Jumatatu, 17 Juni 2013

WAPEWA KUONGOZA JAHAZI LA KUSIFU NA KUABUDU – TANGA


Viongozi wa timu ya kusifu na kuabudu kutoka kushoto Dan Manimba, Elizabeth Yohanna na Furaha Mwakasege

Baada ya kuwasimika waimbaji wa timu ya kusifu na kuabudu ya mkoa wa Tanga,jukumu la kuongoza timu hii wamekabidhiwa viongozi watatu ambao ni Ndugu Furaha Mwakasege yeye anakuwa ni mratibu mtendaji wa timu, Daniel Manimba yeye anakuwa msimamizi wa ufundi na jukwaa na Elizabeth Yohana yeye 
anakuwa  msimamizi wa waimbaji wa kike katika timu. Akiongea baada ya kuwekewa mikono katika nafasi hiyo Daniel Manimba amemuelezea blogger kwamba anajihisi amekabidhiwa dhamana kubwa na atahakikisha anaitumikia kwa akili na kwa nguvu zake zote. Akiongea baada ya kumalizika ibada hiyo Mratibu wa timu hii furaha Mwakasege alisema kwamba muundo wa katiba unahitaji timu hii kuwa na mwenyekiti,katibu na viongozi wengine ambaoa kwa sasa bado hawajachaguliwa ila viongozi waliopo sasa hivi ni wa muda na ikifika wakati wajumbe wenyewe ndio watakaochagua viongozi wao. Akiwaweka mikononi mwa Mungu Mchungaji Singano amewaeleza watu katika ibada hiyo kwamba kwa majukumu yake kama mchungaji ni vigumu sana kwake kusimamia kikamilifu timu hii,ndio maana anawaweka viongozi watakaomsaidia.

HOTUBA YA FURAHA MWAKASEGE


 SIKU YA KUSIMIKA TIMU YA KUSIFU NA KUABUDU YA JIJI LA TANGA
Leo ni siku ya historia kubwa sana katika jiji la Tanga kwa sababu yamezaliwa mawazo mapya ambayo hayajawahi kufanyika tangu injili ianze kuhubiriwa katika jiji hili na ninamshukuru Mungu kwamba wewe mchungaji Dominic Singano unakuwa ni sehemu ya historia hii. Watu wanaweza wasielewe sana ni nini kinafanyika na kina umuhimu gani katika familia ya waimbaji wa nyimbo za injili katika jiji la Tanga,lakini Bwana leo anafanya jambo jipya kama ambavyo waimbaji wameimba katika wimbo wao. Ambalo linakwenda kuleta mabadiliko makubwa na mapinduzi kwa waimbaji wote wa nyimbo za injili wa jiji la Tanga ambao kwa muda mrefu uimbaji wao umekuwa wa kiwango cha kanisani kwao tu. Lakini sasa jambo hili litakwenda kubadilisha mawazo yao na kuwafanya wajiandae kufanya huduma hii kwa lengo la kimataifa zaidi. Ni kweli kwamba tumechelewa sana kuwa na timu kama hii kulinganisha na mikoa 
mingine iliyo juu kwa waimbaji wa nyimbo za injili Tanzania,lakini pia ni lazima tukubali kwamba sasa ni wakati wa Mungu kwa sababu pia timu hii isingeweza kuanza bila kuwepo watu walioandaliwa na Mungu kuisimamia Timu hii na sisi tunaamini kwamba wewe Mchungaji Singano Mungu amekupa jukumu hili akijua kwamba unaweza kuwalea vijana japo wanatoka katika katika makanisa mbalimbali na sisi tunakuahidi kukupa ushirikiano,utii na nidhamu ya hali ya juu katika kufanikisha maono ambayo Mungu ameyaweka ndani yako.

Tunaposema chombo hiki kitakuwa ni ukombozi kwa waimbaji wa nyimbo za injili Tanga, tuna maana ya kwamba kitashughulika zaidi na huduma hii ya kusifu na kuabudu,kwa maana hiyo tutahakikisha zana zote zinazotakiwa kutumika katika huduma hii ya kusifu na kuabudu tunakuwa nazo na tunazimiliki wenyewe na tukizimiliki sisi ina maana waimbaji wote waliopo katika jiji hili la Tanga watanufaika nazo kwa maana ya kwamba watakuwa na uhuru wa kuvitumia kwa utaratibu ambao tutakuwa tumeweka ambao utakuwa nafuu zaidi tofauti na sasa ambapo vyombo vingi vinamilikiwa na makanisa na utaratibu wa kuvitumia kwa makanisa mengi ni mgumu sana, na hasa ukizingatia kwamba makanisa mengi vyombo vyao havijakamilika na kama ukitaka kupata seti iliyokamilika inabidi kuunganisha vyombo vya makanisa zaidi ya moja sasa hapo si kazi ndogo.

Lakini pamoja na changamoto hizo tunapenda kuwashukuru watu wote ambao wanatupenda na kutuelewa nini tunachotaka kufanya na kwa namna ya pekee kabisa niwashukuru viongozi na washirika wa kanisa lako kwa upendo wanaotuonyesha na kuhakikisha wanatusaidia kila tunapokwama hata kama wewe haupo.
Tunashukuru kituo cha malezi ya vijana Novelty pamoja na kanisa la FPTC ambao tumekuwa tukitumia kanisa lao pamoja na vyombo katika matayalisho yetu.
Tunamshukuru Rev Steven Bombo wa kanisa la Elim Elim Pentekoste kwa kutupa nafasi ya kutumia vyombo pamoja na kanisa lake kwa mazoezi.
Tunamshukuru Rev na mama James GH Lee ambao wamekuwa karibu na sisi kutusaidia kila tunapokwama.
Tunamshukuru Mchungaji Bright Mashauri ambaye hata kwa sasa hivi mnamuona anaendelea kuchukua picha za kumbukumbu za tukio hili. Kwa ujumla watu wengi wameonyesha kutuunga mkono baada ya kujua nini tunachokifanya.

Kuhusu vijana ambao utawasimika leo ili waanze kufanya kazi katika timu hii ni vijana ambao tumekuwa nao na tumewapima katika kipindi hiki kigumu ambacho ni kama tupo kwenye giza,lakini tunawaonyesha vijana kwamba wasihofu kuna nuru kubwa sana mbele,tunawapenda wanatupenda,wanatutia moyo wakati mwingine tunakata tama kama mipango yetu haijakaa sawa lakini wao wanatutia moyo kwamba tunapoona mambo magumu hapo ndio tujue kwamba kuna Mungu. Kwa kweli sisi tumefurahi sana kuanza na vijana hawa wakati huu ambao tupo kwenye giza, kwa sababu kuna wengine wanakuja wanachungulia wakiona giza hawarudi tena, na sisi tunawasubiri wakija kwenye nuru tutawakataa. Hawa vijana wamekuwa wakija kwenye mazoezi kwa kujitegemea na karibu wote ni wanakwaya na wanategemewa katika makanisa yao,hivyo ni lazima wamalize kwanza huduma walizonazo katika makanisa yao ndipo wautumie muda wa ziada kuja kwetu bure. Na wengine wanalipwa na makanisa yao kwa huduma hii ya kusifu na kuabudu,lakini wameona ni bora tukae gizani pamoja ili nuru itukute kwa pamoja,napenda kukuhakikishia kwamba thamani ya vijana hawa kwetu itakuwa kubwa kuliko hao ambao watakuja wakati timu imeanza kuwa na jina.
Kulingana na maagizo uliyotupa kwamba unataka timu hii isiwe ya kufanya matamasha ya burudani bali iwe timu ya huduma,imebidi hata kazi ya kuwachagua vijana hawa ifanyike kwa umakini wa hali ya juu kwa sababu tunategemea timu hii ihudumu katika viwango vya kimataifa ndani na nje ya nchi yetu kwa hiyo tunahitaji wawakilishi waliochaguliwa vizuri watakaoleta sifa kwa waimbaji wa jiji la Tanga,nchi yetu na kwa Kristo,tunahitaji kuwa na vijana wasiopungua 16 hivi lakini leo utawawekea mikono vijana tisa tu, ambao tayari tumeshawapima kwamba tunaweza kuhudumu pamoja nao. Tumeandaa nyimbo kama ishirini hivi lakini lakini leo tutaonyesha nyimbo chache ili na wenzetu wapate nafasi, na baada ya ibada hii jukumu litakalofuata ni kujitambulisha sehemu mbalimbali lakini pia na kuzitambulisha kazi zetu. Tunapenda ikiwezekana  tungo zetu ndizo zitumike na watu wengi katika sifa na kuabudu. Tunaomba ndugu zetu waimbaji ambao mko hapa tufahamu kwamba tunahitajiana sana  kwa sababu sisi ni kama madereva wa kampuni moja ya Yesu,mwenzako akikwama njiani msaidie au ukimkuta njiani amesimama unamuuliza tatizo ni nini kama spea msaidie atakurudishia mbele hii ni kazi ya Mungu. Mwisho napenda kukuhakikishia kwamba kazi hii itasimama kwa sababu si ya kwetu ni ya Yesu Kristo hata kama sisi au wewe ukihama Tanga utaendelea kuwa mlezi wa timu hii.