Jumanne, 22 Agosti 2017

KUSIFU NA KUABUDU NA UKUAJI WA KANISA



Kusifu na kuabudu kama kutafanyika kama inavyopaswa, ni njia mojawapo kubwa inayoweza kukuza kanisa kwa kasi kubwa ya ajabu.
Lakini ni masikitiko makubwa sana kwamba maana hasa ya sifa imeanza kupotea kwa sehemu kubwa katikati ya wana wa Mungu, na kwa waimbaji wa nyimbo za injili ndio hali mbaya kabisa.

Wengi wao hawapo kiroho, ila wapo zaidi kibiashara. Wapo tayari wasimpendeze Mungu lakini wawapendeze wanadamu. Kwa maana hiyo wanajali zaidi utukufu wa wanadamu, kuliko utukufu wa Mungu.

Na ili wawafurahishe wanadamu, wanajaribu kuchukua kila kitu cha kimwili na kukifanya kuwa ni cha kiroho. Matokeo yake ni kuzidi kufifisha nuru ya Kristo katika kusanyiko la wana wa Mungu.

Kwa Mungu wetu sadaka hii ya sifa hutolewa kwa hiari ya mtu bila kujali ana shida gani au yuko katika hali gani.
-     Ibada ya kusifu na kuabudu inapofanyika ipasavyo husababisha mlipuko na ukuaji wa kanisa,
-     kwani humpa nafasi Roho Mtakatifu kutembea kwa wingi katikati ya watakatifu (2Wakorinto 6:16)
“tena pana patano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wangu”.
-      Matendo ya Mungu huonekana na kanisa huongezeka kiidadi.

Matokeo ya kusifu na kuabudu
Kanisa huongezeka kwa kasi kama ilivyokuwa siku ya pentekoste.
Kushusha uwepo wa Mungu na nguvu za Mungu kusambaa Watu wasioamini huvutwa na nguvu za uwepo wa Mungu na kufanana,
(1Samuel 19:18-21)
a. Mfalme Sauli alikamatwa na uwepo siku tatu
“Hivyo Daudi akakimbia, akajiponya, akamwendea Samweli huko Rama, akamwambia hayo yote Sauli aliyomtendea. Kisha yeye na Samweli wakaenda na kukaa katika Nayothi, Naye Sauli akaambiwa, kusema Angalia yule Daudi yuko katika Nayothi, huko Rama. Basi Sauli akatuma wajumbe ili kumkamata Daudi; nao hapo walipowaona jamii ya manabii wakitabiri, na Samweli amesimama kama mkuu wao, roho ya Mungu ikawajilia wajumbe wa Sauli, nao pia wakatabiri. Naye Sauli alipoambiwa, akatuma wajumbe wengine, wao nao pia wakatabiri kisha yeye mwenyewe akaenda Rama, akafika kunako kile kisima kikubwa kilicho huko Seku akauliza, akasema Je, wako wapi Samweli na Daudi? Na mtu mmoja akajibu. Tazama wako Nayothi huko Rama. Basi akaenda Nayothi huko Rama; na roho ya Mungu ikamjilia yeye naye, akaendelea mbele huku akitabiri, mpaka kufika Nayothi huko Rama, Naye akavua nguo zake, akatabiri mbele ya Samweli, akalala uchi mchana kutwa na usiku kucha siku ile. Kwa hiyo watu husema Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?”
-     Sauli mwenyewe alipokwenda kumfuatilia Daudi Roho wa Mungu alimjilia yeye naye akakamatwa kwa siku tatu.
-     Mtume Paulo anasema kwenye (1Wakorinto 14:24b)
“Siri za moyo wake huwa wazi na hivyo ataamua kumuabudu Mungu akianguka kifudifudi na kukiri kuwa Mungu yu kati yenu bila shaka, matokeo yake mtu huyo ataokoka.”
-     Watu wengi wenye majini na mapepo wanapojihudhurisha au kupita karibu na maeneo ambayo watu wa Mungu wanasifu na kuabudu, mapepo hushindwa kustahimili uwepo wa nguvu za Mungu yanalipuka na watu hao wanafunguliwa na kumgeukia Mungu.
Mungu wetu hufanya kiti chake cha enzi juu ya sifa za watu wake. (Zaburi 22:3) 2Nyakati 5: 13-14)
-     Mahali pa ibada hakuna atakayeondoka akiwa kama alivyoingia,
-     bali ataondoka akiwa na utiisho wa uwepo wa nguvu za Mungu uliojidhihirisha kwake.
-     Watu waliookoka, wahamiaji na wageni hudumu mahali penye uwepo wa nguvu za Mungu na wote waingiao hudumu hapo angalia
b. Makutano walishikwa na uwepo wa Mungu,       
 (Mathayo 15:29-39)
Yesu akaondoka huko akafika kando ya bahari ya Galilaya, akapanda mlimani, akaketi huko. Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake, Hata ule mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona. Wakamtukuza Mungu wa Israeli. Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, nawahurumia makutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekuwa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula; tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani. Wanafunzi wake wakamwambia. Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? Yesu akawaambia mnayo mikate mingapi? Wakasema saba na visamaki vicheche. Akawaagiza mkutano waketi chini. Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba. Wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, makanda saba, yamejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila wanawake na watoto. Akawaaga makutano, akapanda chomboni, akaenda pande za Magadani,”
Hapa unaweza kuona mambo yafuatayo;-
-     Makutano hawa walidhoofu kwa sababu ya kuona njaa,
-     lakini hawakuondoka kwenye mafundisho ya Bwana Yesu kwa sababu ya nguvu kubwa ya uwepo wa Mungu.
-     Ukiona watu kwenye ibada wakiangalia saa, wakihamaki ibada inapochelewa kwisha na wengine kuamua kuondoka kabla ibada haijaisha,
-     Hiyo ni ishara tosha ya kufahamu kwamba mahali hapo hapana uwepo wa Mungu na nguvu zake,
-     Bali panakwenda kimazowea. Au pana namna ya mapokeo ya ibada za kidini.

c.  Kwenye mlima wa ugeuko (Marko 9:5)
Petro alimwambia Bwana Yesu kuwa ni vizuri sisi kuwepo hapa tufanye vibanda vitatu. Maneno ya mtume Petro yalitokana na uwepo wa utukufu wa Mungu. Petro alisahau kwamba alikuwa na familia na pia wanafunzi wenzao tisa waliowaacha walikuwa wanawahitaji pia. Aliona ni vema na kutamani kukaa pale mahali penye utukufu wa Mungu na uwepo wake. Mahali ambapo hapana watu wala mahitaji muhimu ya maisha palionekana ni pazuri zaidi kuwepo kuliko mahali pengine popote, yeyote anayeokoka au kuhamia katika kanisa lenye kushusha uwepo wa Mungu katika ibada ya kusifu na kuabudu, hataondoka mahali hapo.


Matokeo ya kusifu na kuabudu kwa watakatifu.
-     Huleta hofu ya Mungu katikati ya watakatifu.
-     Huyeyusha mioyo migumu katika kupokea mambo ya Mungu.
-     Hulipua vizuizi vya kuikulia neema ya Mungu
-     Nguvu ya Mungu huonekana.
-     Utendaji wa Roho Mtakatifu hujidhihirisha kwa karama kuchanua.
-     Moto wa uamsho hutembea na maelfu ya watu kuokoka.
Matokeo ya kusifu na kuabudu kwa kanisa (Yohana 4:1-23)
-     Mungu hupewa sifa na utukufu
-     Ni ibada ya moyo kwa moyo na Mungu (Yohana 4:24)
-     Roho ya mtu au yule mtu wa ndani ndiye awezaye kuabudu.
-     Mungu ni Roho anawatafuta watu kama hao wamwabudu.
-     Watu hawa ni wachache sana na adimu miongoni mwa wengi waziendeao nyumba za siku za jumapili. Ndio maana Mungu anafanya kuwatafuta.
-     Mungu wetu anayo namna ya kuabudiwa kutoka katika roho ya mtu wa ndani, ni mtu wa ndani pekee ndiye awezaye kumuabudu Mungu ipasavyo.
-     Yeye ndiye mwenye mahusiano na ushirika hai na Mungu.
-     Mtu asiyeokoka hawezi kuabudu Mungu kihalisi (Mt 15: 8-9)
-     Asiye okoka hawezi kuufikia ujuzi wa kweli katika kuabudu.
-     Mtu aliyeokoka ndiye pekee awezaye kuabudu halisi kwa kuwa mwelekeo wa kuabudu ni kutoka kwa mwamini kwenda kwa Mungu
-     Toka kwa mtu wa ndani hadi mawazo kisha maneno.
-     Maneno ni mawazo yaliyovishwa sauti hatimaye kuingia kwenye vitendo (udhihirisho wa mwitikio wa moyo)
-     Twamsifu na kumuabudu Mungu tukijieleza kwake.
-     Upendo wetu,utii wetu,kujitoa kwetu kwake twasema kuwa
§  Mungu ni nani
§  Amesema nini
§  Anafanya nini na alifanya nini
-     Asiyeamini mtu wa litulgia hawezi kufanya yote haya yeye binafsi toka katika vilindi vya moyo wake.
-     Mungu hana ushirika na kiumbe katika kuabudiwa.
-     Katika maandiko (Mt 4: 9-10) majibu ya Bwana Yesu kwa shetani yanaonyesha kuwa Mungu hana mshirika katika kupokea ibada na kiumbe yeyote duniani, mbinguni au kuzimu (kutoka 34:14) Mungu anasema kuwa yeye ni Mungu mwenye wivu.
Wafilisti katika kitabu cha (1Samweli 5:1-5) waliliteka sanduku la Mungu na kulitia katika nyumba ya dagoni mungu wao. Wakaliweka sanduku la Mungu karibu na dagoni mungu wao,
-     hii ilikuwa ni sawa na kumlinganisha Mungu YEHOVA na dagoni.
-     Kwa waisraeli lilipokuwa sanduku la Mungu ilikuwa ni ishara kuwa YEHOVA yuko mahali hapo.
-     Wafilisti walipoamka asubuhi siku ya pili, kumbe sanamu lao dagoni limeanguka kifudifudi mbele ya Mungu wa Israeli.
-     Huku kichwa cha dagoni na vitanga vya mikononi vimekatika vipo vimelala kizingitini dagoni imebaki kiwiliwili.
YEHOVA Mungu wetu ni Mungu mwenye wivu, na hatalinganishwa na chochote, maana yeye ndiye muumbaji.
-     Iwe binadamu, malaika au shetani na mapepo yake ambao awali walikuwa ni sehemu ya malaika wa Mungu kisha wakaasi, hapo ndipo walipopoteza nafasi zao katika ufalme wa Mungu mbinguni.
-     Kumbuka kwamba tumeumbwa ili tumuabudu Mungu. Hii ndio moja ya sababu kubwa ya kuumbwa kwa jinsi tulivyo. (Zab 103:1).
Kama vile wanadamu waundapo magari na mitambo mbalimbali, wanaunda wakilenga kutosheleza uwezo wa kutendea kazi iliyokusudiwa.
-     Hali kadhalika ndivyo ilivyo hata tunapoamua kujenga nyumba, barabara, n.k.
-     vivyo hivyo kwa wanadamu kila kiungo chetu kimekuwepo pia kutuwezesha kufikia makusudi ya Mungu ya kumwabudu tuwapo katika dunia tuliyoumbiwa. (Tazama Isaya 45:12).
Viungo vyetu pia hutuwezesha kuwa na mahusiano na dunia lakini tukishatoka duniani na kuvishwa mwili mpya (1Wakorinto 15:40) tujapokuwa katika mwili mpya lakini katika umbo la kibinadamu tutakuwa na;-
-     Miguu inayoweza kucheza kwa urahisi
-     Magoti yanayoweza kujikunja tuabudupo
-     Kiuno na mgongo uwezao kuinama na kuinuka
-     Mabega yawezayo kucheza
-     Mikono iwezayo kupiga makofi kunyanyuliwa juu
-     Kichwa kiwezacho kucheza
-     Kinywa chenye kutoa sauti zenye tuni mbalimbali.
Hakuna kiumbe aliyeumbwa huru kutenda vitendo vingi kama binadamu tazama (Zaburi 139:15).
Sifa za Bwana ni bubujiko la moyo (Yoh 4:10)
-     Bwana alimfananisha Roho Mtakatifu na maji yabubujikayo, ampokeaye humuondolea kiu milele.
-     Maji hayo hububujika kutoka utu wa ndani wa mtu hadi kudhihirika katika utu wan je (utu wa asili)
-     Hali ya ukame kiu haitakuwapo tena, hutasifu na kuabudu kwa dakika 2 na kujisikia kuchoka.
-     Hutakuwa na moyo unaokerwa na bubujiko la Roho Mtakatifu.
-     Hutazuwia kunena kwa lugha (1Wakorinto 14:39)
Kuna watu wanaodhani kuwa utaratibu wao wa ibada ni sahihi,
-     Watu hao hupanga kusifu na kuabudu kwa dakika zisizozidi 10.
-     Lakini matengenezo na mipango yao ya kanisa hupangwa husemwa kwa dakika zaidi ya 30.
-     Poroja za kusalimiana na kutambulishana huchukua zaidi ya saa.
-     Hapo wakisahau makusudi ya Mungu kwa wanadamu.


Napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuandika kitabu hiki kuhusu ibada.
Naamini kwamba bila ya himizo la Roho Mtakatifu ndani yangu nisingeweza kukamilisha kazi hii.
Ni matumaini yangu kwamba kila atakayesoma atapata msaada na kukua kiroho.
Wito wake kwa Kanisa la Kristo ni kuwataka waamini waijue ibada ya Kiroho na ya Kweli yenye upako wa Roho Mtakatifu. Ambapo waabuduo watamwabudu Mungu katika Roho na Kweli, na kurejesha maana ya sifa, ibada na kuabudu kulikopotea hekaluni mwa Bwana. Ibada ya kweli italeta furaha ya Roho Mtakatifu maishani mwa waamini na kurejesha tumaini la utukufu mioyoni mwao maana tayari wameona uwepo wa Mungu katikati yao, kisha kujenga imani zao, na shauku yao kwenda kuwa pamoja na Bwana Mbinguni.

IBADA NI NINI?
Ibada ni tendo la heshima ya hali ya juu linalofanywa na mtu kwa kiumbe aliye mkuu katika mazingira yake yote, kiroho na kimwili na kiumbe huyo akaaminiwa kuwa ni MWENYE ENZI asiyefananishwa na kiumbe kingine mkamilifu katika matendo yake.
Kuabudu Mungu katika Roho na Kweli kunaweza kukafanywa wakati wowote na mahali popote mradi lengo ni kumfanyia Mungu IBADA.
-     Jambo la muhimu ni yule tunayemwabudu kuliko mahali tunapofanyia ibada
-     ingawa mahali tunafanyia ibada ni kitu chema ,lakini pasipewe nafasi mioyoni mwetu na kuheshimiwa kama sehemu ya ibada.
-     Pamoja na hoja hiyo mahali pa ibada pasipuzwe na kudharauliwa maana pamewekwa wakfu kwa huduma ya Mungu pametakaswa.
-     Mtu akionyesha dharau au kuto paheshimu anaweza kupata madhara,
-     hivyo ni muhimu kila mtu ajue jambo hili na kuenenda kwa utaratibu na kwa heshima mahali hapo.

Kwa vile Ibada ni shughuli ambayo inashikamana sana na mfumo wa maisha ya mwanadamu, na kwamba ibada hutofautiana sana katika maana na mitazamo kulingana na imani ya mtu juu ya Mungu anayemwabudu, ni vema tukaelewa kwa usahihi ibada ninini kwa mujibu wa Biblia ifundishavyo.
“Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema , ya kupendeza, na ukamilifu”. (Rumi 12:1-2)

Tendo la Ibada ni tendo la kujitoa kama dhabihu, lakini ibada ya kweli lazima dhabihu hiyo iwe hai na takatifu, Mwili, Roho na ufahamu viwe na lengo moja lakumfanyia Mungu Ibada takatifu basi, ambapo ibada nje ya utakatifu si ibada inayompendeza.

IBADA – MAANA YAKE



Ibada ni kumshangaa Mungu. Kwa ufahamu tulio nao na akili ya kibinadamu tuliyo nayo hatuwezi kumwelewa Mungu kikamilifu tukamfahamu.
Isaya 55:8-9:,
“Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.”

Mungu ni mkuu kuliko uwezo wa ufahamu wa mwanadamu na yuko juu sana kuliko mawazo ya mwanadamu  na yuko juu sana kuliko njia za mwanadamu
kwahiyo hatuwezi kumfahamu vyema. Hivyo basi siku zote tutakapokusanyika pamoja au mtu akiwa peke yake kumwabudu na kukutana naye atamshangaa (tutamshangaa).
Hutaweza kukaa mbele za Mungu ukimwabudu katika Roho na Kweli ikawa jambo la kawaida maana Mungu huyo ni Mfalme Mkuu lazima utamshangaa Mfalme huyo. Utukufu wake utakushangaza na kutamani kumwangalia.

Wafalme wa dunia japokuwa ni wanadamu, raia wao hutetemeka na kuwaheshimu wanapojitokeza mbele na kila mtu hutamani kumwona na kumshangaa, na kukusanyika mahali pamoja ili wamsikilize Mfalme wao. Mungu ni Mfalme wa ajabu anayejihudhurisha kati ya watu wake wanapomfanyia ibada kwa kumwabudu na kuwashangaza waabuduo ambapo na wao wanazama katika mshangao. Zab. 47:7, 66:3, 68:35, 71:16, 89:7

Ibada inayokubalika
Si kila Ibada inayofanywa na mwanadamu ni halali na kukubalika na Mungu, hapana. Mungu ni Mungu wa utaratibu na mipango mikamilifu.
Mungu amesema wazi ni ibada ipi anaikubali na kuipokea akaisikiliza. Lakini kwa kuwa ulimwengu ni mpana na wenye tofauti za watu walio na itikadi tofauti na ibada za walimwengu pia ni tofauti.

Mungu wa kweli ni mmoja na njia ni moja ya kumfikia ambayo ni Yesu. Yohana 14:1-6, ITim 2:15.
Ni katika Yesu ambaye ni mpatanishi wetu na Mungu na ambaye ni kweli, njia na uzima tutasikilizwa na kukubaliwa,

Yesu anasema mtu yeyote hawezi kwenda kwa Mungu isipokuwa kwa njia yake, hakuna njia ya mkato kwenda kwa Mungu, bali ni kwa njia ya Yesu tu. Kwa hiyo ibada lazima iwe,
a.  Ibada katika Roho na Kweli yenye kumtambua Yesu kuwa kiini na mlengwa wa Ibada hiyo Mdo 4:11-12 Waef 2:4-8

b) Si ibada ya mdomoni wala makusanyiko ya kidini na taratibu za kibinadamu zilizobuniwa kwa umahiri na wala si mapokeo ya mila na desturi za watu. Mdo17:22-27

c) Ibada ambayo haimchanganyi Mungu aliyejifunua katika maandiko na miungu mingine, japokuwa miungu hiyo inaabudiwa na mamilioni ya watu pamoja na vitu vilivyotukuzwa kiasi cha kukubalika kuwa Mungu. Zab 115:4-8

Sanamu zao ni fedha na dhahabu, kazi ya mikono ya wanadmu. Zina vinywa lakini havisemi, zina macho lakini haioni. Zina masikio lakini hazisikii, zina pua lakini hazisikii harufu. Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, wala hazitoi sauti kwa koo zake. Wazifanyao watafanana nao, kila mmoja anayezitumainia.
Sasa ili tujiridhishe na ibada ya kweli inayokubaliwa na Mungu hebu tuangalie ibada ya mbinguni ilivyo, na jinsi viumbe wa mbinguni wanavyomwabudu Mungu.

IBADA KUU MBINGUNI Ufunuo 5:6-14
Biblia inafunua ibada kuu inayoendelea mbinguni ambayo washiriki wa ibada hiyo ni wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne,
-     Wenye vinubi na vitasa vya dhahabu vyenye maombi ya watakatifu, wakiwa mbele za kiti cha enzi cha Mungu.
-     Viumbe hawa wapo hapo kufanya ibada maalum ili kumwabudu na kumpa sifa Mwanakondoo,
-      wanafanya hivyo kwa kuimba wimbo mpya wenye sifa kwa Mwanakondoo kisha malaika wengi, elfu kumi mara elfu kumi, elfu mara elfu, ambao wamekizunguka kiti cha enzi wanajiunga katika SIFA hizo. Uf 4.8-11
-     Hapa ndipo ibada hii kuu inaanzia, ambapo wenye uhai wanne wasiopumzika mchana na usiku wanamsifu Mwanakondoo wakisema Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu na kusababisha wazee ishirini na nne kuanguka chini na kumsujudia aliye Hai milele na milele,
-     huku wakivua taji zao na kuzitupa mbele ya kiti cha Enzi, wakisema, Umestahili wewe Mungu kupokea utukufu na heshima na uweza kwakuwa ndiwe uliyeviumba vitu vyote kwa sababu ya mapenzi yako vilikuweko navyo vimeumbwa.
Kisha kwa sauti ya pamoja wanasema: Anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, heshima, utukufu, na Baraka Mwanakondoo aketiye kwenye kiti cha enzi.
Maneno haya saba ni sifa kuu kwa Yesu ambaye ni Mwanakondoo wa Mungu.
Hatimaye baada ya ngurumo hizo za sauti ya sifa, kila kiumbe kilichoko mbinguni, duniani, na baharini vikamsifu Mwanakondoo,
-     na wote wakaanguka wakamsujudia Mwanakondoo. Sifa hii ikatikisa ulimwengu,
- ulimwengu mzima ukamwabudu Mwanakondoo, Ibada hii haifanywi kwa mtume, nabii, malaika ,miungu wala kwa mwanadamu bali Ibada hii inamlenga Yesu Mwanakondoo.
-     Ibada inayofanywa kwa mtu mwingine mbali na Yesu siyo Ibada ya kweli na Mungu haisikilizi.
-     Inasikitisha kuona Ibada za mamilioni ya watu hazisikilizwi na Mungu kwa kuwa zinafanywa nje ya kumwabudu Yesu.
-     Katika Zaburi 98:1-9 na 96:1-8 Mfalme Daudi anatoa mwaliko wa kumwabudu Bwana kwa wimbo mpya kwa sababu Bwana Ametenda mambo ya ajabu,
-     Daudi anasema, “Inueni sauti, imbeni kwa furaha,
-     Nayo mito ipige makofi, na kulibariki jina lake,
-     Na kutangaza wokovu wake,
-     Kwa kuwa Bwana ni mkuu na mwenye kusifiwa sana.
Wito huu ni wito wakumwabudu BWANA peke yake.
Paulo naye anatia mkazo wa kumwabudu Mungu kwa kutoa mwongozo jinsi ya kufanya ibada katika roho ya uimbaji anasema
Neno la Kristo likae kwa wingi mioyoni mwenu (ndani yenu) katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkimwimbia Mungu kwa Neema mioyoni mwenu. Mkisemazana kwa zaburi na tenzi, na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Mungu mioyoni mwenu, nakumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo” (Kol 3:16-17),

Ef 5:19-20.
-     Ibada ya kweli ni ile inayomlenga Yesu na si vinginevyo.
-     Unaweza kuona jinsi mwanadamu anavyotoa muda wake, nguvu na mali katika ibada hewa kwa viumbe na sanamu, badala ya kumfanyia Mungu ibada katika Kristo Yesu,
-     wito huu ungali na nguvu ile ile kwetu kumgeukia Mungu na kujiunga na viumbe hawa wa mbinguni kumfanyia ibada sahihi Mwanakondoo.
-     Mungu ni mtakatifu na wa haki hana kigeugeu na habadiliki, ni mwadilifu.
-     Hawezi kuweka njia tofauti tofauti za kumwabudu kwa kila mtu.
-     Hiyo ingekuwa sawa na wasafiri wawili waendao mji mmoja lakini kwa njia tofauti zinazoweza kuwafikisha pale waendapo,
-     hilo haliwezekani kwa Mungu maana ni Mtakatifu, kwa utakatifu huo, Mungu ameweka njia moja ya kumwabudu ambayo ni Yesu Kristo.

IBADA NA UIMBAJI

“Mwimbieni BWANA wimbo mpya, Mwimbieni BWANA, nchi yote.” (Zaburi 96.1)
“Mwimbieni BWANA wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, mkono wake mtakatifu umetenda wokovu.” (Zaburi 98:1)

Mungu anapenda uimbaji na anapenda kuimbiwa wimbo mpya kama tuonavyoona katika zaburi hizi,
-     Kwa asili yake yeye ni mpya kila siku hajawahi kuzeeka wala kuchakaa,
-     basi kwa asili hiyo hupenda vitu vipya, ni muhimu kuwa na nyimbo mpya na pambio mpya katika ibada zetu.
-     Ibada inayofanywa katika Roho na Kweli haiwezi kuendeshwa bila ya kumwimbia Mungu nyimbo za sifa na za kumwabudu.
-     Huu ndio utaratibu na mfumo wa ibada ya kiroho, kuanzia mbinguni mbele ya kiti cha enzi na katika Agano la kale na Agano jipya mpaka leo.
-     Asilimia sabini na tano ya shuguli za kanisa ni kuabudu,
-     na asilimia tisini ya kuabudu ni uimbaji yaani kuimba. Nyimbo zinazoimbwa ziimbwe katika Roho na akili pia,
-     zikielekezwa kwa Mungu, zikikoleza maombi na sala zetu,
-     zikiibua sifa za dhati toka moyoni nakunyosha misisimiko ya nafsi, fikra, mwili isipotoke kwenda nje ya ibada ya kweli,
-     kwa hiyo nyimbo zisiimbwe kwa lengo la burudani, bali ziimbwe kwa lengo la kumsifu Mungu, kumshangilia, kumshukuru, kufariji, kutia moyo, kumkaribisha Mungu, kusaidiana, kuonyana nakujengana na kuachilia neema ya Mungu iwafunike wanaomwabudu mahali hapo.
   Matokeo ya Ibada kama hii ni makubwa,
2Nyakati 5:11-14.

“Wakamfanyia Bwana ibada kuu, Bwana akaijaza nyumba utukufu, makuhani wakashindwa kufanya kazi zao maana Bwana ameshuka katikati yao na kuwabariki”.
 Ibada inayoendeshwa bila uimbaji ni ibada bubu na haitaleta matokeo mazuri kwa waabuduo.Kwa kuwa Mungu ni mpenzi wa uimbaji ndani ya ibada zetu, hivyo ni muhimu mno kuimba kwa sauti zilizopangiliwa vizuri ili tumbariki.

UIMBAJI NDANI YA IBADA

Ni vigumu kutenganisha uimbaji na ibada, uimbaji umetawala matendo ya mwanadamu kwa asilimia kubwa, kiasi kwamba uimbaji ni lugha inayomuwezesha mtu kujieleza alivyo,
-     ni kama chakula cha lishe chenye virutubisho vya aina zote kwa afya ya mwanadamu.
Uimbaji unagusa maeneo yote ya utu wa mtu na mahitaji ya mwanadamu, kiroho na kimwili. Uimbaji ni chakula kilicho bora kabisa kukidhi matamanio ya mtu mzima.
-     Mtu akiwa na huzuni, msiba, ataimba ili afarijike na kujiliwaza au ataimba ili aomboleze,
Katika sherehe umetawala, dhifa, mikutano ya aina zote ya kiroho na ile ya kisiasa, matambiko, kazi, hata katika vita, matangazo ya biashara, vyombo vya habari, matukio yote haya hutanguliwa na uimbaji na kumaliziwa na uimbaji.
-     Uimbaji huleta uponyaji wa Roho na mwili na huondoa mkandamizo na msongo wa mawazo.
-     Hii ndiyo nguvu iliyomo katika uimbaji. Ni vema basi kila mmoja wetu akaelewa uimbaji ni nini,
-     na unafanyikaje ili aweze kutumia katika kumwabudu Mungu wakati wa ibada.
-     Si jambo jema kuimba ovyo bila mpangilio ama bila kujua nakuelewa.
NYIMBO NA AINA YA IBADA
Kila ibada ni muhimu na ina malengo yake na madhumuni, ama makusudi ya kufanya ibada hiyo. Kwa hiyo ni lazima kila ibada ipewe nafasi katika nyimbo zinazoimbwa katika ibada hiyo.
-     Iwapo nyimbo zinazoimbwa haziendani na lengo, kusudi au madhumuni ya ibada, basi ibada hiyo imevurugika na watu watashindwa kuabudu kuelekea lengo la ibada hiyo.
-     Mwisho watu watachanganyikiwa na kuwa watazamaji na kuwaondoa kabisa katika ibada inayoendelea hapo Ingawa kimwili watakuepo.
Si vema kuimba wimbo wa maombolezo katika ibada ya arusi au wimbo wa pasaka katika ibada ya krismasi ama wimbo wa uinjilisti katika ibada ya meza ya Bwana.
-     IBADA si jambo la mzaha bali ni tendo la kumuabudu MUNGU,
-     Kwa hiyo ni lazima ufanyike upangaji na uchambuzi makini wa nyimbo zipi ziimbwe katika ibada ipi ili kukidhi hitaji la ibada husika
Ufuatao ni mchakato wa aina ya ibada.
Ibada ya kuabudu ziimbwe nyimbo za kuabudu,
-     Ibada ya SIFA, Ibada ya uinjilisti, Ibada ya maombi na kujitoa, Maisha ya Kikristo kwa ujumla wake.
Imbisha nyimbo zinazoendana na ibada hizo.
Nyimbo za Matukio. Hakikisha unaimba nyimbo zinzokwenda na matukio hayo.
Meza ya Bwana, Krismas, Pasaka, Arusi, Maziko na Maomboleza, Siku kuu, Mwaka mpya, Watoto, Mwaliko wa mtu kwa Yesu, Nyimbo za taarifa au ushuhuda wa matendo makuu ya Mungu, Utakaso na Kutia moyo na IMANI, Ujasiri, Mashambulizi kwa shetani au Vita ya kiroho, Roho Mtakatifu na nyimbo zenye ujumbe maalum kwa matukio maalum kama vile, uzinduzi wa nyumba ya IBADA, au jambo lolote linalogusa kanisa au jamii.

Ni muhimu kuimba nyimbo zinazogusa ujumbe wa matukio hayo. Huu ni mwongozo wa jinsi ya kuendesha ibada na uimbaji utakaoleta Baraka na kutufikisha katika kusudi la ibada husika.
Uimbaji ni somo pana lenye kuwa na mielekeo tofauti tofauti kulingana na matumizi ya mtu anavyotaka.

-     Ingawa kanuni za muziki (uimbaji) ni zilezile kwa kila mwelekeo.