Jumamosi, 22 Aprili 2017

ROHO MTAKATIFU NI KAMA ALIVYOKUWA ELIAZARI KWA REBEKA.


Katika kitabu cha mwanzo sura ya 24, tunasoma juu ya watu wane maarufu katika neno la Mungu. Hapa tunasoma habari ya mzee Ibrahim akimpatia huduma mtumishi wake ajulikanae kwa jina la Eliazari kwenda nchi ya mbali kumtafutia mwanae isaka mwanamke atakayeishi nae. Biblia inatuambia kuwa huyo mtumishi wa Ibrahimu hakuwa mtumishi wa kawaida bali alikuwa ni mzee wa nyumba yake aliyetawala vitu vyake vyote. Mtumishi alifanya kama alivyoelekezwa, akaenda nchi ya mbali na Mungu akamtangulia hata akampata Rebeka awe mke wa Isaka mtoto pekee wa Ibrahimu. Tunaweza kusema kuwa Ibrahimu ni mfano wa Mungu Baba, Eliazeri naye ni mfano wa Roho Mtakatifu na Rebeka ni mfano wa kanisa na Isaka ni mfano wa Yesu Kristo Mwana pekee wa Mungu Baba. Ni jambo linalojulikana wazi kuwa Mungu alimtuma Roho Mtakatifu duniani ili amtayarishie Mwana bibi harusi aliye mkamilifu. Tunapoangalia huduma na wajibu wa Eliazari kabla na baada ya kumpata Rebeka, tunaiona picha halisi ya huduma ya Roho Mtakatifu katika kanisa la Mungu. Baada ya Eliazari kumpata Rebeka iliwalazimu kuanza safari ndefu jangwani kuyaendea makao ya Isaka. Katika jangwa lile Rebeka hakupungukiwa na kitu maana Eliazari alifanya yafuatayo kwa ajili yake;-
ALIMUELEZA YOTE YANAYOMUHUSU ISAKA
Rebeka hakuwa amewahi kumwona Isaka mume wake lakini Eliazari alimweleza Rebeka vile ambavyo Isaka anafanana. Alimweleza yale anayoyapenda na yale asiyoyapenda au ambayo yako kinyume naye. Kwa ujumla alimweleza tabia yote ya Isaka.
Hivyo japokuwa walikuwa hawajaonana, lakini Rebeka tayari alishafahamu yote yamhusuyo bwana wake. Hivi ndivyo ilivyo kwa kanisa, kanisa linaitwa bibi harusi wa Mwana pekee wa Mungu Yesu Kristo. Kanisa halijawahi kuonana na Bwana wake uso kwa uso, hata hivyo linamfahamu mno, maana kama Eliazari alivyomweleza Rebeka yote yamhusuyo Isaka, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu wa Mungu ana huduma ya kulielezea kanisa mambo yote yamhusuyo Mwanakondoo Yesu Kristo.
ELIAZARI ALIMPATIA REBEKA MAHITAJI YOTE NJIANI
Safari ya kupitia jangwani ina mahitaji mengi sana, kwa wingi wa mahitaji wengi huanza safari wasiweze kuimaliza. Katika jangwa Rebeka angeona kiu na njaa au pengine angeliona shida fulani, haya yote yalipotokea Eliazari alimpa kila alichohitaji. Roho Mtakatifu naye hulipa kanisa yale yote linalohitaji ili kulipatia kanisa au Bibi harusi wa Mwanakondoo furaha idumuyo.
ELIAZARI ALIMPATIA REBEKA ULINZI.
Katika jangwa kuna hatari nyingi mno, zikiwemo hatari za wanyama wakali. Hatari za majambazi na hatari za magonjwa. Kwa hatari hizi haingekuwa rahisi kwa mwanamke kusafiri peke yake katika jangwa. Hatari hizi hazikumletea Rebeka hofu yoyote ile kwani alikuwa mikononi mwa Eliazari aliyempatia uponyaji na ulinzi aliouhitaji. Kanisa nalo linapita katika magumu mengi katika safari ya kwenda mbinguni, katika mazito haya, Roho Mtakatifu ndiye anayelilinda na kulipigania kanisa katika mambo yote.
ELIAZARI ALIMWONYESHA REBEKA NJIA
Kwa ujumla safari ndani ya jangwa inahitaji uangalifu wa hali ya juu mno. Nasema hivi kwani sehemu nyingi za jangwa zimefanana hivyo ni rahisi sana mtu kupotea katika jangwa, Eliazari aliifahamu mno njia itakayowafikisha kwa Isaka hivyo alimuongoza Rebeka jangwani hadi pale walipokutana na Isaka. Kanisa nalo haliijui njia ya kuwafikisha kwa Mungu, linahitaji kushikwa mkono na kuongozwa.

Roho Mtakatifu ndiye aliye na wajibu huu mkubwa wa kuliongoza kanisa hadi pale litakapokuwa limekutana na Bwana wake Yesu Kristo. Kwa ujumla Eliazari alifanya mambo mengi mno kwa ajili ya Rebeka, tunaweza hata kukesha kuchambua na kuelezea yale yaliyotendwa na Eliazari kwa Rebeka. Tuseme tu kuwa mtumishi huyu alikuwa ni yote kwa Rebeka kazi ya Roho Mtakatifu kwa kanisa nazo ni nyingi mno. Yeye ni Mungu, hivyo tunaweza kumaliza kalamu zote duniani na kalatasi zote bila kumaliza masimulizi ya kazi zake hizo tulizozitaja katika sura hii ni msingi tu wa kazi zake na matendo yake makuu na nimeziandika ili ujue kuwa Roho Mtakatifu ni Nafsi hai nan i Mungu kweli.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni