Jumamosi, 22 Aprili 2017

MAISHA BAADA YA KUBATIZWA NA ROHO MTAKATIFU.


Mtu anapozaliwa mara ya pili kwa kumkaribisha Bwana Yesu ndani ya maisha yake, huingia katika maisha mapya na kutembea katika uongozi wa Mungu aliye hai. Mtu huyu aliyezaliwa mara ya pili anapofikia mahali pa kukutana na Nafsi ya tatu ya Mungu (Roho Mtakatifu) ana kwa ana katika kipimo cha kufurika (tele), huingia katika ufunuo mpya na maisha mapya ya kushuhudia uthihirisho wa nguvu za Mungu katika maisha yake. Katika maisha haya ya kutembea na Roho Mtakatifu, ni vema kila mwamini apate mafundisho yaliyo sahihi jinsi ya kutembea na Roho Mtakatifu huyu wa Mungu ili kwa kufanya hivi “moto uendelee kuwaka ndani yake daima pasipo kuzimika”(Law 6:12) hebu sasa tuendelee kuwa katika Roho ili tujifunze yale yatupasayo kufanya baada ya kupokea ubatizo huu wa Roho Mtakatifu udhihirishwao na ishara ya lugha mpya.
JENGA TABIA YA KUMWOMBA MUNGU.
Akawaambia mfano ya kwamba imepasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa (Luka 18:1). Ni vyema ufahamu kuwa maombi ni mkono uwezao kuyaleta mapenzi ya Mungu duniani, na kila adumuye katika kuomba hudumu katika ushirika (Fellowship) na Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Katika maombi tunavuta hazina ya Mungu iliyofichika kutoka katika ulimwengu wa Kiroho kuja katika ulimwengu unaoonekana. Maombi n kusema na Mungu Baba kama vile baba wa dunia anavyoweza kusema na watoto wake awapendao. Sehemu nyingine Yesu alipokuwa anaongea na wanafunzi wake aliwakazania kuwa inawapasa kuomba ili wasije kuingia majaribuni. Maombi yanamfanya mtu ayaone majaribu hata kabla hayajatokea, badala ya kushitukizwa na majaribu hayo. Yesu alipokuwa anasema ombeni ili msije mkaingia majaribuni, hakuwa na maana iliyo nyepesi bali alikuwa anawatahadhalisha kuwa waangalie wasije wakaingia majaribuni na kushindwa. Nasema hivi kwani kuingia majaribuni  hilo si jambo lililo geni katika kanisa na hata tunasoma kuwa; “Ni Furaha tupu mtu anapoangukia katika majaribu mbalimbali” (Yak 1:2) kwa hiyo maombi ni silaha zinazomwezesha mwamini kutoka akiwa mshindi, baada ya kuingia au kuangukia katika majaribu. Mtu anapoingia majaribuni na akishindwa kuendelea na hali ya kiroho aliyokuwa nayo, basi husababisha ubaridi mkubwa ndani ya roho ya mtu, na kwa ubaridi huo Roho yule aliyempokea huzimika ndani yake. Roho anapozimika ndani si rahisi tena kulisikia bubujiko la uzima ndani ya mtu na hapo huyapoteza maisha ya ushindi yaletwayo na Roho Mtakatifu. Kwa maneno haya nataka kusema kuwa mara tu baada ya kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu anza kujenga tabia ya kuomba. Hii ni hatua muhimu sana katika maisha haya mapya ya kutembea na Roho wa Mungu. Maombi hayatakiwi kuwa mzigo, yaani kitu cha kujilazimisha badala yake lazima iwe tabia ya mwanafunzi. Ninaposema tabia ninapenda kuyafananisha na kuvuta hewa ya oxygen. Mtu havuti hewa kwa kujilazimisha bali hufanya hivyo kwa sababu ni raha tena ni afya tunapofanya hivyo. Tunapojenga tabia hii ya kuomba ni lazima tuombe kwa ufahamu pia tuombe kwa kunena kwa lugha mpya. Maana tukinena kwa lugha tunakuwa tunajijenga kama tulivyotangulia kusema katika sura zilizopita. Kumbuka kuwa hujapokea Roho Mtakatifu ili tu unene kwa lugha, bali umepokea Roho Mtakatifu ili uwe na manufaa katika kuujenga ufalme wa Mungu.
DAMU KATIKA USHIRIKA WA ROHO NA WATU WA MUNGU.
“Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na Roho mmoja na wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu chochote alichonacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika” (Matendo 4:32)
Katika maisha haya mapya uliyonayo, unahitajika kujengwa na kujifunza zaidi mafundisho haya na kuimarika, vitu hivi vinaweza kupatikana  pale watu wa Mungu wanamtafuta Mungu katika Roho na kweli, maana ndivyo yesu alivyomwambia yule mama Msamaria. Alimwambia wakati unakuja ambao wamwabuduo Mungu halisi watamwabudu Baba katika Roho na kweli (Yohana 4:23). Wewe sasa ni kondoo mchanga mwenye moto wa kuijua kweli ya Mungu, basi tafuta malisho (chakula cha kiroho) toka kwa mchungaji wa kweli, maana huyo ana uchungu na maisha yako ya kiroho. Nasema hivyo kwani ni vema ujitambue kuwa u msafiri wa kwenda mbinguni na kwa sababu hiyo lazima utafute gari litakalokupeleka mbinguni. Mchungaji ni sawa na gari la kuwapeleka watu mbinguni, tatizo linalotokea ni kuwa yako magari (wachungaji) ambayo yameegeshwa mahali na hayatembei, ni jambo la kuchekesha kuwaona wakristo wengine wakiingia mle ndani na huku wanategemea kusafiri! Kama kweli u msafiri wa mbinguni tafuta gari (mchungaji) linalotembea.
Kwa maneno haya nataka kukutafutia malisho zaidi au mahali utakaponeemeka kiroho na mafundisho yaliyo hai. Katika ushirika huu, ni vema usifungwe na madhehebu, bali uwe tayari kukumbatiana na mwamini yeyote wa dhehebu lolote, maana hao ndio ndugu zako wa kweli. Pia ukumbuke kupima yale uliyoyasikia kama yanaendana na neno la Mungu, ni vema uwe karibu na yule aliyekabidhiwa kwako kama baba yako wa kiroho.
VIPINGE NA KUVISHINDA VIKWAZO VYOTE ATAKAVYOKULETEA SHETANI.
“Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yeyote kwa jina hili, wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. Petro na Yohana wakawajibu wakamwambia, kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe. Maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia” Matendo 4:17-20
Mtu anapompokea YESU kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake, husababisha chuki na hasira kubwa kutoka kwa shetani dhidi yake. Tendo la mtu kuamua kutoka kwenye ufalme wa giza na kuingia kwenye UFALME WA MUNGU, humsisimua shetani mnoo hata kumfanya aende vitani dhidi ya mwamini huyu mpya. Ili katika vita hiyo aweze kumrejesha tena mikononi mwake.
Katika vita hii ya shetani dhidi ya mwamini, ibilisi hutuma mishale ya kila namna ili kumwangusha mtu, na hachoki katika mapambano hayo, ila siku kwa siku huzidisha makali ya mapigo yake kwa mwamini. Kwa kusema hivi nina maana kuwa kila mwamini anapopiga hatua moja mbele kiroho, shetani naye huongeza mapigo yake ili ikibidi kumteketeza mtu wa Mungu. Mwamini anapobatizwa kwa Roho Mtakatifu huwa amepiga hatua kubwa mno kiroho, hatua ambayo huutetemesha sana ufalme na mamlaka ya shetani.
Kwa sababu hii, mtu anapojazwa Roho Mtakatifu kwa kipimo cha tele, atakumbana na matatizo ambayo hayakuwepo kabla ya kuingia katika hatua ya kuzaliwa upya. Majaribu yatakuwa yamezidishwa ukali wake kama alivyofanya mfalme Nebukadneza kwa kina Shadraka , Meshaki na Abednego. Biblia inatuambia kwamba Nebkadneza alizidisha moto wa tanuru mara saba kuliko ulivyokuwa kawaida yake, ili uwateketeze watu wa Mungu (Danieli 3:19) kwa vijana hawa watatu wa kiebrania, shetani aliwatumia watu mbalimbali hata wafalme ili kushusha imani yao. Hata kwako wewe pia anaweza kutumia vitu kama hivyo, au ndugu zako, marafiki na hata viongozi wa dhehebu lako ili kumpinga Roho Mtakatifu uliyempokea, basi kwa vyovyote vile itakavyokuwa lazima uyashinde majaribu na vishawishi vyote vile vya yule mwovu. Kumbuka kuwa hata mitume walipita katika majaribu makali mno mara tu baada ya kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, wengine walipigwa kwa mawe, au kukatwa shingo kwa msumeno, au kuwekwa ndani ya mafuta yaliyochemka hadi kufa. Ni jambo la Baraka na la kutia moyo kuona kuwa katika mambo yote hayo waliyofanyiwa na shetani, wao walikaza uso wao kama gumegume na kuchagua hata kufa kwa ajili ya imani waliyopokea, kuliko kuishi wakiwa wameasi imani waliyopokea kwa njia ya mauti ya mwana pekee wa Mungu pale msalabani.
Niseme tena kuwa sasa kwa kuwa umejazwa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya, endelea kuvipiga vita vile vyema vya imani maana katika kila gumu litakalokupata, hutakuwa peke yako; bali yule aliyeanza kazi njema ndani yako ndiye atakayekushindia. Kumbuka kuwa kila utakapompinga shetani atakimbia, na kwa kufanya hivyo utaendelea kumpendeza Mungu aliyekununua.
ILI UIMARIKE ANZA KUTOA USHUHUDA WA KUFUFUKA KWA BWANA YESU.
Dunia leo ina watu zaidi ya bilioni moja wanaojiita wafuasi wa Kristo. Watu hawa wanadai kuwa ni mashahidi wa Bwana wetu Yesu Kristo na ya kwamba wanao ushuhuda wa Yesu kwa dunia nzima. Ukichukua maana halisi ya ushahidi kwa kuzingatia lugha kongwe kwa mfano kiyunani, utaona kuwa watu hawa si mashahidi.
Katika kiyunani neno shahidi linaitwa Martyria yaani kufa au kuuawa kwa ajili ya kitu fulani kwa hiyo shahidi wa Yesu ni yule anayeusimamia ushuhuda wake pasipo kuyumbishwa hata kama ikibidi auawe kwa sababu ya ushuhuda huo. Shahidi na yule anayesimamiwa kwa ushahidi huo ni kitu kimoja, hawatenganishwi kwa namna iwayo yeyote ile. Kwa kuwa wakristo wanatakiwa kuwa mashahidi wa Yesu, ni lazima watene na kuishi kama Yesu anavyotaka na kuyashikilia maungamo yao hata mauti.
Tunapowaangalia wakristo wa leo, utaona kuwa hawafai kuitwa mashahidi, maana yale Kristo anayoyakataa ndiyo wanayoyafanya. Dhambi imeharibu ushahidi wao kwa ukweli huu, unaweza kuona kuwa wakristo hawa hawatoi ushuhuda wa kufufuka kwa Yesu, bali hutoa ushuhuda wa kufa kwa Yes utu. Na mtu anayetoa ushuhuda wa Yesu na kuishia hapohapo tu asiendelee mbele, huyo ni shahidi wa uongo. Kwa maneno haya tunaweza kusema kuwa kuna mashahidi wa uongo wa Yesu zaidi ya bilioni moja duniani, ukiwaondoa wale wanaomwabudu Yesu Kristo kwa roho na kweli.
Mtu anaposhuhudia juu ya mauti ya Bwana pamoja na kufufuka kwake, huyo anaudhihirishia ulimwengu kuwa yeye anamwabudu yesu aliye hai anaweza kufanya mambo yafuatayo;-
-         Yesu aliye hai analeta ondoleo la dhambi. Tayari nimekwambia kuwa kuna zaidi ya wakristo wa uongo 1,000,000,000 duniani. Watu hawa humwabudu Yesu aliyekufa, maana ni yesu aliyekufa tu ndiye anayeweza kuabudiwa na majambazi, waasherati, wazinzi, walevi, waongo,wavutaji wa unga, wezi na watu watendao mambo ya jinsi hiyo. Hata hivyo katika dunia hii, wapo wanao mwabudu Yesu kwa roho na kweli, watu hawa hawakwenda na Yesu hadi kaburini tu, bali walifufuka pamoja naye! Kufa na kufufuka pamoja na Bwana ni kupokea ondoleo la dhambi na kuzaliwa mara ya pili kwa kupokea asili mpya kutoka kwa Mungu aliye hai. Yeye alipokea ondoleo la dhambi hawi tena mtumwa wa mwili na tamaa za kidunia, bali hupokea asili mpya ya kiMungu na kwa msaada wa Roho wa Mungu huishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi.
-         Yesu aliye hai hutenda miujiza, ishara na maajabu “Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo” (Marko 16:20) ni vema tufahamu kwamba kuna imani na dini nyingi mno duniani, katika imani au dini hizo zimesimamia kati ya imani hizo ni hii ya ukristo, chini ya kinara au nguzo yake iitwayo YESU KRISTO. Imani hii imekuwa ya pekee mno ukilinganisha na zile zingine zilizopo, naweza kusema kuwa ni imani iliyo hai. Maana kila inapokigusa kitu kilichokuwa katika hali ya kufa kiroho au kimwili, uhai mpya uliweza kuonekana ndani ya kitu kile. Mtu aliyepoteza uhai wake kiroho na kupotea katika dhambi, anapoamini na kujiunga na imani hii; roho yake hufufuliwa na kuwa hai tena, na kwa mgonjwa aliyekata tamaa ya kuishi hurejeshewa afya yake kwa kumwamini Yesu huyu aliye hai. Miujiza na ishara zinazotokea katika imani hii ya ukristo na maajabu mengine mengi huifanya imani hii ya ukristo kuwa ya pekee kuliko imani nyingine zote duniani. Mhubiri mmoja alisema kuwa ukristo pasipo miujiza ni sawa na imani nyingine zilizokufa na hii ni kweli kabisa. Na hapa uelewe kuwa miujiza tunayoizungumzia ni pamoja na ule wa mtu kuzaliwa mara ya pili na kuachana na dhambi. Kwa kumalizia hebu tuseme kuwa ni vema uanze sasa kutoa ushuhuda kwa watu wengine, ukiwaeleza kule Yesu alikokutoa , na pale alipokuweka sasa, pale atakapokuweka baada ya maisha haya na jinsi anavyokupa ushindi siku hadi siku
-         Toa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana “Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao” (Matendo 4:32) baada ya kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, ile chemchem inayojaa hata kufurika, hatua au jambo jingine hutokea kutoka katika chemchem hiyo. Kwa maneno mengine ni kuwa ndani yako sasa kuna mito ya Roho Mtakatifu iliyojaa uzima kwa ukweli huu ni lazima ufahamu kuwa mito sio kwa ajili ya mtu mmoja peke yake, bali mito ni lazima ilete maendeleo na mabadiliko kwa wale wote watakaofikiwa na mto huo. Mtu anapoamua kufunga chanzo au pale mto unapoanzia, huyo ni muuaji; maana atasababisha hasara kubwa ikiwa ni pamoja na mauti kwa wote waliokuwa wakiutegemea mto huo. Mto ni lazima uachwe utiririke wakati wote pasipo kufungwa.
-         Kutoa ushuhuda ni sawa na kuuacha mto ububujike daima neno hili kushuhudia linatokana na neno ushuhuda, shuhuda na shahidi ni maneno ambayo unapoyachambua hatima yake unapata kitenzi hiki, kushuhudia , shahidi ni mtu aliyekuwepo jambo lilipokuwa linatokea, ni mtu anayelifahamu jambo kwa usahihi na kwa mapana marefu yake. Kwa hiyo yale shahidi atakayo yasema kuhusiana na jambo fulani alilolishuhudia, ndiyo tunayaita ushuhuda, yaani maelezo yaliyo sahihi na hai yaliyotolewa na yule aliyekuwapo wakati wa kutukia jambo hilo. Ninaposema maelezo yaliyo hai, hapa nina maana kuwa ushuhuda kamwe si hadithi za uongo, au habari za kutungwa, bali ni maelezo ya kweli yanayothibitishwa na nafsi ya mtu, roho yake na mwili wake pia.
-         Tumia mamlaka uliyonayo kwa jina la Yesu. “Lakini Petro akasema, mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilichonacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende” (Matendo 3:6) kwa miaka mitatu, wanafunzi wa Yesu walikuwa wameshuhudia matendo makuu ya Mungu yaliyotendwa kwa mkono wa Bwana wao na mwokozi wa ulimwengu Yesu Kristo. Biblia inatuambia kuwa, kwa mamlaka Yesu aliamuru pepo wabaya nao wakamtii, vilema, viziwi, bubu, na wenye maradhi mengi waliponywa pale Yesu alipoamuru ifanyike hivyo kwa mamlaka aliyokuwa nayo. Kwa mamlaka aliweza hata kuamuru upepo na dhoruba vitulie navyo vikatulia. Wanafunzi walipoona haya yakitendeka walishangaa mno, huku wakitamani mamlaka ile iliyotenda kazi ndani ya Bwana wao hata wakafikia hatua ya kumwambia Yesu kuwa awaongezee imani! Yesu alipopaa aliwaacha wanafunzi wake katika huzuni nzito huku wakiwa wamevunjika moyo, haya yalitokea kwani waliamini kuwa kwa kuondoka kwa Bwana wao basi na ile mamlaka nayo inmeondoka pamoja naye. Kujihisi kupungukiwa huku kuliendelea sana hadi pale hadi pale walipobatizwa Roho Mtakatifu mara tu baada ya kumpokea Roho Mtakatifu kwa kipimo cha tele. Moto ulilipuka tena ndani yao na wakapata ufunuo mpya wa kuitumia mamlaka iliyokuwa ndani yao, angalia hapa; KWA MUDA MREFU Petro na Yohana walikuwa wanampita huyu kiwete akiwa katika mlango wa hekalu pasipo kumsaidia. Lakini baada ya ubatizo wa Roho Mtakatifu uliotokea katika sura ya pili ya kitabu cha matendo ya mitume, sasa Petro anajitambua kuwa yeye ni nani katika mitume, tena anatambua kuwa mamlaka ileile iliyotenda kazi ndani ya Yesu ipo ndani yao. Nasema hivyo kwani Yesu aliwaambia katika Luka 10:19 kuwa “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka, nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru “Kwa ufunuo huo mpya Petro aliweza kumwendea yule kiwete na kumwamuru atembee katika jina la YESU na ikatendeka hivyo. Ni vema ufahamu kuwa sasa umefanya safari ya kuendea mti wa uzima na ile mana iliyofichwa, katika safari hii mambo hayatakwenda kama unavyotaka, bali daima shetani atataka mambo yaendekama atakavyo yeye, basi kama utakunja mikono na kujihisi mnyonge na duni, utashindwa kuishi maisha ya ushindi, kumbuka kuwa yeye ashindaye ndiye atakayepewa kula matunda ya mti wa uzima ulio katika bustani ya Mungu (Ufunuo 2:7b). ili upate ushindi ni lazima ujifahamu kuwa wewe ni mtoto wa Mungu na mrithi pamoja na Yesu Kristo nay a kuwa una haki ya kisheria ya kutumia mamlaka iliyo katika jina la Yesu Kristo. Kwa hiyo unapoona hali isiyobariki inajitokeza katika safari yako, iamuru kuwa ihame katika jina la Yesu na kwa kutumia jina hilo, fungulia ile hali unayotaka iwepo. Kwa maneno haya napenda ufahamu kuwa mambo hayatakuwa marahisi kila wakati maishani mwako; hivyo pale yanapokwenda visivyo, tumia mamlaka kukemea na kuharibu kila kilicho kiovu, na itatendeka kama ulivyoamuru. Wakati wa kufanya hayo usijisikie upweke na duni, ujue kuwa uko pamoja na Yesu na kwa jina lake kila goti litapigwa na kila ulimi utakiri kuwa YESU NI BWANA. Baada ya kubatizwa na Roho Mtakatifu ishi maisha matakatifu. “hata masaa matatu baadae mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea, Petro akamjibu, niambie mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema ndiyo, kwa thamani hiyo, Petro akamwambia, imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Anagalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. Mara akaanguka miguuni pake akafa” (Matendo 5: 7-10) tunasoma kuwa Mungu hapo zamani katika Agano la kale aliishi katika hema la ushuhuda au katika hekalu. Katika Agano jipya, Mungu anaendelea kuishi katika hema au katika hekalu, ila safari hii si katika hema iliyojengwa kwa mikono ya wanadamu, bali hema lile alilolijenga yeye mwenyewe yaani mwili wa Kristo. Na Yesu alipopaa mbinguni alimwomba Mungu baba ili Roho Mtakatifu aje duniani na kuchukua nafasi aliyoiacha, naye akashuka siku ya hamsini baada ya kufufuka kwake. Katika sura katika sura ya mwanzo ya kitabu hiki tumejifunza juu ya kusudi la kuja kwake, basi alikuja ili kuyakamilisha makusudi haya, na alifanya au anafanya hivyo pale anapopata maskani hiyo si kwenye majumba yam awe  na mbao bali ni kanisa lake, yaani wale waliozaliwa mara ya pili kwa kutakaswa kwa damu ya thamani ya mwana pekee wa Mungu YESU KRISTO.

-         Kwa kuwa wewe mwenyewe umeshuhudia  kuja kwake Mungu Roho Mtakatifu na kufanya makao ndani yako; ni vema ufahamu kuwa Roho Mtakatifu ni mtakatifu kweli. Yeye huichukia sana dhambi ikiwa katika umbo lolote lile, nan i rahisi kumkasirisha na kumhuzunisha pale utakaporuhusu dhambi maishani mwako. Katika maandiko yaliyotangulia tunawaona watu hawa waliokuwa wamezaliwa mara ya pili na kupokea uwezo wa Roho Mtakatifu lakini wakashindwa kuishi maisha ya utakatifu. Kwa maisha yao ya dhambi waliweza kupokea tunda la mauti, sawasawa na maandiko yasemavyo kuwa mshahara wa dhambi ni mauti. Kwa hiyo pale unaposhindwa kuishi maisha ya utakatifu baada ya kumpokea Roho huyu wa BWANA. Matokeo yake ni kumzimisha Roho Mtakatifu uliyempokea awe msaidizi wako katika mambo ya kiroho. Roho akishazimika na ule moto wa wokovu nao huzimika, hatimaye mtu hupatwa na mauti ya kiroho. Basi muda wako uliobakia sasa ishi kwa kumpendeza Mungu. Daima msalaba ukiwa mbele na dunia nyuma; kwa kufanya hivi utazaa matunda mema na watu watakuja kutoka kila kona kuonja matunda hayo. Na ufahamu kuwa kila atakayeonja matunda yatokanayo na maisha yako ya ujazo katika Roho Mtakatifu, atafanyika sadaka katika ufalme wa Mungu, na kama yanenavyo maandiko pale roho yako ilipo ndipo na sadaka yako itakapokuwepo.

JINSI YA KUPOKEA UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU



Tayari tumeshajifunza mambo mengi yamhusuyo Roho Mtakatifu, asili yake, huduma yake katika kanisa na faida ya kunena kwa lugha mpya inayoambatana na ubatizo huu wa Roho Mtakatifu.
Katika kulielezea hili, napenda kusema kuwa hakuna utaratibu maalumu uliowekwa katika Biblia kama kanuni ya kufuatwa katika kupokea ubatizo huu. Kwa sababu hiyo, hapa nitatoa mwongozo uwezao kusaidia kupokea na nitaongea kama vile neno la Bwana linavyosema.
KUSUDI LA KUTANGAZA UBATIZO LIWE LA KIBIBLIA.
“lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu. Nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu na katika uyahudi wote na Samaria, na hata mwisho wa nchi” Matendo ya mitume 1:8
Ahadi ya Roho Mtakatifu ni kwa wote, ila wengi wameshindwa kupokea kwa kule kukusudia isivyopaswa juu ya kuhitaji kwao ubatizo huu.
Wengi wanamwomba Mungu kipawa hiki kwa kusudi la kusema kwa lugha tu, ili wafanane na watu wengine wanaonena kwa lugha.
Lugha mpya ni kitu muhimu mno kwa wanafunzi wa Yesu, lakini kusudi la ubatizo wa Roho Mtakatifu sio ili watu wanene kwa lugha mpya tu, ni zaidi ya hapo.
Mistari iliyotangulia hapo juu, inatuonyesha kusudi la kutaka kumpokea Roho Mtakatifu na utendaji wa nguvu zake. Ni lazima kila anayehitaji ubatizo huu, auhitaji tu ili awe shahidi mwaminifu wa Mungu. Na kwa sababu kuna nguvu inayojizalisha ndani ya Roho Mtakatifu lazima liwe lile la kumzalia Mungu matunda. Kupokea ubatizo huu na hatimaye kuendelea kukaa bila kufanya chochote kwa ajili ya kuong, yaani kuwafanya eza kuujenga ufalme wa Mungu huko ni kumzimisha na kumhuzunisha Roho wa Mungu. Kusudi kuu la kupata ubatizo huu ni kuwa shahidi mwaminifu wa kufa na kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kufanya kile alichoagiza kabla ya kupaa kwake, yaani kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi na kuwafundisha kuyashika yote
LAZIMA UJUE KUWA NI HAKI YAKO KUPOKEA ROHO MTAKATIFU.
Biblia ni kitabu kilichojaa ahadi za Mungu kwa watu wake, kwa ujumla kuna ahadi zaidi ya elfu thelathini kutoka katika kitabu chwa mwanzo hadi kile cha Ufunuo. Kati ya ahadi hizo ni ile ahadi inayomhusu Roho Mtakatifu, iliyotolewa na Mungu kupitia kwa nabii Yoeli 2:28 “Hata itakuwa baada ya hayo, ya kwamba nitamimina  Roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume  kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono”.
hii ni ahadi kutoka kwa Mungu, kwenda kwa watu wake wa siku za mwisho, katika hili sote tunafahamu kuwa sisi ni watu wa siku za mwisho, kwani ahadi hii ilitimia duniani siku kumi tu baada ya Yesu kupaa. Katika matendo ya mitume tunasoma hotuba ya mtume Petro siku ya pentekoste, kati ya mambo aliyoyasema ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, kuwa itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Basi kwa kuwa wewe na mimi tu waumini wa Mungu wa siku za mwisho, ni vema tuelewe kuwa ahadi hii ya kumpokea Roho Mtakatifu na nguvu zake inatuhusu, ni ahadi yetu. Waumini wengi wameshindwa kupokea ahadi hii, pale walipoisukumia ahadi hii mbali kwa watu wengine, nakutia moyo wewe na yeyote aliye mwanafunzi wa Yesu, kuomba kutimia kwa ahadi hii ndani yako kwa maana Roho Mtakatifu amekuja kwa ajili ya kila aaminiye.
LAZIMA KUWA NA KIU YA KUPOKEA ROHO MTAKATIFU
“Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, mtu akiona KIU na aje kwangu anywe” Yohana 7:37
Watu wengi wamekosa kupokea ahadi hii kwa kule kutojenga kiu ndani yao na kuhitaji kipawa hiki. Mtu yeyote anayehitaji kitu kutoka kwa Mungu ni lazima awe na kiu ya kupokea kile kitu kutoka kwa Mungu.
LAZIMA KUWA NA IMANI YA KUPOKEA.
Imani ni pale mtu anapokuwa na uhakika juu ya yale yatarajiwayo, ni kuwa na uhakika kuwa Mungu ana uwezo wa kufanya yale aliyoahidi.
Kwa imani tunasema kuwa tumepokea, tunayo na pasipo imani haiwezekani kabisa kumpendeza Mungu. Hatuwezi kupokea lolote kutoka kwake. Wasiwasi na mashaka ni adui mkubwa mno wa kupokea miujiza kutoka kwa Mungu. Kwa maana kila amwendeae Mungu akihitaji kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, ni lazima awe na imani ya kupokea yaani kuwa na uhakika kuwa Mungu aliye hai ana uwezo wa kufanya yale aliyoahidi.
ONDOA HOFU JUU YA KUPOKEA AHADI HII
Roho Mtakatifu amesemwa vibaya mno na watu wengi hasa pale ishara ya kunena kwa lugha inapojidhihirisha. Mara nyingine wenye hekima wa dunia hii, hudiriki kusema kuwa kunena kwa lugha ni mapepo! Kwa jinsi hii watu wengi, wameweza kuogopa hasa wanapoyasikia haya yakisemwa na viongozi wa madhehebu yao au vikundi vyao vya faragha. Kwa hofu hii, wengi hukubali kuhudumiwa ili wapokee ahadi hii ya Roho Mtakatifu huku wakiwa na hofu ya aina fulani hasa juu ya kunena kwa lugha mpya. Tukumbuke kuwa lile tuombalo kwa Mungu, ndilo tunalopokea, hivyo hakuna sababu ya kuwa na hofu wakati wa kupokea ubatizo huu.
Roho Mtakatifu ni nafsi hai ya Mungu nan i Mungu, hivyo anapoingia ndani huwa Baraka, hivyo badala ya watu kuwa na hofu ni vema watu kuchangamka na kuifungua mioyo yao ili kupokea kipawa hiki.
NI LAZIMA KUKIRUHUSU KINYWA CHAKO KINENE
“Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka” matendo 2:4
Hiki ni kipengele muhimu sana katika somo hili, wengi kwa kutokuelewa kile ninachoenda kikeleza sasa wameshindwa kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu pamoja na ishara ya lugha mpya. Waumini wengi wanaposikia juu ya lugha mpya wanafikiri kuwa ni lugha inayotamkwa na nguvu fulani ndani ya mtu. Kwa kufikiria hivi, hufikiri nguvu hiyo ndani ya mtu inaweza kumlazimisha kufunguka kwa kinywa cha mtu, na maneno yakaanza kutoka kama bubujiko la maji mwambani. Kwa fikira hizi potofu, wengi wametamani kupokea wasiweze kupokea. Mistali tuliyosoma inatuonyesha yale yaliyotokea wakati mitume wa Bwana, walipojazwa Roho Mtakatifu, walianza kusema kwa lugha mpya. Kwa maneno haya, tunaona kuwa mitume walifunua vinywa vyao na kuanza kusema na walipofanya hivyo, Roho Mtakatifu akawajalia maneno ya kusema. Maneno yanatoka kwa Roho Mtakatifu na kazi ya kuyasema ni ya mwanafunzi wa Yesu.
USIRUHUSU AIBU IKUTAWALE
Mambo mengi ya Mungu yanaenda kwa imani, na mambo ya imani ni upumbavu mbele za dunia. Ndio maana wapumbavu wa dunia hii hawaishi kusema kuwa hakuna Mungu. Tunapoongea juu ya ubatizo wa Roho Mtakatifu unaoambatana na kunena kwa lugha mpya. Dunia inatushangaa na kutucheka sana, mara nyingi mawazo ya dunia huingia ndani ya Kanisa la Mungu na kuwafanya waamini wengi kuanza kuyatazama mambo ya kiroho kama vile dunia inavyoyatazama, matokeo yake ni kanisa kupooza kwa kumzimisha Roho Mtakatifu.
Kwa kuwa lugha mpya ni moja ya mambo yasiyoeleweka katika dunia, basi watu wengi wanaona aibu kusema kwa lugha hiyo. Hivyo wanapojazwa Roho Mtakatifu na kuanza kunena kwa lugha mpya, huanza kuipeleka lugha hiyo katika akili zao na hapo kuiona lugha hiyo ni jambo lisilokubalika katika ustaarabu wao, na kuona kama kichekesho. Akili zao zinaposhindwa kukubaliana na hali hiyo, hujiona kuwa wanafanya jambo la kitoto, hivyo huamua haraka sana kunyamaza kimya. Hii ni kwa sababu ya kuona aibu. Jambo hili linapotokea huharibu tendo zima takatifu la kunena kwa lugha mpya. Maandiko yanasema kuwa atakayemwonea Yesu aibu, nay eye ataonewa aibu mbele ya Mungu na malaika zake.

Wengine wanashindwa kupokea kwa kule kusita kwao wakati wa mwanzo wa huduma hii. Hili hutokea mara tu mtu anapoanza kunena kwa lugha kwa mara ya kwanza. Wengi wanapousikia ule mtiririko wa ile lugha, hudhani kuwa wanaongea lugha yenye makosa, kwa hisia hii huruhusu ukavu ndani ya mioyo yao, na kushindwa kupokea. Ni vema unapoomba kitu kwa Mungu, inatakiwa kuwa kama mtoto mdogo na kumruhusu Mungu akufanyie kama anavyotaka.

ISHARA ZA LUGHA NA FAIDA ZAKE.


Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni muujiza wa ajabu mno unapotokea kwa mtu. Muhusika huelewa fika kuwa amepokea kitu ambacho sio cha kawaida. Wengi wanaodai kupokea  ubatizo wa Roho Mtakatifu wakati bado hujipoteza kwa hiari yao wenyewe, na kama yanenavyo maandiko kwamba huangamizwa kwa kukosa maarifa. Ninasema hivi kwa sababu Mungu ametoa ishara za wazi mno hata kwa wale walio nje kuthibitisha kuwa mtu huyu amepokea ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Kwa ujumla ziko ishara nyingi zinazothibitisha tendo hili, ishara nyingi zinatokea ndani ya mtu mwenyewe, lakini zipo zingine zinazotokea nje ya mtu na kuwa ushuhuda hata kwa watu wengine. Tunapoziangalia zile zitokeazo nje tunaweza kuona kuwa iko ishara moja inayotokea mar azote kwa kila mwamini anayepokea ubatizo huu; ishara hii ni ile ya mwamini kunena kwa lugha nyngine kama vile Roho anavyomjalia kutamka.
Katika hili, mtu yoyote asije akadanganywa na shetani kwamba mtu anaweza kubatizwa kwa Roho Mtakatifu bila ishara hii kutimia au kuonekana kwa kulielewa jambo hili vizuri zaidi hebu tuangalie jinsi wale waliotutangulia walivyopokea ahadi hii.
WALE 120 WAKIWEMO MITUME WALINENA KWA LUGHA MPYA
“Hata ilipotimia siku ya pentekoste walikuwa wote mahali pamoja, kukaja ghafla toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukatokea ndimi zilizogawanyika kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka” (Matendo 2:1-4)
Biblia inasema wazi kuwa kanisa limejengwa katika msingi wa Mitume na manabii, Yesu mwenyewe akiwa jiwe kuu la pembeni, kwa usemi huu ni vema kuangalia jinsi mitume walivyopokea Nafsi hii ya Mungu. Nasema hivi kwani mitume ndio wa kwanza katika Agano la kale na jipya kumpokea Roho Mtakatifu ikiambatana na ishara ya kusema kwa lugha nyingine na wale waliowazunguka walishuhudia tendo hilo, hata wakadhihaki wakisema kuwa wamelewa kwa mvinyo mpya.
MTUME PAULO ALISEMA KWA LUGHA NYINGINE.
“Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote” 1Wakorinto 14:18
Paulo alipookoka, Mungu alimtumia Anania ili amwekee mikono Paulo apate kuona tena kiroho na kimwili. Biblia inasema kuwa Anania alifanya hivyo pale Dameski Paulo alijazwa Roho Mtakatifu maana ndilo lilikuwa kusudi la kutumwa kwake.
Tunaposoma ushuhuda wa Paulo katika mistari iliyotangulia, Paulo anatuambia kuwa yeye ananena kwa lugha; kwa hiyo ni wazi kuwa siku ile alipoombewa na Anania alipokea Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya.
KORNELIO NA WALIOKUWA PAMOJA NAYE WALINENA KWA LUGHA NYINGINE.
Kornelio alikuwa mtu aliyekuwa na kiu ya kuurithi uzima wa milele, hata hivyo kiu yake haikumzalia matunda aliyoyatazamia kwa kutoielewa njia ya wokovu kwa usahihi. Mungu alipoiona kiu na njaa yake hii ya muda mrefu, alimtuma mtume Petro ilia pate kumwelezea njia ya Bwana kwa usahihi.
Katika mji huu wa Kaisaria Mtume Petro alipata nafasi ya kuongea mambo mengi yahusuyo usahihi wa njia ya Bwana na wale walioyasikia waliyaamini kuwa ni maneno yatokayo kwa Mungu aliye hai. Kwa kule kuamini kwao, maandiko yanasema kuwa;-
“Roho Mtakatifu akawashukia wote waliosikia lile neno, na wasiotahiriwa walioamini wakashangaa watu wote waliokuja na Petro, kwa sababu mataifa mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha na kumwadhimisha Mungu” Matendo 10: 44-46
Maandiko haya yanatuthibitishia kuwa kanisa la Kaisaria lilipokea ubatizo wa Roho Mtakatifu, kila mmojawapo alinena kwa lugha mpya; nasema hivi kwani maandiko yanasema kuwa wale waliokuja na Petro walishangaa? Kwa sababu mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha na kumwadhimisha Mungu.
WANAFUNZI KULE EFESO WALISEMA KWA LUGHA
“Basi, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha yote niliyowaamuru ninyi, na tazama mimi nipo pamoja nanyi hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28: 19-20)
Maandiko haya yanaonyesha kazi kubwa iliyoachwa mabegani mwa mitume na kanisa kwa ujumla, wakati Yesu alipokuwa tayari kupaa kuelekea mbinguni wengi walioachiwa huduma hii hapo mwanzo ukiondoa mitume, hawakuwa na ufahamu mkubwa jinsi wawezavyo kuifanya huduma hii kubwa, hawakuwa pia na zana za kazi kama hizi tulizonazo sasa, pamoja na upungufu huu, walikuwa waaminifu kukifanyia kazi kile kidogo walichonacho ili kuonyesha utii wao mbele za Mungu kwa ufahamu huu mdogo huduma nyingi ziliweza kufanywa nusunusu bila ya kukamilika.
Katika mji wa Efeso mtume Paulo alikutana na waamini ambao licha ya kuokoka bado walibakiza mambo fulani fulani waliyotakiwa kufundishwa. Maandiko yanasema kuwa
“Ikawa Apolo alipokuwa Korinto, na wanafunzi kadhaa wa kadhaa huko; akawauliza, je mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, la hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia (Matendo 19:1-2)
Paulo alihojiana na wanafunzi hawa aligundua kuwa walihitaji kuelezwa na kufundishwa mambo fulani fulani waliyopungukiwa ndani yao, likiwemo hili la ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Baada ya kuwafundisha maandiko yanasema kuwa;- 
“Paulo akaweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha na kutabiri”(Matendo 19:6)
Wanafunzi hawa hawakuwa wachache, neno linasema walikuwa kumi na wawili, wanaume tu, bila kutaja wanawake, na hawa wote walijazwa Roho Mtakatifu na kusema kwa lugha nyingine.
WAAMINI WA SAMARIA WALISEMA KWA LUGHA.
Wakati wa mateso ya mwanzo kwa kanisa, wandugu walitawanyika huko na huko wakihubiri neno. Mtu mmoja aliyeitwa Filipo alipata nafasi ya kuhubiri katika Samaria, lakini kwa sababu ambazo hazikutajwa; mtumishi huyo hakuwafanyia huduma ya ubatizo wa Roho Mtakatifu. Maandiko yananena kuwa, mitume waliposikia wakamwendea na kuwaombea ili wapokee ahadi hii. Kwa kweli hatuoni mahali palipotamkwa wazi kuwa walinena kwa lugha nyingine, ila hapa kuna maneno yanayonifanya namini kuwa ishara hii ilitokea.
Biblia inatuambia;-
“Hata Simoni alipoona ya kuwa wanapokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mkono ya Mitume, akataka kuwapa fedha akisema nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemuwekea mikono yangu apokee Roho Mtakatifu. (Matendo 8:18-19)

Hapa kuna swali la kujiuliza, Je! Simoni alijuaje kuwa watu wale wamepokea Roho Mtakatifu? Ni dhahiri kuwa hawakuwa kimya; asingelielewa kuwa wamepokea Roho Mtakatifu. Ni lazima kuwa kuna ishara ya wazi iliwatokea watu wale na kwa Simoni mwenyewe. Ninaamini kuwa hata hawa walinena kwa lugha nyingine kama ilivyokuwa kwa wengine.

ROHO MTAKATIFU NI KAMA ALIVYOKUWA ELIAZARI KWA REBEKA.


Katika kitabu cha mwanzo sura ya 24, tunasoma juu ya watu wane maarufu katika neno la Mungu. Hapa tunasoma habari ya mzee Ibrahim akimpatia huduma mtumishi wake ajulikanae kwa jina la Eliazari kwenda nchi ya mbali kumtafutia mwanae isaka mwanamke atakayeishi nae. Biblia inatuambia kuwa huyo mtumishi wa Ibrahimu hakuwa mtumishi wa kawaida bali alikuwa ni mzee wa nyumba yake aliyetawala vitu vyake vyote. Mtumishi alifanya kama alivyoelekezwa, akaenda nchi ya mbali na Mungu akamtangulia hata akampata Rebeka awe mke wa Isaka mtoto pekee wa Ibrahimu. Tunaweza kusema kuwa Ibrahimu ni mfano wa Mungu Baba, Eliazeri naye ni mfano wa Roho Mtakatifu na Rebeka ni mfano wa kanisa na Isaka ni mfano wa Yesu Kristo Mwana pekee wa Mungu Baba. Ni jambo linalojulikana wazi kuwa Mungu alimtuma Roho Mtakatifu duniani ili amtayarishie Mwana bibi harusi aliye mkamilifu. Tunapoangalia huduma na wajibu wa Eliazari kabla na baada ya kumpata Rebeka, tunaiona picha halisi ya huduma ya Roho Mtakatifu katika kanisa la Mungu. Baada ya Eliazari kumpata Rebeka iliwalazimu kuanza safari ndefu jangwani kuyaendea makao ya Isaka. Katika jangwa lile Rebeka hakupungukiwa na kitu maana Eliazari alifanya yafuatayo kwa ajili yake;-
ALIMUELEZA YOTE YANAYOMUHUSU ISAKA
Rebeka hakuwa amewahi kumwona Isaka mume wake lakini Eliazari alimweleza Rebeka vile ambavyo Isaka anafanana. Alimweleza yale anayoyapenda na yale asiyoyapenda au ambayo yako kinyume naye. Kwa ujumla alimweleza tabia yote ya Isaka.
Hivyo japokuwa walikuwa hawajaonana, lakini Rebeka tayari alishafahamu yote yamhusuyo bwana wake. Hivi ndivyo ilivyo kwa kanisa, kanisa linaitwa bibi harusi wa Mwana pekee wa Mungu Yesu Kristo. Kanisa halijawahi kuonana na Bwana wake uso kwa uso, hata hivyo linamfahamu mno, maana kama Eliazari alivyomweleza Rebeka yote yamhusuyo Isaka, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu wa Mungu ana huduma ya kulielezea kanisa mambo yote yamhusuyo Mwanakondoo Yesu Kristo.
ELIAZARI ALIMPATIA REBEKA MAHITAJI YOTE NJIANI
Safari ya kupitia jangwani ina mahitaji mengi sana, kwa wingi wa mahitaji wengi huanza safari wasiweze kuimaliza. Katika jangwa Rebeka angeona kiu na njaa au pengine angeliona shida fulani, haya yote yalipotokea Eliazari alimpa kila alichohitaji. Roho Mtakatifu naye hulipa kanisa yale yote linalohitaji ili kulipatia kanisa au Bibi harusi wa Mwanakondoo furaha idumuyo.
ELIAZARI ALIMPATIA REBEKA ULINZI.
Katika jangwa kuna hatari nyingi mno, zikiwemo hatari za wanyama wakali. Hatari za majambazi na hatari za magonjwa. Kwa hatari hizi haingekuwa rahisi kwa mwanamke kusafiri peke yake katika jangwa. Hatari hizi hazikumletea Rebeka hofu yoyote ile kwani alikuwa mikononi mwa Eliazari aliyempatia uponyaji na ulinzi aliouhitaji. Kanisa nalo linapita katika magumu mengi katika safari ya kwenda mbinguni, katika mazito haya, Roho Mtakatifu ndiye anayelilinda na kulipigania kanisa katika mambo yote.
ELIAZARI ALIMWONYESHA REBEKA NJIA
Kwa ujumla safari ndani ya jangwa inahitaji uangalifu wa hali ya juu mno. Nasema hivi kwani sehemu nyingi za jangwa zimefanana hivyo ni rahisi sana mtu kupotea katika jangwa, Eliazari aliifahamu mno njia itakayowafikisha kwa Isaka hivyo alimuongoza Rebeka jangwani hadi pale walipokutana na Isaka. Kanisa nalo haliijui njia ya kuwafikisha kwa Mungu, linahitaji kushikwa mkono na kuongozwa.

Roho Mtakatifu ndiye aliye na wajibu huu mkubwa wa kuliongoza kanisa hadi pale litakapokuwa limekutana na Bwana wake Yesu Kristo. Kwa ujumla Eliazari alifanya mambo mengi mno kwa ajili ya Rebeka, tunaweza hata kukesha kuchambua na kuelezea yale yaliyotendwa na Eliazari kwa Rebeka. Tuseme tu kuwa mtumishi huyu alikuwa ni yote kwa Rebeka kazi ya Roho Mtakatifu kwa kanisa nazo ni nyingi mno. Yeye ni Mungu, hivyo tunaweza kumaliza kalamu zote duniani na kalatasi zote bila kumaliza masimulizi ya kazi zake hizo tulizozitaja katika sura hii ni msingi tu wa kazi zake na matendo yake makuu na nimeziandika ili ujue kuwa Roho Mtakatifu ni Nafsi hai nan i Mungu kweli.

ROHO MTAKATIFU HUTUTIA KATIKA KWELI YOTE



“Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote….”Yohana 16:13
Biblia inasema mwanadamu anatakiwa kuwa mtakatifu kama vile Mungu alivyo mtakatifu. Utakatifu ni maisha yasiyowezekana kwa nguvu za kibinadamu, bali ni kwa msaada wa Mungu. Na ninaposema maisha ya utakatifu, ninamaanisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia na kuishi kwa kiasi, haki na utawa katika ulimwengu wa sasa. Tunaposoma kwenye neno la Mungu tunaonyeshwa yale yasiyo mema kwa mtakatifu kuyafanya japo tena si maovu yote yaliyoandikwa kwenye Biblia. Katika hili wengi wamefanya maovu wakidai kuwa hayajakatazwa kwenye neno la Mungu.
Pamoja na udhuru huu wa kibinadamu, hakuna mwanafunzi wa Yesu atakayepona, kwani Mungu alimtoa Roho Mtakatifu akae ndani ya kanisa ili kuufunua ukweli wote wa Mungu katika dunia kama tunavyosoma kwenye maandiko yaliyotangulia kwa hiyo Roho Mtakatifu hulisaidia kanisa kuelewa zaidi mwili wa Kristo na jinsi ya kuutunza mwili wake hasa tukifahamu kuwa Yesu Kristo ndiye kweli.
ROHO MTAKATIFU HULIPA KANISA UJASIRI.
Hofu ni adui mkubwa mno wa imani katika Bwana, hata Biblia inazungumzia kuwa pasipo imani haiwezekani kabisa kumpendeza Mungu. Mwamini au kanisa linapotawaliwa na hofu haliwezi kuishi kwa imani, hivyo basi halitampendeza Mungu daima.
Adui huyu wa imani humsonga mno mtu kabla ya kubatizwa na Roho Mtakatifu na lazima msaada toka mbinguni uingie ndani ya mtu na kuiondoa hofu hiyo. Tunapoyaangalia maisha ya mtume Petro, tunaona kuwa yametawaliwa na hofu hata wakati fulani alikaribia kuzama baharini kwa sababu ya hofu.
Hofu ya mauti ilimfanya Petro pia amkane Bwana na mwalimu wake Yesu Kristo mara tatu, alimpenda Yesu lakini hofu ilimsukuma kumkana Bwana Yesu. Hofu hii ilimpata kwa sababu ya kitu fulani kilichopungua ndani yake. Lakini tunapoyaangalia maisha yake ya baada ya kumpokea Roho Mtakatifu tunayaona kuwa yalikuwa ya tofati kabisa. Mtume Petro hakuogopa tena kumshuhudia Yesu mbele za watu, aliweza kuutangaza umasihi na ufufuko wake, pamoja na kupaa kwake kwa ujasiri alioupata alikuwa hata radhi kufa kwa ajili ya injili na ndivyo livyotokea. Kuhusu ujasiri tunaoupata baada ya kubatizwa kwa Roho Mtakatifu sio jambo la kuzusha, bali Yesu mwenyewe alitamka hivyo kwa wale mia na ishirini wakiwemo wale thenashara katika kitabu cha Matendo ya mitume Yesu alisema;
“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilieni juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika uyahudi wote na hata nje ya nchi” Matendo ya mitume 1:8
Hapa neno shahidi lina maana kuwa jasiri hata hatua ya mauti, haya yanawezekana tu kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
ROHO MTAKATIFU HUFANYA KAZI KAMA NJIWA (HUA)
“Nuhu akangoja siku saba tena, kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, njiwa akamjia jioni, na tazama alikuwa na jani bichi la mzeituni kinwani mwake ambalo amelitunda, basi nuhu akajua ya kwamba maji yamepungua juu ya nchi” (Mwanzo 8:10-11)
Tunapoangalia ndege huyu, tunaweza kuona kuwa ni ndege anayepatikana katika jamii zote za watu wa ulimwengu tulionao. Katika Agano la kale ndege huyu alikuwa ni sehemu ya sadaka iliyoweza kutolewa kwa Bwana; hata Mariamu na Yusufu waliweza kutoa njiwa wawili kama sadaka mbele za Mungu (Luka 2:24) ni jambo la kushangaza kuona kuwa kama vile hua (njiwa) wanavyoweza kupatikana kwa jamii zote tajiri na masikini, vivyo hivyo Roho Mtakatifu naye anaweza kuingia mahali popote ili mradi tu awe amefunguliwa mlango.

Njiwa (hua) ana tabia ya upole kila wakati, tena ni ndege aliye mtulivu mnoo. Roho Mtakatifu anapoingia ndani ya mtu humfanya mtu huyo kuwa na maisha ya utulivu na upole. Mtu aliye mkali kwa kila hali, anapopokea zawadi hii, hali yake hubadilishwa kabisa. Badala ya mbegu ya ukali na hasira hupandwa mbegu ya upole katika BWANA. Jambo lingine tunapomwangalia ndege huyu, tunaona kuwa tangu zamani alitumwa kama mjumbe au msaidizi. Nuhu alimtuma njiwa akayakague maji juu ya uso wa Nchi na kupitia kwa njiwa, Nuhu aliweza kutambua majira ambapo maji yalipungua usoni mwa nchi. Nuhu hakuweza kuifanya huduma hii, bali njiwa aliweza kumsaidia. Kwa hili tunaiona kazi za Roho Mtakatifu iliyowazi, yeye ni msaidizi wa kanisa. Mwanadamu peke yake hawezi kushinda na kumpendeza Mungu, haya huwezekana tu pale mtu anapobatizwa kwa Roho Mtakatifu. Yeye ni msaidizi wa mambo yetu yote yaliyo ya rohoni nay ale ya mwilini, hata Yesu mwenyewe alimwita msaidizi.