Jumanne, 4 Desemba 2012

HALI HALISI YA KANISA LA TANZANIA


Moses Kulola

INGAWA takwimu zilizotokana na Sensa ya taifa zinaonyesha kuwa Ukristo kwa ujumla wake unakua kwa kasi ndogo, ikiwa ni chini ya asilimia 35 ya Watanzania wanaokadiriwa kufikia milioni 40, takwimu hizi haziendani na hali halisi inayoonekana hata kwa macho ya kawaida.

Utafiti wa awali uliofanywa na Tanzania Christian Directory unaonyesha kuwa kasi ya ukuaji wa makanisa ya kiroho, unaoendana na idadi ya kubwa ya watu wanaookoka kila siku inapingana kwa kiasi kikubwa na takwimu za Sensa.
Ingawa takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya Wakristo na wapagani inakaribiana, huku Waislamu wakiwa ni wengi zaidi, vugu vugu la wokovu na ukuaji wa kasi wa makundi ya waumini wa makanisa ya Kiroho vinaashiria kuwa hali si kama inavyodhaniwa.
 Kwa mfano, utafiti kuhusu ukuaji wa makanisa unaonyesha kuwa Huduma ya Kitume na Kinabii ya Efatha imekua kutoka watu 100, miaka kumi iliyopita na sasa ina idadi ya watu 100,000 katika makanisa yake yaliyosambaa nchi nzima.Huu ni mfano wa kanisa moja tu la kiroho, na ikumbukwe kuwa Tanzania ina maelfu ya makanisa yanayokua kwa kasi ya kati. Katika kanisa hilo la Efatha ambalo watafiti walilitumia kama mfano, kwenye mkutano mmoja mwishoni mwa mwaka jana, jumla ya watu 2000, waliokoka baada ya semina ya wiki moja.
Inakadiriwa kuwa waumini 15,000 huhudhuria ibada ya Jumapili katika kusanyiko moja tu na kanisa hilo lina matawi kila kona ya Tanzania. Kulingana na ukweli huu lazima takwimu za Sensa ambayo hufanyika mara moja kila baada ya miaka 5, au 10 haziwezi kutoa hali halisi ya ukuaji wa makanisa. Dar es Salaam, ambayo ni kioo cha ukuaji wa makanisa, ina makanisa mengi yanayokua kiidadi kutokana na:
1.Watu kuyaacha maisha ya dhambi na kuamua kumpokea Bwana Yesu 

2.Kukua kibailojia, kutokana na watu kuzaliwa na kukulia katika imani ya Kikristo
3.Kuhama kutoka dini nyingine kwenda Ukristo wakivutwa na ishara na miujiza ambayo inadhihirika kila kukicha katika makanisa ya Kiroho.
UKUAJI WA UKRISTO NCHINI
Ukiachilia mbali Kanisa la Efatha linaloongozwa na Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira, ambalo linaaminika kuwa linaongoza kwa kukua kwa kasi na kuenea nchi nzima, likiwa na watumishi wanaosoma katika Chuo cha Huduma hiyo kilichopo Kibaha mkoani Pwani, Kanisa la Ufufuo na uzima, chini ya Askofu Josephat Ngawajima (maarufu kama kanisa la Misukule) nalo limekuwa na idadi kubwa ya watu wanaookoka kanisani hapo kila siku na inakadiriwa kuwa umati wa watu 12, 000 wanakutana pamoja kila Jumapili. Msisitizo wa kanisa hilo ni kuwafufua watu waliochukuliwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Mwishoni mwa mwaka jana kiongozi wa kanisa hilo alionyesha hadharani watu 150, ambao wanaaminika kuwa walirejeshwa kutoka mikononi mwa wachawi.

Hata hivyo utafiti unaonyesha kuwa kasi yake ya kujitanua nje ya Dar es Salaam, si kubwa sana na ukilinganisha na Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) linalongozwa na Askofu Zakaria Kakobe, likiaminika kuwa msisitizo wa mahubiri yake ni Utakatifu na kuzingatia maadili.

Pamoja na kuwa na msimamo mkali wa kuzingatia maadili na msimamo wa kuwapiga marufuku wanawake wasiofunika vichwa na waliovaa nywele za bandia kuingia kanisani humo, bado kanisa hilo limebaki kuwa miongoni mwa makanisa ya uamusho na lenye matawi sehemu nyingi za Tanzania.

Ngurumo ya Upako
Huduma hii iko chini ya mwanzilishi wake Mheshimiwa Nabii GeorDavie , na makao makuu yake yako nje kidogo ya jiji la Arusha, katika bara bara ya kuelekea Dodoma. Huduma ya Ngurumo ni miongoni mwa vituo vinavyokusanya idadi kubwa sana ya waumini kwa wakati mmoja.

Inaaminika kuwa zaidi ya watu 12,000 hukusanyika pamoja kumtukuza Mungu kila Jumapili na tayari inapanuka kwa kasi ya kutisha ikiwa na matawi katika mikoa mbali mbali ya Tanzania na nje.

Mafundisho ya Huduma hii yamelenga zaidi kwenye ukombozi na uponyaji. Kuna shuhuda nyingi za watu waliokuwa wamekaribia kufa walipoamini walipona na wako hai wakimtukuza Mungu wa mbinguni.

Pia ni mahali ambapo kuna shuhuda za kurejeshwa kwa watu waliokuwa wamechukuliwa misukule na wale ambao wanateswa na ibilisi.

Makala zake kwenye magazeti na vipindi vya Televisheni vimeelezwa kuwavuta watu wengi katika ufalme wa Mungu.

Living Water Center
Huduma hii kama ilivyo kwa huduma nilizotaja hapo juu, haikuanza siku nyingi sana, lakini pia imekuwa na uamusho mkubwa na tayari ina matawi kadhaa nchini ikiwa ni pamoja na jiji la Arusha na Mwanza.

Mikutano ya hadhara, iliyoongozwa na Kiongozi wake Mtume Onesmo Ndegi, katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha, pamoja na uwezo wake mkubwa wa kutumia njia za kisasa za mawasiliano kuhubiri, inaelezwa kuwa kivutio na uamsho mkubwa.

Muundo wa kanisa lake ambalo limejengwa kwa makuti kitaalamu na kuonekana kama kiota cha kitalii ni miongoni mwa mambo ya kipekee katika huduma hii ambayo huvutia watu wengi.

Kanisa hili ni pia linasisitiza mafundisho ya utakatifu, lakini likijikita zaidi kwenye ukombozi na mafanikio ya mwili na roho.

Kiongozi wake ni miongoni mwa wachungaji wa mwanzo kutumia televisheni kupeleka habari njema za injili ulimwenguni kote.

Mikocheni B. Assemblis of God
HILI ni kanisa la kipekee ambalo linaongozwa na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mchungaji Dk. Getrude Rwekatare, ambaye licha ya kuwa Mchungaji mwenye uwezo mkubwa wa kuhubiri, ni mwanamke ambaye mafanikio ya kimwili pia ni mfano wa mahubiri yake.

Pamoja na kuhubiri injili kwa muda mrefu tangu alipokuwa kiongozi wa wanawake kwenye kanisa la Tanzania Assemblies of God, Ilala, jijini Dar es Salaam, ni mwanaharakati wa haki za akina mama na watoto na mfanyabishara anayemiliki mtandao mpana wa shule za St. Mary’s International, Kenton, na kituo maarufu cha Redio kiitwacho Praise Power, ambacho kinatoa nafasi sawa kwa wahubiri wengine kuhubiri Injili kupitia vipindi vyake mbali mbali.

Kanisa lake pamoja na mambo mengine linahubiri Injili yenye msisitizo wa mafanikio. Pia anaendesha vituo kadhaa vya watoto yatima na tayari kanisa lake limefungua matawi katika jiji la Dar es Salaam.

Kanisa hili lilianzia kwenye majengo ya shule ya msingi Mikocheni mika tisa hivi iliyopita, lakini sasa limekua na kuweza kujenga jengo la ibada lenye uwezo wa kukusanya zaidi ya waumini 8,000 kwa ibada moja ya Jumapili.

Shule alipoanzia kanisa mchungaji huyo ameipa zawadi ya kuijengea majengo ya kisasa ya kufundishia na huu umebaki kuwa mfano wa jinsi kanisa linavyojali jamii.


HAKUNA LISILOWEZEKANA
Hii ni huduma ya Kiroho iliyoanzishwa na Askofu Sylvester Gamanywa, mmoja wa maaskofu vijana na shupavu mwenye jicho la kuona mbali na kushiriki katika harakati kadhaa.

Mara nyingi ni mtu wa kuingia katika kila jambo na kutumia mamlaka yake kutafuta ufumbuzi. Katika uchaguzi mkuu uliopita alikuwa miongoni mwa wahubiri wa kwanza kujitoa katika kuendesha kampeni ya kuhimiza amani na kuliombea taifa.

Akitumia kituo chake cha Redio ya Kikristo itwayo Wapo F.M, Askofu Gamanywa, aliongoza pia harakati za kuhimiza watu kubadili tabia ili kujikinga na gonjwa la UKIMWI, hapo serikali ikatambua mchango wake na akateuliwa kuwa mmoja wa Makamishina wa Tume ya kupambana na ugonjwa huo Tanzania.

Ingawa alikuwa mhubiri kwa muda mrefu, akimiliki pia Gazeti la Kikristo la Msema Kweli, Askofu Gamanywa alipata mafanikio makubwa katika miaka sita tu iliyopita ambapo uamsho mkubwa umedhihirika katika huduma yake.

Baada ya huduma yake kupanuka alifungua kituo cha miujiza na uponyaji huko Mbezi Beach, jijini kiitwacho BCIC, ambacho mbali ya kuwa ni kituo cha maombi na uponyaji kwa damu ya Yesu, ni mahali ambapo semina na masomo maalumu yanayolenga kuibadili tabia ya Watanzania hufanyika kwa mafanikio makubwa.

Kwa wakati huu Askofu Gamanywa, anaendesha kampeni iliyolenga kuokoa kizazi kijacho kwa kupambana na uharibifu wa maadili kwa vijana.

Calvary Assemblies of God (CAG)
Huduma hii ni moja kati ya huduma za kiroho hapa nchini, Ilianza miaka 15 iliyopita na imekuwa ikikua kwa kasi na kupata mafanikio makubwa sana ya kiroho. Mbeba maono wa huduma hii ni Mtume Dustun Maboya, ambaye yeye ndiye kiongozi mkuu wa huduma.

Hudumu hii chini ya Mtume Dustun Maboya, ilianzia mjini Morogoro mwaka 1994 huku ikiwa na waumini 200 tu, katika ibada moja na hadi kufikia sasa inakadiriwa kufikia zaidi ya waumini 5000 kwa ibada.

Msimamo na mkazo wa mafundisho ya huduma hii ni kuhubiri mafundisho ya wokovu na mafanikio ya kiroho na kimwili pia.

Mtume Dustan Maboya aliokoka mwaka 1977 na mwaka 1978 mara baada ya kupata wito wa kumtumikia Mungu alijiunga na chuo cha biblia cha mkoani Arusha na kuhitimu mwaka 1981. Baada ya hapo aliacha kazi na kuamua kumtumikia Mungu kwa kuanzisha huduma hii.

Kwa sasa Calvary Assemblies of God, chini ya Mtume Dunstun Maboya, imeenea nchi nzima na kufikisha idadi ya makanisa 460 kwa nchi nzima mjini na vijijini.

Silioam Ministry International
Huduma hii, ikiwa chini ya mbeba maono Mtume N.Z.Munuo, ilianza miaka mitano iliyopita na kuwa na makao yake makuu jijini Dar es salaam.

Huduma hii ambayo inaonyesha kukua kwa kasi sana, ilianza ikiwa na washirika watatu tu waliokuwa wakifanya ibada nyumbani kwa Mtume Munuo. 

Kwa sasa huduma hii imetanuka nchi nzima na kuwa na matawi kila Wilaya na inakadiriwa ibada moja inakusanya waumini zaidi ya 3000 kwa jumapili.

Msimamo na mkazo wa mafundisho ya huduma hii ni kuvunja misingi mibovu ya shetani ndani ya watu na kisha kuwajenga watu hao katika nguzo nne, NENO,IMANI, UTAKATIFU na UTII.

Mtume Munuo, alipata wito wa kumtumikia Mungu na kumjengea nyumba ya ibada ambayo watu watamwabudu katika roho na kweli akiwa mwajiriwa wa Shirika la Umeme nchini na baadaye aliamua kuacha kazi na kwenda kumtumikia Mungu. Hiyo ilikuwa mwaka 2003.

Kwa sasa huduma hii tayari imekwishaanzisha chuo cha Biblia kinachoitwa Siloam Bible College, ambacho kimetumika kuwaandaa watumishi mbalimbali wa Mungu kutoka katika makanisa na huduma mbalimbali hapa nchini. Kwa sasa hudumu hii ya Siloam hapa nchini, chini ya mtume N.Munuo, ina jumla ya makanisa yapatayo 70 nchini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni