba 2012

KUKWAMA KWA MALENGO




Tunaposhindwa kufikia malengo yetu tuliyojiwekea, kwa mfano kufeli mitihani, kushindwa kuendelea na ujenzi au kufanya hiki na kile tulichokusudia, mara nyingi hutuingiza kwenye huzuni, lakini kanuni za mafanikio yoyote duniani zinaanzia katika mkwamo.

Hivyo basi tunapoona tumeshindwa kufikia lengo la kile tulichotaka kukifanya haimaanishi kuwa hatuwezi, bali tumepungukiwa nguvu ambazo lazima tuzitafute kutoka katika miili yetu kwa kutumia uwezo na uelewa wetu ambao ni mkubwa mara 1000 ya tunaotumia kila siku katika maisha yetu.

Unapokuwa umekwama katika kitu chochote, jiulize sababu  kwanini umeshindwa. Baada ya kupata sababu hizo tafakari njia na mbinu mpya za kuelekea kwenye ushindi huku ukiamini kuwa mafanikio yanatokana na juhudi pamoja na kutorudia makosa yaliyoleta mkwamo. Haifai kukata tamaa, hata kamaumekwama mara elfu moja.

Tunapokwama mara kwa mara ni vema tukawashirikisha watu katika kila jambo tunaloona kuwa linasumbua akili, ushirikishaji huo unaweza kutusaidia kupata uzoefu kutoka kwa wenzetu ambao pengine wamevuka vikwazo vikubwa tofauti na hivyo tunavyokabiliana navyo.
Jambo la mwisho la kuzingatia tunapoanza hatua mpya za kuelekea katika ushindi tusikubali kurudia kosa, kama kufeli kwako mtihani kulitokana na kutosoma kwa bidii, usirudie kosa hilo ongeza bidii za kusoma au kama umeshindwa kujenga nyumba kwa sababu ya kuwa na matumizi makubwa ya pesa usikubali kuendelea na matumizi hayo, badala yake jibane na utimize nia yako.

MKE KUANZA/KUACHISHWA KAZI

Inaelezwa katika uchunguzi wa kitaalamu kuwa wanaume wengi huhofia wake zao kuanza kazi, hii inatokana na wivu wa kimapenzi . Wanaume hudhani kuwa mke anapokwenda kuajiriwa atakuwa na nafasi kubwa ya kushawishiwa kuanzisha uhusiano mpya na wanaume wengine.

Lakini ukweli ni kwamba huzuni hii mara nyingi huwa ni ya bure na matokeo yake huzaa wivu ambao husambaratisha ndoa na uhusiano. Kitu cha msingi kinachotakiwa kufanywa na mwanaume ni kuwa karibu na mkewe kumjengea hali ya kujiamini na kumtimizia yote anayostahili kama mke, likiwemo tendo la ndoa na ukaribu ambao mara nyingi unatajwa kuwa tiba kubwa ya usaliti.

Aidha kwa wale ambao wake zao wanafukuzwa kazi, jambo la muhimu ni kutiana moyo na kushirikiana kwa ukaribu kutumia muda wa dhahabu kupata kazi. Hili linatakiwa kwenda sambamba na kujaliana wakati wote wa tatizo. Hali yoyote ya kumtenga na kumwacha mkiwa ni hatari kwa uhusiano.
Pamoja na hilo endapo kipato cha mwanamke kilikuwa ni sehemu ya matumizi ya nyumbani basi mume na mke wanawajibu wa kukaa pamoja na kupanga upya matumizi yao ili kuondoa pato ambalo lilikuwa linatumika kutoka katika mshahara wa mwanamke ambaye kafutwa kazi.

CHANZO: Kutoka katika mitandao

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni