Ijumaa, 18 Machi 2016

SOMO : KUFUNGA


Kufunga ni tendo la hiari la kuacha kula chakula na kinywaji,   au kuacha kinywaji,kwa kipindi fulani. Biblia imeandika mifano mingi ya watu waliofunga wengine waliacha kula vyakula vya aina fulani tu kwa muda wa mfungo wao.

Mfano wa hili la mwisho ni ule mfungo wa Daniel wa majuma matatu ambao Biblia inasema;-
 hakula chakula kitamu...nyama wala divai (Daniel 10:3)  

Vilevile kuna mifano michache katika maandiko yawatu waliofunga kula chakula na maji,lakini aina hii ya mfungo kamili si wa kawaida na unatakiwa uhesabiwe kuwa wa ki Mungu ikiwa utazidi siku tatu. 

Kwa mfano wakati Musa alipokaa siku arobaini bila kula wala kunywa chochote,alikuwa mbele za Mungu mwenyewe mpaka uso wake uling'aa (ona kutoka 34:28-29).

alirudia mfungo wa siku arobaini tena,muda mfupi tu baada ya ule wa kwanza (ona kumbu 9:9-18) 

kwa maana hiyo mifungo yake haikuwa ya kawaida. na si vizuri kwa yeyote kujaribu kuiga bila ya msaada wa Mungu. kwa hali ya kawaida haiwezekani mtu kukaa zaidi ya siku chache bila maji. unaweza ukaishiwa maji mwilini na hatimaye kusababisha kifo.  

hatari kwa afya sio kukaa bila maji muda mrefu tu, bali hata kuacha kula chakula kwa vipindi virefu huweza kuwa hatari pia, hasa kwa watu ambao wana matatizo yanayohusu vyakula.

lakini pia hata wenye afya nzuri wanapaswa kuwa makini kuwa makini ikiwa wanapanga kufunga kwa muda mrefu zaidi ya wiki moja.

                           KWA NINI WATU WAFUNGE
Kusudi la msingi la kufunga ni kujipatia muda wa ziada ili kuomba na kumtafuta Bwana, ukisoma Biblia hakuna mahali ambapo kufunga kunatajwa bila kuhusisha maombi. hivyo inatufanya tuseme kwamba kufunga bila kuomba ni sawa na kazi bure.

kwa mfano katika kitabu cha matendo tunasoma sehemu mbili kuhusu kufunga na kote maombi yanatajwa, sehemu ya kwanza (ona matendo 13:1-30) manabii na waalimu katika kanisa la Antiokia walikuwa wakimfanyia Mungu ibada ya kufunga. 

walipofanya hivyo wakapokea mafunuo ya kinabii, na kwa sababu hiyo wakamtuma Paulo na Barnaba kwenda safari yao ya kwanza ya kimisheninari. katika sehemu ya pili Paulo na Barnaba walikuwa wanaweka wazee wa kusimamia mapya huko Galatia.

Tunasoma hivi,na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa na kuomba na kufunga,wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini (Matendo 14:23)

pengine katika mfano huu wa pili, Paulo na Barnaba walikuwa wanafuata mfano wa Yesu,maana yeye aliomba usiku kabla ya kuchagua wale thenashara.(ona Luka 6:12)

Maamuzi muhimu kama kuchagua viongozi wa kiroho yanahitaji kuombewa mpaka mtu awe na uhakika kwamba ameongozwa na Bwana. Kufunga kutatoa nafasi nzuri zaidi ya kuomba kwa habari hiyo.

Ikiwa Agano Jipya linashauri wanandoa kuacha kushirikiana kimwili ili kuongeza muda wa kuomba (ona 1Wakor.7:5) basi ni rahisi kuelewa jinsi ambavyo kuacha chakula kwa muda kuna fanikisha kusudi hilo.

kwa hiyo tunapohitaji kuomba ili Mungu atuelekeze kwa maamuzi muhimu ya kiroho,kufunga ni kitu cha kufanya. Maombi kwa ajili ya mahitaji mengine yanaweza kufanywa kwa muda mfupi sana. (mfano hatuhitaji kufunga ili kuomba sala yaBwana)

                      SABABU MBAYA ZA KUFUNGA.

 Kwa kuwa nimetoa sababu sababu za kimaandiko za kufunga katika agano jipya.hebu tutazame sababu zisizo za maandiko za kufunga.
 Kuna watu wanafungakwa matumaini kwamba itaongeza uwezekano wa Mungu kujibu maombi yao,sivyo,maana Yesu alituambia kwamba msingi wa kujibiwa maombi ni imani,si kufunga (ona Mathayo 21:22). tukumbuke kwamba kufunga hakumbadilishi Mungu hata kidogo.
 Yeye yuko vilevile kabla hatujafunga,na tunapofunga na hata baada ya kufunga.
 kufunga si njia ya kumbana Mungu au namna ya kumwambia lazima ujibu maombi yangu au la sivyo nitafunga mpaka nife!
 huko si kufunga ki Biblia- huko ni kugomea chakula wakuu!
 Kumbuka Daudi alifunga na kuomba kwa siku kadhaa ili yule mtoto wake mgonjwa waliyezaa na Batsheba asife. lakini mtoto alikufa kwa sababu Mungu alikuwa anamwadhibu.
 Kufunga kwa Daudi hakukumbadilisha Mungu kwa sababu hakuwa anaomba kwa imani,hakuwa na ahadi yeyote ya kusimamia.alikuwa anafunga na kuomba kinyume na mapenzi ya Mungu kama matokeo yalivyoonyesha.

Kufunga si sharti la kupata uamsho,kama wengine wanavyofikiri katika Agano Jipya hakuna mfano wa yeyote ambaye akifunga kwa sababu ya uamsho.

Badala yake tunawaona mitume wakimtii Yesu kwa kuhubiri injili. Kama mji haukupokea injili walikung'uta mavumbi miguuni pao na kusafiri hadi mji uliofuata (ona Luka 9:5 Matendo 13:49-51) hawakuketi mahali na kufunga wakisubiri uamsho.

Vilevile kufunga si njia ya kutiisha mwili maana shauku ya kula chakula ni kitu halali na si dhambi (ona Wagalatia 5:19-21) uone orodha ya tamaa za mwili ila kufunga ni zoezi la kujitawala -au kiasi- na hiyo ni sifa inayohiyajika ili kuenenda katika Roho,si katika mwili.

Kufunga kwa kusudi la kuboresha kiroho chako au kutangaza jinsi unavyompenda Mungu ni kupoteza wakati na ishara ya unafiki hiyo ndio sababu iliyowafanya mafarisayo kufunga na Yesu aliwasema kwa hili (ona Mathayo 6:16;23:5)

Watu wengine hufunga ili kumshinda shetani hilo nalo si maandiko. maandiko yanatuahidi kwamba tukimpinga shetani kwa imani katika neno la Mungu naye atatukimbia (ona Yakobo 4:7; 1Petro 5:8-9) hapo kufunga hakupo.

LAKINI NI YESU ALISEMA KWAMBA KUNA MAPEPO MENGINE YASIYOTOKA ISIPOKUWA KWA KUFUNGA NA KUOMBA.
 maneno haya yalisemwa kwa habari ya kumweka mtu huru kutokana na pepo lililokuwa limempagaa,si kwa habari ya mwamini anayehitaji kupata ushindi juu ya mashambulizi ya shetani kinyume chake.
 SWALI? 
Jee maneno ya Yesu hayaonyeshi kwamba tunaweza mamlaka makubwa zaidi juu ya mapepo kwa kufunga kumbuka kwamba baadhi ya wanafunzi wa Yesu walipomuuliza kwa nini wao walishindwa kumtoa pepo.

kwanza alijibu ni kwa sababu ya imani yao ndogo (ona Mathayo17:21), na pengine aliongeza. Namna hii haiwezekani isipokuwa kwa kufunga na kuomba.(Mathayo 17:21 

mimi bado naamini kwamba kufunga hakuwezi kuongeza wala kupunguza mamlaka ambayo Yesu aliwapa wanafunzi wake (ona Mathayo 10:1) 

kama Yesu alitupa mamlaka kufunga hakuwezi kuyaongeza ila kufunga kunatoa muda zaidi wa kuomba na kutafakari na kwa njia hiyo kunaongeza imani katika mamlaka tuliyopewa na Mungu.

            MKAZO KUPITA KIASI KUHUSU KUFUNGA.
Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya Wakristo wameunda dini kwa habari ya kufunga,na kufanya kuwa jambo la kawaida sana na hivyo kutotoa matunda yanayotakiwa.

kufunga kunatakiwa kufanyike katika kutafuta jawabu la jambo mahsusi sio kufunga tu bila mpango inakuwa ni sawa na kutumia nguvu kubwa bila sababu sawa na kuua mbu kwa nyundo.

namshukuru sana Mungu kwa uaminifu wake,mara nyingi amekuwa akinionyesha hatari ambazo ziko mbele yangu ama katika familia, kazini au kanisani na amekuwa akinielekeza namna ya kufunga. 

ninayo mifano mingi sana ambayo nafasi haitoshi kukuelezea lakini kila tatizo kabla halijatokea nilikuwa naambiwa funga ama siku moja, mbili au tatu na jambo linapotokea unakuta halina nguvu kabisa  
kuna wakati watu walinitegea mtego mbaya kazini ili wanifunge kwa rushwa Mungu alinielekeza kufunga siku moja tu na usiku ule nilimuona Mungu kama moto unaoteketeza kile chuo nikamuuliza Mungu kwa moto huu kuna mtu atabaki hapa akanijibu hatabaki mtu. 

huu ni ushuhuda wa ajabu sana na ni mrefu lakini kwa kifupi kile Chuo hakubaki mtu wote walisambaratika na wengine kushitakiwa. na hapo nilifunga siku moja tu lakini kwa maelekezo.

nasisitiza tena kwamba kufunga ni moja ya silaha kubwa ya kuongeza imani ambayo haipaswi kuitumia hovyohovyo.inapaswa kutumiwa kama silaha ya mwisho yenye nguvu ambayo inapaswa kutumiwa kwa uangalifu sana.

Tatizo lingine ninaloliona ni kwamba hakuna mafundisho yanayotolewa kwa waamini kuhusu jinsi ya kufunga,au watu wafunge vipi. kwa kweli ukiangalia katika Agano Jipya habari za kufunga hazijatatiliwa mkazo na inawezekana ndio sababu 

mafundisho ya kufunga ni machache na watu wanafanya kama jadi tu, tofauti na Agano la kale kufunga kulikuwa na sehemu kubwa zaidi mara nyingi kuhusisha na wakati wa maombolezo au wakati wa toba kwa taifa na wakati wa maombi ya dhati katika vipindi vya matatizo kitaifa au kibinafsi.

ukiangalia Isaya 58:1-12 na Zekaria 7:1-14).inaonyesha kwamba watu wa agano la kale walitia bidii zaidi katika kufunga na kupuuza amri zingine muhimu zaidi kama vile kuwajali maskini.
 Bwana Yesu ambaye alifanya huduma yake wakati wa agano jipya hatuwezi kusema kwamba alitilia mkazo sana kufunga alishtakiwa na mafarisayo kwa kutotilia mkazo wa kutosha kuhusu kufunga (ona Mathayo 9:14,15) na aliwasema wao kwa kutilia mkazo kupita kiasi kuhusu kufunga (Luka 18:9-12)
 lakini pia Yesu aliwafundisha wanafunzi katika mahubiri yake ya mlimani aliwaagiza wafunge kwa sababu maalum kama kielelezo kwamba sio kila nyakati tunafunga bali kwa wakati maalumu na jambo mahsusi.
na pia aliahidi kwamba Mungu angewapa thawabu kwa sababu ya kufunga kwao na yeye mwenyewe alifunga kwa kiasi fulani (ona Mathayo 17:21)

SOMO: KUUTAFUTA KWANZA UFALME WA MUNGU



MWL: Furaha Amon














Utangulizi;
Wakati nilipokuwa nikifiria kuandika hili somo, nilikuwa namkumbuka mchungaji wangu mmoja ambaye alikuwa ni mchungaji msaidizi katika kanisa nililokuwa mshirika. Huyu mchungaji ni kama alikuwa hana swali jingine, kila tukikutana ananisomea mstari huu wa Biblia
“Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa”. (Mathayo 6:33)
Halafu ananiuliza nijibu ufalme ni nini na haki yake ni nini? Kila jibu nililompa alikuwa haridhiki, halafu yeye mwenyewe hatoi jibu. Na kila jibu ninalompa analikataa, hatimaye nikaamua kuwa jeuri na mimi nikawa namjibu kwamba sijui nay eye mpaka wakati naandika somo hili hajawahi kunipa jibu na tumepoteana kwa karibu miaka saba sasa. Lakini hii haikunifanya niache kufikiria kutafuta jibu sahihi ya swali hili, kwa sababu natambua kwamba Biblia haijawahi kuweka maandiko hewa, kwa sababu kila andiko lenye pumzi ya Mungu liko hai. Kwa hiyo ni muhimu tukashirikiana pamoja katika kujifunza na kutafakari kwa mapana kuhusu ufalme wa Mungu na haki yake. Biblia inasema;-
Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa na kila mtu hujiingiza kwa nguvu. (Luka 16:16)
UFALME NI NINI?
Ufalme ni mamlaka, ni utawala wenye uwezo wa juu wa kufanya maamuzi katika maeneo yanayomilikiwa na ufalme huo. Tofauti na utawala mwingine wa kidemokrasia ambao unatafsiriwa kama utawala wa watu uliowekwa na watu kwa ajili ya kuwatala watu. Ambao ki- msingi hauna nguvu na unaweza kuondolewa tu maandamano ya watu waliokuweka, na kila uamuzi unaofanya unaweza kuhojiwa na taasisi mbalimbali zikiwemo za utawala bora na haki za binadamu. Ufalme ni tofauti kabisa na tawala za kidemokrasia, katika ufalme watu na vitu vyote ambavyo viko katika miliki ya mfalme ni mali yake. Na anaweza akaamua vyovyote anavyotaka bila kuhojiwa na mamlaka yeyote, kwa sababu vitu vyote ni mali yake, ikiwa ni pamoja na watu walioko katika himaya yake.
HAKI NI NINI?
Haki ni hukumu inayotolewa bila ya kuwa na chembe chembe za upendeleo wa aina yeyote kulingana na sheria zinazohusika kutoa haki katika utawala fulani ama wa nchi husika au katika miliki yeyote ambayo watu wanaishi kulingana na sheria zinazowaongoza kama ilivyo kwamba kuna utawala wa Mungu na pia kuna utawala wa shetani.
Mtu mmoja ambaye Biblia inasema ndio mtu mkuu zaidi kati ya watu waliozaliwa na mwanamke Yohana Mbatizaji wakati anawaandaa wayahudi kuhusu ujio wa Yesu,  alikuwa na kauli mbiu moja kubwa ambayo Yohana aliwaambia wayahudi.
“Tubuni; kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia. Mathayo : 3:2
Kwa maana hiyo Yesu alikuja duniani pamoja na kuleta wokovu kwa wanadamu lakini pia alikuja kuleta ufalme wake. Ufalme wa Mungu, ambao ni tofauti  na ufalme wa dunia hii au ufalme wa shetani.
Kwa kawaida kila utawala unakuwa na sheria zake ambazo zinaweza kuwa za kikatiba kwa maana ya kuandikwa, au kutokuandikwa yaani kwa kutumia amri, lakini Yesu alikuja kuleta ufalme na haki yake na ili uweze kuingia na kuishi katika ufalme huu unahitaji zaidi kujua maana ya haki yake. Tafsiri nyepesi ya ufalme ni kama udikteta sababu unalimbikiza nguvu na madaraka kwa mtu mmoja ambaye ndie mfalme.
Kwa hiyo ili uweze kuwa mfalme mzuri inatakiwa uwe mtu ambaye unazingatia haki katika kutoa maamuzi yako kwa sababu ya nguvu kubwa na mamlaka uliyonayo. Usipotenda haki ni hatari sana kwa watu na vitu unavyomiliki. Kwa maana hiyo Yesu alipokuja kuuleta ufalme wake ni muhimu kujua kwamba ili uishi katika ufalme huo ni muhimu kujua haki yake, kwa maana hiyo haki ndio sheria yenyewe itakayokuwezesha kuishi katika ufalme wa Mungu.
SIO LAZIMA HAKI NA SHERIA ZIFANANE KATIKA NCHI
Inawezekana sheria za nchi moja zikawa tofauti kabisa na sheria za nchi nyingine, kwa mfano hapa kwetu Tanzania kutumia mirungi ni kosa, sawa na kutumia madawa ya kulevya mengine kama bangi na heroin. Lakini kwa sheria ya nchi kama ya Kenya, kukutwa na Mirungi sio kosa, huko ni zao la biashara. Na inaruhusiwa kutumiwa na kuuzwa popote. Kwa hiyo raia wa Kenya akija Tanzania analazimika kuacha kutumia mirungi vinginevyo akikamatwa na mirungi akiwa katika ardhi ya Tanzania anakuwa na kosa, hata kama kwao anaruhusiwa, lakini sheria za ufalme wa Tanzania hiyo kitu ni marufuku, hapa lazima apate haki yake ambayo ni kifungo.
kama leo utaenda katika nchi zilizotawaliwa na mfaransa, mfano nchi jirani kama Rwanda na Burundi, wao sheria yao ya barabarani inaruhusu magari yanapotembea barabarani kutumia upande wa kulia wa barabara, kinyume na utawala wa nchi ambazo zimetawaliwa na Mwingereza kama nchi za Tanzania, Uganda na Kenya ambazo magari yanatumia upande wa kushoto wa barabara.
Sasa wewe unapoendesha gari kutoka kwenye utawala wa Tanzania ukaingia Rwanda ni lazima ubadilishe upande wa barabara na kama utaendelea kutumia sheria za barabara za Tanzania katika nchi ya Rwanda basi uwe na uhakika kwamba hutafika mbali kabla ya kugongwa au kukamatwa na watunza sheria wa nchi husika.
Sasa Bwana Yesu alikuja kuleta ufalme wake na haki yake,ufalme aliouleta Bwana Yesu una sheria zake za namna ya kuishi, kwa mfano wewe umetoka kuishi kwenye ufalme wa giza, utapata shida sana kuishi kwenye ufalme wa nuru. Kwa tafsiri nyingine ni kwamba, kinachokuwezesha kuishi katika ufalme wa Mungu ni kwa kufuata sheria ambazo ziko katika ufalme wa Mungu. Na moja kati ya kazi za mfalme ni kutoa hukumu au kufanya maamuzi ya haki, Biblia inasema;-
Tazama, Mfalme atamiliki kwa haki. Na wakuu watatawala kwa hukumu (Isaya 32:1)
Kwa maana hiyo Yesu anapoongelea haki kama kitu muhimu katika kuupata ufalme wake. Maana yake ni lazima wakati wote tusimame katika kweli na haki ndipo ambapo tutakuwa tunaishi katika ufalme wa Mungu. Na  hii inamhusu mtu binafsi jinsi anavyoyatawala mazingira yake, familia yake, jamii yake, mji na Taifa kwa ujumla. Kitu cha kwanza ambacho kinaashiria kwamba ufalme wa Mungu uko ndani yako, ni jinsi ambavyo wewe unaamua mambo mbalimbali katika familia yako, kwa ndugu, jamaa, marafiki na majirani zako, sehemu yako ya kazi, kwa watu walio juu yako na kwa watu walio chini yako.
Ni namna gani unavyoamua mambo yao. Je unaamua kwa haki au kwa woga na upendeleo? Je wewe mwenyewe unapokosea upo tayari kukiri kosa lako? Kama unaamua kwa haki, na unatimiza mambo yote, basi uko ndani ya ufalme wa Mungu na utakuwa na nguvu katika kutawala mahali popote utakapokuwa katika ulimwengu wa roho na mwili.
“Na alipouzwa na mafarisayo, ufalme wa Mungu utakuja lini? aliwajibu akawaambia ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza;. Wala hawatasema tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama ufalme wa Mungu umo ndani yenu” (Luka 17:20-21)
Ufalme wa Yesu hautaonekana kwa kila mtu. Yesu alikuja na kuleta ufalme wake na akasema ufalme wa Mungu upo hata sasa ila ni siri kuujua na ukiugundua utaishi maisha ya kifalme bila kujali mazingira utakayopitia.
Mambo yanayohusu ufalme wa Mungu ni mambo ya siri. Na ni muhimu kujifunza masomo kama haya ili uweze kupata ufunuo wa siri ambazo ziko kwenye maandiko. Ndio maana Yesu anawaambia wasifikiri ufalme wa Mungu utaonekana waziwazi au tutautazama toka mbali.
Wakati ninatafakari mambo haya nikaona nitafute mtu mmoja ambaye alipitia maisha magumu lakini bado alijitahidi kuhakikisha anaishi akiwa ndani ya ufalme wa Mungu.
Hebu tuangalie kidogo maisha ya Yusufu mtoto wa Yakobo. Huyu alipata bahati ya kupendwa na baba yake kama ambavyo Biblia inasema;-
“Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia wala hawakuweza kusema naye kwa amani”. (Mwanzo 37:3-4)
Ukifuatilia kwa makini kisa hiki cha kusisimua unaweza kujifunza mambo mengi sana aliyopitia Yusufu ambayo yanasikitisha na kuumiza sana nafsi hata ya msomaji, wengi tunajua kuwa kulikuwa kuna tabia ya upendeleo katika taifa na tunajua kwamba hata isaka alimpenda sana mwanae wa kwanza Esau na Rebeka akampenda zaidi Yakobo, inawezekana kwa sababu ya tabia zao, maana Esau alikuwa mwindaji aliyeleta nyama nyumbani na Yakobo yeye alikuwa kama mtoto wa mama akishinda nyumbani kumsaidia mama kazi. Tunajua uadui ambao ulitokea kwa Esau na Yakobo ambapo ilibidi Yakobo akimbie maana ndugu yake aliapa kumuua. Lakini cha kushangaza Yakobo naye anafanya kosa kama hilo la baba yake la kuonyesha kumpenda Yusufu kuliko watoto wake na hivyo kusababisha chuki kwa ndugu zake ambao yeye aliwapenda na kujisikia yupo salama akiwa karibu nao, lakini matokeo yake walitaka kumuua na hatimaye kuishia kumuuza kwa potifa akida wa jeshi la farao. Biblia inasema;-
“Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa Farao mkuu wa askari, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao waishmaeli waliomleta huko. Bwana akawa pamoja na Yusufu naye akasitawi naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, Yule Mmisri. Bwana wake akaona ya kwamba Bwana yu pamoja naye, na ya kuwa Bwana anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake. Na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo. Bwana akabariki nyumba ya Yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mikononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu chochote chake, ila hicho chakula alichokula tu.” (Mwanzo 39:1-6)
Katika maandiko haya tunaona kwamba pamoja na ugumu wa mazingira ya maisha ya Yusufu, kutoka kwa baba  yake mzazi aliyempenda na kumshonea kanzu ndefu na kuwa mtumwa wa mkuu wa majeshi katika nchi ya kigeni, hapo inahitaji uwe na moyo safi usio wa kawaida ili uweze kumuona Mungu na kuuvuta ufalme wake. Lakini tunaona Yusufu aliweza kutulia na kutawala katika nyumba hiyo ya potifa, alikabidhiwa kila kitu kasoro mke wa Potifa na chakula cha potifa, hapo kwenye chakula nafikiri ni kwa sababu ya usalama kwa sababu huyu Potifa ni mkuu wa majeshi na huyu kijana ni raia wa kigeni kwa hiyo kiusalama hawezi kumwandalia chakula. Lakini mambo mengine yote alikuwa anaamua yeye, akiamua kuchinja ng’ombe, kuku, bata n.k.
Lakini baadae linatokea tena balaa lingine mke wa bosi wake anaanza kumtamani azini naye, sharia hiyo ni kinyume na sharia za ufalme wa Mungu, huyu mama alikuwa anataka kuizima nuru ya ufalme wa Mungu na haki yake Yusufu akaona sio sawa akaamua kukimbia. Tunafundishwa katika hili kwamba dhambi ya zinaa inakimbiwa usijadiliane nayo. Baada ya kitendo hicho hatimaye Yusufu anajikuta yupo jela, mazingira yamebadilika tena kutoka mtumwa aliyekabidhiwa kila kitu na kuwa mfungwa jeuri asiye na adabu anashitakiwa kwa kosa la kutaka kumbaka mke wa bosi wake, Biblia inasema;-
“Ikawa baada ya mambo hayo mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu chochote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu? (Mwanzo 39: 7-9)
Kwa hiyo Yusufu akajikuta matatani tena lakini bado pamoja na kuwa jela akajikuta ameupeleka tena ufalme wa Mungu kiasi kwamba biblia inasema;-
“Lakini Bwana akawa pamoja na Yusufu akamhifadhi. Akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza. Mkuu wa gereza akawatia mikononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya. Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu kwa kuwa Bwana alikuwa pamoja naye. Bwana akayafanikisha yote aliyoyafanya”. (Mwanzo 39:21-23)
Hapa tunaona Yusufu anajikuta anaishi tena kama mfalme ndani ya gereza! watu wote wamewekwa chini yake, kwa hiyo na mipango yote ya kazi juu kazi gani zifanyike na nani azifanye alikuwa anapanga yeye. Mtu mwingine anaweza akafikiria kwamba ilikuwa kazi rahisi sana, lakini matukio yote mawili yaliyompata yalikuwa yanaiharibu kabisa nafsi yake, kumbuka waliotaka kumuua ni kaka zake ambao kwa kawaida walipaswa kuwa walinzi wake yaani kujihisi kuwa salama ukiwa nao, na hakuwa na kosa kwa sababu sio yeye aliyemwambia baba yake mzazi ampendelee, mbele za Mungu alikuwa na haki. Fikiria inavyouma kutenganishwa na baba yako ambaye unajua kwamba yeye ni kipenzi chako, wakati mwingine unaweza usijifikirie wewe zaidi bali ukafikiria ugumu wa zile taarifa atakazopatiwa kuhusu wewe na uchungu atakaokuwa nao akikaa huku anaamini kwamba umekufa. Biblia inatuambia mzee Yakobo aliomboleza kwa siku nyingi sana na akajiapiza kwamba mpaka siku anakufa atakuwa anahuzunika kwa ajili ya mtoto wake aliyempenda sana. Halafu anafika ugenini mambo yameanza kukaa sawa halafu linkuja balaa ambalo unazushiwa jambo na mtu ambaye ndio kama mama mlezi wake, harafu anakuwa huwezi kujitetea, kisha anatupwa kwenye gereza ambalo sio la kawaida tunaambiwa ni gereza wanalofungwa wafanyakazi wa mfalme na viongozi wengine wakuu, magereza ya namna hii ni magereza wanayofungwa wahaini. Maana kuwakosea viongozi ni sawa na kuasi, haya matukio mawili pekee yalitosha kabisa kumkatisha tamaa, na pengine ingemfanya atumie muda mrefu sana kutuliza maumivu na majeraha aliyoyapata kutokana na majanga aliyopata. Lakini yeye alikubaliana na mazingira yote aliyopitia na kuhakikisha anautafuta ufalme wa Mungu na haki yake. Ambayo hatimaye alijikuta Mungu amemuinua kutoka gerezani hadi kuwa waziri mkuu. Hii ni habari ya ajabu sana. Yusufu anakuja kuivusha dunia katika kipindi kigumu cha miaka saba ya njaa. Na tunaona jinsi anavyoungana na ndugu zake katika namna ambayo inasisimua sana. Kiasi ambacho unaona kabisa anavyowapenda kiasi cha kutoka machozi. Kuna wakati fulani Mungu anatulazmisha kukaa kimya hata tunapozuliwa mambo magumu sana. Shetani yuko kila mahali na kwa viwango tofauti. Shetani anayeishi kanisani anakiwango kikubwa kuliko shetani anayeishi vilabuni na kwenye madangulo. Wakati mwingine uongo unaotengenezwa ndani ya makanisa unakuwa ni mbaya zaidi kuliko unaotengenezwa vilabuni na kwenye madangulo. Mtumishi mmoja rafiki yangu alikuwa na neema kubwa sana kanisani kwake, kiasi kwamba washirika wengi walikuwa wanakwenda kwake kuombewa na kufanyiwa huduma zingine za kiroho, na wengine walimwalika maeneo mengine mbalimbali majumbani kwao, hali hii haikumfurahisha shetani na wajumbe wake wakasema yeye ni nani anataka kujifanya zaidi ya mchungaji, wakaamua kutengeneza fitina wakajipanga vizuri na kuweka ushahidi wa uongo kwamba huko anakokwenda kufanya huduma anazini na wakaweka watu kiasi cha kwamba neno hilo lilipofika kwa mchungaji mchungaji akaamua kuitisha kikao cha wazee na kusikiliza ushahidi ule wa kupangwa na wakaamua kufanya maamuzi ya kumfukuza Yule mtumishi kanisani kumtangaza katika makanisa yote katika jji lile ili asipokelewe na kumtumikia Mungu kwa namna Yeyote. Waswahili wanasema watu watakunyima chakula lakini hawakunyimi neno. Habari zikamfikia Yule mtumishi juu ya kila kilichoongelewa na uamuzi ambao umechukuliwa dhidi yake, alikasirika na kukata tamaa kabisa akapania kwamba wakimwita kwenye hicho kikao, ndio watajua kwamba kukaa kwake kimya sio kwamba hajui kusema. Kwa hiyo alipania kwenda kupambana nao kwa akili zake yaani kuwapa vidonge vyao. Siku iliyofuata wakati huo hakuna simu alitumwa mjumbe kuja kumwita aende kanisani kukutana na mchungaji, anasema wakati analetewa huo ujumbe alikuwa yupo kitandani lakini hana usingizi bali anapangilia maneno magumu atakayokwenda kuwapaka wabaya wake mbele ya wakuu wake wa dini. Kwa hiyo baada ya kupata huo ujumbe huku akiwa na hasira kiasi kwamba hata wakati anavaa nguo alikuwa anatetemeka kwa hasira. Wakati anatoka chumbani kwake kwenda sebuleni ilia toke kwenda nje ndipo akaona kitndo ambacho sio cha kawaida. Vile anafungua tu mlango anakutana na mtoto wake ambaye alikuwa ni mdogo sana hajui hata kuongea, anakaribia miaka mitatu hivi akasimama halafu akamwambia kwa sauti ya ukali, huku amemnyooshea kidole “wewe nakwambia usiende kuja juu kanisani, umesikia, nasema usiende kuja juu kanisani” huyu mtumishi akashituka inakuwaje mtoto ambaye hajui hata kusema aongee kwa ukali namna hii! Akamwita kwa jina lake akamuuliza kwa upole unasemaje mwanangu, akaona yuko kimya wala haelewi hata anachoulizwa. Ndipo akajua kuwa hiyo ni sauti ya Mungu na ikabidi kutii huku machozi yanamtoka.
Alipofika kwenye kikao alionekana mtulivu sana maana maneno yaliyokuwa akiambiwa alikuwa anayajibu kwa utlivu na hekima ya hali ya juu. Mwisho Askofu wake anamwambia kwa kweli tulikuwa tumepanga kukufukuza na kutwanya barua nchi nzima ili usipokelewe, lakini kwa jinsi ulivyoongea kwa ushirikiano hatuoni kosa lako, lakini pamoja na hayo mimi nakuruhusu uende kesho uniletee jina la kanisa lingine unalotaka kwenda, maana hapa umeshachafuka sana. Akwajibu basi sawa. Sasa kivumbi kikatokea wakati wanasema tuombe kwa ajili ya kufunga kikao, anasema ilishuka nguvu kubwa na kila mtu alianguka chini na kunena kwa lugha kama watu wanaoomboleza na hawakuacha mpaka mama mmoja alipopata ufunuo na kuwaambia jamani hili jambo liishe na huyu mtumishi asiondolewe hapa kanisani, ndio wakapata nguvu na kutawanyika. Na baada ya siku si nyingi wale watu waliopanga uovu huo wakaeleza ukweli kwamba walipanga maneno.
Mwisho napenda kukushauri ndugu yangu utafute kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote utazidishiwa.
MUNGU AKUBARIKI. Tunaweza kuwasiliana na mimi kwa namba ya simu 0677 609056