IJUMAA YA TAREHE 19
October 2012 ILIKUWA NI SIKU YA HUZUNI SANA KLPT MAJANI MAPANA TANGA.
Marehemu Austeria Deo wa pili kulia akiwa na wanakwaya wenzake wakiimba nyimbo za maombolezo katika msiba wa mzee Elias Ludamila |
Lakini ndugu hatutaki msijue habari zao waliolala
mauti,msije mkahuzunika kama wengine wasio na matumaini. Maana ikiwa twaamini
ya kwamba Yesu alikufa akafufuka,vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu,Mungu
atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana,kwamba sisi
tulio hai,tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana,hakika hatutawatangulia
wao waliokwisha kulala mauti kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni
pamoja na mwaliko,na sauti ya malaika mkuu,na parapanda ya Mungu,nao waliokufa
katika kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai tuliosalia tutanyakuliwa pamoja nao katika
mawingu,ili tumlaki Bwana hewani na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.
Farijianeni kwa maneno hayo. (Wathesalonike 4:13 17).
Mchungaji George Nywage akiwa pamoja na waombolezaji nyumbani kwa marehemu wakisubiri kufanya ibada ya kuaga mwili wa marehemu ambao ulisafirishwa kwenda kuzikwa nje kidogo ya mji wa Mbeya. |
Nimetanguliza maneno
hayo ili kukupa nguvu msomaji wangu
ambaye uliguswa na msiba wa ndugu yetu Austeria Deo (mama Suzi) habari za msiba
wa dada yetu huyu zilimshitua kila mtu aliyezisikia. Ninaamini Mungu wetu
alifanya siri kubwa sana kwa namna alivyoweza kumpumzisha dada yetu huyu,hakuna
mtu wa karibu ambaye ameshasema kwamba Mungu alimuonyesha kwamba kuna mtu mmoja
muhimu sana anaweza akaondoka katika familia ya wana Shalom Tarbenacle KLPT
majani mapana. Siwezi kusema kwamba ninamfahamu sana marehemu kwa maana ya
kwamba labda nimefanya naye huduma katika idara moja ndani ya
kanisa,hapana ninamfahamu kama mshirika
mwenzangu ndani ya kanisa, kwa hiyo nitamuelezea kwa kiwango ninachomfahamu.
Nianze kwa kusema kwamba ndani ya kanisa kuna wapambanaji wanaoonekana katika
mstari wa mbele kwa ajili ya kuhamasisha watu katika mapambano, na hawa mara
nyingi wanakuwa na nafasi za uongozi zinazoheshimika. Lakini wapo wapambanaji wengine
ambao hawajulikani sana na watu lakini Mungu anawafahamu na shetani pia anajua
kazi yao. Hawa ni watu ambao ukiwaona kwa macho
ya kawaida unaweza ukadhani kuwa si lolote lakini ni watu wanaoweza kuutetemeha
ufalme wa shetani,nilimuona dada huyu kila kitu alichoamriwa kukifanya,iwe
kufundisha wakristo wachanga,kuongoza maombi,kuongoza ibada n.k. alifanya kwa
bidii kutoka ndani ya moyo wake kabisa,hakupenda kufanya mambo kinafiki ili
kwamba watu wamuone. Bali alifanya kile alichoamini kwamba kina manufaa kwa
Bwana Mungu wetu. Alikuwa ni mtu anayejituma katika mambo ya Mungu na kuna
ushahidi wa kutosha kwamba hata mauti yanamkuta alikuwa amemaliza maombi siku
chache kabla ya kifo chake. Pamoja na kwamba sikuwa karibu naye sana ,lakini
nakumbuka maongezi yetu ya mwisho mwezi mmoja kabla ya msiba. Kuna tukio
nilikuwa nimelifanya mimi katika ibada ya jioni ambalo yeye
Marehemu Austeria Deo akiwa na washirika wengine wakifuatilia mahubiri kwa makini. |
halikumpendeza, nilikuwa nimetoka na mtu mmoja nje kwa mazungumzo ya dharura
wakati ibada ya maombi inaendelea. Yeye binafsi hakutukasirikia ila alihisi
kwamba kuna watu tumewakwaza kwa kitendo chetu. Mimi nilijitetea na kumwambia
kwamba wokovu sio ndani ya ibada peke yake ndio uwe na nidhamu kama watu wa
dini nyingine wanavyonyenyekea. Nilimwambia wokovu ni kumcha Mungu, na kumcha
Mungu ni mfumo wa maisha ambayo huyo Mungu unayemcha anakutaka uishi,haijalishi
uko nyumbani,kanisani, kazini,n.k. na kwa pamoja tulikataa dhana ya watu
wengine wanaotaka kuonyesha unyenyekevu kanisani tu na nje ya hapo hawako
hivyo. Dada yetu ametutoka ghafla sana,hakuna aliyejua na ninaamini manabii
walioko kanisani wangejua
jambo hili mapema pengine wangemsihi sana Mungu
ahairishe au asogeze mbele msiba huu,na wangetoa sababu na Mungu angekubali.
Lakini inaonekana Mungu mwenyewe alimuandaa kimya kimya hakuna aliyejua hata
yeye mwenyewe hakujua. Ameamka vizuri asubuhi kawatayarisha watoto wake kwenda
shule na wakati anapiga mswaki ili naye ajiandae kwenda katika shughuli
zake,ndipo alianguka na kupoteza fahamu na ndio ukawa mwisho wa maisha
yake,tumeumizwa sana na tukio hili,lakini Mungu anabaki kuwa Mungu na sisi
ataendelea kuwa Baba na rafiki yetu. TUTAKUKUMBUKA DAIMA MILELE NDUGU YETU NA
BWANA ATAKUFUFUA SIKU YA MWISHO TUTAFURAHI PAMOJA NA BWANA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni