Jumamosi, 22 Aprili 2017

ROHO MTAKATIFU HUTUTIA KATIKA KWELI YOTE



“Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote….”Yohana 16:13
Biblia inasema mwanadamu anatakiwa kuwa mtakatifu kama vile Mungu alivyo mtakatifu. Utakatifu ni maisha yasiyowezekana kwa nguvu za kibinadamu, bali ni kwa msaada wa Mungu. Na ninaposema maisha ya utakatifu, ninamaanisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia na kuishi kwa kiasi, haki na utawa katika ulimwengu wa sasa. Tunaposoma kwenye neno la Mungu tunaonyeshwa yale yasiyo mema kwa mtakatifu kuyafanya japo tena si maovu yote yaliyoandikwa kwenye Biblia. Katika hili wengi wamefanya maovu wakidai kuwa hayajakatazwa kwenye neno la Mungu.
Pamoja na udhuru huu wa kibinadamu, hakuna mwanafunzi wa Yesu atakayepona, kwani Mungu alimtoa Roho Mtakatifu akae ndani ya kanisa ili kuufunua ukweli wote wa Mungu katika dunia kama tunavyosoma kwenye maandiko yaliyotangulia kwa hiyo Roho Mtakatifu hulisaidia kanisa kuelewa zaidi mwili wa Kristo na jinsi ya kuutunza mwili wake hasa tukifahamu kuwa Yesu Kristo ndiye kweli.
ROHO MTAKATIFU HULIPA KANISA UJASIRI.
Hofu ni adui mkubwa mno wa imani katika Bwana, hata Biblia inazungumzia kuwa pasipo imani haiwezekani kabisa kumpendeza Mungu. Mwamini au kanisa linapotawaliwa na hofu haliwezi kuishi kwa imani, hivyo basi halitampendeza Mungu daima.
Adui huyu wa imani humsonga mno mtu kabla ya kubatizwa na Roho Mtakatifu na lazima msaada toka mbinguni uingie ndani ya mtu na kuiondoa hofu hiyo. Tunapoyaangalia maisha ya mtume Petro, tunaona kuwa yametawaliwa na hofu hata wakati fulani alikaribia kuzama baharini kwa sababu ya hofu.
Hofu ya mauti ilimfanya Petro pia amkane Bwana na mwalimu wake Yesu Kristo mara tatu, alimpenda Yesu lakini hofu ilimsukuma kumkana Bwana Yesu. Hofu hii ilimpata kwa sababu ya kitu fulani kilichopungua ndani yake. Lakini tunapoyaangalia maisha yake ya baada ya kumpokea Roho Mtakatifu tunayaona kuwa yalikuwa ya tofati kabisa. Mtume Petro hakuogopa tena kumshuhudia Yesu mbele za watu, aliweza kuutangaza umasihi na ufufuko wake, pamoja na kupaa kwake kwa ujasiri alioupata alikuwa hata radhi kufa kwa ajili ya injili na ndivyo livyotokea. Kuhusu ujasiri tunaoupata baada ya kubatizwa kwa Roho Mtakatifu sio jambo la kuzusha, bali Yesu mwenyewe alitamka hivyo kwa wale mia na ishirini wakiwemo wale thenashara katika kitabu cha Matendo ya mitume Yesu alisema;
“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilieni juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika uyahudi wote na hata nje ya nchi” Matendo ya mitume 1:8
Hapa neno shahidi lina maana kuwa jasiri hata hatua ya mauti, haya yanawezekana tu kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
ROHO MTAKATIFU HUFANYA KAZI KAMA NJIWA (HUA)
“Nuhu akangoja siku saba tena, kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, njiwa akamjia jioni, na tazama alikuwa na jani bichi la mzeituni kinwani mwake ambalo amelitunda, basi nuhu akajua ya kwamba maji yamepungua juu ya nchi” (Mwanzo 8:10-11)
Tunapoangalia ndege huyu, tunaweza kuona kuwa ni ndege anayepatikana katika jamii zote za watu wa ulimwengu tulionao. Katika Agano la kale ndege huyu alikuwa ni sehemu ya sadaka iliyoweza kutolewa kwa Bwana; hata Mariamu na Yusufu waliweza kutoa njiwa wawili kama sadaka mbele za Mungu (Luka 2:24) ni jambo la kushangaza kuona kuwa kama vile hua (njiwa) wanavyoweza kupatikana kwa jamii zote tajiri na masikini, vivyo hivyo Roho Mtakatifu naye anaweza kuingia mahali popote ili mradi tu awe amefunguliwa mlango.

Njiwa (hua) ana tabia ya upole kila wakati, tena ni ndege aliye mtulivu mnoo. Roho Mtakatifu anapoingia ndani ya mtu humfanya mtu huyo kuwa na maisha ya utulivu na upole. Mtu aliye mkali kwa kila hali, anapopokea zawadi hii, hali yake hubadilishwa kabisa. Badala ya mbegu ya ukali na hasira hupandwa mbegu ya upole katika BWANA. Jambo lingine tunapomwangalia ndege huyu, tunaona kuwa tangu zamani alitumwa kama mjumbe au msaidizi. Nuhu alimtuma njiwa akayakague maji juu ya uso wa Nchi na kupitia kwa njiwa, Nuhu aliweza kutambua majira ambapo maji yalipungua usoni mwa nchi. Nuhu hakuweza kuifanya huduma hii, bali njiwa aliweza kumsaidia. Kwa hili tunaiona kazi za Roho Mtakatifu iliyowazi, yeye ni msaidizi wa kanisa. Mwanadamu peke yake hawezi kushinda na kumpendeza Mungu, haya huwezekana tu pale mtu anapobatizwa kwa Roho Mtakatifu. Yeye ni msaidizi wa mambo yetu yote yaliyo ya rohoni nay ale ya mwilini, hata Yesu mwenyewe alimwita msaidizi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni