Ijumaa, 16 Novemba 2012

JE WANASAYASI WANASEMA UKWELI KUHUSU MWANZO WA MWANAADAMU?



Mada ya Yasinta aliyoipa kichwa cha habari kisemacho,Je Binadamu na Nyani ni jamii moja? imenifanya na mimi nifungue mjadala mpya.

Kuna wakati nilisoma habari iliyoandikwa na Bwana
Bwaya juu ya sayansi ya viumbe aliyoipa kichwa cha habari kisemacho;
Viumbe na mabadiliko ya “kubahatisha”

Naomba ninukuu maelezo ya makala hiyo hapa chini;
‘Marehemu Darwin amejaribu kuonyesha kwamba viumbe vilitokea kwa bahati, vikapitia mabadiliko ya uasili wao kufanya asili nyingine iliosababisha kugeuka na kuwa viumbe vya aina nyingine kabisa.Ili kufafanua anachosema Darwin na rafiki zake, tuchukulie mfano wa viumbe kama samaki.

Samaki, kwa mujibu wa kanuni ya “natural selection”, walipitia mageuzi kadhaa yaliyosababisha tofauti katika kundi lao la samaki. Tofauti hizi ziliendelea kuwa kubwa kiasi cha kusababisha kutengenezeka kwa aina fulani ya samaki waliokuja kufanya kundi la viumbe tofauti kabisa na samaki wengine waliobaki.

[Kundi hili linafahamika kama amphibia lenye mifano ya viumbe kama mamba na vyura].

Maana yake ni kwamba katika samaki, walitokea samaki waliokataa asili yao na kufanya asili nyingine iliyosababisha kutokea kwa viumbe vingine. Utetezi wa mabadiliko haya yanayosemwa na akina Darwin, ni mazingira. Kwamba samaki hawa, kwa mfano, waliishi katika mazingira yanayotofautiana kiasi cha kugeuka kwa asili yao.

Kwamba asili hugeuzwa na mazingira kwa maana ya samaki kubadili tabia zake ili kuendana na mabadiliko ya mazingira alimo, ni jambo ambalo linatupasa kufikiri kwa tahadhari.Kwamba asili ya kiumbe ndiyo inayomsaidia kugeuka ili kukabidili mabadiliko katika mazingira yake na kwamba asili yake ilibadilika, ikimtenga na wenzake, ili kufanya kundi lingine linalojitegemea la viumbe jamii nyingine, hilo si jambo rahisi’.

Kisha akaendelea kusema katika makala nyingine aliyoipa kichwa cha habari kisemacho:
Fossil kwa sababu gani?

Katika makala hiyo alisema, naomba kunukuu:

‘Kwa mfano inavyoonekana, maisha hasa ya viumbe yalianzia baharini. Kwa maana hii, viumbe wa kwanza waliishi majini wakibadilika badilika na kuishia kufanya aina nyingine ya maisha yasiyotegemea maji, yaani maisha ya nchi kavu. Sasa katika kuangalia mlolongo huu, tunaambiwa viumbe walijikuta wakijiongezea “viungo” (adaptive features) vilivyowawezesha kukabiliana na aina vyingine ya maisha’

Kisha akaendelea kuandika:

’Kwa ule mfano wetu wa samaki, ni kwamba baadhi ya samaki walianza kupoteza uwezo wao wa kupumua kwa kutegemea maji, na badala yake, wakaanza kuwa na vitu kama mapafu vilivyowasababisha kugeukia maisha nje ya maji. Baadae makoleo yao yaliyotumika kuogelea (fins) yakatengenezeka kuwa (miguu?) ili waweze kuishi vizuri nchi kavu. Na mlolongo kama huo unaotufikisha kwa viumbe kama binadamu.’
Mwisho wa kunukuu.

Labda ningependa kuweka bayana kuwa wakati nasoma habari hii sikuwa mwanablog lakini nilivutiwa sana na habari hiyo ambayo aliiandika kwa kirefu sana.


Hivi karibuni nilikuwa nasoma habari moja juu ya nadharia ya hayati Charles Darwin juu ya wanasaikolojia kutumia Panya katika tafiti zao .

Je Darwin anasemaje kuhusu hili?

Kwa mujibu wa utafiti wake anasema kuwa Binadamu na panya ni viumbe wenye asili moja wanaofanana kitabia,. Wote ni mamalia wanaofanana kisaikolojia.
Mfumo wa viungo vyao vya ndani vinafanana na pia mfumo wao wa ubongo katika mawasiliano unafanana vile vile.

Chembe chembe za kwenye ubongo wa binadamu zinazotumika katika kutoa taarifa unafanana na mfumo wa panya.
Kwa mfano majaribo yoyote ambayo yameshindikana kufanyika kwa mwanaadamu kutokana na sababu mbalimbali za kiusalama yamefanyika kwa panya.

Kwa kawaida Ubongo wa mwanaadamu ni mkubwa kuliko wa panya, lakini ukubwa unapolinganishwa na mwili ni dhahiri kuwa tofauti hiyo itatoweka

Ukweli ni kwamba ukubwa wa ubongo wa binadamu ukilinganisha na wa panya ni kutokana na ukubwa wa kitu kinachoitwa Neocortex.
Hili ni eneo linalohusiana na kuona na kusikia.

Darwin anaendelea kubainisha kuwa mwanaadamu, nyani na panya wana asili moja (common ancestors)

Kwani wanafanana kitabia kwa asilimia kubwa sana kwa sababu wote ni mamalia na wana mfumo wa viungo vya mwili vinavyoshabihiana, na ndio maana ikasemekana kuwa binadamu anatokana na nyani.

Je kuna ukweli juu ya jambo hilo?


Hapa naomba msaada wa bwana Bwaya.

Je Samaki walianza kuwa nyani katika hatua ya kuelekea kuwa wanaadamu, au walibadilika moja kwa moja na kuwa wanaadamu?

Je kama ni hivyo panya wanaingiaje kwenye mkumbo huu?

Nilikuwa najaribu kupitia vitabu mbali mbali vya kisayansi katika maktaba yangu nikakutana na na ndharia nyingi za kuchekesha, kiasi kwamba ziliniacha nimechanganyikiwa.

Kama Bwaya alivyowahi kusema katika mfululizo wa makala zake za kisayansi kuhusiana na nadharia hizi za akina Darwin hata kufikia kumwita Fyatu,

Katika makala yake ya ‘
Sayansi na ghiliba zake

Naweza kukubaliana na yeye.

Lakini ninayo maswali ambayo najaribu kuyatafutia majibu

Hivi nadharia hizi zina ukweli kiasi gani?

Kwa kuwa nadharia hizi ni za miongo kadhaa iliyopita, Je hakuna wanasayansi wapya wanaoweza kutupa jibu sahihi?

Kwa nini tuendelee kuaminishwa na kukaririshwa na nadharia hizi zenye utata?

Je dini nazo zinasemaje kuhusu jambo hili?

Je tusimamie wapi?

Naomba kufungua mjadala.
Shabani Kaluse

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni