Jumapili, 20 Agosti 2017

UMUHIMU WA VIONGOZI WA IBADA NA WAIMBISHAJI WA SIFA NA KUABUDU KANISANI




Mara nyingi sana kanisa Linategemea sana uwezo wa kiroho wa kiongozi wa ibada na sifa, lakini pia na vikundi vya sifa, au kwaya kama vipo. Ambavyo mara nyingi vinatakiwa kuwa vimeundwa na watu waliochaguliwa kwa uangalifu sana, kutoka katika vikundi vya waombaji waliopo kanisani, au pia katika vikundi vingine na hasa katika idara mbalimbali za kanisa kama vile vijana, wanawake, wanaume, watoto, n.k.

Hatua za kanisa kwenda katika kilele cha sifa (Patakatifu pa Patakatifu)
Kanisa huwa linapitia katika hatua tatu ili kufikia katika kilele katika kusifu na kuabudu. Kwa kawaida watu wanapofika kanisani huwa wako mwilini halafu kwa msaada wa viongozi wa sifa huenda kwenye nafsi na hatimaye huingia rohoni. Baada ya kanisa kufikishwa rohoni hapo ndipo mhubiri anaweza kufikisha ujumbe wa Mungu bila vikwazo.

Ili kurahisisha kanisa zima kuingia katika hatua ya patakatifu yaani kwenye nafsi na hatimaye kuingia patakatifu pa patakatifu (rohoni) mapema iwezekanavyo, inategemea pia na waumini wenyewe wana uelewa kiasi gani wa jinsi ya kupaendea patakatifu pa patakatifu.

 Waongoza ibada

Kuongoza ibada ni jukumu zito linalohitaji unyenyekevu na usikivu wa hali ya juu sana, kwa sababu unachukua jukumu la kuwa kiunganisho kati ya Mungu na watu. Ukikosea kidogo tu, basi umeharibu maana yote ya Mungu kuabudiwa.
1.          Wanajukumu la kuhakikisha kuwa wanatimiza makusudi ya Mungu kwa watu wake.
2.          Hivyo kabla hujaabudisha watu, ni lazima wewe kwanza uwe tayari umeshamwabudu Mungu
3.          Unatakiwa uwe mahala ambapo unataka kuwapeleka watu ambapo wewe mwenyewe umeshawahi kufika.
4.          Ni lazima uijue njia sahihi ya kufika unapotaka kuwapeleka watu.
5.          Unaoabudu nao waone na kuiga kutoka kwako, sio unawaongoza ili mradi kutimiza wajibu tu.
6.          Fikiri juu ya Mungu, mwelekezee mawazo yako yeye, hisia zako zishikwe kwake.
7.          Epuka sana kwa namna yoyote kufanya vitu ambavyo vitaumiza nafsi ya watu, kama vile kuwalaumu kwamba wamepooza, au hawajachangamka n.k.
Wakati mwingine kwa kutokujua hili utaona kiongozi wa sifa kabla hata hajaanza kuwaongoza watu kwenda mbele za Mungu anaanza kuwalaumu mbona hamchangamki! mbona mmepooza hivyo, lazima mchangamke maana tunaenda kwa Mungu aliye hai.
Hapo ni lazima ujiulize kuwa ina maana watu hawajitambui kwamba wanakwenda kwa Mungu wao aliyewanunua kwa damu yake? Sasa kanisa kama lina watu makini watajua kwamba kiongozi wao ibada “amechemsha,” yaani anajihami kwa kuwa hana maandalizi kiroho ya kutosha kuwaandaa waumini wake kukutana na Mungu, na hivyo anataka kuhamisha jukumu lake kwa watu wengine ambao wanatakiwa kuhudumiwa na yeye. Anajaribu kukwepa wajibu wake na kulaumu watu ambao wamekuja kutafuta faraja kutoka kwa Mungu wao badala ya kuwapa faraja yeye anawatwisha mzigo wa lawama.
-     Unakuta kiongozi anaanza kuimbisha wimbo mara anasimamisha na kuanza kuwalaumu watu,
-     kwa kufanya hivyo ndio anawatoa kabisa katika mtiririko wa hisia za kwenda mbele za Mungu ambazo walikuwa wameanza ili kuwasaidia kuhama kutoka mwilini kwenda kwenye nafsi.
Unawarudisha tena mwilini na matokeo yake mpaka muda unafika muhubiri anapanda kwenye madhabahu kanisa bado liko kwenye kiwango cha mwili.
Kwa muhubiri makini hawezi kuhubiri katika hali hiyo, unaweza kuona anaanzisha tena nyimbo ili kuwaweka watu sawa, ingawa inakuwa ni kazi ngumu kiasi.
Kuongoza ibada ni taaluma jifunze sana,
na ni huduma ya Rohoni, kwa maana hiyo mtegemee Mungu akuwezeshe usiyoyaweza.
Kwa sababu upako ni wake Mungu na ni yeye pekee awezaye kukupaka Biblia inasema;-

Ila sasa niletee mpiga kinanda Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga, mkono wa BWANA ukamjia juu yake. Akasema BWANA asema hivi, Fanyeni bonde hili lijae mahandaki kwa kuwa BWANA asema hivi hamtaona upepo, wala hamtaiona mvua, ila bonde hilo litajaa maji, nanyi mtakunywa, ninyi na ngo’mbe zenu na wanyama wenu. Na jambo hili ni jepesi machoni pa BWANA pia atawatia Wamoabi mkononi mwenu. Nanyi mtapiga kila mji wenye boma na kila mji ulio mzuri, na kila mti mwema mtaukata, na chemichemi zote za maji mtaziziba, na kila mahali palipo pema mtapaharibu kwa mawe ikawa asubuhi wakati wa kutoa sadaka ya unga, tazama maji yakaja kwa njia ya Edomu hata nchi ikajaa maji. (2Wafalme 3:15-20)
Inakubidi kiongozi wa ibada uwe mnyenyekevu na mtii kwa Mungu, Lakini pia unyenyekevu na utii kwa uongozi wa kanisa.
-     Unyenyekevu, heshima na upendo kwa watu wote unaowaongoza, huku ukijua kuwa msingi wa huduma na vipawa mbalimbali vya Mungu hutiririka kwa mtu aliyefurika upendo kwa Mungu na kwa watu pia.
Ukitaka ufanikiwe katika huduma hii ni lazima huduma yako ijengwe katika msingi wa upendo na unyenyekevu kwa Mungu na kwa watu wa aina zote.
-     Katika Biblia Tunaona Mungu anawaita watu maalumu kuongoza, kupiga kuimba katika kwaya kwa niaba ya ndugu biblia inasema;-

“Akawaagiza baadhi ya Walawi kwamba watumike mbele ya sanduku la BWANA, wamfanyie ukumbusho, na shukrani, na sifa, BWANA, Mungu wa Israel; Asafu mkuu wao, na wa pili wake Zekaria, na Yeieli, na Shebamiramothi, na Yehieli, na Matithiya na Eliabu, na Benaya, na Obed- Edomu, na Yeieli, wenye vinanda na vinubi naye Asafu mwenye kupiga matoazi; nao makuhani Benaya na Yahazieeli wenye baragumu daima, mbele ya sanduku la agano la Mungu. Ndipo siku hiyo Daudi alipoagiza kwanza kumshukuru BANA kwa mkono wa Asafu na nduguze.1Nyakati 16:4-7

Ukisoma zaidi kitabu cha mambo ya Nyakati wa pili sura ya tano utaona maelekezo jinsi huduma ya kweli ya kuabudu inavyofanya uwepo wa Mungu uonekane na Mungu kujulikana kwa nguvu na ajabu.

a.         Uwe na matayarisho yako binafsi
Lazima uwe mahala ambapo unataka kuwapeleka watu. Ujiandae kuteka hisia za watu ambazo zimevurugwa na shida za dunia yenye mifadhaiko mbalimbali kutoka kazini, na sehemu zingine, zina matatizo, zimejaa michezo ya TV,
vyakula, Wachumba wa kike au wa kiume n.k.

Ni jukumu la kiongozi wa ibada na sifa, kuwachukua wote hawa, kwa upole wa hali ya juu katika hisia zao, na kuwapeleka mahali ambapo yeye mwenyewe kama kiongozi unapotaka wafike, hakikisha unazingatia mambo yafuatayo;-
1.          Kuishi maisha matakatifu, na kuhakikisha uko salama kiroho wakati wote.
2.          Hakikisha kuwa uko msafi mbele za Mungu yaani huna hatia katika uhusiano wako na Mungu kabla hujaenda kwa watu ili uende nao kwa Mungu.
3.          Mwombe Roho Mtakatifu mwelekeo, wakati unapanga nyimbo akupe thyme inayoeleweka kwa washirika wako.
4.          Fanyia mazoezi mapema nyimbo ulizochagua, huku ukizitafakari maana zake kwa kwa hisia za ndani sana.
5.          Jiombee mwenyewe, waimbaji wenzako pamoja na nyimbo zako mpate upako wa Roho Mtakatifu.
6.          Jiandae kuteka hisia za watu zimwelekee Mungu, kwa maneno ya Mungu ambayo atakupa nawe uyaamini.
7.          Wakati wa ibada, uwe makini katika mawasiliano na watu unaowaongoza, hakikisha wanakusikia vizuri
8.          Nenda nao hatua kwa hatua kwa kutumia lugha nzuri ya kujenga na kutia moyo, maneno ya kinabii (tabiri yale unayoyatarajia).
9.          Uwe na ujasiri kuwa unaijua vizuri njia unayo waelekeza waiendee.
10.      uwe mwepesi kutambua Roho wa Mungu anapoanza kufanya kazi mwachie aendelee kuwahudumia watu, hili ndilo kusudi la kuabudu (tuogelee katika Bahari ya upendo wa Roho mtakatifu)
11.      Uwe tayari kutumika jinsi ulivyo bila kujaribiwa kuiga kuwa kama mtumishi fulani.

12.     Mungu amekuchagua wewe jinsi ulivyo, mtegemee Roho Mtakatifu, huu ni mwito mkuu na wa heshima yeye atakuongoza mtegemee.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni