Alhamisi, 30 Agosti 2012

FAIDA YA KAZI ZINAZODHARAULIKA


Faida za kufanya kazi au shughuli inayodharauliwa


Rais wa marekani Barack Obama akiwa na bibi mzazi wa baba yake husein Obama alipokuja kuwatembelea nyumbani kwa mababu zake Kenya
BINADAMU wengi wana tabia ya kuchagua vitu na hasa vizuri kwa lengo la kulinda heshima yao mbele ya wenzao. Kwa tabia hiyo ya utukufu wengi wetu tunapenda kuwa na kazi nzuri si itakayotusaidia kuishi bali kukidhi heshima yetu mbele ya jamii.
Vijana wengi waishio hasa maeneo ya mijini wako radhi kuishi maisha ya kubangaiza kwa kukaa vijiweni kupiga soga na kuvuta bangi lakini si kwenda kuuza mboga za mitaani, kubeba zege kwenye kandarasi za ujenzi au kuuza maji kwenye mikokoteni.
Edward Lowasa Waziri mkuu mstaafu ambaye ameonya mara nyingi kuhusu ajira kwa vijana.


Hawataki kazi au shughuli zinazochukuliwa kama fedheha licha ya kwamba wanaozifanya wanajipatia kipato cha kuendesha maisha yao na familia zao kwa sababu tu ya ule umwinyi mkuu wa kutaka utajo mzuri mbele za watu.
kuna watu wengine bado wanaishi kwenye utumwa huu wa utukufu, wanajiona hawawezi kufanya kazi dhaifu hata kama zina kipato, kwa fikra tu kwamba akiniona msichana fulani pale mtaani atanidharau.  Kumbe kwa upande mwingine wanajikuta wanadharaulika zaidi kuliko hata nilivyojikinga kwa kukwepa kazi.



Kwa namna yoyote ile, heshima ya mtu ni kazi na mafanikio ndiyo kipimo cha akili. Hii haijalishi unafanya shughuli ya heshima kimtazamo au yenye kudharauliwa na wengi kimawazo. 
Haiwezi kutokea kijana muuza maji aliyejenga nyumba yake ya vyumba vitatu na kujiendeshea maisha yake akadharauliwa na mfanyakazi wa benki anayetangatanga kwa ufujaji wa fedha na kukosa tija ya maisha, akaheshimiwa kwa lemba la kazi yake tu. Kamwe hilo haliwezekani.


Ikiwa ni hivyo, kwa nini watu wanachagua kazi? Je, hatuna ushuhuda wa mafundi viatu kuwa na

nyumba, miradi na biashara kubwa huku wafanyakazi maofisini wakigeuka wakopaji kwenye maduka ya Wamachinga wanaotembeza nguo mikononi kwenye mitaa ya mijini? Naamini ushahidi upo wa kutosha.

Maeneo mengi ya wakulima wa zao la tumbaku katika mkoa wa Tabora, kwa mfano, na vijana wanaomiliki maduka madogomadogo maarufu kama vioski ni wageni ambao walifika kwenye mkoa huo kama watumishi au wasaidizi wa mashambani, wakifanya kazi dhaifu ambazo wenyewe huzitafsiri kama shughuli zisizokuwa na heshima.  Lakini pato la kazi hizohizo ndilo hatimaye huwapatia vioski ambavyo wenyeji huenda kukopa bidhaa. 

Katika hali ya kawaida, kazi zinazoonekana dhaifu ni funzo kubwa sana katika maisha na mara nyingi hujenga ari  ya aina yake katika uwajibikaji wenye lengo la kujikomboa na hiyo zana ya kudharaulika.
Watu wengi matajiri historia zao huanzia kwenye kazi dhaifu.  Huko ndiko kulikowafunza nidhamu ya matumizi ya fedha. Kwenye dharau kumejaa maarifa na mbinu za ukombozi kuliko mahali penye maisha ya heshima ambako hupumbaza na kuwafanya wahusika wasipige mbio kuelekea kwenye mafanikio zaidi.
 
Wito wangu kwa vijana wenzangu, Watanzania wote, tusikubali kuishi na ufalme, heshima na utukufu usioweza kutusaidia, badala yake tukubali kufanya kazi hata zinazoonekana dhaifu kwa lengo la kujipatia kipato ili hatimaye tutafsri hali ya kudharauliwa kuwa heshima

Jumatatu, 27 Agosti 2012

FAHAMU NDEGE KUBWA DUNIANI



rr
Fahamu ndege kubwa duniani;Boeing kuwasilisha 787 ya kwanza kabisa

Kampuni ya utengenezaji ndege ya Marekani - Boeing - itawasilisha rasmi ndege ya kwanza aina ya 787 Dreamliner kwa shirika la ndege la All Nippon Airways (ANA) la Japan.

Dreamliner

Awali Dreamliner ilipangwa kuwa tayari mwaka 2008, lakini Boeing imekumbwa na mfululizo wa vikwazo, ambapo hivi karibuni moto uliwaka ndani ya ndege za majaribio mwezi Januari.
Ndege hiyo isiyotumia mafuta mengi imetengenezwa kwa kutumia malighafi nyepesi.
Boeing inapanga kutengeneza ndege 10 kwa mwezi kuanzia mwaka 2013.

Ndege hiyo itakabidhiwa kwa ANA katika kitongoji cha Everett, Washington kabla ya kuruka na kwenda Tokyo ambapo itawasili siku ya Jumatano.
Dreamliner
Boeing imesema ndege hiyo yenye safu mbili na ukubwa wa kati ina madirisha makubwa na hali nzuri ya unyevunyevu ndani ya ndege na hewa safi hali ambayo itaruhusu abiria kuwasili wanapokwenda wakiwa katika njema zaidi.
Lakini matatizo ya Dreamliner yameharibu sifa ya Boeing, na kampuni hiyo ina matumaini kuwa uzinduzi wenye mafanikio utasaidia kufuta ucheleweshwaji uliotokea.

Mashaka

Makamu wa rais wa masuala ya masoko wa Boeing, Randy Tinseth ameiambia BBC: "Huu ni mradi ambao umetoka mbali. Tunaamini itakuwa ndege nzuri.
"Hatimaye tunaona matumaini ya maelfu ya 787 katika siku za mbele."
Alipoulizwa sababu za kuchelewa kutoka kwa ndege ya Boeing 787 Bw Tinseth amesema "kuna mashaka katika kila ndege mpya".
Amesema: "Tumetumia fedha zaidi katika ndege hii kuliko tuliyotarajia, lakini kwa mara nyingine tena bado tupo katika nafasi nzuri, tunaamini mradi huu utaendelea kuwa na faida."

Uzalishaji

Uzalishaji wa Dreamliner kwa sasa unatoa takriban ndege 2.5 kwa mwezi.
Mpaka sasa ndege zipatazo 821 aina ya 787 zinatakiwa kununuliwa kutoka Boeing, ambayo inasema inatumia 20% pungufu ya mafuta yanayotumiwa na ndege za kawaida za ukubwa huo.
Boeing na Airbus
Ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 290 katika ndege yake kubwa ya 787-9, lakini 787 ni ndogo kuliko jumbo jet 747 ya Boeing.


Hata hivyo, Boeing inadhani kuwa 787 itakuwa maarufu katika makampuni ya ndege, kwa kuwa itakuwa na uwezo wa kuruka moja kwa moja kwenda katika viwanja vidogo vya ndege.

Mahasimu

Mahasimu wa Boeing wa Ulaya, Airbus, kwa sasa inatengeneza mshindani wa moja kwa moja wa 787, iitwayo Airbus A350 XWB.
Airbus imepokea maombi ya ununuzi yanayozidi ndege 550 ya A350 XWB, lakini ndege hiyo haitakuwa tayari hadi mwaka 2013.


ANA inatazamia kuanza kutumia ndege ya kwanza aina ya 787 katika safari kutoka Tokyo kwenda Okayama-Hiroshima tarehe 11 Novemba.
Baadaye itaruisha ndege hiyo kimataifa kutoka Tokyo kwenda Frankfurt Ujerumani, mwezi Januari.
"Watu wengi wanasema kuwa ndege hii [787] itakuwa maarufu sana," amesema George Hamlin, rais wa taasisi ya washauri wa usafirishaji ya Hamlin.