Kusifu
na kumwabudu Mungu katika roho na kweli ni jukumu kuu la wakati wote katika
maisha yetu binafsi na katika makanisa yetu, hii ni kwa sababu Mungu alituumba
sisi kwa ajili yake mwenyewe. Anasema
“Watu wale niliojiumbia nafsi
yangu ili watangaze sifa zangu”. (Isaya 43: 21)
Hii
inatuthibitishia kwamba, kumbe tuliumbwa na Mungu kwa kusudi moja tu, la
kumsifu na kumuabudu. Ili siku zote hisia zetu zimwelekee yeye, Mungu Baba yetu
na tutangaze sifa zake Mungu muumbaji wetu. Biblia inasema,
“Bali
ninyi ni mzao mteule ukuhani wa kifalme, taifa takatifu watu wa milki ya Mungu,
mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika
nuru yake ya ajabu” (1Petro 2:9.)
Kusifu.
Kabla
ya maelezo juu ya kuabudu, ni vizuri kwanza tugusie japo kidogo juu ya kusifu
ni nini? Kwa sababu ukiangalia kwa makini, kusifu na kuabudu ni vitu viwili
tofauti, ingawa vinaenda pamoja.
-
Kwa kawaida unaweza kuwa na ibada ya
sifa bila kuabudu, na inaweza ikawa nzuri tu.
-
Lakini siyo rahisi kuwa na
ibada ya kuabudu bila kusifu.
Ni
mara chache kutokea kuwa na ibada ya kuabudu bila kusifu, hii hutokea tu pale
mtu anapovamiwa na mguso wa Roho Mtakatifu wa Mungu kwa namna isiyo ya kawaida.
Kusifu
kwa vyovyote vile iwavyo, huwa ni tendo la kutangaza kwa nguvu, na kwa uwazi
tena hadharani. Ukielezea na kuonyesha uhakika ulionao juu ya unachokitolea
sifa.
Kwa
maana hiyo, popote panapokusudiwa kuwa pawepo na sifa, kuna hekaheka na
matendo, sauti na nyimbo, vyote huonekana na kusikika.
-
Kusifu ni utaratibu unaopangwa na
ufahamu wako jinsi gani udhamirie kusifia, sio kulazimishwa na mtu kama tuko
kwenye gwaride, kuna ule mtindo ambao viongozi wa sifa huutumia, mara bariki
kushoto, bariki kulia, bariki mchungaji, bariki wanakwaya! Hayo ni mambo ya
stage show katika ibada haiko hivyo. Ingawa unaweza kufanya hivyo mwanzo kabisa
katika kuhamasisha, lakini baada ya hapo waachie watu wapambane wenyewe kuingia
barazani pa Mungu.
Mara
nyingi nimeongea na viongozi wa sifa sehemu mbalimbali tunapokutana kwamba, sio
wajibu wao kuwaambia watu hebu simameni ili tumsifu Mungu.
-
Inatakiwa mtu mwenyewe aguswe toka
ndani, yaani mtu wa ndani ndio anatakiwa amuamulie mtu wa nje (mwili) kufanya
vile mtu wa ndani anavyotaka.
Ukienda
mahali ambako sifa zinafanyika kwa uhakika utashangaa! Utaona wengine wamelala
chini, wengine wananesanesa, wengine wanarukaruka, wengine wanapiga ukuta kwa
ngumi ili mradi ni hekaheka, na hakuna mtu mwenye habari za kushangaa shangaa.
Sasa
kiongozi wa sifa, kwa mfano unapowaambia watu wasimame! Kwani nani alikwambia
kwamba kusimama ndio tafsiri ya heshima? Ingawa ni kweli kwa jadi zetu
tunaamini kwamba kusimama ni dalili ya heshima.
-
Kwa wengine kitendo cha kusimama ni
dharau. Kina mama wa makabila fulani wanapotaka kukusalimia kwa heshima wanakaa
chini, au wanapiga magoti.
-
Mama wa aina hiyo binti yake
akisalimia watu kwa kusimama, anamuona hana heshima hiyo ni anadharau kabisa.
Makabila
mengine ya kusini mwa Tanzania kama wangoni akikuheshimu au akitaka kukushukuru
kwa kiwango cha juu analala chini kabisa.
-
Kwa hiyo ndio maana ninashauri kuwa ni
vema viongozi wa ibada na viongozi wa sifa, kutokuwaamulia watu nini cha
kufanya kulingana tafsiri zao za mila ya kwao.
Kusifu
ni njia ya lango kuu la kuingilia katika kiini cha kuabudu. Hivyo kusifu ni
ibada yenye umuhimu wa kipekee kwa Mungu wetu, kikundi cha sifa ni askari wa
mstari wa mbele na ndio wanaotengeneza njia ya muhubiri kupitisha neno la Mungu
katika mioyo ya watu ambayo tayari imeshalainishwa na sifa. Zaburi 22:3.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni