Ijumaa, 27 Januari 2017

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU (1)



Mwl Furaha Amon
Utangulizi;
Kichwa cha somo hili ni baadhi ya maneno machache, ambayo wachungaji humalizia katika kukamilisha kiapo cha ndoa kwa wawili wanaopendana. Lakini swali la kujiuliza hapa ni je? Maneno hayo yamesaidia kutatua tatizo la watu kuachana na kuoa au kuolewa tena? Jibu ni kwamba hapana! Maneno hayo bado hayajasaidia sana kutatua masuala ya ndoa, kwa sababu bado tunashuhudia migongano na watu kuachana katika makanisa ya watu waliookoka.
Ukweli ulio wazi ni kwamba hakuna mtumishi wa Mungu, Mchungaji au mwalimu yeyote ambaye anaweza kusema kwa hakika kuwa, yeye amefanikiwa sana katika taasisi hii ya ndoa. Kwa sababu unaweza kweli  ukawa umefanikiwa katika maeneo fulani ya maisha ya ndoa, lakini pengine ukawa dhaifu sana katika maeneo mengine fulani ya ndoa. Ijapokuwa wewe unaweza ukawa unajiona uko imara, lakini wanaokuangalia kwa nje wanaona ni udhaifu.

MAFUNDISHO KUHUSU KUACHANA, KUOA AU KUOLEWA TENA
Jambo la kupeana talaka na kuoa tena baada ya talaka limekuwa na changamoto sana miongoni mwa Wakristo wanaopenda kuishi katika kweli. Yapo maswali mawili ambayo ndiyo msingi wa changamoto hizo.
(1)      Ni wakati gani – kama upo – ambapo talaka     
inaruhusiwa machoni pa Mungu? Na
(2)      Ni wakati gani – kama upo – ambapo kuoa
tena  kunaruhusiwa machoni pa Mungu?

Madhehebu mengi, na makanisa binafsi yana msimamo rasmi kimafundisho kuhusu kinachoruhusiwa, na kisichoruhusiwa kuhusu kuoana na kuachana, kutokana na tafsiri yao ya Maandiko. Nafikiri kwa busara, tunapaswa kuwaheshimu wote kwa kuwa na misimamo, na kuishi kulingana misimamo yao – ikiwa kama kweli misimamo hiyo inasukumwa na kumpenda Mungu kwao. Ukweli ni kwamba, ingekuwa vizuri kama sisi wote tungekuwa na misimamo ambayo inaungwa mkono na Maandiko mia kwa mia. Lakini bahati mbaya sana imani yetu imetufanya kupishana sana katika kutafsiri Biblia kulingana na maslahi mbalimbali ya kiroho na kimwili. Katika makanisa na madhehebu yetu.

Nafikiri hakuna Mchungaji anayependa kuona ndoa anazofunga zinavunjika. Nakumbuka siku moja nikiwa nimeambatana na mke wangu, baada ya ibada tukiwa tunasalimiana na washirika wa kanisani, Mchungaji wangu aliongea maneno ambayo hapana shaka kabisa yalitoka katika uvungu wa moyo wake. Alisema ninapowaona mkiwa wawili nawafurahia sana, kwa sababu katika ndoa ambazo nimefunga na hazijanisumbua kabisa ni hii ya kwenu. Nafikiri ni maneno yanayotia moyo sana yanapotoka kwa kiongozi wako wa imani, na ni kweli hatukuwahi kupeleka kesi ya aina yeyote kwa mchungaji. Na sio kwamba tulikuwa hatupishani katika mitazamo, lakini Mungu alikuwa anatusaidia kumaliza kwa amani. Nafikiri mchungaji wangu alikuwa anajiuliza bila majibu kwamba ni kitu gani cha ziada alichotupa katika mafundisho yake ya awali ya ndoa yetu. Maana mchungaji wetu alikuwa na kawaida ya kuwafundisha wachumba siku kadhaa kabla hawajafunga ndoa, aliwahi kuniambia kwamba utaratibu huu umemsaidia sana katika kupunguza changamoto katika ndoa.
 Wachungaji wengine hujaribu kwa hila kufundisha wanandoa kitu kinachopungua kwenye kusudi la Mungu, wanajaribu kuwatisha kama wainjilisti wa zamani ambao wanawaambia watu habari za kutupwa katika ziwa la moto wa milele, badala ya kuwaelezea kuhusu upendo wa Mungu na urithi wa ufalme wa milele. Watumishi hawa hutumia mafundisho kuweka mizigo ya sheria za vitisho juu ya watu wanaofunga ndoa, kwamba ni pingu za maisha, ukiingia umeingia hata kama ulikosea, ndio milele. Hii ni mizigo ambayo Mungu hakukusudia wanandoa waibebe niliwahi kumwambia mwanandoa mmoja kwamba ndoa yenu ilijengwa katika msingi wa imani ya wokovu, kama mmoja ameamua kuacha wokovu zile sheria za wokovu hazimbani. Kwa hiyo anapiga ukahaba kama kawaida tena waziwazi, hatimaye atakuletea maradhi ufe kabla ya wakati.

Katika somo hili ambalo kwa kweli ni gumu, nitajitahidi kutafasiri baadhi ya Maandiko yanayohusiana na somo hii tata, na kukuacha wewe mwenyewe binafsi uamue kama unakubaliana na tafsiri hiyo au hapana. Maana kila dhehebu na makanisa yana mafundisho yao, hapa ni kuongeza maarifa tu. Inaweza kukusaidia.
Nianze kwa kusema kwamba mimi – kama wewe – nahuzunishwa sana na watu wawili ambao walipendana, na wengine ambao mimi na mke wangu tumesimamia harusi zao, lakini baadae wanafika mahali ambapo wote wawili wanaamua kwamba haiwezekani kuendelea kuishi tena pamoja. Na hapa nikiri kabisa kwamba wako baadhi ya wengine ilibidi niwashauri waachane kwa amani baada ya kuona wanakoelekea yanaweza kutokea maafa, unaweza kuona misingi ya ndoa yao haikuwa ya ki-Mungu bali waliongozwa na tamaa za mwili, sasa inapofika mwisho hali inakuwa ya hatari wanaweza kuuana. Nakumbuka wakati mwingine imenilazimu kusafiri kilometa nyingi sana mikoani kwa gharama zangu kwenda kutafuta suluhu, na wakati mwingine kufanya vikao mpaka usiku wa manane bila mafanikio. Ukiwasikiliza huoni sababu za maana ambazo zinawafanya wafikie uamuzi wanaoutaka kuufikia, ambao unaumiza mpaka watoto. Kibaya zaidi ni kwamba kuna hata Watumishi, wachungaji na maaskofu wanaoachana na wake zao na hiyo huathiri sana kanisa, nakumbuka wakati fulani nilikwenda kwa askofu mmoja kutafuta ushauri fulani wa kiroho kuimarisha eneo fulani la mahusiano na mke wangu. Badala yake nikajikuta mimi ndio natakiwa nimshauri yeye katika ndoa yake. Na hatimaye haikusalimika waliachana kwa talaka. Hata wengine walio katika huduma mbalimbali za kanisa ndoa zao zina shida. Hili ni zaidi ya tatizo, tunaita janga! kubwa sana. Tunahitaji kufanya kila kinachowezekana ili kuzuia aibu hii isiendelee kulitesa kanisa la Mungu. Na ufumbuzi mzuri zaidi wa tatizo la hili ni kufundisha katika hali halisi, na kuwaita watu kutubu kwa kuwaongoza sala ya toba upya. Wakati watu wawili wenye ndoa watakapokuwa wamezaliwa tena upya, kweli kweli na wote wakaingiwa na hofu ya kweli ya Mungu kupita Yesu Kristo, hawataachana daima. Na mtumishi atakayefanikiwa katika eneo hili, anatakiwa awe kielelezo kwa wengine kufanya kila anachoweza kuimarisha ndoa yake, akijua kwamba mfano wa maisha yake ndiyo mwalimu mkuu. Maana kuna unafiki mwingi sana katika taasisi hii ya ndoa.
Niseme pia kwamba mimi nina ndoa yenye furaha sana ya miaka zaidi ya ishirini na tatu wakati huu ninapoandika somo hili, na sijawahi kuoa kabla ya ndoa hii. 
Na kwa kweli sijawahi kufikiria kwamba ipo siku tutakuja kuachana na mke wangu. Kwa hiyo, sina sababu au maslahi yoyote ya kurahisisha maandiko magumu yanayohusu kuachana kwa faida yangu mwenyewe. Ila, ninawahurumia sana watu walioachana, nikijua kwamba hata mimi nilipokuwa natafuta mchumba niliomba maombi mepesi na ninayakumbuka hata maneno niliyoyasema nilimwambia BWANA Yesu hii njia ninayoiendea sijawahi kupita, na ninajua nikikosea nitashindwa kukutumikia. Naomba  niruhusu niende kwa akili zangu, ila unitangulie na nikikosea naomba uingilie kati na kuweka mapenzi yako ndivyo Mungu alivyofanya, kwa uaminifu sana. Kwa hiyo uzoefu ninaoupata ninaposuluhisha ndoa za wenzangu naona hata mimi kama sio kwa msaada wa Mungu ningeweza kufanya uamuzi mbaya kirahisi tu, na kuingia kwenye ndoa na mtu ambaye kwa vyovyote vile baadaye ningejaribiwa sana kumwacha. Na kutokana na uwezo wangu wa kuamua mambo na kusimamia uamuzi wangu, ingekuwa vigumu sana kuishi na mtu ambaye asingeweza kuchukuliana nami kama huyu niliye na ndoa naye. Yaani, ningeishia kwenye talaka, lakini haijawa hivyo kwa sababu ya neema ya Mungu tu.
Nadhani watu wengi walio kwenye ndoa wanaelewa ninachosema. Kwa kweli, tunahitaji kujizuia sana tusiwalaumu kabisa watu walioachana. Kwani sisi ni nani, wenye ndoa ambazo angalau zinavumilika zisizo na matatizo sana. Kuwahukumu walioachana, bila ya kujua wamepitia nini? Mungu anaweza kuwahesabu wao kuwa wenye haki kuliko sisi. Katika somo hili siwezi kukueleza mengi ambayo nimeshuhudia katika kutafuta suluhu za ndoa. Ndio maana mwanzoni nimekiri kwamba kuna wengine ilibidi niwashauri waachane, sasa hapo lazima unielewe kwamba pamoja na huzuni nilizonazo kwa rafiki zangu lakini unaona busara ni kuwatenganisha maana nyumba imekuwa tanuri la moto. Nafikiri Mungu mwenyewe anajua kwamba sisi, kama tungekuwa katika hali kama hizo, pengine tungevunja ndoa zetu mapema zaidi kuliko wao.
Kila mtu anayeoa au kuolewa anakuwa na picha fulani (ndoto) ya maisha yake ya ndoa ambayo mara nyingi huwa ni maisha bora ya ndoa. Hakuna anayeoa akitazamia kuvunja ndoa yake, ndio maana kwenye kiapo huwa tunasema tutaishi mpaka kifo kitutenganishe, na sidhani kama kuna wanaochukia kuachana kama waliokwisha achana. Kwa hiyo, tujaribu kuwasaidia watu wenye ndoa kuendelea kuwa katika ndoa, na tuwasaidie walioachana kupata neema yoyote ile ambayo Mungu anaitoa kwa watu kama wao. Ninaandika ninayoandika kwa misingi hiyo.
Nitajitahidi sana kuruhusu maandiko yafafanue mengine. Nimeona kwamba mistari inayohusu somo hili mara nyingi hutafsiriwa kwa njia kwamba inapingana na Maandiko mengine, ambayo ni ishara kwamba haijaeleweka vizuri kwa sehemu.

Somo hili ni refu litaendelea, tukutane katika sehemu ya pili. Unaweza kuwasiliana nami kwa msaada zaidi kwa simu namba 0677 609056

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni