Jumanne, 22 Agosti 2017

UMUHIMU WA IBADA YA KWELI




Ibada ya kweli ambayo ni BORA ni pale tunapomgusa MUNGU katika ENZI YAKE kwa roho ya unyenyekevu na kupondeka kwa moyo. (Zab 100:1-4)
-     Zaburi hii inatuonyesha njia nzuri ya kumwabudu Mungu na kuhimizwa kumfanyia Bwana shangwe, sifa na shangwe ni stahili ya Mungu.

Uimbaji wa sifa – ni ufunguo Mkuu wa kuingia ndani ya nyumba ambamo Mungu yumo (ibada ni huduma, na kuabudu ni kazi) kuabudu ni utumishi angalia anavyosema
-     Mtumikieni Bwana kwa furaha Njooni mbele zake kwa kuimba
-     Huwezi kuingia ndani ya nyumba pasipo kufungua mlango lazima uwe na ufunguo.
Kama Zaburi ya 100 inavyosema Ingieni malangoni mwake kwa kusifu na kwa kushukuru.
Isaya 1:12 Naye anasema,
“Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliye taka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu?”
Mungu anauliza mnapoingia nyuani mwake Kwa utaratibu upi maana huwezi kukanyaga nyua za Bwana kiholela, hapo ni Ikulu pana heshima yake na jinsi ya kuingia. Mungu kama Mfalme yumo ndani ya ikulu, nyumba yake, hekalu, yaani mahali palipowekwa wakfu kwa Ibada.

Tunapaswa kwenda hapo na ufunguo.
“Jueni Bwana ndiye Mungu, ametuumba na sisi ni watu wake na kondoo wa malisho yake”. Zab 100:1-4
-     anasema kwa msisitizo, Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru,
-     haya ni malango ya hekalu (hekalu la kale) Nyuani au barazani mwake kwa kusifu na kwa kushukuru na kuhimidi Jina lake.
-     Uimbaji ndiyo ufunguo wa malango ya Bwana kuingia barazani pake, Hodi yetu ni sifa, kuimba na kushukuru kunatupa kibali cha kuingia patakatifu pa patakatifu.
Kanisa na Mkristo asiyeimba na kusifu ni bubu, kamwe hawezi kuingia na kumwona mfalme Barazani pake. Mkristo huyo amekosa ufunguo hawezi kujieleza, hana shangwe, hana shukrani ni kama mtoto mchanga aliyezaliwa wodi ya wazazi lakini bado hajalia, ana kasoro ni kilema, ipo hatari ya kupoteza maisha.
-     Hivyo hivyo mkristo asiye na ufunguo huo atapoteza maisha ya kiroho, ibada ya kweli yenye funguo hizo ni uhai wa Mkristo.
-     Kusifu na kuabudu kunaonyesha uhai wakati tunapomwimbia nyimbo za sifa na shangwe namshnagaa mtu wa aina hiyo ambaye haabudu maana hana uhai.

INJILI ilienezwa kwa nyimbo katika karne ya 17 huko ulaya – Martin Luther, John Wesley, John Calvin, John Hus, John Wyclife walitumia nyimbo kuhubiri neno. Kwa sababu kuna nguvu yenye uhai wa Mungu katika sifa. Katika Mathayo 26:26-30 Hapa Yesu aliimba pamoja na wanafunzi wake, aliimba Zaburi 115 hadi 118. Zab 89:5-7 inasema mbingu zitayasifu maajabu yako na uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu. Hii inaonyesha kwamba walioko mbinguni wanaabudu.
Kutojali na kudharau uimbaji ni kumdharau Yesu ambaye aliimba  ni kupoteza ufunguo mkuu ambao hufungua nyumba na baraza la Mungu. Kumbuka Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu.
Baraza la watakatifu ni pale watakatifu wanapokusanyika kuabudu Mungu.
Katika 1Kor. 14:26 Paulo anasema mkutanapo pamoja kila mmoja ana Zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri, mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga. Hizi ndizo faida za kuwepo barazani pa watakatifu, na umuhimu wa ibada ya kweli, Vidokezo vya msaada unaopata unapoimba:
a.   Unawezeshwa kujieleza kwa undani jinsi unavyompenda na kumwabudu Mungu
b.   Uimbaji unakupa ufasaha wa kumsifu Mungu kwa furaha na uchangamfu.
c.    Utakaso na toba huambatana na kuimba bila kizuizi.
d.   Unawezeshwa kumfanyia Mungu ibada kama alivyo kuagiza na kwa wepesi.
e.   Ibada huongozwa na kuendeshwa vema kwa muziki na kumwabudu Mungu kwa utamu na kwa raha.
f.    Unawezeshwa kuonyesha upendo wako tena baada ya maungamo na ukiri wako kwa Mungu na kudhihirisha kwamba moyo wako umefunguliwa na umewekwa HURU.
Dondoo hizi ni nyenzo za muhimu kutusaidia kumwabudu Mungu ili tusipungukiwe na kukosa neema na Baraka zake zilizomo barazani mwake. Ingia na uzichote baraka kwa funguo ulizojifunza na utazipata tu kadiri unavyonyenyekea moyoni mwako.

JINSI YA KUIMBA
Zab 150:1-6, 33:1-3, 98:1-9, 100:1-4
Maandiko haya yanatuelekeza jinsi ya kumwabudu Mungu kwa vifaa mbalimbali vinavyotumika katika muziki, ikiwa ni pamoja na hali ya mtu anayeabudu inavyotakiwa kuwa. Huduma ya muziki wa kikristo ni muhimu iwe na mwelekeo wa kibiblia mifumo na malengo pamoja na utekelezaji wake lazima upatikane ndani ya maandiko matakatifu.
-     Kwa maana lolote tulifanyalo tunalifanya kama kwa Bwana. Basi kama ni hivyo tuyaangalie maandiko mbalimbali:
“Tumwimbie Bwana wimbo mpya, tumshangilie, tumpe shangwe, na sifa, shukrani, furaha, faraja na kumtukuza, vigelegele na kucheza”. (Zab 98:1)

-     Mambo haya ni sehemu ya muziki wa kikristo na wa kiroho.
-     Ni muhimu na lazima tuimbe kwa ustadi na kwa ubora, kwa ari kubwa na shauku, kwa kupania bila kujibakiza wala kujihurumia, hii ni kazi nzito sana.
“Akawaagiza baadhi ya walawi kwamba watumike mbele ya sanduku la BWANA, wamfanyie ukumbusho, na shukrani, na sifa, BWANA, Mungu wa Israeli Asafu mkuu wao, na wa pili wake Zekaria, na Yeieli, Shemiramothi, na Yehieli, na Matithiya, na Eliabu, na Benaya, na Obed –edomu na Yeieli, wenye vinanda na vinubi; naye Asafu mwenye kupiga matoazi; nao makuhani Benaya na Yahazieli wenye baragumu daima, mbele ya sanduku la Agano la Mungu…………….(I Nyak 16:4-11, 23-34)
-     Hapa tunaona uimbaji ni huduma ya makuhani
-     hii ndiyo ofisi ya mwimbaji ni kuhani wa Mungu afukizaye uvumba mbele ya madhabahu kwa sadaka za sifa na shukrani, (INyak 6:31)
-     tunaona Walawi waliimba kwa utaratibu ulioeleweka (INyak 16:4-11, 23:35)
-     Waliimba kwa zamu, walikaa kwa mtindo wa kueleweka wakati wa huduma.
-     Walijifunza kwa waalimu wao kwa bidii. walitabiri kwa kinubi, waimbaji ni manabii wanatabiri kwa vinanda wanavyovipiga kwa ustadi. (1Nyak 25:1-9)

HALI YA MOYO NA JINSI YA KUTUMIKA

Mungu ndiye anatoa karama na huduma hii, basi ni lazima watumishi waishi maisha matakatifu na moyo safi. Na unyofu wa moyo yaani mwenendo wenye tabia njema. hilo halikwepeki, wakiwa wamejitakasa mwili na roho, Ibada  ni tendo la kumcha Mungu. IIKor 7:1 Amos 5:21

Yatupasa kumwimbia Mungu tukiwa na vifaa vya muziki au vyombo vya muziki. Accompanyments au vikolezo.

Maandiko yanakazia sana kuimba pamoja na vyombo vinubi, vinanda, zeze la nyuzi kumi, filimbi na matari,


Mungu wetu ni mpenzi wa muziki kuliko mfalme yoyote wa duniani. Ili ibada ya sifa na kuabudu ikamilike, muziki wa vyombo ni muhimu, bila kusahau mfumo, mtindo na utaratibu mzuri.

UIMBAJI  NI TAALUMA
Mwimbaji asiyejua kuimba hawezi kuwa huru kuhudumu ni muhimu afahamu uimbaji, ili aimbe kwa uhuru na kwa ufanisi. Ufanisi unahitaji muda wa mazoezi yakutosha pamoja na mwalimu mwenye uwezo wakukuelekeza jinsi ya kuimba Muziki (uimbaji) upo katika mafungu makuu mawili:
1.          Vocal
2.          Instrumentals
VOCAL:
-     Ni sauti ya wanadamu. Sauti isiyochanganywa kitu chochote. Sauti asilia ya mtu (Natural voice)
INSTRUMENTALS:
-     Ni sauti zitokanazo na vyombo. Sauti pasipo kuchanganywa na kitu chochote yaani ala za muziki.
Sehemu hizi mbili zikichanganywa pamoja hufanya kitu kinachoitwa muziki (uimbaji) na kukamilisha maana ya neno muziki.
SAUTI.
Ni hisia inayonaswa na masikio na (hutengenezwa) na msuguano wa hewa katika mzunguko, mgongano wa vitu au mkwaruzo kiasi cha kutoa mlio (sauti).

SAUTI –MLIO (AUDIBLE, SOUND)
Kitaalamu Sauti ina misingi au kanuni. Misingi hiyo ni Miwili. Ni kwa misingi ya sehemu hizo mbili kuu- Sauti
hujengwa/huumbika, tutaelewa misingi hiyo vizuri kwa kuziangalia tabia za sauti
(Characteristics of Musical Sound) Au tabia za milio.
-     Msingi wa kwanza:
Sauti ina tabia ya – Melody – Yaani kwa Kiswahili – Ghani
Melody – Ghani – Ni mistari ya sauti ya muziki inayotambulisha chanzo (tone) cha wimbo
ni sauti yenye kuelekeza ubora wa mtiririko wa ghani (melody) unaokupa hisia ya mlio unaohusika au unaousikia.

Rhythm – Ni utaratibu au mfumo wa aina ya mwendo wa sauti katika wakati au mfululizo wa sauti katika muda, mwendo, pigo, mdundo au msisimko. Uwezo wa sauti wa kutembea katika wakati usiobadilika.
Harmony – Mkusanyiko wa sauti unaopendeza, utaratibu au mfumo wa ulinganifu wa sauti, usawa, muafaka, kusikilizana pasipokuachana kwa sauti au kuwa nje ya tune hasa wakati kuna watu wengi wanaimba, katika ngazi tofauti yaani sauti ya msitari wa 1, 2, 3 na 4 pamoja.
Unison—Ni sauti ya aina moja inayoimbwa na watu wengi bila ya kutofautisha ngazi za sauti ya kwanza, pili, tatu na nne. Na kwa kawaida sauti ya unison hutumia sauti ya kwanza.
Form – Ni mwonekano wa kipekee, utaratibu au mfumo wa kuweka uimbaji katika aina ya mfumo unaojitambulisha katika mtindo wake wenyewe kama vile mtindo wa kizungu, wa kiafrika, kinyakyusa, kibena nakadhalika.
Tone Color – Aina mbalimbali za sauti kufuatana na chombo au mtu anayeimba
– kwa mwanadamu sauti hutegemea mapafu yake na mishipa ya fahamu ya kichwani.
Yaani sauti kavu, sauti laini, yenye mikwaruzo, yenye mawimbi nakadhalika,
kusikika kwa sauti kipeke, kivyake kwa kadri ya mtu anavyotoa sauti au chombo kinavyo toa sauti kwa namna ya mlio wake
Msingi wa Pili:
Sehemu ya kwanza Nimetaja nadharia ya tabia za sauti, tabia hizi huwezi kuziona wala kuzihisi, ama kuzisikia, ila unaweza kuzifikiria katika mawazo.
-     Kuimba sio nadharia wala mawazo ni matendo halisi.
-     Nadharia hiyo lazima itafsiriwa katika vitendo tunavyoweza kuviona, kuhisi, kusikia tabia za sauti au milio hiyo.
-     Haya yanawezekana kwa kutumia nyenzo, njia za muziki za kiufundi zinazotuwesha kutenda.
(Musical Skills Performance Methods)
Nyenzo au njia hizo ni:
(a)      Kuimba – (Singing – Melody)                  Unapoimba ndipo Ghani itajitokeza katika mpangilio wa sauti kwa njia inayopendeza na kwa utaratibu, hapo Tone Color itasikika yaani kwa kuimba wimbo, ghani na aina za sauti katika ubora wake utasikika.
(b)      Kupiga vyombo vya muziki Accompanyments vikolezo. Melody ambayo ni Ghani itasikika – Tone color pia itasikika.
(c)       Form, Kutenda vitendo – (Moving Movement Steps) Rhythm Na Form itaonekana yaani kucheza kwa mwendo   wa mapigo. Yaani sauti na maneno unayoimba    yataenda kwa kufuata mapigo na midundo ya wimbo na kuwa na muonekano wa kipekee.
(d)      Harmony. Kusikiliza ndiko kutakuwezesha kuleta ulinganifu katika mkusanyiko wa sauti za kupendeza na kukuwezesha uimbe sawasawa na sauti nyingine bila kuhitilafiana wala kuachana au kuwa nje ya ghani.
(e)      Kuunda au Ubunifu (Creation – Form, Rhythm na melody) Wimbo utakamilishwa kwa kuunganisha nyenzo hizo nakuwa halisi yaani wimbo halisi wenye kusikika vizuri.


Katika msingi huu wa pili tunafika katika kukamilisha muziki na ndiyo uimbaji. Muziki ni sayansi lakini kila mmoja wetu anayo na anaweza kuitendea kazi kwa kujifunza na kujizoeza.

SIFA ZA MWIMBAJI.
Kazi ya kumwimbia na kumsifu Mungu ni huduma inayodai maisha ya mtu kujitoa kikamilifu na kuwa na mwenendo ulio safi.
-     Mungu aliwaweka waimbaji katika hekalu waifanye huduma hiyo maalumu.
-     Kwa hiyo ni lazima pawepo na sifa za kutosha na mchakato yakinifu kuhusu mwimbaji anayefaa kuifanya huduma hii kubwa.
-     Mwimbaji ni chombo cha sifa za Mungu ni lazima chombo hicho kiwe na sifa zinazoendana na sifa za Mungu na heshima kimfaacho Bwana kwa kazi hiyo.
“Mpigieni BWANA vigelegele enyi wenyi haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo (Zaburi 33:1 1)

ROHO YA UIMBAJI
Ni kujaa Neno, kusemezana, kushangilia, kuimba kufundishana, kuonyana, kujaliana, umoja na shukrani,
“Tena msilewe kwa mvinyo ambamo mna ufisadi ;bali mjazwe roho, mkisemezana kwa zaburi natenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo” (Waefeso 5:18-20)
Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na nyimbo, na tenzi za rohoni, huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu”. (Wakolosai 3:16-17)

hii ndiyo Roho ya uimbaji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni