Ijumaa, 21 Septemba 2012

MBINU ZA KUFANIKIWA KIMAISHA.




Watu wasioweza kufanikiwa hujaa fikra za kutofanikiwa na mara nyingi hulalamikia sana matatizo yao. Wakati mwingine wasioweza kufanikiwa hugeuza mambo mema na kuyafanya yaonekane mabaya, jua likiwaka watalalamika joto, likipoa watalaumu baridi, watalaumu foleni za barabarani, yaani kwao kila jambo wataligeuza na kulipa sababu mbaya. Hata wanaposhindwa kutekeleza jambo hutoa sababu, yote ni kuzilinda fikara zao za kutofanikiwa.
Tabia hii hukua mpaka kufikia hatua wanapowatazama wenzao hudhani kuwa wanawasengenya, kuwafanyia mambo mabaya, kuwasaliti, ilimradi tu ni kuwa kinyume na mambo mema. Watu wa namna hii hata kama watasaidiwa namna gani hugeuza misaada hiyo kuwa ya kujipendekeza na mara nyingi hupuuza wema haraka na kueneza mabaya ya mtu. Lakini pamoja na yote kutokana na fikra zao kuwa za kushindwa watu wa tabia hii hukata tamaa mapema, pale wanapofanya jambo na kuonekana lina ugumu kidogo.
Hutenda kabla ya kufikiri
Tabia ya pili ya watu wasioweza kufanikiwa kimaisha ni hii ya kutenda jambo kabla ya kufikiria. Watu wa aina hii, kuwa wepesi sana kununua vitu barabarani mara tu wanaposhawashiwa na macho au wauzaji. Utakuta mtu bila hata kujiuliza faida za kitu hicho anaamua haraka kukipata. Ataamua kwa haraka kuoa, kuolewa, kukubali kujiingiza katika mapenzi na hata kufanya jambo lo lote bila kujiuliza atanufaika vipi?
 
Hupenda kuzungumza zaidi ya kusikiliza

Watu ambao wako katika hatari ya kutofanikiwa ni wale ambao daima ni wazuri katika kuzungumza kuliko kusikiliza. Wao huwa ni wajuajia wa kila kitu, hawako tayari kupokea ushauri. Siku zote wanapokuwa kwenye makundi ya watu pengine wajuzi zaidi yao wao huwa hodari kujenga hoja kutetea mambo yao hata kama hayafai. Unaweza kumkuta mtu ni kiongozi wa ngazi za juu, amefanya kosa na watu wote wameona kuwa kakosea lakini mhusika hujiona si mikosaji.
Mtu anapokuwa muongeaji sana huwa mgumu kupokea ushauri wa ye yote, anachoamua yeye hukifanya kwa imani kuwa kinafaa. Ukiwa mtu mwenya tabia ya aina hii huwezi kufanikiwa kabisa katika maisha yako. Watafiti wa masuala ya biashara ulimwengini waliwahi kushauri kuwa mipango mizuri ya kibiashara hutoka kwa watu masikini, ambao walisema hufikiri zaidi namna ya kujikomboa kuliko matajiri wanavyofikiri katika kujiendeleza, hivyo wakasema kama mtu anataka kufanikiwa kibiashara lazima asikilize mawazo ya masikini si kuwapuuza kwa kujiona ni bora zaidi yao.
Hukata tamaa mapema
Watu wanaotaka kufanikiwa huchukulia ushindwa kama hatua ya kuelekea kwenye mafanikio, lakini watu wasioweza kufanikiwa wanapojaribu mara moja au mbili kuvuka kikwazo fulani cha kimaisha na kushindwa hukata tamaa na kutotaka kujaribu tena kusonga mbele. Wanye tabia ya kushindwa kimaisha hawako tayari kudumu na jambo moja linaloonekana kushindikana kwao kwa muda mrefu. Akiona mwanamke ambaye ni mkorofi kidogo, haraka hukimbilia kumwacha na kutafuta mwingine, mara nyingi si watu wavumilivu.
Akijaribu biashara ya vitumbua kwa wiki moja na akaona havinunuliwi, anaaza kupika maadazi, wiki moja baadaye yuko kwenye mihogo, basi ilimradi ni kuhangaika kusikokuwa na tija katika maisha. Ukitaka kuwa mmoja kati ya watu wasiweza kufanikiwa kimaisha, basi jaribu kuishi maisha ya kukata tamaa mapema unapofanya mambo.
Hujaribu kuwarudisha nyuma wengine
Wasioweza kufanikiwa katika maisha huwa na tabia moja ya ajabu ambayo ilianzishwa na Hawa mwanamke anayetajwa katika Kitabu cha Biblia kuwa ni mtu wa kwanza kufanya dhambi. Mwanamke huyu alipodanganywa na nyoka na kuchuma tunda hakutosheka na dhambi zake, bali alimpelekea na mumewe Adamu naye akala. Mara nyingi watu walioshindwa kimaisha kuwa na tabia za kuwashawishi watu wengine wawe kama wao katika mawazo na matendo.
Tabia za watu wa aina hii huwa si za kimaendelezo kwa vile wao hudhani kuwa njia zao ni sahihi na hivyo hujaribu kwa nguvu zao kuwarudisha wengine nyuma ili wawe kama wao. Ni watu wenye wivu wa ‘kijinga’ wakiona mwingine anaendelea katika hiki na kile humpiga vita ili afilisike. Ni wingi wa fitina, uchonganishi. Wenye tabia za kutofanikiwa hudhani kuwa kukwama kwao hutokana na vikwazo vinavyoletwa na wengine. “Kwa sababu jamaa kanikwamisha hiki na kile, nimkwama kwa sababu ya kaka yangu”
Hupoteza muda mwingi
Watu ambao hawawezi kufanikiwa ni wale ambao hupoteza muda mwingi kufanya mambo yasiyokuwa na tija, kwa kuangalia Tv, kusengenya watu, kunywa pombe, kufanya starehe na kutumia muda hovyo kwenye kazi ambazo hazina msaada kwao. Wapo watu mahodari kutembelea kwenye nyumba za wengine na kuongea huko kutwa nzima bila kujali kama muda waliopoteza wangeweza kufanya kazi na kujipatia kipato.
Huchagua mambo rahisi
Wakati mwingine mafanikio huhitaji kufanya kazi ngumu zenye kuchosha, lakini watu wasiokuwa na uwezo wa kufanikiwa wanapoletewa mambo mawilii huwa wepesi zaidi kuchagua jepesi kulifanya. Kama ni kazi, basi zisiwe ngumu sana ziwe nyepesi nyepesi ambazo watazifanya bila jasho. Watu wasiokuwa kwenye njia ya mafanikio hawapendi kujituma, wepesi kuchoka na mara nyingi hupenda sana kufanya kazi kidogo na kulala sana.
Tabia za watu wasioweza kufanikiwa huwa ni za kukwepa kuwajibika. Hata kama kuna mtu anataka kumpatia kitu na akamwambia awahi kesho yake asubuhi, huchelewa kwa vile hawezi kujihimu asubuhi na kuacha raha ya usingizi, wakati mwingine hata akiambiwa asubiri mpaka muda fulani huwa hayuko tayari kusubiri.
 
Leo naomba niishie hapa, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri zaidi.
Labels: SAIKOLOJIA
Chanzo: Sasali blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni