Jumamosi, 14 Januari 2017

SOMO: KUNENA KWA LUGHA SEHEMU YA PILI

UMUHIMU WA KALAMA YA KUNENA KWA LUGHA


Pamoja na kwamba Roho Mtakatifu hugawa karama kama apendavyo yeye mwenyewe, kwamba huyu anapewa hii na Yule anapewa ile. Lakini karama ya kunena kwa lugha Roho Mtakatifu amekuwa akiigawa kwa kila mkristo aliyejazwa Roho Mtakatifu. Biblia inasema;-
“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio: kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;” (Marko 16:17)
Hivyo kutokana na agizo hili, maana yake ni kwamba kila mkristo anayejazwa Roho Mtakatifu amepewa karama ya kunena kwa lugha kama kitu cha lazima.
Kunena kwa lugha ni karama muhimu sana kwa mtu aliyeokoka. Na kwa sababu hii, ndio maana Mungu kupitia  Roho Mtakatifu amekuwa akimgawia kila mkristo. Kwa maana hiyo kila mtu aliyejazwa Roho Mtakatifu, pamoja na karama zingine atakazojaliwa na Mungu kuwanazo lakini karama hii ya kunena kwa lugha ni ya lazima iwe kwa kila mtu aliyejazwa Roho Mtakatifu.
Hivyo kwa mkristo ni lazima kuokoka na kujazwa Roho Mtakatifu, hapo ndio utapewa karama hii ya kunena kwa lugha.
Hii inaonyesha jinsi karama ya kunena kwa lugha ilivyo muhimu sana  katika utendaji kazi kazi wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu wa Mungu mmojammoja. Kukosekana kwa karama hii ndani ya mkristo, kutazuwia baadhi ya kazi za Mungu ambazo Roho Mtakatifu anatakiwa kuzifanya kwa kila mkristo mmojammoja, katika maeneo fulani fulani ya kiroho.
Hii itasababisha mkristo asipate baadhi ya huduma za msingi na ambazo ni muhimu sana za Roho Mtakatifu zilizokusudiwa zifanyike kupitia karama hii ya kunena kwa lugha.
Huduma hizi muhimu kiroho ndizo ambazo zimemfanya Roho Mtakatifu ampe kila mtu wa Mungu karama hii ya kunena kwa lugha.
UMUHIMU WA MAFUNDISHO YA KUNENA KWA LUGHA
Wakristo wengi siku hizi wamejazwa Roho Mtakatifu na wakanena kwa lugha. Lakini kutokana na kukosekana kwa mafundisho kama haya wengi wao hawajui madhumuni ya wao kunena kwa lugha, na utendaji kazi wa karama hii ndani yao. Na bahati mbaya sana watu wanaowasimamia pia hawajui umuhimu wa kalama hii.
Hii imesababisha wakristo kuwa hawana nguvu ya kiroho ya kupambana na dhambi na majaribu mbalimbali ya shetani yanayowakabili. Shetani anawaweza na kuwashinda wakristo ambao wamejazwa Roho Mtakatifu, sambamba na anavyowaweza na kuwashinda wakristo ambao hawataki ujazo wa Roho Mtakatifu. Hii imesababisha kutoonekana umuhimu wa kujazwa Roho mtakatifu.

BIBLIA IMETOA NAFASI KUBWA
Maandiko yanaonyesha jinsi kunena kwa lugha kulivyo muhimu sana.  Ukisoma katika Biblia kitabu cha Wakorinto wa kwanza sura yote ya kumi na nne inazungumzia habari za kunena kwa lugha tu.
Karama zingine zote zimeelezwa kwa sentensi moja au neno moja tu. Lakini karama hii imeelezwa kwa kirefu katika sura nzima. Hii ni kuonyesha jinsi ambavyo karama hii ilivyo muhimu na ya lazima katika maisha ya kila siku ya mkristo.
Unaweza kusoma sura yote ya kumi na nne, lakini mimi nachukua mstari mmoja katika sura hiyo unaosema;-
Maana yeye anenaye kwa lugha hasemi na watu bali husema na Mungu maana hakuna asikiaye lakini anena mambo ya siri katika roho yake (1Wakorintho 14:2)
Biblia inasema mtu anapokuwa ananena kwa lugha huwa anasema mambo ya siri katika roho yake. Kwa maana nyingine ni kwamba, hii ndio njia pekee ambayo Roho Mtakatifu huitumia ili mkristo amweleze Mungu mambo ya siri kati yake na Mungu.
Sasa hapa ni rahisi sana kwa mtu mwenye mafunzo ya kivita kujua umuhimu wa mawasiliano katika mapambano yeyote. Ndio maana majeshi yote ni lazima yawe na mfumo wa mawasiliano ambao mtu mwingine hawezi kuelewa hata kama anasikia! Hata katika mapambano ya kiroho ni hivyohivyo pia, adui huwa anataka kujua unaongea nini na Mungu. Na hivyo anaweza akakupiga au akajihami kulingana na habari alizopata. Kwa maana hiyo kama hujui kunena kwa lugha unakuwa umepoteza fursa ya kuongea mambo ya siri baina yako na Mungu.
Maandiko hayo tuliyoyasoma yametupa maana ya kunena kwa lugha. Hivyo tumeona kuwa, kumbe kunena kwa lugha ni kuongea na Mungu. Kuongea na Mungu maana yake huko ndiko kuomba. Roho Mtakatifu huitumia midomo ya muhusika kuzungumza na Mungu kwa niaba ya muhusika. Hii ndio njia ambayo Roho Mtakatifu huitumia kuwaombea watu wa Mungu, kama tulivyoainisha baadhi ya kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni kutuombea. Na hutuombea kwa njia hii, kwa watu ambao hufikiri kwamba Roho Mtakatifu huweza kumuombea mtu bila muhusika kunena kwa lugha wanajidanganya wenyewe. Huwezi ukamwabudu Mungu kwa kutumia taratibu za kubuni mwenyewe, nimetanguliza kukueleza kuwa Roho Mtakatifu huzifanya kazi zake zote kupitia mojawapo ya karama tisa. Kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni kukuombea. Roho mtakatifu huifanya kazi hii kwa kupitia karama ya kunena kwa lugha nje ya hapo hakuna.

KUOMBEWA NA ROHO MTAKATIFU
Wakristo waliojazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha ikaonekana hata wao pia hawawezi kuombewa na Roho Mtakatifu wakati hawaneni kwa lugha. Roho Mtakatifu huwaombea watu wakati wakinena kwa lugha pekee. Kutokana na hili wakristo wengi waliojazwa Roho Mtakatifu, na ishara ya kunena kwao kwa lugha hawaitumii ipasavyo, inakuwa haina maana kwao. Wala huwezi kuwatofautisha na wakristo ambao hawajajazwa Roho Mtakatifu. Kwa sababu wao nao wamekosa kuitumia fursa na Baraka zinazotokana na kunena kwa lugha, sawasawa na ambavyo wamekosa wakristo ambao hawajajazwa Roho Mtakatifu.

TATIZO LA WAKORINTO
Kanisa la korinto lilikuwa limebarikiwa sana na karama hii. Lakini, hata hivyo hawakujua matumizi na madhumuni ya karama hii ya kunena kwa lugha. Ndipo Paulo alipowaandikia waraka akiwafundisha. Kanisa la Korinto lilibarikiwa kwa karama zote tisa zikifanya kazi. Lakini  kanisa la leo karama hazionekani, kwa sababu ya upeo mdogo wa kulijua neno la Mungu.
Wakristo hawafundishwi kwa undani kuhususiana na karama na jinsi zinavyofanya kazi, pia wakati mwingine karama zinazuiwa zisifanye kazi kanisani kwa makusudi, pengine tu kwa viongozi kutokuwa na ujuzi Paulo anasema;-
Wala msizuie kunena kwa lugha (1 Wakorinto 14:39)
Kunena kwa lugha ni muhimu sana kusizuiwe bali waumini wafundishwe jinsi ya kuitumia karama hii ili isilete makwazo bali ilete Baraka.
Mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu (1 Wakorinto 14:40)
Paulo ilibidi awafundishe wakorinto. Baada ya kujazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana. Wakorinto walifurahi sana, lakini hawakujua matumizi ya kunena kwa lugha, kutokujua matumizi ya karama hii kulileta makwazo.
Waumini hawakutaka tena kuomba kwa akili, Kila walipotaka kuomba wao walinena kwa lugha. Hata kama mmoja wao alitakiwa kuomba sala kwa niaba ya wengi, aliomba hiyo sala kwa kunena kwa lugha.
Mfano ndugu fulani ameombwa kuombea chakula wanachotaka kula, yeye aliombea chakula hicho kwa kunena kwa lugha na baadaye kusema amina.
Ndugu fulani anaombwa kwa ajili ya kufunga ibada au kwa kufungua ibada, huyu ndugu anaomba kwa kunena kwa lugha. Kumbuka kuna matumizi ya aina mbili ya kunena kwa lugha, aina ya kwanza ni matumizi ya hadhara na aina ya pili ni matumizi ya faragha. Unapoomba kwa niaba ya wengine au unapoomba kwa kuwakilisha wengine, unaomba kwa niaba yao ni muhimu wasikie yale unayoomba na wayaelewe. Hivyo unatakiwa uombe kwa kutumia akili zako na kwa lugha inayoeleweka kwa hao unaowawakilisha ili nao waelewe ulichoomba. Haya ndiyo matumizi ya hadhara ya kunena kwa lugha, Paulo anasema,
Nashukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote; lakini katika kanisa napenda kunena maneno matano kwa akili zangu, nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno elfu kumi kwa lugha. (1Wakorintho 14: 18 – 19).
Paulo anatuambia anapoomba kanisani kwa niaba ya wengine alikuwa anaomba kwa akili yaani kwa lugha inayoeleweka kwa wengine. Inapobidi kunena kwa lugha alinena maneno matano, lakini zaidi alikuwa anaomba kwa akili zake ili wengine waelewe ni nini ambacho anaomba.
Pamoja na hilo Paulo anasema yeye ndiye alikuwa ananena kwa lugha kuliko waumini wote. Sasa hapo ni lazima tujiulize swali na kujijibu. Swali je? ni wakati gani ambapo Paulo, aliweza kuhakikisha kuwa amenena kwa lugha kwa kutumia muda mwingi sana hadi ahakikishe kwamba yeye ananena kwa lugha kuliko wengine wote. Jibu ni kwamba, huu ulikuwa ni wakati wa maombi yake mwenyewe binafsi, maombi ambayo sio ya kuomba sala fulani kwa niaba ya wengine. Maombi haya hata kama utakuwa unayaomba ukiwa katikati ya waumini lakini ni maombi ambayo mtu mwingine hana umuhimu wa kuelewa kuwa unaomba nini.
Maombi haya pia unaweza kuwa katikati ya waumini wengi sana kila muumini anaomba kivyake. Maombi ya jinsi hii yanaitwa maombi ya faragha, maombi binafsi. Maombi ya faragha ndiyo unayotakiwa ujenge nafsi yako, pia ndiyo unatakiwa uyatumie ili uongee mambo ya siri kwa Mungu, haya ndiyo maombi unayotakiwa unene kwa lugha. Maombi haya ambayo Paulo anasema;-
Nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote (1 Wakorinto 14:18)
Matumizi ya hadhara ya kunena kwa lugha maandiko matakatifu yanasema ni ishara ya kuonyesha kuwa wewe umeokoka na umejazwa Roho Mtakatifu. Biblia inasema,
Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio watasema kwa lugha mpya (Marko 16:17)
Pamoja na ishara zingine zilizotajwa katika Marko 16:17 na 18 ambazo ni kwa jina langu watatoa pepo watasema kwa lugha mpya watashika nyoka hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru kabisa na wataweka mikono juu ya wagonjwa nao watapata afya. Tunaona ishara ya kunena kwa lugha ni mojawapo.
Kunena kwa lugha ilitumika kwa matumizi ya hadhara katika siku ile ya pentekoste wakati wanafunzi wa Yesu mia moja na ishirini walipojazwa Roho Mtakatifu na wakaanza kunena kwa lugha. Tukio hili lilipelekea watu wengi kukusanyika na kuanza kushangaa.
Wakristo wengi kwa kukosa mafundisho wanakutumia kunena kwa lugha kwa Matumizi ya hadhara pekee ambayoni ISHARA. Kususdi la Mungu kuiweka karama hii ya kunena kwa lugha ni zaidi ya ishara, karama hii ipo ili Roho Mtakatifu aweze kutusaidia kuomba maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo kuomba. Kupitia somo hili tunahitaji watu wajifunze kazi kubwa ya karama hii ili ufaidike na Baraka nyingi sana zipatikanazo katika karama hii. Wakristo kwa vile hawajui matumizi ya faragha na ya hadhara ya kunena kwa lugha wanachanganya matumizi. Hili limewafanya kuzikosa Baraka zilizoko kwenye kunena kwa lugha. Biblia inasema;-
Yeye anenaye kwa lugha na aombe kutafsiri. Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda. Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; nitaimba kwa roho tena nitaimba kwa akili pia;kwa maana wewe ukibariki kwa roho yeye aketiye katika mahali pa mjinga ataitikiaje, amina baada ya kushukuru kwako, akiwa hajui uyasemayo? Maana ni kweli wewe washukuru vema, bali Yule mwingine hajengwi (1 Wakorinto 14: 13 – 17)
Maandiko haya, Paulo anawafundisha wale wakristo waliokuwa wanataka kunena kwa lugha wakati wwa sala za hadhara. Paulo anasema iwapo kunena kwa lugha kutatumika katika sala ya hadhara basi uhakikishe unatafsiri hiyo sala ili na wenzako unaoomba kwa niabayao nao wasikie unayoyaomba. Hivyo wewe kama unapenda kutumia kunena kwa lugha katika matumizi ya hadhara ni sawa lakini uombe Mungu akupe karama ya kutafsiri lugha. Lakini unapokuwa unanena kwa lugha maombi yako wewe binafsi hapo hakuna haja ya kutafsiri.
Karama za uvuvio yaani unabii, kunena kwa lugha na tafsiri za lugha. Karama hizi mtu anayetumiwa anakuwa na uwezo wa kunena kwa lugha mahali popote na unao uwezo wa kutokunena kwa lugha.
Japokuwa umejazwa Roho mtakatifu. Kama unayo karama ya unabii unao Roho Mtakatifu anayo hekima sio dikteta hivyo utendaji wake katika karama ya kunena kwa lugha kutategemea na wewe unavyomruhusu, wakristo weni wasiojua sana habari za kunena kwa lugha hufikiri kuwa unaponena kwa lugha Roho Mtakatifu ni lazima aje kwa nguvu kubwa ambayo itamfanya anayenena kwa lugha anene kwa nguvu na kwa sauti kubwa sana. Hii sikatai inakuwa hasa kwa mkristo ambaye ndio amejazwa Roho Mtakatifu katika siku zake za mwanzo za kunena kwa lugha mkristo huyu kwa vile hajazowea mdomo wake kutumiwa na Roho Mtakatifu inabidi Roho Mtakatifu atumie nguvu kubwa ili kuufanya mdomo uongee anayotaka Roho mtakatifu. hii pia inatokea kwa wakristo ambao hawana mazoea ya kunena kwa muda mrefu kila siku. Pia hutokea kwa waristo ambao walikuwa wananena kwa lugha hapo zamani baadae wakamzimisha Roho Mtakatifu sasa inapotokea wameanza kunena kwa lugha tena Roho Mtakatifu huja kwa nguvu kubwa.
Mkristo ambaye ni mnenaji kwa lugha wa kila siku au mara kwa mara na katika unenaji wake kwa lugha anaponena kwa lugha ananena kwa masaa mengi, Roho Mtakatifu hahitaji kutumia nguvu kubwa kwa mkristo huyu. Hivyo mkristo wa 
Mwl: Furaha Amon

namna hii anaweza kunena kwa lugha kwa ulaini na anaweza hata kutumia sauti ndogo kiasi chochote anachotaka yeye hivyo anaweza asiwakwaze kwa kuwapigia kelele watu waliomzunguka.
Hapa nataka kuzungumza kuwa mkristo anaweza akanena kwa lugha kwa kutumia sauti ndogo au kwa kutumia sauti kubwa kutegemeana na maamuzi yake mwenyewe hivyo hata kama mahali ulipo uhuru ni mdogo usiache kunena kwa lugha kwa sauti ya kunon’goneza basi iwapo kuna uhuru omba kwa sauti yeyote unayoweza.

usikose kufuatilia sehemu inayofuata ya somo hili na kama unahitaji msaada zaidi tunaweza kuwasiliana kwa simu 0677 609056

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni