Jumanne, 31 Julai 2012

JIJI LA TANGA NI CHIMBUKO LA BONGO MOVIE




Waswahili wana msemo mmoja maarufu sana usemao mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Msemo huu unastahili kabisa kupewa mkoa wa Tanga kulingana na historia yake ya sanaa hii ya filamu.Kama tunavyofahamu kwamba jiji hili lenye bandari na hali inayokubalika kwa utengenezaji wa filamu kwa sababu lina hali zote zinazohitajika kwa watengenezaji wa filamu, yaani bahari  misitu milima havipo mbali pia kuna vivutio vingine vingi sana vya kitalii ambavyo ni muhimu sana kwa viwanda vya kutengeneza filamu.
Kumbuka kwamba Tanga ni moja kati ya miji ya mwanzo kabisa kupewa hadhi ya kuwa  manispaa. Hata katika hali ya kiuchumi jiji hili lilikuwa ni moja kati ya miji yenye viwanda vingi katika miji iliyokuwa inakua kwa kasi kubwa sana kiuchumi hapa nchini Tanzania. na kwa sababu hiyo ilikuwa ni moja kati ya miji iliyokuwa inawavutia sana watu wengi kutoka miji mbalimbali ya Tanzania kuja kufanya kazi katika viwanda na katika mashamba ya mkonge ambayo yalikuwa mengi sana wakati huo.
Kwa sababu hiyo na nyingine nyingi,tunaweza kukubali kwamba jiji hili lilikuwa ni moja kati ya miji ya starehe sana katika miaka hiyo na moja kati ya vivutio vya starehe hizo ilikuwa ni majumba ya kuonyeshea filamu ambayo yalikuwa yapo katikati ya jiji hili ambalo limepangika vizuri sana kwa ardhi ya tambarare pamoja na barabara zake 21 pamoja na ardhi nzuri yenye rutuba na ustawi wa maua mazuri ya kuvutia.Kwa hiyo ninaposema kwamba jiji hili ni chimbuko la filamu za kitanzania, ambazo kwa sasa zimeshika kasi kabisa katika nchi yetu,na hasa katika jiji la Dar es salaam. Ndio maana naona umuhimu wa kuwakumbusha watanzania wenzangu kwamba tunapofurahia mafanikio haya na kupongezana,tusiwasahau watu waliojitoa muhanga kuhakikisha sanaa hii inasimama. Ijapokuwa ilikuwa katika hali ngumu sana ya teknolojia duni, na hamasa hafifu ya watanzania kukubali filamu za ki- Tanzania.

Hapo ndipo inatupasa kuwakumbuka 

watu maarufu wa jiji hili kama AbdulHakem S Bayakub, Said El Siag na mzee Amri S A Bawji maarufu kama mzee SANI ambaye ni mkurugenzi wa gazeti la sani na mtunzi wa hadithi za kusisimua. Yeye kupitia gazeti lake aliandika hadithi maarufu sana iliyowavutia watu wengi sana kwa wakati huo ikijulikana kama “Love story Tanganyika na Unguja” 

Hadithi hii baadaye alikuja kuibadilisha na kuwa filamu iliyotengenezwa na Abdulhakem S Bayakub. ambayo naweza kusema kuwa ndiyo ilikuwa ni mojawapo ya filamu za kwanza kwa mtindo ule ukiacha filamu nyingine ya hapa Tanga iliyokuwa ikijulikana kama “SHAMBA KUBWA”mtindo huu sasa ndio unaotumika kwa filamu za kitanzania maarufu kama Bongo Movie. Kwa hiyo tutakapokuwa tunawatafuta mashujaa wa filamu za kitanzania tusiache kuwapa heshima yao watu hawa.

Kwa watu wasiojua sana habari zinazohusu sanaa ya maonyesho ni vizuri nikawakumbusha kwamba katika sanaa za maonyesho kuna tanzu kama maigizo(tamthilia),nyimbo kama za kwaya,taarabu na bendi,ngoma za kiasili,mashairi,ngonjera,majigambo,ada za harusi,utambaji wa hadithi,chemsha bongo,jando na unyago na mazungumzo ya ana kwa ana.Tangu zamani watanzania wamekuwa wakizitumia tanzu hizi za sanaa za maonyesho katika shughuli mbalimbali za kila siku kwa karne nyingi sana na kwa kutumia tanzu hizi jamii iliweza kukosolewa,kufundishwa,kuelekezwa,kuongozwa vyema,kutahadharishwa kurithishwa utamaduni kutiwa ujasiri n.k.

Kwa hiyo tunapoongelea filamu tunaongelea hadithi iliyotayarishwa ama kwa kuandikwa au kwa ufaraguzi(kuelekezwa na mtu) ambayo ndani yake ina matukio,migogoro,visa,mikasa na hata vitimbwi ambavyo vinaweza kuvaliwa na wahusika na kuwasirishwa kwa njia ya matendo mbele ya hadhira kwa minajiri ya kuikosoa,kuifunza,kuishawishi,kuirekebisha na hata kuitahadharisha.Mara nyingi filamu hutoa hata burudani kwa wanajamii wakati likitimiliza maudhui yake niliyoyataja hapo mwanzo.



Ingawa filamu ni aina ya simulizi,lakini inatofautiana sana na aina nyingine ya simulizi kutokana na jinsi inavyowasilishwa kwa walengwa.Kwa mfano unaposoma kitabu cha simulizi (Novel), huwa
kinaelezea habari ambayo inawahusu wahusika wakuu ambao itakubidi wewe msomaji utafute sura zao na maumbile yao kutoka kichwani mwako, na pengine kwa msaada wa kutumia maelezo machache ambayo mwandishi atakupa kulingana na wasifu wa muhusika. Novel inaelezea habari (hadithi) yake katika muunganiko wa dialogue and narrative na inakuwa tayari katika kurasa iliyochapwa. Baadhi ya filamu huwa zinafanya vizuri sana kiasi kwamba watu wengi wanaamini kwamba maandishi hayafikishi ujumbe unaofaa mpaka iigizwe mbele ya jamii.

Filamu zinakubalika sana kutokana na kuweza kumuamuru na kumsahihisha mwanadamu katika ung’amuzi wake.

Kwa mtu asiyejua kabisa habari za utengenezaji wa filamu anaweza akafikiri ni kitu chepesi sana, kinachoweza kufanywa na mtu yeyote mwenye video camera ambaye amezowea kupiga picha harusi na mikutano.Kama nilivyosema awali kwamba filamu ni mojawapo ya sanaa za maonyesho inayopendwa zaidi duniani kote,kila siku mamilioni ya watu duniani kote huangalia filamu katika kumbi mbalimbali za kuonyeshea filamu au kupitia katika televisheni au kwenye video CD na video Tape majumbani kwao.

Wakati wa kutengeneza filamu,mawazo ya mtayarishaji na kundi la watengenezaji hufafanuliwa katika hisia za ndani kabisa kiasi ambacho walengwa hujihisi kwamba wanaona vitu halisi na wala sio vya kuigiza.
Katika nchi zilizoendelea,watengenezaji wa filamu ni watu wanaotegemewa sana na serikali zao katika kutangaza sera zao au propaganda zenye nia ya kuonyesha uwezo wa mataifa yao kiuchumi,kijeshi,kisiasa n.k. Hata katika mashirika makubwa ya kijasusi yanawatumia sana wataalamu hawa katika kufichua mipango ambayo wanahisi inakusudiwa kufanywa na magaidi au maadui wa Taifa lao.


Filamu ni sanaa yenye gharama kubwa sana,kwa nchi zilizoendelea kama Amerika filamu ndefu inaweza ikatumia gharama inayopindukia dola milioni hamsini $50,000,000 na watu wengi sana hupata mikataba ya ajira na kusafiri sehemu nyingi za dunia katika kukamilisha filamu. Na inagharimu si chini ya miezi sita mpaka miaka miwili kukamilisha filamu moja ndefu.
Kiwango nafuu kabisa kwa gharama ya kutengeneza filamu katika Hollwood ni kiasi kisichopungua dola $ 250,000.
Kazi ya kutengeneza filamu katika nchi yetu inahitaji nguvu kubwa na msukumo sana kutoka kwa watu wenye uwezo kifedha na hasa serikali kupitia katika wizara inayohusika na utamaduni na michezo,sipendi ukose kufahamu kwamba, Serikali yetu kwa kushirikiana na nchi mojawapo za skandinavia’ inao mfuko wa kufadhili vitu kama hivi unaojulikana kama mfuko wa utamaduni wa Taifa. Lakini katika eneo la filamu ningependa wizara hii iende mbali zaidi ya hapo,kwa sababu ni eneo ambalo nchi inaweza kukuza uchumi kwa kupitia sanaa hii.

Katika nchi nyingine kwa mfano India,watengenezaji filamu wa “Bollywood” waliingizia serikali yao mapato makubwa sana ambayo yalisaidia sana kukuza uchumi wa nchi yao.Hii ilitokana na mauzo ya filamu zao za kihindi zilizokuwa zinashabikiwa karibu katika dunia nzima,wale watu waliozaliwa siku nyingi watakumbuka jinsi ilivyokuwa hata hapa kwetu Tanzania nyakati zile.
Hata sasa hivi tunavyoweza kuona soko la filamu kama za Nigeria lilivyoshika kasi katika nchi yetu. Ni dhahili kwamba kama wafanya biashara wetu hawafanyi ujanja ujanja wa kukopi nakala hizo, au wanigeria wakiamua kusimamia kazi zao zisiibwe na mataperi wanaozisambaza hapa nchini. Ni wazi kwamba serikali yao itanufaika na mapato yanayopatikana kutokana na kuuza kazi zao katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki.
Hata hapa kwetu Tanzania,watengenezaji wa filamu wakijiweka katika mikakati ya kuhakikisha filamu zetu zinashika kasi, na kuitangaza nchi yetu watafanikiwa sana na hasa wakitumia mtaji mkubwa wa lugha yetu mwanana ya Kiswahili ambayo ni moja kati ya lugha zinazopewa umuhimu na mataifa ya afrika mashariki na kati.
Kinachotakiwa hapa ni ushirikiano wa dhati kati ya watengenezaji wa filamu kwa upande wao,vikundi vya sanaa za uigizaji na serikali kwa maana ya kuviwezesha vikundi na kufanikisha malengo kwa nia ya kuongeza ajira na kukuza soko la filamu kwa nchi za ukanda wa Afrika mashariki na kati.
Kitu ambacho hakiepukiki katika mipango hii,ni pamoja na serikali kutenga eneo la ardhi au kijiji maalumu kwa shughuli za uigizaji. Ikiwezekana kwa kila Mkoa kama vile kilivyo kijiji cha makumbusho kwa jiji la Dar es salaam. Lakini eneo linatakiwa liwe kubwa na ambalo waigizaji watapatiwa viwanja na kujenga kijiji ambacho kinatakiwa kiwe na kila kitu ili kuepusha migongano ya kijamii kwa mfano,mahospitali,mashule, vituo vya polisi,mahakama,nk

Vitu ambavyo vinaleta usumbufu sana mnapotaka kurekodi kipindi chenu katika mahospitali ya jumuiya au vituo vya polisi au mahakamani na wakati,kwanza sheria ya nchi yetu hairuhusu kufanya vitu kama hivyo au kufunga mtaa fulani kwa shughuli za kurekodi. Na kwa jinsi filamu ilivyo na kanuni zake haitakiwi kabisa kudanganya makusudi,kuwaonyesha watu chumba fulani halafu unawaambia watu hapa ndio mahakamani wakati wanaona kitu tofauti. Kwa maana hiyo unakuwa umetoa ule uhalisia wa filamu ambao ndio unaotakiwa,Kwa hiyo iwapo kutakuwa na vijiji vya wasanii kutasaidia sana kuzifanya kazi zao kwa uhuru na kuongeza ubora wa kazi zao.

Tatizo lingine ambalo lipo wazi kwa waigizaji wetu na watengenezaji wa filamu wa Tanzania,wao wanafikiri wakishaonekana kwenye vituo vya televisheni ndio kilele cha mafanikio yao. Wakati ukweli wanaishia kupata umaarufu bila kuwa na pesa. Mpaka wakati naandika makala hii naambiwa kwamba kwa jiji la Dar es salaam peke yake kuna vikundi vya uigizaji zaidi ya mia tatu 300 ambavyo vimesajiliwa lakini vyote vinasubiri kufanya kazi na vituo vya TV ambavyo havifiki saba.



Naamini watu hawa wangetegenezewa soko la ndani, na kujitahidi kutengeneza kazi zao katika kiwango kinachovutia,Wasingekuwa na ndoto za kusubiri vituo vya luninga. Watu wangetafuta masoko ya kazi zao kwenye maduka na wangeuza hata nje ya nchi.Kitu kingine ambacho naamini kwamba kitaweza kuinua kiwango cha sanaa ya uigizaji,ni mafunzo kwa waigizaji wenyewe. Kwa mfano nikiangalia filamu za Nigeria kitu cha kwanza kinachonivutia ni namna waigizaji wao walivyo makini na nidhamu kwa kile wanachotakiwa kuigiza. Kwa watu kama mimi,ambao tunapenda kuangalia makosa katika kazi za wenzetu,tunashindwa kabisa kuwakosoa wanaigiza katika uhalisia wote.
Lakini hapa kwetu inaonekana sivyo.Watu hawatumiwi kulingana na uwezo wao bali ni kwa urafiki na kujuana, matokeo yake wanapewa nafasi ambazo ukiziangalia zinaonekana kuwapwaya kabisa.

KAZI YA UPIGAJI WA PICHA ZA FILAMU
Kama nilivyoeleza mwanzo kwamba kazi ya upigaji wa picha za filamu sio kitu chepesi, katika filamu mpiga picha huchukua picha moja kutoka katika kona tofauti tofauti na anapokuwa studio huzichanganya na kutafuta kona iliyotoka vizuri na kuleta ladha nzuri kwa mtazamaji.
Makosa mengi na mafanikio tunayoyaona katika filamu zetu yanatokana na wasimamizi ingawa katika filamu sifa nyingi anapata muigizaji lakini ukweli ni kwamba kuna kundi kubwa la watu walio nyuma yake wanaomuelekeza nini cha kufanya. Na kama hawajaridhika na kipande chochote cha filamu hakiwekwi katika filamu au watarudia upigaji wa kipade hicho cha filamu mpaka kiendane na mawazo ya mtayarishaji.

WATANZANIA WANABADILIKA
Siku hizi watanzania wameanza kuwa na tabia ya kupenda na kuthamini vitu vyao kama huamini hebu angalia nidhamu inayokuwepo nyumbani wakati familia inaangalia michezo ya kuigiza katika luninga hata kama walikuwepo watoto wasumbufu wanaodeka ikifika wakati huo wote wanatulia kabisa
Ili kuleta heshima kwa filamu za Kitanzania ni muhimu sana kwa kundi la watengenezaji wa filamu ambalo linawahusisha waongozaji wa filamu, (Directors), watunzi wa hadithi (Story writers) wataalamu wa mavazi (Costume designer), wataalamu wa kubadili maumbo (make up people) watengenezaji wa mandhari (set designer) wasanii (actors), n.k. Katika ushirikiano huu lengo kubwa ni kuendeleza mawazo yaliyozalishwa na mtu mmoja kuhusiana na lengo la filamu husika.
INATAKIWA MIKUTANO YA KUTOSHA.
Wakati wa kutengeneza filamu,Mara nyingi hutumika mikutano na majadiliano ya pamoja ya mara kwa mara ili kuhakikisha kila msanii ameelewa vizuri lengo la filamu,na pia katika mikutano hii inasaidia sana urahisi wa kutafuta wafanyakazi wenye ujuzi mzuri kwa sababu wataalamu hawa wanakuwa wanajuana vizuri, hivyo watapatikana watu wenye ujuzi unaokubalika.

Wakati filamu inatoka katika hatua ya kabla ya uzalishaji,watunzi, waongozaji na watu wote wanaohusika katika hatua za mwanzo za uzalishaji wa filamu. Wataandaa  mpango wa kuelezea namna wanavyotaka kuwasilisha ujumbe wao na mfumo wa vitendo (Action) kwa kila sentensi itakayotamkwa, kwa mfano utasema neno fulani wakati ama umeshika glass, na utakapoanza kumimina utamalizia na sentensi fulani. Na mpangilio wa maandishi ya wahusika yatakavyoonekana kama wanavyopanga katika maamuzi yao.
katika hatua hii ndipo hupangwa wasanii na nafasi watakazoigiza vifaa na vitu muhimu vitakavyohitajika katika kila kipande cha filamu scene ya utengenezaji wa filamu.
MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOANDIKA HADITHI ZA FILAMU
Ninachowashauri waandishi wa hadithi za filamu za Tanzania. Ni Kutulia kwa makini sana na kuzingatia kanuni zinazotakiwa. Wasiwe wavivu katika kutafuta undani wa tatizo tunapoandika hadithi za filamu kwa sababu uzuri wa filamu unaanzia katika hadithi na hubebwa na waigizaji. Kumbuka kuwa kabla ya kuanza kutayarisha hadithi ya filamu jiulize na kujibu kwanza masuali yafuatayo;-
1.   jamii ina tatizo gani?.
2.   je tatizo hilo linajulikana kwa jamii unayoilenga?
3.   kama linajulikana walichukua hatua gani?
4.   je hatua walizochukua au wanazochukua zinasaidia kutatua au hapana?
5.   kama hazikuwasaidia je wewe unawashauri wafanye nini?
Majibu ya maswali haya yote ndio msaada mkubwa sana kwa mtayarishaji katika kutayarisha maudhui (Theme) ya filamu yake. Na ni lazima afahamu kwamba, hatimaye atatakiwa aonyeshe anataka kutoa ushauri gani juu ya jambo hilo katika hisia zake. Na anataka hatima ya jambo hilo iweje katika hisia zake,na anataka hatima ya jambo hilo iweje kwa mtazamo wake.
Katika hatua ya uzalishaji wa filamu


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni