Jumamosi, 22 Aprili 2017

ISHARA ZA LUGHA NA FAIDA ZAKE.


Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni muujiza wa ajabu mno unapotokea kwa mtu. Muhusika huelewa fika kuwa amepokea kitu ambacho sio cha kawaida. Wengi wanaodai kupokea  ubatizo wa Roho Mtakatifu wakati bado hujipoteza kwa hiari yao wenyewe, na kama yanenavyo maandiko kwamba huangamizwa kwa kukosa maarifa. Ninasema hivi kwa sababu Mungu ametoa ishara za wazi mno hata kwa wale walio nje kuthibitisha kuwa mtu huyu amepokea ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Kwa ujumla ziko ishara nyingi zinazothibitisha tendo hili, ishara nyingi zinatokea ndani ya mtu mwenyewe, lakini zipo zingine zinazotokea nje ya mtu na kuwa ushuhuda hata kwa watu wengine. Tunapoziangalia zile zitokeazo nje tunaweza kuona kuwa iko ishara moja inayotokea mar azote kwa kila mwamini anayepokea ubatizo huu; ishara hii ni ile ya mwamini kunena kwa lugha nyngine kama vile Roho anavyomjalia kutamka.
Katika hili, mtu yoyote asije akadanganywa na shetani kwamba mtu anaweza kubatizwa kwa Roho Mtakatifu bila ishara hii kutimia au kuonekana kwa kulielewa jambo hili vizuri zaidi hebu tuangalie jinsi wale waliotutangulia walivyopokea ahadi hii.
WALE 120 WAKIWEMO MITUME WALINENA KWA LUGHA MPYA
“Hata ilipotimia siku ya pentekoste walikuwa wote mahali pamoja, kukaja ghafla toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukatokea ndimi zilizogawanyika kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka” (Matendo 2:1-4)
Biblia inasema wazi kuwa kanisa limejengwa katika msingi wa Mitume na manabii, Yesu mwenyewe akiwa jiwe kuu la pembeni, kwa usemi huu ni vema kuangalia jinsi mitume walivyopokea Nafsi hii ya Mungu. Nasema hivi kwani mitume ndio wa kwanza katika Agano la kale na jipya kumpokea Roho Mtakatifu ikiambatana na ishara ya kusema kwa lugha nyingine na wale waliowazunguka walishuhudia tendo hilo, hata wakadhihaki wakisema kuwa wamelewa kwa mvinyo mpya.
MTUME PAULO ALISEMA KWA LUGHA NYINGINE.
“Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote” 1Wakorinto 14:18
Paulo alipookoka, Mungu alimtumia Anania ili amwekee mikono Paulo apate kuona tena kiroho na kimwili. Biblia inasema kuwa Anania alifanya hivyo pale Dameski Paulo alijazwa Roho Mtakatifu maana ndilo lilikuwa kusudi la kutumwa kwake.
Tunaposoma ushuhuda wa Paulo katika mistari iliyotangulia, Paulo anatuambia kuwa yeye ananena kwa lugha; kwa hiyo ni wazi kuwa siku ile alipoombewa na Anania alipokea Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya.
KORNELIO NA WALIOKUWA PAMOJA NAYE WALINENA KWA LUGHA NYINGINE.
Kornelio alikuwa mtu aliyekuwa na kiu ya kuurithi uzima wa milele, hata hivyo kiu yake haikumzalia matunda aliyoyatazamia kwa kutoielewa njia ya wokovu kwa usahihi. Mungu alipoiona kiu na njaa yake hii ya muda mrefu, alimtuma mtume Petro ilia pate kumwelezea njia ya Bwana kwa usahihi.
Katika mji huu wa Kaisaria Mtume Petro alipata nafasi ya kuongea mambo mengi yahusuyo usahihi wa njia ya Bwana na wale walioyasikia waliyaamini kuwa ni maneno yatokayo kwa Mungu aliye hai. Kwa kule kuamini kwao, maandiko yanasema kuwa;-
“Roho Mtakatifu akawashukia wote waliosikia lile neno, na wasiotahiriwa walioamini wakashangaa watu wote waliokuja na Petro, kwa sababu mataifa mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha na kumwadhimisha Mungu” Matendo 10: 44-46
Maandiko haya yanatuthibitishia kuwa kanisa la Kaisaria lilipokea ubatizo wa Roho Mtakatifu, kila mmojawapo alinena kwa lugha mpya; nasema hivi kwani maandiko yanasema kuwa wale waliokuja na Petro walishangaa? Kwa sababu mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha na kumwadhimisha Mungu.
WANAFUNZI KULE EFESO WALISEMA KWA LUGHA
“Basi, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha yote niliyowaamuru ninyi, na tazama mimi nipo pamoja nanyi hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28: 19-20)
Maandiko haya yanaonyesha kazi kubwa iliyoachwa mabegani mwa mitume na kanisa kwa ujumla, wakati Yesu alipokuwa tayari kupaa kuelekea mbinguni wengi walioachiwa huduma hii hapo mwanzo ukiondoa mitume, hawakuwa na ufahamu mkubwa jinsi wawezavyo kuifanya huduma hii kubwa, hawakuwa pia na zana za kazi kama hizi tulizonazo sasa, pamoja na upungufu huu, walikuwa waaminifu kukifanyia kazi kile kidogo walichonacho ili kuonyesha utii wao mbele za Mungu kwa ufahamu huu mdogo huduma nyingi ziliweza kufanywa nusunusu bila ya kukamilika.
Katika mji wa Efeso mtume Paulo alikutana na waamini ambao licha ya kuokoka bado walibakiza mambo fulani fulani waliyotakiwa kufundishwa. Maandiko yanasema kuwa
“Ikawa Apolo alipokuwa Korinto, na wanafunzi kadhaa wa kadhaa huko; akawauliza, je mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, la hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia (Matendo 19:1-2)
Paulo alihojiana na wanafunzi hawa aligundua kuwa walihitaji kuelezwa na kufundishwa mambo fulani fulani waliyopungukiwa ndani yao, likiwemo hili la ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Baada ya kuwafundisha maandiko yanasema kuwa;- 
“Paulo akaweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha na kutabiri”(Matendo 19:6)
Wanafunzi hawa hawakuwa wachache, neno linasema walikuwa kumi na wawili, wanaume tu, bila kutaja wanawake, na hawa wote walijazwa Roho Mtakatifu na kusema kwa lugha nyingine.
WAAMINI WA SAMARIA WALISEMA KWA LUGHA.
Wakati wa mateso ya mwanzo kwa kanisa, wandugu walitawanyika huko na huko wakihubiri neno. Mtu mmoja aliyeitwa Filipo alipata nafasi ya kuhubiri katika Samaria, lakini kwa sababu ambazo hazikutajwa; mtumishi huyo hakuwafanyia huduma ya ubatizo wa Roho Mtakatifu. Maandiko yananena kuwa, mitume waliposikia wakamwendea na kuwaombea ili wapokee ahadi hii. Kwa kweli hatuoni mahali palipotamkwa wazi kuwa walinena kwa lugha nyingine, ila hapa kuna maneno yanayonifanya namini kuwa ishara hii ilitokea.
Biblia inatuambia;-
“Hata Simoni alipoona ya kuwa wanapokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mkono ya Mitume, akataka kuwapa fedha akisema nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemuwekea mikono yangu apokee Roho Mtakatifu. (Matendo 8:18-19)

Hapa kuna swali la kujiuliza, Je! Simoni alijuaje kuwa watu wale wamepokea Roho Mtakatifu? Ni dhahiri kuwa hawakuwa kimya; asingelielewa kuwa wamepokea Roho Mtakatifu. Ni lazima kuwa kuna ishara ya wazi iliwatokea watu wale na kwa Simoni mwenyewe. Ninaamini kuwa hata hawa walinena kwa lugha nyingine kama ilivyokuwa kwa wengine.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni