Kwa
watu wanaofuatilia sanaa ya muziki wa kizazi kipya katika ukanda huu wa Afrika
Mashariki na kati pamoja na sehemu nyingine mbalimbali duniani na hasa kwa watu
wanaopenda kusikiliza nyimbo za kitanzania. Jina hili la “Mr Ebbo” sio
jina geni kwao,nasema hili ni jina kubwa kwa sababu nyimbo zake zimechezwa na
zinaendelea kuchezwa hata na mashirika makubwa ya utangazaji kama BBC,DW,VOA
n.k. lakini ukweli unabaki palepale kwamba watu wengi walimfahamu Mr Abel
kupitia picha za video au katika vipindi vya TV vinavyorusha nyimbo zake. Lakini
ilikuwa kumuona Abel ana kwa ana akiwa hapa Tanga sio lahisi na unaweza kukaa
miaka mingi usimuone kwa macho. Hii ni
kutokana na tabia yake ya kutokukupenda kutembea ovyo mitaani kwa hiyo muda
mwingi utamkuta yupo nyumbani kwake ama katika studio yake akitengeneza
mashairi ya nyimbo zake ambazo ni tofauti sana na nyimbo za wasanii wengine, na
muda mwingi akiwa nyumbani kwake akiangalia filamu za kitanzania ambazo yeye ni
mpenzi mkubwa wa filamu hizo.
Nakumbuka
ilikuwa kama saa saba mchana nikiwa na rafiki yangu wa kazini Mr Boniface Lyimo
tukiwa tumetoka kwenye mapango ya Amboni kikazi nilimuomba tupitie nyumbani kwa
Mr Ebbo ambaye nilikuwa nimeahidiana naye kufanya mahojiano kwa ajili ya gazeti
la kazini kwetu linaloitwa SAMAWATI. Mimi
binafsi nimefahamiana na Mr Ebbo mwaka 1998 wakati bado alikua hajakuwa na jina
kubwa katika muziki wa kizazi kipya. Na mimi wakati huo nilikuwa naandaa filamu
mojawapo ya Kiswahili inayojulikana kwa jina la KOSA KUBWA ambapo tuliomba
kutumia nyumba yake kuigizia baadhi ya vipande vya filamu hiyo.
Kwa ujumla Mr
Ebbo naweza kumuelezea kama alikuwa mtu mchangamfu anayeheshimu watu pamoja
na kazi zao. Na kama ukienda kwake utatamani usitoke upesi kwa sababu ya
uchangamfu na maneno ya utani utani mwingi wa kuchekesha.
Nilipokutana naye
wakati natayarisha makala hii pamoja na kwamba tulikuwa na muda mchache sana
lakini ulikuwa ni muda ambao ulikuwa wa kurahisha sana na alinipa ushirikiano
wa kutosha kabisa.
HISTORIA YAKE KWA KIFUPI
Kwa kifupi nilimuomba anieleze historia yake na
alinieleza kama ifuatavyo: Abel Motika
alizaliwa 1974 katika Hospital ya Mount Meru Arusha na amesoma elimu ya msingi
toka darasa la kwanza hadi la tatu hapo hapo Arusha na baadae akahamia Nairobi
ambapo alisoma darasa la nne na la tano ndipo akahamia Tanga kwa wazazi wake,
ambapo alimalizia elimu ya msingi na baadae akasoma elimu ya sekondari hapahapa
jijini Tanga.
ALIANZA VIPI SHUGHULI ZA MUZIKI?
Kuhusu muziki
Abel alisema kwamba alianza kuupenda muziki tangu akiwa mtoto mdogo, na
anakumbuka kuwa alikuwa akisikiliza zaidi muziki na hatimaye alijiapiza kwamba
ni lazima siku moja atakuja kuwa mwanamuziki. Alipomaliza darasa la saba tu
tayari alikuwa amejiunga na kwaya ya kanisa la K.K.K.T usharika wa Kisosora na
huko ndiko ndoto yake ilipoingia katika vitendo kwani alijifunza kwa bidii sana
misingi ya muziki, pamoja na matumizi ya ala za muziki,mpangilio wa sauti ya
kwanza hadi ya nne na mpaka nilipokuwa nikiongea naye aliniambia kwa wakati huo
alikuwa na uwezo wa kufundisha watu kupanga sauti na kuziimba na ndivyo alivyokuwa
anafanya ukienda kurekodi katika studio yake ya Motika Record Studio ambayo kwa
sasa hivi inamilikiwa na mke wake Baby na ameihamishia mjini Arusha ambako
ameiboresha zaidi.
Abel alikuwa
kwenye kwaya kwa kipindi kirefu na yeye mwenyewe alisema huko ndiko
alikojifunza mbinu za muziki,mpangilio wa vyombo sauti pamoja na vitu vingine
vingi vya kinidhamu katika sanaa hii ya muziki.
Katika eneo hilo Mr
Abel alipenda kuwashukuru sana walimu wake wa kwaya pamoja na watu wote
waliomsaidia kujenga kipaji chake katika Muziki na hatimaye kuweza kufanya kazi
inayokubalika katika jamii.
ALISEMAJE KUHUSU KUPIGA MUZIKI LIVE ?.
Nilimuuliza Abel
ni kwa nini wanamuziki wa Bongo flavor hawapendi kupiga muziki wa wazi (Live)
na badala yake wanatumia studio na kupiga nyimbo kwenye maholi kwa mtindo wa
kukandamizia kupitia kwenye CD walizotengeneza studio? na nilimuuliza
kwamba haoni hatari za kupoteza hamasa ya watu kujifunza vyombo au ala za
muziki iwapo jamii itaendekeza mtindo wa kutengeneza muziki studio na kuacha
kupiga muziki live?
Abel alisema
inawezekana watu wengi wakaamini hivyo na hasa wanamuziki na wapenzi wa muziki
wa zamani. Lakini yeye kwa maoni yake kama mwanamuziki wa kizazi kipya haoni
ubaya wa kutengeneza muziki studio kwa sababu ni kazi yenye gharama nafuu na
inayohitaji watu wachache kufanya kazi ya watu wengi kwa ubora uleule au na kuzidi pia.Anasema binadamu kila
siku amekuwa akiumiza kichwa na anabuni mbinu za kurahisisha maisha na ndio maendeleo
yenyewe kwani maendeleo ni mabadiliko.
Alisema hata
magari ya zamani yalitengenezwa na mfumo wa gia za manual,lakini
wataalamu wamegundua magari ya mfumo mpya wa gia wa automatic ambayo ni
rahisi zaidi kuyaendesha na sasa hivi mengi yanakuja nchini kwetu inawezekana
baada ya muda tusiweze kuyaona tena magari yenye mfumo wa gia wa manual
yakiingia sokoni kwani sasa hivi kuna mabasi na magari makubwa malori yanayotumia mfumo wa gia wa Automatic.
Kwa hiyo kama ilivyo kwenye magari hata na kwenye muziki ni hivyo hivyo.
Abel
anaamini kwamba muziki live utaendelea kuwepo na utakuwa na wapenzi wake lakini
pia na muziki wa studio utaendelea kuwepo na utakuwa na wapenzi wake na
wote utaendelea kuwepo kama vile ambavyo sasa hivi kuna magari yenye mfumo wa
gia wa manual na automatic yameendelea kuwepo na watu wamekuwa
wakitumia kwa kadri wanavyopenda wapo wanaopendelea yenye mfumo wa manual
lakini pia wapo wanaopendelea yenye mfumo wa automatic.
Abel
aliamini kwamba hata kwenye muziki utakuwepo muziki live ambao utakuwa na
wapenzi wake na utaendelea kuwepo lakini pia utakuwepo muziki wa kutengenezwa
studio ambao pia utakuwa na wapenzi wake upo ambao ukiwapeleka kwenye muziki
live hawatakuelewa. Alisema kwamba muziki kama vile muziki wa reggae na
jazz ni aina ya miziki inayopendeza zaidi ikipigwa live kuliko miziki ya Pop
na RnB
Abel aliamini kwamba muziki wa studio hauwezi kuua vipaji vya
watu wenye nia ya kujifunza vyombo vya muziki kama watakuwepo.Kwani fursa
zitaendelea kuwepo kwa watu wanye nia ya kujifunza, lakini hapendi watu
walazimishwe kurudi nyuma kimaendeleo au kuogopa kutumia teknolojia mpya
kwa hofu ya kuua vipaji kwa sababu hata huko kwenye teknolojia mpya pia
kutahitaji vipaji ndio maana pamaja na kuwa na teknolojia mpya lakini
sio kila mtu ndio sasa anaweza kufanya kazi ya muziki au kuwa mwanamuziki.
KWA
NINI KUMEKUWA NA TEKNOLOJIA YA KISASA KATIKA MUZIKI.?
nilimuuliza
Ebbo swali hili nay eye alinijibu kwamba Teknolojia inakuja kwa lengo na
makusudi ya kupunguza ugumu wa kazi na gharama. Hivyo watu wanapotumia akili ya
kuvumbua vitu ni muhimu kuvitumia ili kuheshimu mawazo yao. Kabla watu
hawajavumbua magari yanayokwenda kwa injini ya mvuke wa mafuta waliwakuta
wenzao wanatumia magari yanayokokotwa na wanyama. Kwa maana hiyo na sisi
hatuwezi kuwalazimisha watu kutembea na punda kama zama za mawe wakati sasa
hivi kuna vyombo vyenye kasi kubwa ya kurahisisha safari,tukifanya hivyo
tutakuwa wapinga maendeleo na wasaliti wa utandawazi na tiknolojia.
Kwa hiyo Abel anasema kwamba sio vizuri kuwalazimisha watu
wapende muziki live wakati sio kila mtu anayependa muziki uwe live wapo watu
katika kizazi hiki ambao hawajawahi kwenda kwenye tamasha linalopiga muziki
live na hata ukimpeleka atashangaa
NI NINI SIRI YA NYIMBO ZA MR EBBO KUKUBALIKA
Nilimuuliza
Abel ni kwa nini nyimbo zake zinakubalika na zinapendwa na kada ya watu wa rika
na hadhi tofauti. Abel alinijibu kwamba Tangu zamani alijiwekea misingi ya aina
ya nyimbo alizotaka kuziimba. Alipenda aimbe nyimbo ambazo hazitamkwaza mtu, Nyimbo
zenye aina ya ujumbe unaowakilishwa kama ucheshi lakini ambao ndani yake kuna
ujumbe utakaomfanya mtu afikiri. Alisema kuwa kama angekuwa anapenda kuimba nyimbo za
mapenzi au za kisiasa pengine kila siku angekuwa anatoa nyimbo. Lakini nyimbo
anazotunga yeye ni za aina yake tofauti na za mtu mwingine kwa sababu hazimkwazi mkubwa,mtoto,mwanamke,mwanamume
kijana mzee na zinapendwa hata na watumishi wa Mungu. Aliniambia kuna wachungaji na mashehe wanazifurahia nyimbo
zake na kumueleza waziwazi kuwa wanaikubali sana kazi yake. Hii ni kwa sababu
ya aina ya tungo zake alisema Mr Ebbo kuwa anatengeneza nyimbo zenye ujumbe
unaoleweka, na video zake anajitahidi ziwe safi ambazo hazitasababisha wazazi
wakimbiane na watoto sebuleni,hiyo ndio siri kubwa ya mafanikio yake katika
sanaa hii. Anasema yeye kama hajapata wazo la kuimba anaona ni bora atulie
kuliko kulazimisha kutoa nyimbo ili kuwahi soko na hili ndilo tatizo kubwa
linalowapata waimbaji wengi wa muziki wa kizazi kipya.
NI MWANAMUZIKI GANI AMBAYE EBBO ALIYEMPENDA?
Nilimuuliza
Mr Ebbo ni mwanamuziki gani anayempenda na ambaye angependa awe kielelezo chake
katika mafanikio yake kimuziki. Alinijibu kuwa ni mwanamuziki wa zamani wa
Jamaika Robert Nesta Marley (Bob Marley). huyu ni mwimbaji ambaye ndio
aliyempenda na kumfanya kuwa kielelezo chake katika muziki tangu zamani. Abel
alisema kwamba yeye ni mpenzi wa muziki wa reggae na alipenda sana
kufanya muziki wa reggae lakini kulingana na soko la muziki kwa nchi
yetu ingekuwa ni vigumu sana kwake kupata mafanikio aliyokuwa ameyapata kama
angepiga muziki wa reggae. Lakini alikiri kwamba ameamua kupiga muziki
anaopiga sasa ili kuwashika watu wanaomkubali lakini muda mwingi akiwa nyumbani
nyimbo kwake nyimbo nyingi anazosikiliza ni za reggae
NI WANAMUZIKI GANI WA TANZANIA WANAOMVUTIA?
Baada
ya kunijibu aina ya muziki na wanamuziki anaowapenda katika dunia nilimgeuzia
kibao aniambie wanamuziki anaowapenda Katika nchi yetu ya Tanzania nay eye
alinijibu kuwa anapenda sana wanamuziki
wote ambao wapo makini na wanaoheshimu muziki kama taaluma na sio sehemu ya
kupotezea muda au kujifurahisha na kuwafurahisha watu tu. Anapenda wanamuziki wote wanaojua kwamba muziki ni kazi
inayohitaji staha na kujiheshimu kama ofisa au mwakilishi wa wananchi.
Lakini bado nilijitahidi sana kumbana aniambie
mwanamuziki mtanzania ambaye yupo ndani ya uvungu wa moyo wake ndipo
aliponifichulia kwamba anavutiwa sana na kazi inayofanywa na Msanii Mrisho
Mpoto na Saida Kaloli. Anasema kwamba Mpoto anapenda sana muziki wake
kwa sababu ni muziki wa kufunga na sio
wa kuimba mambo waziwazi alisema katika wimbo wake mpya ambao aliamini kuwa ungetoka
karibuni alitegemea kuwa utakuwa na
fikra mpya. Na atajaribu kuwakumbusha Watanzania na hasa wakazi wa Tanga
kwamba pamoja na kuwepo kila kitu katika Super Market lakini wasisahau
walikotoka wakumbuke na masoko yao ya ngamiani mgandini na masoko mengine ya
mitaani ikiwa ni pamoja na magenge. Alisema vitu kama super market sio
utamaduni wetu kwa asili ni utamaduni wa Ulaya hivyo tusiuuwe utamaduni wetu na
kuukumbatia utamaduni wa Ulaya.
Anasema popote
uendapo katika dunia hii kitu cha kujivunia ni cha kwako. na usipende kujivunia
cha mtu mwingine. Abel ambaye mpaka wakati naongea naye tayari ana Albam kadhaa.
Alisema kwamba wimbo ambao anauheshimu
ni ule uliomtambulisha kwenye ramani ya muziki wa Tanzania wimbo wake wa kwanza “mimi maasai bwana”ambao ulikuja kubeba na nyimbo
nyingine nyingi.
Abel ambaye ni
baba wa watoto watatu hakutaka kabisa kuongelea suala la mgogoro wa ndoa yake
na mzazi mwenzake ambayo ililipotiwa sana kwenye vyombo vya habari na hasa
magazeti ya udaku yaliyotoka kila wiki. Nilimuuliza kama anaweza kutoa ufafanuzi
kwa mashabiki na wapenzi wake wajue ni nini hasa kilichotokea?
Abel aliniambia
kwamba anayaacha yaliyoandikwa yabaki kama yalivyo kwa sababu ni mambo ambayo
yanaigusa sana nafsi yake na hawezi kusema neno baya lolote kwa sababu yule ni
mzazi mwenzake na ndugu yake kwa maana wanaunganishwa na watoto kwa hiyo
akimsema vibaya au akimtukana ni kama anajitukana yeye mwenyewe.
Baada
ya mazungumzo haya sikuwahi kumuona tena Ebbo na wala sikusikia habari zake
mpaka wakati naandaa shindano la kusaka vipaji. Nilimuweka katika orodha ya
watu watakaotembelea kambi yatu ya washiriki. Lakini siku moja alfajiri sana
nilipigiwa simu ya kunitaarifu kwamba Ebbo ameaga dunia. Na mtu aliyenipa
taarifa hizo namheshimu sana lakini nilifikiri labda taarifa zake sio sahihi lakini
baada ya muda nikanza kupata simu za watu mbalimbali ikawa ni habari mbaya sana
iliyofunika jiji la Tanga nasi tukasema Jina la Bwana litukuzwe
Huyu
ndio MR EBBO mwanamuziki,rafiki,shujaa wetu aliyetufurahisha wakazi wa jiji la
Tanga na watanzania wote kwa ujumla.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni