Mwl Furaha Amon
Utangulizi;
Watu wengi wanaofuatilia
masomo ninayofundisha wanaonyesha kiu kubwa ya kutaka kufahamu kwa undani
kuhusu kunena kwa lugha, kunakotokana na ujazo wa Roho Mtakatifu. Inaonekana kuna
tatizo kubwa sana linalohusiana na jambo hili ambalo ni kubwa na muhimu sana
katika maisha ya kiroho ya mtu mmoja mmoja na kanisa kama kundi. Kwa kuwa kiu
hii bado ni kubwa kwa wasomaji wangu, nimeona ni vema nitumie nafasi hii kutoa
mchango kidogo wa kuwasaidia kuelewa kwa kiasi habari za kunena kwa lugha. Naamini
kwa kupitia mafundisho haya, wale wenye kiu ya kunena kwa lugha wataweza kuanza
kunena kwa lugha ili mradi kama walipokea ujazo wa Roho Mtakatifu.
AHADI YA KUJA ROHO
MTAKATIFU.
Yesu baada ya kufufuka
alipaa mbinguni, lakini kabla ya kufa na
kufufuka, alikuwa ameahidi kuleta msaidizi, ambaye ni Roho Mtakatifu ambaye
angekuwa msaidizi wa watu watakaomwamini Yesu.
“Mkinipenda
mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba naye atawapa msaidizi mwingine. Ili
akae nanyi hata milele. Ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea,
kwa maana hauwezi kumwona wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa
kwenu, naye atakuwa ndani yenu.” (Yohana 14: 15-17)
Siku kumi baada ya Yesu
kupaa mbinguni Roho Mtakatifu alishuka. Roho Mtakatifu alikuja duniani ili kuzisimamia
kazi zote za Mungu zilizopo hapa duniani. Na kuanzia wakati huo, kazi zote za
Mungu zinamilikiwa na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ndie mtendaji wa kazi zote za Mungu
zilizopo hapa duniani. Nje ya Roho Mtakatifu hakuna kazi yoyote ya Mungu
inayoweza kufanyika. Kazi zinazofanywa na Roho Mtakatifu zipo nyingi sana
lakini zimeanishwa na Biblia ni kama zifuatavyo;-
· Anatufundisha
· Anatuonya
· Anatuongoza
· Anatufariji
· anatutia
moyo
· anatuombea
· anatenda
miujiza
· anaponya
n.k
Kazi zote hizi za Roho
Mtakatifu, anazifanya katika maeneo yote ya maisha ya mkristo. Hapa ni muhimu
kufahamu kwamba ili Roho Mtakatifu aweze kuzifanya kazi zote hizo bila ya
kusahau eneo lolote la maisha ya mkristo, Roho Mtakatifu huzifanya kazi hizo kwa
mpangilio maalumu.
Hebu tujaribu kuangalia
mfano wa utendaji kazi wa serikali za kidunia. Kila mtu anajua vizuri kabisa
kwamba kazi ya serikali yeyote ile duniani, ni kuongoza wananchi wake katika
maeneo mbalimbali ya maisha yao ya kila siku. Kwa sababu hiyo ili serikali
iweze kutimiza wajibu wake huu bila kusahau eneo lolote la maisha ya watu
inaowaongoza. Serikali imegawa majukumu yake
katika wizara mbalimbali ambazo hutekeleza majukumu hayo.
kwa mfano mambo yote
yanayohusu afya katika nchi nzima yanashughulikiwa na wizara ya Afya. Na maswala
yanayohusiana ulinzi, yanashughulikiwa na wizara ya Ulinzi. Hali kadhalika mambo
yanayohusu elimu yapo chini ya wizara ya elimu. Ni hivyohivyo pia kwa wizara ya
mambo ya ndani, wizara ya mali ya asili,
wizara ya kilimo, wizara ya ujenzi, wizara ya mambo ya nje n.k.
Kwa kutumia mfano huo
itakusaidia kujua kuwa kwamba hivyo ndivyo ilivyo hata kwa Roho Mtakatifu. Na yeye,
ili aweze kufanya kila kitu kama kinavyotakiwa kufanyika kwa mkristo, anafanya
kwa kutumia karama tisa ambazo ni kama wizara kwa mpangilio wa serikali za
kidunia. Karama hizo ni kama zifuatazo;-
1. karama
ya neno la hekima
2. kalama
ya neno la maarifa
3. karama
ya kupambanua roho
4. karama
za kuponya
5. karama
ya miujiza
6. karama
ya imani
7. karama
ya unabii
8. kalama
ya aina za lugha
9. kalama
ya tafsiri za lugha.
Nje ya hizi kalama hakuna
kazi yoyote ya Mungu inayoweza kufanyika labda ufanye ujanja ujanja na mazingaombwe ambayo ni kazi ya shetani.
Kazi zote za Mungu
zinazofanyika hapa duniani kwa sasa kila mojawapo inafanyika kupitia mojawapo
ya hizi karama tisa. Huduma zote za Roho Mtakatifu kama vile Mtume, Nabii,
Mwinjilisti, Mchungaji na Mwalimu, pia huduma hizi hufanya kazi zake kupitia
Roho Mtakatifu.
KALAMA YA KUNENA KWA LUGHA
Kunena kwa lugha ni
mojawapo ya karama tisa. Ni karama iliyo
katika kundi la kalama tatu za uvuvio, karama hizi ni kama ifuatavyo;
1. Unabii
2. Kunena
kwa lugha
3. Tafsiri
za lugha.
Kalama hizi zinaitwa karama
za uvuvio kwa sababu, utendaji kazi wake hujidhihirisha kwa mtu anayetumiwa
kushukiwa na kufunikwa na nguvu maalumu, ambayo hudhibiti uwezo wa kuongea wa
mhusika. na Roho Mtakatifu huchukua nafasi ya kutumia midomo ya muhusika kuyazungumza
hayo maneno.
Maneno hayo yanaweza kuwa
katika lugha yoyote atakayoamua Roho Mtakatifu. Hii ni kwa sababu Kuna lugha za
mbinguni (za malaika) na kuna lugha za wanadamu. Pamoja na hayo Roho Mtakatifu
anaweza kuzungumza kwa kutumia lugha inayoeleweka kwa muhusika.
Mtu anayehusika hujikuta
anazungumza maneno ambayo hakuyapanga yeye kwa ufahamu wa akili yake. Mlolongo wa tukio hili ndiyo ambalo huitwa kuvuviwa na
Roho Mtakatifu. Mbali na karama za uvuvio kuna karama za ufunuo ambazo nazo pia
ziko tatu ambazo ni;
1.
Karama ya neno la hekima,
2.
Karama ya neno la maarifa
3.
Karama ya kupambanua roho.
Kwa sababu lengo la somo
hili ni kufundisha kalama moja tu ya kunena kwa lugha. Kwa maana hiyo sitagusia
kwa undani utendaji kazi wa kalama hizo zingine, isipokuwa kwa faida ya msomaji
nitazitaja tu bi kufafanua.
Karama zingine zinaitwa
karama za nguvu, ambazo pia ziko tatu kama ifuatavyo
1.
karama ya miujiza
2.
karama ya imani na
3.
karama ya kuponya
Lakini kama nilivyotangulia
kueleza awali kwamba katika somo hili hatutazungumzia habari ya karama zingine,
bali nitazungumzia karama ya kunena kwa lugha peke yake
Baada ya mtu kuokoka, na kujazwa
roho Roho Mtakatifu, na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana, hiyo ni ishara
kwamba karama zote tisa huwa ndani ya huyo mtu na ni Roho Mtakatifu ndiye
huamua ni karama ipi ndiyo ifanye kazi ndani ya mhusika kama apendavyo yeye.
Kwa kawaida Roho Mtakatifu
humgawia kila mkristo ndani ya kanisa mojawapo ya karama au humgawia karama kwa
idadi kadhaa kulingana na huduma ambayo Mungu amewekeza ndani yake.
Hivyo wakristo hujikuta huyu ana karama hii na Yule
ana karama tofauti na mwingine. Mwingine anaweza kuwa na karama ya imani,
mwingine karama ya unabii na mwingine karama ya neno la maarifa n.k.
Wakristo wote baada ya
kujazwa Roho Mtakatifu, ishara ya kunena kwa lugha huonekana mara tu baada ya
kujazwa Roho Mtakatifu. Inaweza isionekane kwa dhahiri sana kutokana na uzoefu
lakini baada ya kujizoeza na ulimi kuzowea inakuwa kama lugha ya kawaida tu. Hiyo
ndio inaitwa karama ya kunena kwa lugha.
mwisho wa sehemu ya kwanza ya somo. usikose kufuatilia sehemu inayofuata ya so hili na Mungu akubariki sana. kwa msaada zaidi tunaweza kuwasiliana kwa namba 0677 609056
mwisho wa sehemu ya kwanza ya somo. usikose kufuatilia sehemu inayofuata ya so hili na Mungu akubariki sana. kwa msaada zaidi tunaweza kuwasiliana kwa namba 0677 609056
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni