Mwl Furaha Amon
Utangulizi;
Katika sehemu ya kwanza ya somo
hili tumeweza kuweka msingi unaoelezea kwamba somo hili sio jepesi na kila
thehebu na makanisa yana misimamo yao tofauti kuhusu somo hili. hivyo kwa
msomaji unayefuatilia unaweza kukuta baadhi ya mambo hayafanani na jinsi ulivyofundshwa
kwenye dini yako. Hapa tunaweka wazi ili kukupa na wewe utafakari zaidi na
kuongeza ufahamu kuhusu taasisi hii muhimu ya ndoa.
Ili tuanze kulidadavua vizuri somo hili, ni vizuri tuanze
kwa kuangalia ukweli wa msingi wa mafundisho ya ndoa ambayo wote tutakubaliana
nayo. Ukweli wenyewe ni kwamba: Maandiko yanasema waziwazi kwamba Mungu hapendi
wanandoa kuachana kwa ujumla. Biblia inaonesha wazi katika kipindi ambapo
wanaume fulani wa Ki-Israeli walikuwa wanatalakiana na wake zao, alitamka hivi
kupitia nabii wake aitwaye Malaki:
Maana mimi
nakuchukia kuachana … naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia … Basi
jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana (Malaki 2:16).
Hilo si jambo la kushangaza kwa mtu yeyote anayezijua vema
tabia za Mungu kuhusu upendo na haki, au mtu anayejua jinsi kuachana
kunavyoharibu kabisa tabia ya mwanaume, mwanamke na watoto. Mtu anayekubaliana
na watu kupeana talaka kwa ujumla inafaa tungehoji tabia yake. Kwa asili Mungu
ni upendo (ona 1Yohana 4:8), na kwa sababu hiyo anachukia watu wanapoachana.
Kuna wakati fulani ambapo baadhi ya Mafarisayo walimwuliza
Yesu swali kuhusu uhalali wa talaka “kwa sababu yoyote”. Jibu alilolitoa Yesu linaonyesha
jinsi asivyokuwa hakubali wanandoa kupeana talaka. Tena, kwamba talaka halikuwa
kusudi Lake kwa yeyote yule.
Basi
Mafarisayo wakamwendea wakamjaribu wakimwambia, ‘Je! Ni halali mtu kumwacha
mkewe kwa kila sababu?’ Akajibu akawaambia, ‘Hamkusoma ya kwamba yeye
aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo mtu
atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili
mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha
Mungu, mwanadamu asiwatenganishe’ (Mathayo 19:3-6).
Tunajua kihistoria kwamba yalikuwepo makundi mawili
yaliyokuwa na mitazamo tofauti katika vongozi wa kidini wa Kiyahudi wakati wa
Yesu. Tutatazama mitazamo ya makundi hayo mawili kwa upana zaidi baadaye,
lakini kwa sasa inatosha tu kusema kwamba kundi moja lilikuwa na msimamo mkali
na lingine msimamo mwepesi. Wenye msimamo mkali waliamini kwamba mwanamume
aliruhusiwa kumwacha mkewe kwa sababu nzito sana kimaadili. Wale wenye msimamo
mwepesi waliamini kwamba mwanamume aliruhusiwa kumwacha mkewe kwa sababu yoyote
ile, hata kama amempata mwanamke mrembo zaidi. Mitazamo hiyo miwili tofauti
ndiyo ilisababisha swali la Mafarisayo kwa Yesu.
Yesu akarejea kwenye mistari ya Maandiko kutoka kurasa za
kwanza kabisa za kitabu cha Mwanzo, yenye kuonyesha jinsi ambavyo mpango wa
kwanza wa Mungu ulikuwa kuwaunganisha wanaume na wanawake pamoja daima,
si kwa muda tu.
Musa aliwaambia Wayahudi wale kwamba Mungu aliumba jinsia
hizo mbili akilenga ndoa, na kwamba ndoa ni uhusiano wa kiwango cha juu kwa
watu wawili kiasi cha kwamba tunaweza kusema kuwa ndiyo wa msingi – au, ndiyo
wa kwanza kabisa. Ukiisha undwa, ni wa hali ya juu kuliko mahusiano ya mtu na
wazazi wake. Wanaume wanaachana na wazazi wao ili kuambatana na
wake zao.
Tena, muungano wa kimwili katika tendo la ndoa baina ya
mwanamume na mkewe huonyesha mpango wa Mungu kwao kwamba wawe mwili mmoja. Ni
dhahiri kwamba uhusiano wa aina hiyo – ambao unasababisha kuzaa – haukukusudiwa
na Mungu uwe wa muda, bali wa kudumu. Jinsi Yesu alivyojibu swali la Mafarisayo
lilionyesha kuvunjwa moyo Kwake kwamba wamediriki kuuliza hata swali la aina
hiyo. Hakika Mungu hakukusudia kwamba wanaume waachane na wake zao “kwa
sababu yoyote.”
Ni kama vile ambavyo Mungu hakukusudia kwamba yeyote atende
dhambi kwa namna yoyote ile, lakini wote tumefanya dhambi. Kwa rehema zake,
Mungu aliweka mpango wakutuokoa kutokana na utumwa wetu wa dhambi. Tena, ana
mambo ya kutuambia baada ya kufanya yale ambayo hakutaka tuyafanye.
Vivyo hivyo, Mungu hakukusudia mtu yeyote aachane na mwenzake, lakini talaka
ikawa haiepukiki kwa watu wasiojitoa kwa Mungu. Mungu hakushangazwa na talaka
ya kwanza, wala zile zilizofuata kwa mamilioni. Basi, hasemi tu kwamba
anachukia kuachana, lakini pia ana mambo ya kuwaambia watu baada ya kuachana.
Kwa maoni na ushauri zaidi tunaweza
kuwasiliana kwa simu 0677 609056
Somo litaendelea na sehemu ya tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni