Alhamisi, 29 Novemba 2012

BOB MARLEY MHUBIRI WA AMANI NA UPENDO BILA YESU




Mcheza mpira wa miguu, Mhubiri wa amani na upendo, Mwanamapinduzi, Mwanaharakati, Mpiganaji, Mwanasiasa, Mwanamuziki wa Reggae na Nyota ya kwanza katika ulimwengu wa tatu Bob Marley.


Alizaliwa akiitwa Robert Nesta Marley na mama wa Kijamaica mwenye asili ya Afrika, bi Cedella Booker na baba mwanajeshi Mwingereza aliyefariki kijana Robert akiwa bado mdogo sana akiwaacha katika umasikini mkubwa.



Bob Marley alizaliwa panapo usiku wa kuamkia Februari 6, 1945, St Anns Parish kijiji cha Nine Miles (maili tisa) huko Jamaica.

Kumbukumbu zake za utotoni na ujanani zimejaa harakati za maisha na muziki. Harakati zilizomkutanisha na kijana machachari Peter Tosh na pia Bunny Livingstone (Wailer) na hatimaye vijana wengine kama Junior Braithwaite na Beverly Kelso. Panapo mwaka 1963, Bob akiwa na wenzake waliojiita Wailing Wailers waliweza kusaini mkataba na prodyuza maarufu wakati huo Coxsone Dodd na kutoa vibao kadhaa kikiwemo 'Simmer Down' kilichowatambulisha vema katika ulimwengu wa muziki wa Jamaica.



Bob na Rita Anderson walioana mwaka 1966 baada ya Bob kurejea Jamaica akitokea Marekani ambako alikacha kwenda vitani Vietnam. Aliporudi Jamaica, Bob alikuta imani ya Kirastafari ikiwa imepamba moto kufuatia ziara ya Mfalme wa Ethiopia Haile Sellassie (Ras Tafarr Makonen) hapo mwaka 1965. Hotuba ya Sellassie ndicho kibao cha Bob kiitwacho 'War'

Kundi la Wailing Wailers halikudumu sana. Lilivunjika mwaka 1974 na Bob kuunda kundi lake maarufu zaidi katika historia ya muziki wa reggae la 'Bob Marley and the Wailers' wakafanikiwa kutoa albamu ya 'Catch A Fire' panapo mwaka 1975 ikiwa na kibao maarufu kilichopatwa kuimbwa tena na wanamuziki wengi sana cha 'No Woman No Cry'



Mwaka 1976, Bob Marley alifanikiwa kuwapatanisha mahasimu wakubwa wa kisiasa nchini Jamaica, waziri mkuu na kiongozi mkuu wa upinzani, Michael Manley na Edward Seaga. Wajamaica walimwona Bob Marley kama shujaa halisi wa taifa lao. Bob na kundi lake walishambuliwa na risasi siku tatu kabla ya tukio hilo, lakini walipona.

Mwaka huohuo wa 1976, Bob Marley na kundi lake walitoa albamu ya 'Exodus' iliyovunja rekond ya mauzo na kukaa kwenye chati ya Billboard kwa majuma 52 ikikamata namba moja.



Bob Marley alizunguka mabara yote ya ulimwengu kupiga muziki wake uliokubalika sana. Maonesho makubwa zaidi aliyafanya Uingereza, Ujerumani, New Zealand, St. Barbara, California huku pia akishiriki kama mgeni mwalikwa muhimu katika sherehe ya uhuru wa Zimbabwe mwaka 1980.

Maradhi ya kansa iliyoanzia kidoleni mguuni kwake, yaliukatisha uhai wake panapo Mei 11, 1981 huko Miami Marekani akiwa angali kijana wa umri wa miaka 36. Katika kibao chake cha 'Rastaman Chant' alipata kusema, "One bright morning when my work is over, I'll fly away to Zion"
Hata hivyo aliiacha kazi yake kama mhubiri wa amani na upendo.

Serikali ya Jamaica, kwa kuutambua mchango wake, ilimtunukia nishani ya juu zaidi 'Order of Merit.'

Bob Marley aliacha watoto 12, wengi wao wanajihusisha na muziki wa reggae na hip hop.

Bob Marley atakumbukwa zaidi duniani kama balozi na shujaa halisi wa muziki wa reggae. Atakumbukwa kwa kuuweka muziki huu wenye nguvu katika ramani ya ulimwengu.



Muziki wake utaendelea kuishi vizazi na vizazi. Ni urithi muhimu sana kwa wanaoupenda muziki wake. Ama kwa hakika wanajivunia sana miaka 36 ya uhai wake.

Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi daima. Amina.

Maoni 1 :

  1. SAFI SANA NAAMINI TUKO PAMOJA KATIKA SAFARI HII YA KUWAKUMBUKA NA KUWAENZI WANAFALSAFA KAMA BOB MARLEY HONGERA SANA MKUU TUKO PAMOJA NITEMBEE KWENYE BLOG YANGU PIA www.mandelapallangyo.com

    JibuFuta