Alhamisi, 29 Novemba 2012

MKASA WA MELI YA TITANIC

Pichani, meli ya RMS Titanic ikiondoka Southampton Uingereza hapo Aprili 10, 1912


kwa meli ya Titanic kulitokana na tatizo la usukani


LONDON – Meli ya Titanic iligonga siwa barafu (iceberg) tarehe 14 Aprili 1912 mnamo saa 5.40 usiku kutokana na hitilafu ya usukani.  Lakini ikazama kwa kasi zaidi kutokana na Afisa mwandamizi wa meli hiyo kumwamuru nahodha aendelee na safari.  Hayo yameelezwa jana Jumatano na mwandishi wa Kiingereza alipohojiwa na shirika la habari la Reuters.


Louise Patten, mwandishi na mjukuu wa Afisa mwandamizi wa meli hiyo Charles Lightoller, ameamua kusema ukweli juu ya kile kilichotokea karibia miaka 100 iliyopita.  Ukweli huo ulikuwa umefichwa kwa makusudi kwa kiasi cha miaka 100 ili kulinda heshima ya babu yake aliyekuja kuwa shujaa wa vita kuu ya dunia.

Lightoller, afisa mkuu aliyesalimika katika ajali ile ya kihistoria aliuficha ukweli huo alipohojiwa mara mbili.  Alihofu kuwa ukweli huo ungeifilisi kampuni iliyoitengeneza meli hiyo na pia kuwapotezesha ajira wenzake walioajiriwa katika kampuni hiyo.


"Wangeweza kuikwepa barafu ile kama isingekuwa kasoro kwenye usukani," Patten ameiambia Daily Telegraph.


Mabaki ya meli ya Titanic kama yanvyoonekana katika picha hii iliyopigwa hivi karibuni.

"Badala ya kuuelekeza usukani wa Titanic kwa usalama kuelekea kushoto kwa siwa barafu lile, iligundulika kuwa usukani haufanyi kazi upande huo.  Aliyeushika usukani, nahodha  Robert Hitchins, alichanganyikiwa na kuuelekeza upande usio sahihi."


Patten, ameyafunua hayo ili kwenda sambamba na utowaji wa riwaya yake mpya "Good as Gold" ambayo ameitumia kuelezea mazungumzo ya manahodha hao.  Kwa mujibu wa mazungumzo hayo, kulikuwa na mifumo miwili tofauti ya usukani.

Jambo lililokuwa la muhimu sana, mfumo mmoja  ulikusudiwa kuuzungusha usukani kuelekea upande mmoja, na mfumo mwingine, kinyume chake.

Kosa hilo la usukani lilipofanyika,  Patten akaongeza, "walikuwa na dakika 4 tu za kuubadili mfumo huo.  Wakati afisa mkuu William Murdoch alipoligundua kosa la Hitchin na kujaribu kulirekebisha, alikuwa amechelewa."

Babu yake Patten hakuwa akiangalia wakati meli ikigonga siwa barafu, lakini alikuwepo wakati wa kikao cha mwisho cha maafisa wa meli ya Titanic kabla ya meli hiyo kuzama kabisa.


Babu yake Patten si tu alisikia juu ya makosa hayo, bali pia amri kutoka kwa J. Bruce Ismay, mwenyekiti wa White Star Line, kampuni iliyoitengeneza meli hiyo akimwamuru nahodha wa meli kuendelea na safari.  Tendo la kuendelea na safari lilisababisha meli kuzama kwa kasi kubwa sana.  Masaa saba tu hadi kufikia saa 2.20 asubuhi, meli ilikuwa imezama yote.

"Kama Titanic ingesimamishwa pale pale, isingezama kamwe kwani ingeweza kumudu kusubiri meli za uokoaji na pasingekuwepo vifo vile.," alisema Patten.

Meli ya RMS Titanic ilikuwa ndiyo meli kubwa zaidi duniani wakati ikiondoka Southampton, Uingereza, kuelekea New York katika safari yake ya kifahari zaidi melini panapo Aprili 10, 1912. Siku nne baadaye ikiwa safarini iligonga siwa barafu na kuzama.  Ajali hiyo kubwa zaidi ya meli katika historia, iligharimu maisha ya watu 1517 kati ya watu 2227 waliokuwa ndani ya meli hiyo ikijumlisha abiria na wafanyakazi.


Nimeiandika habari hii baada ya kuisoma kwenye mtandao wa Reuters kwa sababu moja.  Nimetaka tuone tofauti ya wenzetu wa Ulaya.  Miaka 100 sasa, wao bado wanajali juu ya chanzo cha ajali.  Sisi meli ya Mv Bukoba iliyozama miaka 14 tu nyuma, nani anajali tena kujua chanzo kilikuwa nini?  Wenzetu na rekodi nzuri ya watu waliokuwemo.  Sisi wala hatujawahi kuwa na idadi kamili ya wahanga

Hebu litazame hili jedwali juu ya rekodi za abiria wa Titanic.  Sisi hadi leo hatuna idadi kamili ya wahanga wa majanga makubwa.  

category
waliokuwa melini
waliopona
asilimia waliopona
waliokufa
asilimia waliokufa
1st class
329
199
60.5 % 
130
39.5 % 
2nd class
285
119
41.8 % 
166
58.2 %
3rd class
710
174
24.5 % 
536
75.5 %
crew
899
214
23.8 % 
685
76.2 %
Jumla
2,223 
706 
31.8 %
1,517
68.2 %

Chanzo jedwali:  wikipedia



 FA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni